IJUE AFYA YAKO

Maelezo kwa akina mama na Wakunga (2)

- Kuvimbewa:

Kunywa maji mengi, kula matunda na vyakula vyenye nyuzinyuzi kama vile mihogo na makapi ya nafaka. Fanya mazoezi mara kwa mara. Usitumie dawa za kuharisha.

 

DALILI ZA HATARI WAKATI WA UJAUZITO:

- Kutoka damu:

Kama mwanamke anatoka damu hata iwe kidogo wakati akiwa mjamzito, hii ni dalili ya hatari. Huenda ikawa mimba inaharibika. Ni lazima alale kimya na daktari aitwe.

Ikiwa damu inatoka mnamo siku za mwisho inaweza kuwa ni kwa sababu kondo la nyuma limezuia mlango wa uzazi. Hii inaweza kumsababisha mama kutokwa na damu hadi kupoteza maisha yake kama hakupata msaada wa mtaalamu. Jaribu kumpeleka hospitali haraka ili achunguzwe na daktari bingwa.

Upungufu mkubwa wa damu:

Mwanamke ni mdhaifu, kachoka na mwenye rangi hafifu, kama hakutibiwa, anaweza kufa kwa kutokwa na damu nyingi wakati anapojifungua. Chakula kizuri peke yake, hakitoshi kutibu upungufu wa damu wa namna hii. Muone mganga akupe vidonge au sindano za chuma (iron salts). Ikiwezekana, ni bora ajifungulie hospitalini hasa akiwa kama atahitaji kuongezewa damu.

Uvimbe wa mgiuu, mikono na uso ukiambatana na kuumwa kichwa, kuona kizunguzungu na kutoona vizuri, ni dalili za Sumu ya mimba.

Kuongeza uzito ghafla nguvu za mwendo wa damu(blood pressure) na wingi wa protini katika mkojo, ni dalili nyinginezo za muhimu. Ni heri ukamuone mkunga au bwana mganga ambaye anaweza kupima vitu hivi.

Ili kutibu sumu ya mimba inambidi mwanamke:

- Alale kimya kitandani

- Aepuke chumvi (asitumie chumvi au vyakula vyenye chumvi)

- Amuone daktari upesi ikiwa haoni nafuu mapema hasa kama anapata matatizo zaidi ya kuona, uvimbe usoni au anaanguka kifafa. Maisha yake yako hatarini.

Ili kujikinga na sumu ya mimba, kula chakula bora, hakikisha unapata protini ya kutosha na tumia chumvi kidogo sana.

Ikiwa miguu tu, ndiyo imevimba, huenda si kitu cha hatari sana lakini, angalia dalili nyingine za Sumu ya Mimba kama zitakazotokea. Tumia chumvi kidogo tu.

UTUNZAJI WA MIMBA:

Vituo vingi vya afya pamoja na wakunga, hushawishi akinamama Kuhudhuria kliniki za wajawazito mara kwa mara ili wapimwe na kushauriwa mahitaji ya afya njema.

Kama u- mjamzito, nenda katika kliniki hizi na utajifunza mengi ya kukusaidia kuepuka matatizo ya mimba na itakusaidia kupata mtoto aliye na afya nzuri.

Kama wewe ni mkunga, unaweza kutoa huduma nzuri kwa mama wajawazito kwa kuwakaribisha wahudhurie kliniki au kuwatembelea TU.

Ni jambo zuri kama watahudhuria kila mwezi kwa muda wa miezi minne kisha, kila wiki katika mwezi wa mwisho.

Hivi ni baadhi ya vitu muhimu ambavyo mjamzito atahitaji kufahamu:-

- Kupeana mawazo

Mwulize mama matatizo na mahitaji yake, amekwisha kuwa mjamzito mara ngapi, alijifungua lini mtoto wa mwisho na alikuwa na matatizo yoyote aliyoyapata alipokuwa mjamzito au wakati wa kujifungua.

Mueleze njia za kumsaidia yeye na mtoto wake wawe katika afya bora pamoja na: kula chakula bora hasa chenye wingi wa protini, vitamin, chuma na kalshiumu

Afya njema:

Ni muhimu kumzindika mtoto ili asipate magonjwa kama pepopunda (dawa hutolewa katika mwezi wa 6,7 na 8 wa ujauzito kama ni safari ya kwanza ikiwa alikwisha jikingia zamani basi mpe nyongeza akiwa katika mwezi wa 7).

Fanya mazoezi ya mwili na mapumziko ya kutosha.

Chakula bora:

Mchunguze kuona kama anakula vizuri, ana upungufu wa damu, kama ndio; mueleze namna ya kula vizuri. Ikiwezekana, hakikisha anapata vidonge vya chuma hasa vilivyo na folic acid na vitamin C. Mshauri namna ya kuzuia kichefuchefu au kutapika wakati wa alfajiri pamoja na kiungulia.

Mchunguze kama anaongezeka uzito wa kawaida.

Ikiwezekana, apimwe kila ahudhuriapo kliniki. Itambidi aongezeke kilo 8 hadi 10 katika miezi 9 ya ujauzito.

Kama haongezeki uzito, ni dalili mbaya.

Kuongezeka uzito ghafla katika miezi ya mwisho, ni dalili mbaya pia. Kama huna mizani, jaribu kumchunguza jinsi alivyo kama anaongezeka uzito. Au tengeneza mizani.

Matatizo madogo

Muulize mama kama ana matatizo ya kawaida ya ujauzito. mueleze kuwa hayana hatari kwake wala kwa mtoto na jaribu kumfariji jinsi iwezekanavyo

Dalili za Hatari

Mpime kuona kama kuna dalili yoyote ya hatari, , mpime mapigo ya damu kila anapohudhuria kliniki. hii itakufahamisha midundo yake ya kawaida ikiwa kama anapata matatizo baadaye, (kwa mfano kuzirai kutokana na Sumu ya mimba au upungufu mkubwa wa damu).

Mpime nguvu za mwendo wa damu na uzito wake, chunguza hasa dalili hizi:

-Kuongezeka uzito ghafla

-Kuvimba mikono na uso

-Ongezeko la nguvu za mwendo wa damu

-Upungufu mkubwa wa damu

-Kutokwa damu ukeni, zote hizi ni dalili za Sumu ya Mimba

Wakunga wengine wanaweza kuwa na karatasi za 'dip sticks' au njia nyingine za kupimia protini na sukari kwenye mkojo. wingi wa protini ni dalili ya Sumu ya Mimba. Wingi wa sukari ni dalili ya Ugonjwa wa kisukari,.

Ikiwa dalili yoyote ya hatari inagunduliwa hakikisha kuwa mama huyo mjamzito anamuona daktari mapema iwezekanavyo.

Jinsi mtoto anavyokua na kukaa ndani ya nyumba ya uzazi

Kila wakati mjamzito anapohudhuria kliniki ni lazima apimwe na kupapaswa nyumba ya uzazi ili kuthibitisha kukua kwa mimba na kika cha mtoto.

jambo hili anaweza kuelekezwa mama na kulifanya mwenyewe.

Kwa kawaida kizazi kitakuwa na upana wa vidole 2 juu zaidi baada ya kila mwezi.

Akiwa mjamzito wa miezi 4 1/2 kizazi kitakuwa usawa wa kitovu

Kila mwezi andika ni upana wa vidole vingapi mji wa uzazi upo juu au chini ya kitovu. kama nyumba hiyo ya uzazi inaelekea kuwa kubwa zaidi au inakua haraka mno, huenda ikiwa ina maji mengi kuliko kiasi chake cha kawaida (polyhydramnious) na itakuwa vigumu kumpapasa mtoto ndani yake.

Kukiwa na maji mengi ndani ya nyumba ya uzazi kunahatarisha kutokwa na damu kwa wingi wakati wa kujifungua na huenda ikawa mtoto huyo akawa ni kilema.

Jaribu kupapasa jinsi mtoto alivyokaa.

Kama amekaa kwa kukingama ni lazima mama amuone daktari kabla uchungu wa mimba haujaanza kwa sababu kuna uwezekano wa kufanyiwa operesheni. .

Mpigo wa moyo wa mtoto tumboni

Baada ya miezi 5 ya ujauzito sikiliza mapigo ya moyo wa mtoto na hakikisha kuwa mtoto anacheza.

unaweza kuweka sikio katika tumbo la mama lakini itakuwa vigumu kusikia chochote ila ni rahisi sana kusikia kwa kutumia kipimo cha moyo wa mtoto (au unaweza kutengeneza kimoja kwa udongo wa mfinyanzi au mti mgumu) (kipimo cha moyo wa mtoto tumboni - )

Kama moyo wa mtoto unasikika vizuri sana chini ya kituvu cha mama katika mwezi wa mwisho wa mimba basi kichwa cha mtoto kipo chini na atazaliwa akiwa amekitanguliza.

lakini kama unasikika vizuri juu ya kituvu cha mama labda kichwa kipo juu na huenda ikawa akatanguliza matako wakati atakapozaliwa.

Kama una saa yenye mkono wa sekunde itumie kwa kuhesabu mapigo ya moyo wa mtoto. mapigo kati ya 120 hadi 160 kwa kila dakika ni ya kawaida kama ni chini ya mapigo 120 kwa kila dakika kuna hitilafu (labda umehesabu vibaya au umesikia mapigo ya moyo wa mama, pima mapigo ya mshipa wa damu wa mama Si rahisi kusikia mapigo ya moyo wa mtoto, inahitaji mazoezi.

Haki za Wafungwa na Hali ya Magereza -Tanzania Bara (2)

KATIKA gazeti hili toleo lililopita, tuliandika habari juu ya kitabu kilichoandikwa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) kiitwacho, HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA-TANZANIA BARA, ambacho kimesambazwa katika magereza mbalimbali ili kuwafanya wanajamii na wafungwa wenyewe, kuzifahamu haki zao na kujua namna ya kujirudi.Kuanzia toleo hili, tutaanza kukichapisha kama kilivyo tukianzia na dibaji iliyooandikwa Februari 5, 2001, na Kamishna Mkuu wa Magereza nchini, Bw. Onel E. Malisa.

UTANGULIZI

Upo msemo usemao ‘kama unamtendea mtu kwa kadiri alivyo, ataendelea kubakia hivyo hivyo alivyo. Lakini kama utamtendea kwa kadiri ambavyo anapswa au angepaswa kuwa basi atakuwa kama anavyotakiwa kuwa au ambavyo angepaswa kuwa’.

Hivyo jamii na vyombo husika inavyowatendea wafungwa inachangia katika kuwabadilisha ama kuwaacha wabakie walivyo au hata kuwaharibu zaidi.

Wapo wengi ambao wana mashaka na hujiuliza kama magereza yanahusiana na haki za binadamu. Hii inadhihirisha ufinyu wa mawazo miongoni mwa wengi kuhusiana na jukumu la magereza katika jamii nzima.

Pengine jitihada za kutosha hazijafanyika kuelimisha watu juu ya nafasi na wajibu wa magereza katika kulinda haki za watu waliomo jela. Hivyo jitihada zinahitajika ili kufikia azma ya kubadilisha fikra za wanajamii na wafungwa wenyewe waweze kubadilisha mienendo yao na kurudia hali ya kuwa raia wema. Na hili ndilo lengo la kijitabu hiki, kuchangia katika kuelimisha umma juu ya suala zima la magereza na wafungwa.

Kwa kupanua uelewa wetu wa nafasi na wajibu wa magereza yafaa tufanye tafakari katika maeneo fulani ambayo inaaminika yatasaidia kutuongoza kuelewa vizuri.

Mtu akiwemo gerezani kwa sababu yoyote iwayo hakumwondolei utu na ubinadamu wake sana sana ananyang’anywa uhuru wake.

Wafungwa wanabakia kuwa watoto wa Mungu na wanahitaji kupewa thamani ya kiutu na kutendewa kiutu.

Ikumbukwe pia miongoni mwa wafungwa katika mazingira fulani haki haikutendeka. Hata kutoka maandiko ya dini mbalimbali tunasoma hayo.

Kutoka imani zetu na historia ya dini zetu tunaona kwamba wapo viongozi na wafuasi wa dini mbalimbali waliotumikia vifungo bila hatia yoyote. Pengine kwa kusingiziwa kutokana na kufundisha ukweli halisi wa maisha ya watu. Je twaweza kuthubutu kusema hawa walipoteza thamani yao mbele ya Mungu kwa kuingizwa gerezani?

Kwa wale waliongia gerezani kwa sababu ya uhalifu wa aina yoyote ile bado tukitafakari upendo wa Mungu kwa binadamu twaona, ni ule usio na mipaka. Yeye anawapenda wote maskini, wadhambi, dhaifu na wanyonge hata wakosaji na anawaita wote kuupokea mwaliko wa upendo wake, kujirudi na kuishi maisha yaliyo bora.

Haya si kutoka maandiko ya kidini tu bali hata yamewekwa katika Katiba za nchi na matamko mbalimbali ya kitaifa na kimataifa juu ya haki za Binadamu. Jitihada hizi zikilenga kuhimiza utekelezaji wake.

Raia wote tunaitwa na tunao wajibu wa pekee hapa kuonyesha huruma yetu kwa wale walio gerezani, na zaidi kufanya jitihada za pekee kusaidia wale ambao hawakutendewa haki waweze kurudishiwa iliyo haki yao.

Kwa upande wa idara ya Magereza tunao wajibu mkubwa wa kuwatendea kiutu na kuwasaidia watoto wa Mungu walio gerezani kujiunda upya ili waweze kutoka gerezani wakiwa raia wema wanaoweza kutoa mchango wao katika kujenga Taifa letu.

Hata hivyo jamii inapaswa kutafuta sababu za watu kufanya vitendo vya uhalifu vinavyopelekea kuhukumiwa kwenda jela, na jamii hiyo hiyo kwa pamoja inao wajibu wa kutafuta njia ya kukabiliana na sababu hizo ili walau kuweza kuzipunguza kama sio kuziondoa kabisa. Mathalan matatizo ya umaskini, kukosa ajira, elimu duni, inafaa kwanza kupunguza matatizo hayo kama ikiwa kweli tunataka kupambana na uhalifu ndani ya jamii yetu.

Inafaa pia ieleweke kwamba kuweka watu gerezani na kuwatunza ni mzigo mkubwa kwa walipa kodi, na wakati huo huo magereza yanaonekana sio njia madhubuti ya kupambana na uhalifu. Utafiti uliofanyika katika nchi nyingi unaonyesha kuwa mbali ya kuongezeka wafungwa bado uhalifu uaendelea kuongezeka hivyo kuna haja ya kufikiri upya.

Sote tunaitwa kujisomea kitabu hiki ambacho inaaminika kitaimsha jamii kufikiri upya. Kijitabu hiki kinaeleza kwa kifupi juu ya aina za wafungwa na haki zao pamoja na taratibu za kumwingiza mtu gerezani.

Upagani unavyochangia mauaji ya vikongwe Shinyanga

Na Mwandishi Wetu

Shija Magoke, alipouguliwa na mwanae alimpeleka kwa mganga wa kienyeji anayeishi kijiji cha jirani na kwao huko Lyabukenda, Shinyanga vijijini.

Magoke anaenda kwa mganga huyo kutokana na shinikizo la jirani yake ambaye anadai kuwa mganga huyo ana uwezo wa ajabu na lazima atakuwa anajua ni nani ambaye amemroga mtoto huyo.

Jirani yake huyo anasema kuwa hata yeye alisaidiwa na mganga huyo na mbali ya yeye, watu kadha wamepata msaada mkubwa kutoka kwa mtaalamu huyo.

Safari inafanyika hadi huko na mganga huyo baada ya kupiga ramli, anamwambia kuwa mtoto wake huyo amerogwa na mwanamke ambaye ana undugu naye.

Mganga huyo anambainishia kuwa huyo aliyemroga alifanya hivyo kutokana na wivu alionao kwa kuwa yeye binafsi (huyo mchawi) hana mtoto.

Mganga anasita kidogo kumtaja moja kwa moja huyo mchawi lakini, mwishoni anatoa sharti la litakalomuwezesha kumtaja mhalifu huyo.

Anadai ng’ombe wa idadi kadha na kwa kuwa mhusika ana shida na mifugo anayo, anakubali na ndipo anapomtaja baada ya kufanya vituko na mambo mengi ya ajabu ambayo anadai kuwa, ni ya kiganga.

Mganga huyo anamtaja mhalifu huyo kuwa ni bibi mdogo wa mtoto ambaye anaishi hapo nyumbani kwao na wakati akimsikiliza mganga huyo mtoto anazidiwa zaidi.

Anahangaika mganga huyo kumtibia kwa dawa za namna mbalimbali mtoto huyo na homa inapanda zaidi hatimaye, anafariki akiwa mikononi mwa baba yake mbele ya mganga huyo.

Baba wa mtoto, mwanae na mtu mwingine aliyemsindikiza, wanarudi nyumbani na hasira zinawaka juu ya bibi wa mtoto huyo na mbaya zaidi anazuiwa hata kuhudhuria mazishi hayo.

Siku tatu baada ya mazishi, watu wasiojulikana wanavamia kibanda cha huyo bibi na kumkata mapanga na kufariki baadaye huku kukiwa na fununu kuwa anahusishwa na mauaji ya mjukuu wake.

Hilo ni moja kati ya matukio zaidi ya mawili ya mauaji ya vikongwe kila wiki yanayotokea katika baadhi ya vijiji vya Mkoa huo kulingana na takwimu za Chama cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).

Mwenyekiti wa chama hicho mkoa huo, Perpetua Magoke anavitaja baadhi ya vijiji ambapo kumeshamiri vitendo vya namna hiyo.

Anavitaja na wilaya vilivyopo katika mabano kuwa ni Lyabukenda, Seseko, Mipa (Shinyanga Vijijini), Ushirombo, Masuibwe (Bukombe) na Mwadoya (Meatu).

Anasema kuwa sababu kubwa ya kuwepo kwa matukio ya namna hiyo, ni upagani uliomo miongoni mwa wakazi wa vijiji vya mkoa huo ambapo wengi wao hawana dini au wamekuwa wakishiriki dini za jadi.

Kuwepo mbali kwa huduma za afya, kumewafanya wanajamii wengi kukimbilia kwa waganga wa tiba za jadi kila wanapokumbwa na tatizo fulani.

Anasema kuwa kwa kutambua hali hiyo, kuna makundi maalumu ya watu ambayo yanajinufaisha na biashara hiyo ya mauaji ya vikongwe ama kwa kuwatuhumu uchawi kutokana na kuwa na macho mekundu.

Vitendo hivyo ni mradi mahsusi kwa baadhi ya watu katika mkoa huo ambapo wamekuwa wakijipatia maelfu ya pesa na mali zingine kusaidia kuuawa kwa vikongwe hao.

Anasema kuwa watu hao wamekuwa wakiitwa kwa majina tofauti ikiwa ni pamoja na Ibulaga bagikulu ( Wauaji Wazee) au Isambula balogi (Wasambaratishaji wachawi) na kutokana na matatizo ya kiuchumi, watu wa namna hiyo wamekuwa wakiongezeka.

Magoke anasema kuwa sababu hizo za kiuchumi, pia zimepelekea wazazi wengi kuwapeleka watoto wao kwa bibi zao na wanapofariki wakiwa huko, tuhuma za mauaji huelekezwa kwa vikongwe hao.

Kiini cha mauaji hayo, anaeleza kuwa ni tabia ya wanaume wa mkoa huo wanaomiliki mali nyingi kutaka kuoa wanawake wengi jambo ambalo linapelekea baadhi ya wanawake kutuhumiwa uchawi pale mwanaume huyo anapofariki.

"Siku hizi hali ni mbaya hasa maradhi haya ya UKIMWI, sasa mwanaume anapougua na kufariki, mmoja kati ya wake zake ndiye ambaye ananyooshewa kidole" anasema Suzzane James ambaye ni Mweka Hazina wa WLAC mkoani humo.

Chanzo cha yote anasema kuwa ni ramli na bao ambapo waganga wamekuwa wakiwalaghai watu wenye matatizo na kula pesa zao na kuwaachia matatizo ikiwa ni pamoja na hayo mauaji.

Suzzane anasema kuwa mauaji ni mradi katika mkoa huo na kuna watu ambao wapo tayari kupeleleza uhusiano wa familia fulani na hata kufuatilia ugonjwa wa ama mtoto au mtu mzima na kuwasiliana na mganga.

Anafafanua kuwa watu hao wachonganishi wamekuwa wakipata malipo mazuri kutokana na mauaji hayo na ingawa serikali imepigia kelele tatizo hilo, lakini jamii inahitaji kuelimishwa zaidi.

Anasema kuwa watu wa mkoa huo wakipata elimu ya dini na kumjua Mungu, wataweza kuepukana na matatizo hayo tofauti na ilivyo sasa ambapo nguvu ya serikali peke yake haitoshi.

Chama hicho cha wanasheria wanawake ambacho kinahitaji msaada kutoka taasisi za dini na vyombo vingine, tangu mwaka 1996 kimekuwa kikitoa elimu kuhusiana na haki za binadamu katika mkoa huo.

Wakati umefika kwa taasisi za dini na mamlaka zingine kuelekeza nguvu zao huko na kusaidia kuwatuliza vikongwe ambao wanaishi kwa wasi wasi na wengine wamekimbia makazi yao na kuwa omba omba mjini humo.

Imani ya dini za asili inapaswa ipigwe vita kwa nguvu zote kutokana na ukweli kuwa inapotosha na kuiongezea jamii mzigo mwingine kutokana na mauaji hayo ambayo chanzo chake kikubwa ni ukosefu wa imani ya kiroho.

Kinyume cha hivyo jamii ya mkoa huo na nchi nzima kwa ujumla itaendelea kushuhudia vikongwe wa mkoa huo wakiendelea kuuawa na kuishi maisha ya dhiki na fadhaa kutokana na wanaowategemea kuwaona maadui na watu wenye hatia.

Walala hoi wasikubali kutumiwa kama madaraja ya kujineemesha

Na Aloyce Ndeleio

FALSAFA za baadhi ya viongozi waasisi wa mataifa kadha yaliyokuwa yanatawaliwa na mwisho yakajikomboa au kujinyakulia uhuru, zinaonesha kuwa walikuwa wanaona mbali katika maono ya kuiepusha jamii na majanga mbalimbali ambayo yangeweza kuzikumba jamii zao na hata za mataifa mengine.

Mmoja wa viongozi hao ni muasisi wa taifa la Ghana; Hayati Osagyefo Kwame Nkrumah aliyesema kuwa, kuna kundi katika jamii aliloliita Déclassé linalojumuisha walalahoi kuanzia wale wasio na ajira maalumu au maarufu kama wamachinga, ombaomba, malaya au changudoa kama wanavyojulikana ambao wakitumiwa vizuri, wanaleta mabadiliko katika jamii.

Kutokana na kuwepo kwa kundi la aina hii katika jamii nyingi, ama limekuwa likifumbiwa macho kuwepo kwake na hakuna anayejali. Pia kuchunguza kwa kina kama kuwepo kwake kunaweza kuiletea jamii madhara au kuijenga kutokana na namna linavyotumika.

Kundi hili la wanajamii limekuwa mara nyingi bila lenyewe kujijua likitumiwa na viongozi au wanasiasa katika kufanikisha azma zao katika uwanja wa kisiasa, kiuchumi na hata katika nyanja za kijamii.

Mwanafalsafa mwingine ni muasisi wa Jamhuri ya Watu wa China Hayati Mao tse Tung ambaye katika kupigania haki, alisema, "Pigania, shindwa, pigania tena, shindwa tena, pigania mpaka upate ushindi" na kuongeza kuwa hii ndio falsafa ya mwanamapinduzi.

Katika enzi hizi za demokrasia, maneno hayo yanaweza kuwa kwenye tafsiri rahisi ya gombea, shindwa, gombea tena, shindwa tena, gombea tena mpaka upate ushindi ndio falsafa ya demokrasia . Hili limeshajionesha kutokana kumwaga sera ambapo baadhi ya wagombea katika nafasi mbalimbali wamefanikiwa kupata ushindi na wengine kushindwa katika chaguzi kadha ambazo zimefanyika hapa nchini na baadhi ya wagombea, kukumbwa na upepo wa mabadiliko ya kupanda na hata kushuka kisiasa.

Ni kundi hili la walalahoi linakuwa mara nyingi mstari wa mbele katika mahudhurio ya kampeni na hata kuwa washabiki wakubwa wa viongozi mbalimbali wa kisiasa.

Kundi hili limekuwa linaingia au kuingizwa jumla jumla kutekeleza wanayoambiwa au kuelekezwa na viongozi wao kwa matumaini ya kupata ufumbuzi wa matatizo. Hii inatokana na mabadiliko wanayoahidiwa kupatiwa na hivyo, kutojua madhara yanayoweza kuwakumba.

Mara nyingi yanapotokea mambo yanayodaiwa ni ya uvunjaji wa amani au kadhia yoyote kinyume na sheria, inaonekana dhahiri waathirika ni wale walio katika kundi hili la walalahoi na kamwe sio wakubwa wao.

Katika maandamano ya hivi karibuni licha ya kutia doa historia ya nchi hii watu wengi wameathirika na iliyojitokeza kuanzia mwanzo wake hadi kuzimwa kwake.

Kwa mtizamo mwepesi, maeneo yalikopangwa kupitia maandamano hayo, ni yale yanayotumiwa kujipatia mahitaji na riziki zao kupitia shughuli mbalimbali za kibiashara na kwa hali hiyo, walalahoi wengi wamejikita katika maeneo haya.

Katika maandamano yenyewe, yalipojitokeza na mwisho kuzimwa ukiondoa hofu kutanda miongoni mwa wanajamii waathirika wakubwa wamekuwa si wengine, bali ni hawa walalahoi ambao ama wamepoteza maisha, ama wengine kujikuta kuambulia vilema na majeraha.

Ni dhahiri kwa muundo huo, hata shughuli zao za kujitafutia riziki na maendeleo yao na taifa kwa jumla, zimeathirika.

Kwa hali yoyote kundi kama hili halina njia nyingine ya kujipatia kipato zaidi ya kile kinachojulikana kama "mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe".

Kwa mlalahoi kujitolea kuwaneemesha wengine, na matokeo yake kuwa kunaswa katika maandamano, sio tu kwamba yanawaathiri wahusika bali hata ndugu na familia zinazowategemea.

Mara nyingi kundi hili limejikuta likiachwa solemba na hata kusota wakati walio wahamasisha kushiriki maandamano ama machafuko hayo wakiwa mbali ama wametangulia mbali, au wako nje kabisa na au hata kuwatoroka.

Tunajua si viongozi wote wa vyama vya siasa wanaofanya hivyo lakini, hao wengi au wachache ndio tunaowazungumzia katika kipengele hiki.

Tayari wengi wamesahaulika baada ya viongozi wao kujipatia umaarufu walioupata kupitia migongo yao walalahoi (wakereketwa, wafurukutwa na hata wenye majina mengine) ambao huenda azma yao (viongozi hao), ilikuwa kuitumia migongo ya walalahoi kama daraja la kuwavusha kisiasa.

Inapojitokeza hali kama hii, dola pia haina budi kuelewa kuwa kuna kundi la aina hii lisiloenda kwa nguvu zake pekee, bali kwa msukumo wa nje. Kundi hili lipo na linatakiwa kuelimishwa na kulindwa kisiasa, kiuchumi na hata kijamii ili kuliepusha na majanga.

Katika nyanja ya uchumi, ni mara nyingi tu, baadhi ya wanajamii wamekuwa wanajitokeza hasa waliopo madarakani au katika nafasi zinazowawezesha kuwarubuni vijana wawafanyie shughuli ili wajineemeshe.

Mara nyingi tu imetokea baadhi ya vijana kutumwa kwenda kuwaletea mabosi wao madawa ya kulevya kutoka sehemu yanakouzwa ambapo wanaolitakia mema kundi hili hawakujui, na hata siku moja haijatokea au kusikika wanaowatuma kukumbwa na mikasa inayowakuta vijana wao.

Ingekuwa bidhaa hiyo haramu inasafirishwa kwa mikoba iliyozoleka au mifuko ya kawaida, ingekuwa ni afadhali kuliko kutumia matumbo yao kama mikoba ya kubebea dawa kwani hali hii, ni hatari mno, kiutu na kiafya.

Kwa tamaa za kujitajirisha ambazo vijana wengi wamezifanya kuwa ni daraja la utajirisho wa tabaka wanalotumikia, ni wazi hakuna anayejali kama afya zao zitadhurika hali na hali hiyo, ni sawa na kuchezea shilingi katika tundu la choo.

Hali inatisha hasa inapoonekana kuwa wabwia unga wengi wapo katika kundi hili. Hii inatokana na kuwatumia vibaya na hivyo, kuibuka kwa kundi la matajiri ambao hata siku moja, hawatasikika kuhusika na biashara hiyo haramu.

Matokeo ya mambo haya ni jamii kukumbwa na tatizo la kuwa na mazezeta ambao kuzinduka kwao ni kugumu. Licha ya kuhusishwa kwao katika biashara hizi haramu na kuathirika, hujikuta wakikumbana na rungu la dola na kuishia kwenye mahabusu na magereza.

Mihadarati imekuwa kichocheo katika kuwepo machangudoa na hivyo, kushamiri kwa biashara ya uuzaji wa miili. Hali hii ni ya kusikitisha kwani matatizo yote yako sambamba na gonjwa la UKIMWI.

Inaposemekana kuwa yapo madanguro yanayoendesha biashara ya ufuska katika baadhi ya miji, inategemewa ni nani awe ni mmiliki wake kama sio watu wanaoeleweka na wanye nafasi nzuri katika nyanja mbalimbali.

Ni katika madanguro hayo kunakofanyika mipango ya vitendo vya kihalifu ukiwamo uporaji wa mali za watu na kuikosesha amani jamii.

Kundi hili la wanajamii likitumika vizuri linaweza likaleta mabadiliko katika jamii. Kwa mujibu wa wanafalsafa kama Nkrumah, sio katika matumizi mabaya ya kufanikisha azma za wakubwa, bali ni kwa kuwaweka katika hali itakayojenga jamii na kuboresha hali zao.

Vimekuwepo vikundi mbalimbali vinavyotoa ushauri kwa baadhi ya vijana wanaoangukia kundi hili vikitoa ushauri nasaha.

Vikundi vingine vimekuwa vikisaidia watoto wa mitaani na kuunda vikundi vidogo vinavyowawezesha kujitegemea lakini, juhudi hizi zinaonekana kama ni za mtu mmoja tu.

Kwa hali yoyote ile, wapo wanajamii wanaolichukulia kundi hili kama sio sehemu yake na wala halistahili kutumika katika kutenda mema bali, kutumika kutenda yale yaliyo maovu kwa manufaa ya kundi jingine linalojiona na kujihesabu kuwa ni bora zaidi.

Katika mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayotokea katika jamii si budi wale wanaolitakia mema kundi hili, waliepushe na balaa kwani, wakati kundi moja linafaidi na linaneemeka, kundi hili lisipoepushwa kutumika vibaya linaweza kuleta mabadiliko yasiyo na mwelekeo mzuri.

Kwa kudhihirisha umuhimu wa kundi hili katika jamii, upo usemi kuwa mpiga viatu rangi anaweza siku moja akamshika mkono rais na akasabahiana naye.

Usemi huu unamaanisha kuwa, kundi la walalahoi lina nafasi na haki ya kutambulika na kuthaminiwa na siyo kutumika vibaya na hivyo kuinusuru jamii na maafa.

Lijue Shirika la Masista Wabenediktini Wamisionari wa Tutzing (3)

Katika toleo lililopita tuliona kuwa, baadhi ya masista wa Shirika la Wabenediktini Wamisionari walihamia St. Ottilia kutoka huko Reichenback. Hapo, palitarajiwa kuwa makao ya mapadre, mabruda na masista wa Shirika la Mtakatifu Benedict.

WANAHAMIA TUTZING:

Masista na mabruda walihamia pole pole huko St. Ottilia. Mpaka Mwezi Juni, mwaka 1887, sehemu kubwa ya masista na mabruda walikuwa wamehamia St. Ottilia. Huko, kulikuwa na nyumba kwa ajili ya watawa wa kiume na wa kike.

Wakiwa huko, masista walivaa nguo za kitawa hadharani. Hata hivyo, mbele ya serikali, iliwapasa kujitambulisha kama umoja (Association) na wala si jumuiya ya masista (religious community).

Namba ya masista iliongezeka. Padre Amrhein alipopeleka ripoti Roma, Aprili 20, 1887, alieleza kwamba jumuiya ya masista inaongezeka. Mpaka wakati huo, palikuwa na masista 24.

Mwezi Juni, 1887, masista wanne walikwenda Starnberg. Huko, walikusudia kuanzisha nyumba ya masista na chekechea. Eneo walilokusudia kujenga majengo hayo, lilikuwa limetolewa na akinamama watatu, Marie, Emilie na Bettina Rengseis.

Eneo hilo lilijulikana Tutzing. Hapa, palionekana kuwa mahali pa kufaa zaidi kwa masista kuliki huko St. Ottilia.

MATAYARISHO YA KUTUMA WAMISIONARI TANGANYIKA

Wakati Padre Amrhein anajishughulisha kuunda mashirika mawili ya kitawa (wanaume na wanawake), jambo lingine lilijitokeza. Hilo lilikuwa kwamba, lilitakiwa shirika moja la dini la Kikatoliki toka Ujerumani, lifike kueneza dini Tanganyika ambayo ilikuwa tayari koloni la Ujerumani.

Wajerumani waliitawala Tanganyika kwa kupitia kampuni ya kibiashara iliyokuwa ikijetegemea, yaani DOAG ambayo iliongozwa na Karl Peters.

Baada ya serikali ya Ujerumani kutangaza Tanganyika kuwa koloni lake, nchi hii iliendeshwa kwanza na maofisa wa DOAG.

Maofisa hao wa DOAG yaani akina Karl Peters, ndio waliowaalika mashirika ya dini kuja Tanganyika kueneza dini ya Kikristo.

HALI ILIVYOKUWA HAPA TANGANYIKA

Kabla ya Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilia kuja nchini Tanganyika, kulikuwa na makundi yafuatayo: Waarabu ambao walikuwa tangu karne ya kumi. Pia, walikuwa Wajerumani walioshughulika na biashara, yaani wanachama wa DOAG wakiongozwa na Karl Peters, na baadaye, wakoloni wenyewe walitumwa na serikali ya Ujerumani kuitawala Tanganyika.

Wafaransa pia walikuwa karibu na maeneo ya Tanganyika. Walipofika, Wajerumani wakawanyang’anya Waarabu ardhi na kumwachia Sultani wa Zanzibar, kisehemu cha umbali wa kilometa 16 tu, huko Bara ya Tanganyika.

Wajerumani waliwaogopa Wafaransa na ili kuondoa athari ya Kifaransa; ilibidi Wafaransa wachukue Visiwa vya Comoro kwa muda wa miaka mitano, na Wajerumani wapewe Tanganyika. Kwa kufanya hivyo, kukawa na uhuru katika kukaa kwao Tanganyika.

Athari ya Wafaransa ambao Wajerumani waliiogopa katika uwanja wa siasa, ilikuwepo pia katika uwanja wa dini, na hivi, Wajerumani wakatafuta kila njia sasa kuzitupilia mbali athari hizo.

Walishafaulu kuondoa athari ya Wafaransa katika uwanja wa siasa kwa kuwaweka Wafaransa mbali kidogo na Tanganyika huko Comoro. Sasa, ilibaki kuondoa athari katika uwanja wa dini kwa kuwaweka mbali wamisionari wa Kifaransa.

Nchini Tanganyika wakati huo, kulikuwa na mashirika ya dini ya wamisionari wa Afrika (White Fathers) na Wamisionari wa Roho Mtakatifu(Holy Ghost Fathers) , yakieneza Ukristo hasa sehemu za Kaskazini mwa Tanganyika. Wengi wa mapadre hao, walikuwa au Wafaransa au Wabelgiji.

Baada ya kuonywa juu ya athari za Wafaransa nchini Tanganyika, viongozi wa DOAG walifanya kila waliloweza kutafuta shirika la Kikristo la Kijerumani kuja kueneza dini Tanganyika. Mwaka 1887, Karl Peters alifanya mkataba na shirika la Kilutheri ili liende kueneza dini ya Kikristo Tanganyika.

Mtu mmoja aliyekuwa mwenzi wa karibu wa Karl Peters, kwa jina Freiherr Von Gravenruth aliyekuwa Mkatoliki mkereketwa, hakufurahi kuona Karl Peters akitafuta shirika la Kilutheri kwenda Tanganyika.

Von Graverenth aliona kwamba mapato ya mkataba huo ni kufutwa kabisa kwa Wakatoliki katika koloni la Tanganyika. Von Gravenruth akaamua kwenda Munich kuonana na Askofu Mkuu Anton Von Steichele, mwezi Machi 1887.

Kisha, alikwenda kumwona Askofu wa Jimbo la Augsburg Pankratius Von Dinkel ili azungumze nao juu ya hatari hii ya kuwekwa pembeni Wakatoliki huko Tanganyika. Jambo ambalo Von Gravenruth alizungumza na maaskofu hao, ni; kupata shirika la Kijerumani ambalo ni la Kikatoliki litakalokwenda Tanganyika kueneza dini ya Kikristo.

Katika mahangaiko hayo, Mkristo mkereketwa huyo, alisikia juu ya shirika changa la Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilia, lililokuwa likiwaandaa mapade, mabruda na masista kwenda nchi za misioni.

Itaendelea