Make your own free website on Tripod.com

Kardinali Pengo ahofia kurudi kwa Ukomunisti

lAfurahia Rais Bush kumjua Mungu

lAeleza historia ya machafuko duniani

l'Mpiganaji hatetei ngao, bali hujitetea mwenyewe’

lUgaidi una Ubepari kama baba na dini kama mama

Na Waandishi Wetu

Na Waandishi Wetu

"MWENYEZI Mungu asipotiwa maanani na kupatiwa nafasi ya kwanza, ipo hatari ya kumalizikia katika mapambano dhidi ya imani ya kidini, hasa Uislamu na dhidi ya mataifa ya Kiarabu... Hii itakuwa imeirudisha dunia katika enzi za Unazi na Ukomunisti."

Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, wakati akihubiri katika Misa ya Kuombea Amani kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea katika miji ya Washington na New-York nchini Marekani Septemba 11, mwaka huu.

Katika ibada hiyo iliyofanyika Jumatatu iliyopita katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu jijini Dar-es-Salaam, na kuhudhuriwa pia na Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Method Kilaini, Kardinali Pengo alisema pia kuwa, amefurahishwa na wito wa Rais George W. Bush wa Marekani, juu ya Siku ya Sala, Septemba 13, mwaka huu.

"...Ni dalili ya kuonekana kwamba Taifa la Marekani limeamua kumweka Mwenyezi Mungu katika shughuli zake za kutafuta ufumbuzi wa mkasa wa ugaidi katika ulimwengu...

Ni dua na sala yangu kwamba dalili hiyo isiwe jambo la kupita. Liwe jambo la kuzingatiwa na wote kwa muda wote wa jitihada za kupambana dhidi ya ugaidi ulimwenguni," alisema.

Katika ibada hiyo ambayo Kardinali Pengo alitoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema duniani kujiuliza endapo mapambano dhidi ya ugaidi na uhalif wote duniani, yanamshirikisha Mungu. "...Lakini je, mapambano ya sasa dhidi ya ugaidi yatatuzalia kitu gani?" alihoji.

Akaongeza, "Tusipojiuliza hayo kwa makini mbele ya Mwenyezi Mungu, tusishangae kwamba hata hatua za sasa zinazokusudiwa kuchukuliwa na Marekani kwa ushirikiano na mataifa mengine dhidi ya ugaidi, zikatuingiza katika hali mbaya yenye maafa makubwa zaidi."

Akielezea historia ya machafuko na vitendo vya kigaidi vilivyoanza katika karne ya 20, Kardinali Pengo alisema kuwa, katika Karne ya 20, kulizuka mifumo ya Kifashisti na Kinazi ambayo ilikuwa wazi wazi ya kibaguzi na kikandamizaji. Alisema Viongozi wa mifumo hiyo walipoona inawezekana kuwafaidia, walijaribu kumkokota Mungu aingie katika mifumo yao.

"...Ingawaje ilikuwa dhahiri kwa watu wote wenye kumheshimu Mungu kwamba, Mungu hawezi katu kukubaliana na mifumo ya kinyama namna ile. Mungu aliyejaribiwa kuingizwa katika mifumo hiyo, alikuwa alikuwa hasa Mwenyezi Mungu kama anavyofundishwa na dini na madhehebu ya Kikristo," alisema.

Akaendelea, "Na wapo waamini wengi waliodanganyika na huyo Mungu wa Ufashisti wa Unazi."

"Kupambana na Ufashisti na Unazi, ulizuka Ukomunisti kwa upande mmoja, Ubepari upande mwingine. Kwa pamoja, mifumo hiyo miwili mipya iliangusha ile ya awali. Mara baada ya kufamikisha lengo lao, mifumo hii mipya ikagawanyika kati yao, kila mmoja ukiwania ubabe pekee.

Hivi, kukazuka mapambano makubwa kati ya Ukomunisti na Ubepari. Ukomunisti uliamua kupambana waziwazi kwa silaha ya kumkana Mwenyezi Mungu na yanayokwenda pamoja na imani katika Mungu kama vile dini na madhehebu," alisema.

Kardinali Pengo akaendelea, "Kwa upande wake, Ubepari ulichukua dini na imani juu ya Mungu iwe ni ngao yake katika kupambana na Ukomunisti. Na kama ilivyo kawaida ya kutumia ngao katika mapambano, mpiganaji hatetei ngao, bali anaitumia ngao kujitetea mwenyewe binafsi.

Kama baada ya kushinda mapambano ngao itakuwa imesalimika au imeharibika, hilo si la muhimu sana kwa mpambanaji.

Kwa hiyo, tunaweza kuelewa vizuri sana hali ya nchi za Kibepari baada ya kuanguka kwa Ukomunisti. Kwao ngao ya Mungu na dini haina maana tena. Ni ya kutupwa tu, au sana sana kulindwa katika nyumba za makumbusho."

Akaendelea, "Kadiri ya kuelewa kwa watu wengi, ugaidi wa sasa ulimwenguni umezalishwa na kukuzwa na Ubepari katika mbinu zake za kupambana na Ukomunisti. Ndiyo kusema ugaidi huo una Ubepari kama baba na imani za kidini kama mama.

Askofu Mkuu huyo alitahadharisha kuwa, endapo jamii haitampa Mungu nafasi katika jitihada hizo, ipo hatari ya kumalizikia katika mapambano dhidi ya amani ya kidini, hasa Uislamu na dhidi ya mataifa ya Kiarabu.

Hata hivyo, aliyaelezea mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Marekani kama tunda lililoulazimisha ulimwengu kulichuma kutokana na mwelekeo wa kujijengea jina na utukufu duniani.

"Maafa ya Marekani ni tunda ambalo ulimwengu wetu umelazimika kulichuma kutokana na mwelekeo wa ulimwengu kujaribu kujijengea jina, utukufu, na maendeleo aidha kwa kumpuuuza kabisa Mwenyezi Mungu kiasi cha kuwania hata kumwondoa kutoka katika jumuiya ya watu, ama kwa kutomtia huyo Mwenyezi maanani katika mipango ya ulimwengu," alisema.

Aliwataka walioathirika na uvamizi huo wa kigaidi nchini Marekani, kuwa na subira na ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na Mungu awapokee mahali pema waliokufa katika shambulio hilo.

Alisema, kitendo cha wanadamu kujaribu kumfukuza Mungu katika jumuiya yao, ndicho kinapelekea baadhi ya watu katika jamii kuhitimisha mambo yao kwa vitendo vya ugaidi na maafa kama yaliyotokea Marekani.

Kardinali Pengo alisema kuwa, tafsiri kwamba maafa ya kigaidi nchini Marekani ni adhabu ya Mungu dhidi ya nchi hiyo, kama ilivyotolewa na kikundi cha baadhi ya Waislamu katika mji wa Jos, nchini Nigeria, ni tafsiri ya kipumbavu.

"... Ni tafsiri ya ya magaidi wanaolitumia jina la Mungu kama kichaka cha uovu na upumbavu wao," alisema na kuongeza kuwa, matokeo ya tafsiri za kijinga namna hiyo, daima huwa ni maafa juu ya maafa.

Katika Misa hiyo iliyohudhuriwa pia na Mwakilishi wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Michael Heath, Kardinali Pengo aliongoza zoezi la kuwasha mishumaa kama ishara ya mwanga na upendo wa Kimungu.

Mashambulizi ya Septemba 11, nchini Marekani, yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa, pamoja na uharibifu wa mali.

Marekani imeahidi kulipiza kisasi kwa wahusika pamoja na nchi zinazowahifadhi jambo linaloitishia dunia kukumbwa na vita kubwa huku ikiapa kumsaka hadi kumpata ama amekufa ama yu hai, gaidi wa kimataifa ambaye ni mshukiwa wa kwanza wa shambulio hilo, Osama Bin Laden.

...Wanaomwasi Mungu ni sawa na magaidi - Kanisa Katoliki

lDini zisitumike kama vichaka vya maovu

Na Eric Samba

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewafananisha Wakristo waliomsahau Mungu, sawa na magaidi wanaosababisha balaa na maafa duniani.

Kardinali Pengo, aliyasema hayo Jumapili iliyopita katika mahubiri yake wakati wa Misa ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 230 wa Parokia ya Mwananyamala, jimboni humo.

Aliwaambia waliopata sakramenti hiyo kuwa,endapo watageuka na kukiuka mafundisho ya kanisa na umuhimu wa sakramenti waliyoipokea, hawatakuwa na tofauti na magaidi wasiojali kuua hata kama wanawaua ndugu zao.

"Siku mkimwacha Mungu na kumweka pembeni, mtakuwa magaidi wakubwa wasiojali kama wanaua mama, baba au ndugu," alisema.

Aliwataka waliopokea sakramenti hiyo ya Kipaimara, kuwa chachu na chimbuko la mafanikio katika jamii, Kanisa, Taifa na ulimwengu mzima.

"Ulimwengu mnapopatia Kipaimara, ni wa watu ambao hawajui wasimame wapi, jukumu lenu ni kuhakikisha kila mnalofanya mnaongozwa na Roho Mtakatifu ili kuleta mabadiliko mazuri ndani ya jamii," alisema Kardinali Pengo.

Kuhusu vitendo vya ugaidi vinavyoitikisa dunia hivi sasa hususan mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Marekani hivi karibuni, Mwadhama Pengo alisema kuwa ni matokeo ya kosa la Mataifa ya Magharibi wakati yalipopambana na Ukomunisti ambapo walimsahau Mungu na kumuweka pembeni.

"Ugaidi una kiini katika mapambano yaliyoongozwa na Marekani kupinga Ukomunisti... Na mimi naamini walifanya kosa moja kubwa sana nalo ni kumweka Mungu pembeni, ndiyo maana baada ya Ukomunisti ukazaliwa ugaidi," alisema.

Alisema wapo magaidi wanaodai kufanya vitendo kwa sababu za kidini na kutafuta haki, lakini akasisitiza kuwa, huo ni uongo na kwamba wanatumia dini kama kichaka, kwani hakuna dini inayomweka Mungu katika kufanya ugaidi.

"Haiwezekani! Huyo ni Ibilisi. Ibilisi ndiye huongoza watu wanaotafuta ubinafsi na hufanya maovu," alisema.

Alisema maafa yaliyotokea huko New York na Washington kuwa ni msiba wa wanadamu na si wa Marekani pekee bali wa mataifa yote.

Alisema miji hiyo kwa kawaida hutembelewa na watu toka pande mbalimbali za dunia.

Aliyaonya mataifa makubwa ikiwemo Marekani, kuwa makini wakati wanabuni mbinu za kupambana na ugaidi ili yasije yakafanya njia ya kuua iliyo mbaya zaidi.

Hata hivyo, pamoja na vitisho na ahadi za kulipiza kisasi zilizotolewa na Marekani; alifurahishwa na hatua ya Rais George W. Bush kutenga siku maalum kwa ajili ya sala na ibada, na akasema hiyo inaonesha jinsi walivyotambua nafasi ya Mungu katika maisha na ustawi wa mwanadamu.

HOFU YA KUZUKA VITA KUU

Wamoravian walia Chonde Chonde Marekani; Chonde!

lMungu anasema jua lisizame bado una hasira

lHakuna dini ya kweli inayofundisha kuua na kujeruhi

lMchungaji ataka watoto wapewe shule wasipotoshwe kiimani

lAhoji, ‘kama ulikimbia darasa, unataka madaraka ya nini?’

Na Eric Samba

MCHUNGAJI Salatieli Mwakamyanda wa Kanisa la Moravian Tanzania, amewasihi Wamarekani kwa udi na uvumba, wasiige upumbavu wa magaidi kwa kulipiza kisasi kwa jazba kwani hali hiyo, itasababisha damu ya wasio na hatia kumwagika.

Mchungaji huyo wa Ushirika wa Keko, Wilaya ya Mashariki katika Jimbo la Kusini, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar-es-Salaam, katikati ya juma.

Alisema, Wamarekani hawana budi kuzingatia mafundisho ya Mungu yanayosisitiza kusameheana na kuyafanya yote chini ya uangalizi na pia, kujiweka mikononi mwa Mungu.

"...Hata Mungu anasema; Jua lisizame ukiwa bado una hasira maana kisasi ni juu yangu mimi. Naomba Wamarekani waangalie wasije wakafanya upumbavu kama wa hao wapumbavu (magaidi).

Wasipomweka Mungu mbele, damu ya watu wasio na hatia itamwagika ovyo. Ni vema wamtafute tu, mpaka wampate lakini wakichukulia jazba, wataweka watu kwenye mtego wa panya, unaoshika walimo hata wasio kuwamo," alisema.

Akifafanua juu ya athari za kulipiza kisasi kwa kutumia jazba, Mchungaji Mwakamyanda alisema, hali hiyo itapotosha amani zaidi duniani na hivyo, mambo mengi ya kiuchumi yataathirika vibaya.

Alisema, hali hiyo itawakwaza hata Wacha-Mungu, kiimani na sasa, wengine watajiingiza katika vitendo vya kishetani.

"Kukiwa na athari mbaya za kiuchumi, jamii pia itapoteza mwelekeo mzuri wa kiroho maana neema ikipungua, roho nayo itayumba,"

Alisema mapigano yatasababisha kukosekana kwa baadhi ya bidhaa na mahitaji muhimu na kwamba hali hiyo ni hatar kiroho kwani itawashawishi watu kujiunga katika vitendo vilivyo kinyume na mapenzi ya Mungu.

"... Hii ni hatari mno maana kama kitu ulizoea kukipata kwa urahisi halafu sasa kikakosekana, itabidi wengine wenye tamaa waanze kutumia njia ambazo ni kinyume na Mungu. Mfano mzuri ni kipindi kile cha wahujumu, kama Mungu angekuja wakati ule, sidhani kama kuna mtu angeokoka. Hali hii itaingiza watu katika dhambi na uhalifu mwingi," alisema.

Alitoa wito kwa waamini mbalimbali kukesha wakiomba kwa sala ili Mungu atumie uwezo wake kuwatuliza Wamarekani.

"Mungu atawafunulia na atawasaidia tu, wote tukazane na maombi ili Mungu awapunguze jazba," alisema.

Hata hivyo, Mchungaji Mwakamyanda alisema, maovu mengi duniani yakiwamo maandamano, vurugu na vitendo vya kigaidi, yanatokana na baadhi ya wanadini kupotoshwa kuwa vitendo hivyo, ni tiketi ya kwenda peponi.

Alisema Watanzania hawana budi kufumbuka macho na kujua kuwa, kwa Mungu hakuna peponi kwa ajili ya watu wanaofanya vurugu na mauaji duniani.

"Hakuna dini ya kweli inayofundisha kuua na kujeruhi. Tatizo ni kwamba dini nyingine zinajaza watoto imani bila kuwapa elimu ya kujua mambo kwa usahihi," alisema.

Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa, hali ya kuwapa watoto imani bila elimu, ndiyo inayosababisha baadhi ya dini kukosa viongozi wengi katika jamii.

Alisema hali hiyo huzua manung’uniko yasiyo ya msingi juu ya kutokuwapo uwiano wa idadi ya viongozi na dini.

"Kama ni madaraka yanahitaji elimu na uwezo wa kuongoza. Sasa kama ulikimbia darasani unataka upewe nini?" alihoji na kuongeza kuwa, hata katika dini na madhehebu hayo, wachache waliosoma, wako madarakani hadi sasa.

Aliwaasa Watanzania wasiige mikumbo ya kutumiwa na baadhi ya watu kwa kutumia mgongo wa dini kwa kuwa mara nyingi yanapotokea maafa, kujeruhiwa au kukamatwa, wakuu wa uchochezi huwa hawahusiki.

Waislamu, Wahindu, Wakristo, waungana na Serikali kuiombea Marekani

l Dk Shein ataka Nyerere aenziwe

Na Mwandihi Wetu

Serikali na viongozi mbalimbali wa dini wameitaka Marekani na nyingine duniani kutumia busara zaidi katika jitihada zake za kupambana na ugaidi duniani.

Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein na viongozi wa dini za kikristu, kiislamu na kihindu waliyasema hayo wakati wa ibada ya kukumbuka waliofariki kwenye mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani, iliyofanyika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake siku hiyo, Makamu wa Rais aliiomba serikali ya Marekani kutumia busara katika kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua wahusika wote walio nyuma ya kitendo hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

"Tunaiomba serikali ya Marekani itumie busara katika kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua zinazofaa wote waliohusika na kitendo hiki kiovu, kwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria," alisema Dk. Shein.

Alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Marekani ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa kikamilifu.

Aidha aliwataka watanzania kuendelea kuienzi kazi na urithi aliouacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefanikiwa kutokomeza ukabila, udini, ubaguzi wa rangi na uonevu wa aina zote, na kujenga nchi ya amani na utulivu.

Pia hakusita kuwaomba watanzania kujenga mshikamano na kuvumiliana ili kudumisha, kuimarisha na kuendeleza umoja, amani na utulivu. Hii itajenga mazingira mazuri ya kupambana na umaskini, UKIMWI na maovu mengine ili kuleta maendeleo.

Naye Muhashamu Methodius Kilaini, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), aliwataka watu wote kumtanguliza Mungu katika shughuli zao zote.

Aidha amewaombea viongozi wa dunia busara na hekima katika kupambana na ugaidi.

" Tunaombea serikali na watawala wa dunia nuru, hekima na busara katika kupambana na ugaidi ulimwenguni," alisema Askofu Kilaini katika sala yake.

Askofu John Mkola, kwa niaba ya Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCT), aliwaomba waathirika kuwasamehe waliowatendea uovu huo na na akawaomba vingozi kutumia busara kupambana na ugaidi.

"Tunaomba busara na hekima kwa viongozi itumike katika kupambana na ugaidi kuepuka kuleta mitafaruku zaidi duniani," alisema Askofu Mkola.

Kwa upande wake Sheikh Seleman Gologosi, kwa niaba ya jumuiya ya Wislam pamoja na kuombea amani, na walioathirika katika vitendo vya kigaidi huko Marekani hakusita kuitaka Marekani kutumia busara katika mapambano dhidi ya Ugaidi.

"Tunaomba hekima na busara kwa viongozi katika kupambana na ugaidi," alisema Sheikh Gologosi.

Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa, Jaji Mkuu, Barnabas Samata, Mawaziri, wabunge, mabalozi, viongozi wa dini, viongozi wa serikali na vyama vya siasa pamoja na wananchi wengine.

Hospitali za Kanisa Arusha zafadhiliwa magari

Na Festus Mwangwangi, Arusha

HOSPITALI za Endulen wilayani Ngorogoro na Mt. Elizabeth ya Arusha mjini(SEHA), zinazomilikiwa na Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, zimepata ufadhili wa magari mawili yenye thamani ya shilingi milioni 56.5.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, magari hayo yote ni ya aina ya Toyota Land Cruser.

Habari zinasema, gari kwa ajili ya Hospitali ya Endulen, limetoka katika familia ya Bw. na Bi. Fred Mannix, wa nchini Canada. Gari hilo limewekwa friji na "Radio Call". Lina thamani ya shilingi 32,565,000/= Gharama hiyo, ni pamoja na mshahara wa dereva, bima na mafuta ya gari, kwa mwaka mzima.

Msaada huo umepitia katika Kampuni ya Uwindaji ya Robin Hurt & Safari, ya mjini hapa.

Gari kwa ajili ya Hospitali ya Mt. Elizabeth, lenye thamani ya shilingi milioni 24m/=, ni ufadhili wa wanashirika wa "Lions Club International" ya Pforzheim, nchini Ujerumani.

Sambamba na ufadhili wa gari, Hospitali ya Endulen, pia imepata ufadhili wa fedha taslimu shilingi 2,633,679/= toka kwa Bw. Bethold Orschler wa Ujerumani.

Habari za kuaminika zinasema kuwa, pesa hizo zimetumika kununua magodoro 20 na majora matatu kwa ajili ya kushonea nguo za wagonjwa katika hospitali hiyo.

"Familia ya Bw. Mannix ambaye ni rafiki na mteja wa kampuni ya uwindaji ya Robin Hurt & Safari. imetoa gari hili ili kusaidia na kuboresha huduma za Afya ya Msingi ya jamii kwa vijiji vya mbali lakini vinavyohudumiwa na Hospitali ya Endulen" alisema mwakilishi wa familia hiyo ambayo ni Mkurugenzi wa ‘Cullman &Hurt Community Wildlife Project Bi. Sally Capper.

Naye mwakilishi wa Wanashirika wa Lions Club International ya Ujerumani, Bi. Adelheida Meyner, ameusisitizia uongozi wa SEHA kutunza ipasavyo gari hilo na kutaka litumike kwa ajili ya kurahisisha huduma za matibabu kwa wagonjwa wa macho hasa waishio mbali na mji wa Arusha.

Akitoa shukrani kwa niaba ya jimbo lake kwa nyakati tofauti baada ya kupokea funguo za magari, magodoro na majora hayo ya nguo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Josaphat Lebulu, aliwahakikishia wawakilishi wa wafadhili kuwa jimbo litahakikisha kuwa ufadhili utatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na wala si vinginevyo.

KOLPING -Tanzania yawa Mwenyekiti wa AKA

Na Pd. Marcell Mutakyamirwa, Bukoba

CHAMA cha Kitume cha Kanisa Katoliki kinachoshughulikia Maendeleo ya Mwanadamu Kimwili na Kiroho nchini (KOLPING-Tanzania), kimepokezwa jukumu la kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya za Kimataifa za KOLPING barani Afrika (AKA).

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, KOLPING- Tanzania ilipewa jukumu hilo na Mkutano Mkuu wa AKA (Africa Kolping Association), uliofanyika mjini Hoima nchini Uganda hivi karibuni.

Kabla ya nafasi hiyo kukabidhiwa Tanzania, KOLPING- Kenya, ndiyo iliyokuwa Mwenyekiti.

Makao Makuu ya Jumuiya ya Kimataifa ya KOLPING, yapo mjini Cologne, Ujerumani. Jumuiya za KOLPING zipo katika zaidi ya nchi 60 duniani.

Barani Afrika, zipo katika nchi za Kenya, Tanzania, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Togo, Benin, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Nchini Tanzania, KOLPING ipo katika majimbo ya Kikatoliki ya Bukoba, Rulenge, Kigoma, Tanga, Singida, Sumbawanga na majimbo Makuu ya Kikatoliki ya Mwanza na Dar-es-Salaam.

Jumuiya ya KOLPING nchini Tanzania, inajishughulisha na uboreshaji wa maisha ya Watanzania hususan wa maeneo ya vijijini katika nyanja za maendeleo ya jamii kiafya, kielimu, kilimo na ufugaji wa kisasi.

Kazi nyingine inayofanywa na KOLPING -Tanzania, ni usambazaji wa nishati itokanayo na mionzi ya jua, na utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana ili waweze kujiajiri.

Baada ya kumalizika kwa Mkutano huo, kulifanyika tamasha la kusherehekea miaka 10 tangu kuzaliwa kwa AKA. Katika tamasha hilo, burudani za nyimbo, ngoma na michezo mbalimbali zilioneshwa.

Kufanikiwa kwa tamasha hilo, ni ishara wazi kuwa Umoja wa Afrika unawezekana kuboreshwa na kuendelezwa zaidi.

‘Elimu ya maumbile kwa watoto ni balaa’

Na Jenifa Benedicto, DSJ

MWENYEKITI wa Shirika la Uchumi na Huduma za Jamii, Mabula Ernest, amesema elimu ya maumbile ya mwanadamu haipaswi kufundishwa kwa watoto wadogo kwani itawachochea watoto kufanya mazoezi katika vitendo vya ngono na hivyo, kuongeza balaa la UKIMWI na mimba zisizotakiwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar-Es-Salaam, katikati ya juma, Ernest aliilaumu pia tabia ya baadhi ya taasisi zinazojihusisha na elimu kwa watoto wadogo, kuwa na vitabu vyenye "mambo ya utu uzima". Alisema hali hiyo ni hatari kwani huwafanya hata watoto wenyewe kuvisoma vitabu hivyo kwa kujificha kwa kuwa wanajua kuwa wanasoma vitu ambavyo hawajafikia.

Alisema madai ya kwenda na wakati kwa kuwafundisha watoto elimu juu ya mambo ya ngono kabla ya umri, ni hatari kimwili, kiroho na kimaadili kwani ni kuwafanya watoto wajue na kutamani kushiriki mambo wanayofundishwa kwa vitendo kabla ya wakati muafaka.

"Kuwafundisha watoto elimu juu ya UKIMWI, haisadii kuutokomeza ugonjwa huo na pengine inachochea maana watoto wengine wana utundu wa kutaka kujaribu kila jambo wanalofundishwa ili waone uzuri na ubaya wake," alisema.

Alisema yapo mambo mengi muhimu ambayo watoto hawana budi kufundishwa katika umri wao kuliko kuwawahisha kufikia hatua hizo kubwa kabla umri wao haujaruhusu.

Makanisa bora yana wasomi wengi- Askofu Sendoro

Na Neema Dawson

ASKOFU Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Elinaza Sendoro, amesema makanisa na dini zilizokomaa kiimani, zina wasomi wengi na wanaojua wanachohubiri.

Askofu Mstaafu Sendoro aliyasema hayo, katika hafla ya kumpongeza Askofu wa Dayosisi hiyo, Jerry Mngwamba, kwa kufuzu masomo na kutunukiwa Shahada ya Juu ya Udaktari katika Neno la Mungu.

Kwa miaka mitano iliyopita, Askofu Mngwamba (sasa ni Dokta), alikuwa Chicago, nchini Marekani kwa masomo ya Teolojia.

Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na uongozi wa dayosisi hiyo na kufanyika katika Usharika wa Kariakoo jijini Dar-es-Salaam, Askofu Mstaafu Sendoro, alisema kuwa, kazi ya kuhubiri Neno la Mungu inahitaji mtu aliyesomea elimu hiyo kwa kiasi cha kutosha ili kuwaongoza wanadamu kuufikia Ufalme wa Mungu.

Alisema, kwa kawaida wahubiri wa Neno la Mungu wasio na elimu juu ya Maandiko Matakatifu, ndio hupotosha jamii katika mahubiri yao yaliyojaa hadithi na simulizi zisizo za kweli.

Hata hivyo, alisema makanisa yasiyo na wahubiri wasomi na ambayo kwa kawaida hutumia ishara na miujiza, hushawishi na kuvuta watu kujiunga nayo wakidhani kuwa matendo hayo ya ishara, ndio utakatifu wa Kimungu.

Alisema, wanaodanganyika na kuvutika kuyahama makanisa yao yaliyowalea, wanafanya kosa kwa kuwa wanapotea na kuangamia katika mashimo ya kimwili na kiroho kutokana na mafundisho batili wanayoyapata huko uhamishoni.

Akaongeza kuwa viongozi wa makanisa yanayoshawishi watu kuhamia kwao, kwa kawaida huwa na agenda binafsi ya kujineemesha na kuwafanya kama miradi yao ya uzalishaji mali na vitega uchumi.

Askofu Mstaafu huyo alisistiza kuwa, kabla muumini hajaamua kuhamia madhehebu yoyote, hana budi kufanya uchunguzi wa kina ili kujua mfumo mzima wa huduma za kiroho katika makanisa hayo.

Katika hafla hiyo, Askofu Mngwamba aliwashukuru wana dayosisi wake kwa kumuombea na hatimaye kufanikisha masomo yake.

Msihame makanisa kukwepa michango - Kauli

Na Neema Dawson

MWINJILISTI mmoja wa Huduma za Kiroho katika Maisha (Life Ministry), amesema tabia ya baadhi ya watu kukimbia na kuyahama makanisa yao ili kukwepa kuchangia ujenzi, ni udhaifu katika imani na kwamba, haina budi kuepukwa.

Mwinjilisti huyo, Bibi Ruth Mdoe, aliyasema hayo wakati akizungumza katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kawe, jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.

Alikuwa akihamasisha uchangiaji wa hali na mali, ili kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo la Kawe unaogharimu shilingi milioni 200.

Alisema ni vema kila mmoja akazingatia kuwa, kanisa si mali ya mchungaji, askofu wala padre, bali ni mali ya waamini wote. Akasisitiza kila mmoja kujua kuwa, ni wajibu wake kuchangia ili kuliimarisha na kuliendeleza Kanisa.

"Makanisa si mali ya wachungaji. Wanapohama kwenda sehemu nyingine, huwa hawahami nayo bali wanayaacha hapo hapo," alisema.

Alisema anasikitishwa na tabia ya baadhi ya waamini kukimbia makanisa yao yanapokuwa na miradi inayo hitaji nguvu zao za hali na mali.

"Inasikitisha kuwa Wakristo wengine pesa wanazo lakini, wanaposikia kuna uchangiaji, wanahama na kukimbilia katika makanisa yaliyojengwa kwa mahema. Tabia hii si nzuri kwa Mkristo safi," alisema.

Aidha, aliilaumu tabia ya baadhi ya waamini kukataa kujituma na kumtumikia Mungu huku wakikwepa kuchangia kufanikisha kazi ya Mungu kwa madai kuwa, michango hiyo ni kwa ajili ya manufaa ya wachungaji au walezi wengine wa kiroho katika maeneo husika.

Alisema Mkristo mwenye imani thabiti ya Kimungu, hapaswi kuwa na mawazo duni ya namna hiyo. Aliongeza kuwa, ujenzi ujenzi na maendeleo ya kanisa, hutegemea wanakanisa wenyewe.

Wakati huohuo: Mwinjilisti huyo amesema kuwa, baadhi ya watu wamekuwa wakifunga kwa ajili ya maombi mbalimbali ili Mungu awasaidie lakini, wanapofanikiwa kumudu maisha, humwasi Mungu na kumweka kando.

"... hao inapotokea tena wakapata misukosuko, na kuanguka, huanguka kabisa na wakakosa msaada. Na hapo huonekana tena wanaanza kuja kanisani na kufanya maombi. Hivyo si vizuri, lazima udumu na Mungu siku zote," alisema.

Mwinjilisti huyo alisema kuwa, mtu anayemtumaini na kumtumikia Mungu kwa uaminifu katika maisha yake yote, kamwe Mungu hawezi kumwacha aanguke bali huendelea kuwa naye daima.

Aidha, alisema kuwa, baadhi ya watu wenye vyeo na nyadhifa mbalimbali katika jamii, hufanya makosa kwa kutumia nafasi zao kwa manufaa yao na familia zao badala ya kuzitumia kama njia ya kutimiza utukufu na mapenzi ya Mungu.

Parokia ya Mwananyamala yazindua shule ya kompyuta

l Wajipatia gari kwa jasho lao

Na Maryam Salums DSJ

KITUO cha mafunzo ya kompyuta kinachoendeshwa na Parokia ya Mwananyamala katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-salaam (St. Martin's Computer Training Centre), kimefunguliwa rasmi sambamba na kubariki gari laosambamba na kubariki gari lililotolewa na waamini.

Ufunguzi wa kituo hicho ulifanyika Jumapili iliyopita parokiani hapo ambapo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alikuwa mgeni rasmi na alibariki gari la parokia hiyo aina ya Toyota Hilux (double cabin) lenye thamani ya shilingi milioni 8, lililopatikana kwa nguvu na michango ya waamini wa parokia hiyo.

Akisoma risala wakati wa ufunguzi, Mkurugenzi wa Mfuko wa Udhamini wa shule hiyo, Bw. Gabriel Mwakalinga, alisema hivi sasa jamii haina budi kuelekeza nguvu zake katika kujipatia mafunzo ya kompyuta ili kwenda na wakati.

"Mtu asiyejua kutumia kompyuta katika Karne ya 21, ni sawa na asiyejua kusoma na kuandika," alisema.

Alifafanua kuwa, katika mfumo wa sasa wa mabadiliko ya sayansi na teknolojia ulimwenguni kiuchumi na kiutendaji, kompyuta ni zana ambayo kila mmoja hana budi kufahamu kuitumia kwani ni nyenzo muhimu kwa matumizi na mazingira ya wakati huu.

Alisema, kutokana na umuhimu wa matumizi yake, kila mmoja awe kijana, mzee au mtoto, hana budi kujifunza somo la Kompyuta ili aende sambamba na mabadiliko katika maendeleo ya dunia.

Katika risala yake, alisema ili kufikisha ujuzi huo kwa watu wengi, kituo chake kimeanzisha kampeni mbalimbali zinazowalenga wahusika kunufaika na masomo yake.

Alizitaja kuwa ni pamoja na iitwayo, "Millenium Operation MULIKA-1", inayolenga kutoa mafunzo kwa wakulima, wafanyabishara na wafanyakazi mbalimbali.

Nyingine ni "Millenium Operation MULIKA-2", inayokusudia kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo.

Bw. Mwakalinga alisema kampeni nyingine ni ile iitwayo, "Millenium Operation MULIKA-3", inayolenga kutoa elimu ya kompyuta kwa viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, madiwani na wajumbe wa nyumba kumi kumi.

Lengo la mafunzo hayo yanayokusudiwa kutolewa pia katika seminari za Kanisa Katoliki nchini ni kumuandaa mhitimu wa sekondari na chuo, kukabiliana na mazingira ya sasa ya utandawazi.

Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Paroko wa Parokia ya Mwananyamala, Padre Priscus Jumamosi,

Hofu ya kupanda kwa Petroli yatanda Dar

Na Peter Dominic

WAKATI mashambulizi ya kigaidi katika Kituo cha Biashara ya Kimataifa, nchini Marekani yanatishia athari za kiuchumi kwa mataifa mengi duniani, jijini Dar-Es-Salaam, kumezuka hofu ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Baadhi ya madereva jijini Dar-es-Salaam, wameliambia gazeti hili kuwa, baada ya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Marekani Septemba 11, mwaka huu, tayari baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta vimekwisha pandisha bei hususan petroli na kwamba ipo hatari ya bei kupanda zaidi.

Walisema, badiliko la bei ya petroli limekuwa kati ya shilingi 550/= za awali, hadi shilingi 575/=. Hata hivyo, uchunguzi wa KIONGOZI umebaini kuwa, bei hiyo inatofautiana kutoka kituo kimoja hadi kingine.

Wameiomba Serikali kuwa makini kudhibiti mlipuko wa kupanda kwa bei kwa kisingizio cha shambulio la Marekani.

"Nafikiri bei hii inaweza kubadilika na kupanda zaidi wakati wowote iwapo Marekani itaanza kupigana vita. Tulikuwa hatununui kwa bei hiyo," alisema mmoja wa madereva wa daladala TZK 4263,inayofanya safari zake kati ya Mtoni-Mtongani na Kariakoo.

Hata hivyo, wasiwasi wa kupanda bei kwa baadhi ya bidhaa muhimu hususan mafuta, umewakumba wanajamii wengine. "Nimeshtuka, itabidi ninunue lita zangu 20 niweke ndani; vita haina macho bwana," alisema Mpiga picha mmoja anayefahamika kwa jina la Yuda Mhozya, akihofia kuadimika kwa bidhaa hiyo.

Katika kituo cha kuuzia mafuta cha GAPCO kilichopo Mtoni- Mtongani, hadi Alhamisi iliyopita, lita moja ya petroli ilikuwa inauzwa shilingi 570/=. KOBIL cha Sabasaba, katika Manispaa ya Temeke, lita moja ilikuwa 575/=.

TOTAL cha Kariakoo, kilikuwa kinauza shilingi 575/= kwa lita moja ya petroli wakati AGIP cha Msimbazi kiliuza kwa shilingi 515/=.

Padre ataka ushirikiano kusomesha watoto

Na Jenifa Benedicto DSJ.

PAROKO Msaidizi wa Parokia ya Chang’ombe, katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam, Padre Paul Njoka, amewataka Wanajumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, kuimarisha umoja baina yao wakati wote; iwe katika shida au raha.

Aliyasema hayo katika Siku ya Mavuno iliyofanyika Septemba 18, Mwaka huu, katika Kigango cha Don Bosco Kituo cha Kulelea Watoto, Kanda ya Veterinari.

Siku hiyo, watoto 37, walipata Sakramenti ya Ubatizo.

Padre Njoka alisema kuwa, kuimarisha umoja zaidi katika kujumuiya, kutasaidia wanajumuiya kushirikiana katika kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili kwani, kupitia Jumuiya hizo, Yesu hukutana na watu wenye shida mbalimbal.

Alitoa wito kwa wanajumuia zote, kujenga utamaduni wa kusaidiana katika mambo muhimu ya kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na kusaidiana kuwasomesha watoto wa wazazi na wajane wasio na uwezo wa kuwasomesha.

Fedha zilizopatika na katika Siku hiyo ya Mavuno katika Kanda ya Veterinari na Mikoroshini, ni shilingi 267,105.

Matabibu asilia, pelekeni dawa zenu zipimwe- Rai

Na Meryna Chillonji, DSJ

MWENYEKITI wa Chama cha Waganga wa Jadi nchini, Dk. Rwezaura V. Kigeli, ameilaumu tabia ya baadhi ta waganga na matabibu asilia, kutopeleka dawa zao kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi kubaini endapo zina madhara kwa wanadamu, au la.

Dk. Kigeli aliyasema hayo mwishoni mwa juma wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar-es-Salaam.

Alisema tabia ya kutopeleka dawa za waganga hao kuthibitishwa ubora wake na Mkemia Mkuu wa Serikali, ni hatari kwa kuwa zinaweza kutumika hata dawa zenye madhara kwa matumizi ya binadamu.

Aliongeza kuwa, kupeleka dawa kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi, pia kutasaidia kupatikana kwa matumizi mengine bora zaidi ya dawa hizo badala ya matumizi yaliyopo sasa.

Aidha, Dk. Kigeli alisema kuwa, tabia ya kuibuka kwa waganga na matabibu asilia kudai kuwa wanatibu ugonjwa wa UKIMWI, ni hatari kwani ugonjwa huo hadi sasa hauna kinga wala tiba.

Alitoa wito kwa waganga asilia wenye tabia ya kudai hivyo, waache kwani ni kuipotosha jamii na kujipatia pesa pasipo kuponya.

Alisema, kutokana na udanganyifu huo wa baadhi ya waganga na matabibu asilia; pamoja na kukosekana kwa dawa kamili ya kutibu UKIMWI, baadhi ya wagonjwa wamevutika kutumia dawa za asili.

Hata hivyo, Dk. Kigeli alisema kuwa, ushirikiano unaotolewa na Serikali kwa waganga hao katika kufanya tafiti mbalimbali juu ya dawa zao za asili, ni mdogo na akatoa wito kwa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, kuwasaidia waganga hao ili wapate vifaa vya kisasa vitakavyowasaidia kufanya kazi zao vema zaidi.

Alisema Serikali haiwapi nadharia wala mbinu za kundesha tafiti zao mbalimbali na kwamba, hali hiyo inasababisha waganga hao kukosa ufundi wa kuendeshea tafiti. Aliongeza kuwa, udhaifu huo ni hatari kwani utafiti wowote wa dawa ni muhimu ili kutoa vipimo sahihi kwa matengenezo na matumizi.

Hata hivyo, Dk. Kigeli alisema chama chao kinakabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwamo ya ukosefu wa pesa za kuendeshea tafiti, ukosefu wa eneo la kujengea kliniki ya kisasa.

Hivi sasa huduma zao zinatolewa katika nyumba ya kupanga.

Pia, chama kinakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya kisasa ikiwa ni pamoja na kompyuta kwa ajili ya utunzaji wa kumbukumbu.