Make your own free website on Tripod.com

Mauaji, ugaidi si dawa ya matatizo - Baba Mtakatifu

Mwandishi Wetu na Mashirika ya Habari

"HATA kama nguvu za giza zikionekana kushinda, wanaomwamini Mungu wanajua wazi kuwa uovu na mauaji si ufumbuzi wa matatizo".

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alisema hayo wakati akivilaumu vitendo vya mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika katika Kituo Kikuu cha Biashara Duniani cha mjini New-York na Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Marekani.

Katika mashambulizi hayo, maelfu ya watu wanahofiwa kupoteza maisha yao huku wengine wakiwa wamejuruhiwa vibaya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Catholic Information Network (CIN), Baba Mtakatifu alisema, kamwe vurugu na uovu, haviwezi kuwa njia mwafaka za kutatua matatizo ya watu.

Ameviita vitendo hivyo kuwa ni giza katika historia ya mwanadamu na ufedheheshaji wa kutisha wa heshima ya utu na maisha ya wanadamu.

Katika taarifa yake, Baba Mtakatifu alisema kuwa, Neno la Kristo ndilo njia pekee ya kutatua matatizo na kutoa majibu kwa maswali yanayoisumbua mioyo ya watu hata kama nguvu za giza zitajaribu kuvuruga.

Katika taarifa hiyo, Baba Mtakatifu amewaombea kwa Mungu, wote walioathirika na ugaidi huo wa kutisha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tayari Papa ametolea Sadaka ya Misa Takatifu kwa ajili ya waathirika wote na kuwaombea waliopoteza maisha, Mungu awaweke chini ya huruma yake na pumziko la amani.

"Mungu awape ujasiri wote waliounusurika. Awaimarishe wanaofanya shughuli za kuokoa na wanaojitolea ili kurejesha hali ya kawaida," ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa, anawahakikishia waathirika wote kuwa yupo pamoja nao kimwili na kiroho.

Amemtumia salamu za rambirambi, Rais wa Marekani, George W. Bush na wananchi wake hasa waliojeruhiwa na kupotelewa na wapendwa wao katika tukio hilo lisilofahamika.

Amewaomba watu wote wenye mapenzi mema, kuungana naye kuwakabidhi waathirika wote chini ya upendo wa milele wa Mungu. Hii ni pamoja na kuomba faraja kwa ajili ya familia, majeruhi na wote wanaofanya kila liwezekanalo kuwaokoa walionusurika na kutoa msaada kwa walioathirika.

Aidha, Baba Mtakatifu amewaombea Wamarekani Mungu awape nguvu na ujasiri vitu ambavyo wanavihitaji hasa katika wakati huu ngumu wa huzuni na majaribu.

Wakati huo huo: Shirika la Misaada la Kimataifa la Kanisa Katoliki (CARITAS), limeyataka matawi yake kote duniani, kulichukulia tukio hilo la kigaidi kuwa sio athari mbaya kwa Wamarekani pekee, bali kwa utu wa binadamu wote.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mawasiliano wa CARITAS Kimataifa, Lynn Yuill, Katibu Mkuu wa CARITAS Duniani, Duncan MacLaren, aliyekuwa katika Bara la Amerika Kaskazini wakati maafa hayo yakitokea nchini Marekani, alisema anawatumia salamu za pole na rambirambi wanafamilia wote waliopoteza ndugu zao na kujeruhiwa katika tukio hilo.

Amewataka wanachama na wafanyakazi wote wa CARITAS duniani, na wote wenye mapenzi mema duniani, kuwaombea waathirika katika sala zao.

Kwa sasa Katibu Mkuu huyo wa CARITAS yupo Baltimore, Maryland.

Nalo Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari vya Kanisa Katoliki (UCIP), limesema litatafuta njia za kumaliza machafuko yanayotokana na maendeleo katika utandawazi.

Kwa mujibu wa habari tulizozipata mwishoni mwa juma, Waandaaji na Washiriki wa Kongamano hilo duniani, wamesema Kongamano la UCIP litakuwa sehemu ya kutathmini kiroho na kisaikolojia, njia za kuwasaidia wanachama wake duniani hususan wahanga wa machafuko hayo.

Serikali ya Talaban imekanusha habari za kukamatwa kwa Osama Bin Laden, lakini ikasema iko tayari kumkabidhi Osama kwa Marekani endapo ushahidi wa kutosha, utatolewa kuwa yeye ndiye mhusika wa hujuma za Washington na New York.

Osama mwenyewe amekaririwa na gazeti moja nchini Pakistani akiwapongeza waliofanya mashambulizi dhidi ya Marekani na akamshukuru Mungu kwa hilo, huku akikiita kitendo hicho cha kinyama kuwa ni ushujaa.

Alisema hata kama yeye akiteketezwa, hujuma dhidi ya Marekani zitaendelezwa na wafuasi wake waliosambaa duniani.

Huko Marekani, Rais Geogre Bush ambaye tayari ametangaza vita dhidi ya magaidi na nchi zinazowahifadhi akiungwa mkono na NATO pamoja na nchi kubwa duniani, amekiitaa kitendo cha kushambulia nchi yake kuwa ni Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia katika Karne ya 21.

Jumanne iliyopita ndege nne ambazo inaaminika zilitekwa nyara na magaidi, ziligonga Kituo cha Biashara Duniani kilichopo mjini New York, na Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Marekani, mjini Washington na kusababisha mauaji ya watu wengi na uharibifu wa mali.

Hadi sasa hakuna taarifa rasmi zilizotolewa juu ya idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na shambulizi hilo.

Viongozi mbalimbali duniani akiwemo Rais Benjamini Mkapa wa Tanzania, wametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Marekani, George Bush na wananchi wa Marekani wakilaani vikali matukio hayo ya kinyama wakiwemo maadui wa Marekani.Gaidi la kimataifa, raia wa Saudi Arabia anayeishi uhamishoni nchini Afghanistan na wapinzani wa msimamo wa Marekani kuhusu Mashariki ya Kati, wanashukiwa kuhusika na uovu huo japo wamekana kuhusika.

Jumatano iliyopita nchini Newzealand, ilifanyika ibada ya kuwaombea walioathirika na mashambulizi hayo.

Kanisa Katoliki lina maadui wengi- Padre wa Uganda

l Asema pombe siyo dhambi isipokuwa...

Na Eric Samba

MADAI kuwa Kanisa Katoliki halina wokovu na kwamba linaabudu sanamu na kuwaheshimu Bikira Maria, Watakatifu na viongozi wengine zaidi ya Yesu, yanaonesha ukweli kuwa lina maadui wengi, linafanikiwa na sasa linaonewa wivu; amasema Padre Anthony Musala.

Padre Musala kutoka katika Jimbo Kuu Katoliki la Kampala, nchini Uganda, aliyasema hayo katika siku ya tatu ya semina juu ya uongofu, iliyofanyika katika ukumbi wa Parokia ya Mbagala-Misheni, katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Aliwataka Wakatoliki na Wakristo wa madhehebu yote wenye mapenzi mema, kuyapuuza madai hayo na badala yake, wazidishe imani yao katika Kristo, wakizingatia amani na upendo katika Bwana.

Alisema, anashangaa kuona Kanisa Katoliki linakuwa na maadui wengi wakiwamo ndugu na wafuasi wa Kristo.

Hata hivyo, alionesha wasiwasi kuwa, huenda madhehebu ya Kikristo yanayohubiri mashambulizi dhidi ya Wakatoliki, ni yenye mafundisho batili. Alisema, hayo yanatumia muda mwingi kuwashambulia Wakatoliki kama njia ya kuwarubuni na kuwavuta waamini kuingia madhehebu yao.

"Madai kuwa ndani ya Kanisa Katoliki hakuna wokovu, linaabudu sanamu, linamuabudu Bikira Maria, Watakatifu na viongozi wengine hata zaidi ya Yesu, si ya kweli na yanaonesha wivu na ukweli kwamba Kanisa Katoliki lina maadui wengi wakiwamo ndugu zake; Wakristo," alisema.

Aliongeza, "Haya makanisa pamoja na kwamba ni ndugu zetu, lakini inasikitisha kwamba baadhi ya mafundisho yao ni potofu," alisema

Hata hivyo alisema, licha ya kuwapo kwa fitina na uchochezi dhidi ya mafundisho sahihi ya Kanisa Katoliki kwa muda mrefu, anafurahi kwani bado Kanisa linaendelea kuimarika zaidi kwa kuwa watu wanauona na kuutambua ukweli. Alisema, hali hii inatokana na Kanisa hilo kuongozwa na Roho Mtakatifu.

Padre Musala, aliwataka waamini kupuuza dharau na kejeli dhidi ya Kanisa na badala yake, wazidishe juhudi katika kuijua na kuizingatia imani na hivyo, kujenga zaidi uhusiano wa kibinafsi baina yao na Mungu.

"Wakikwambia kuwa Kanisa Katoliki liko hivi au liko vile, usikilize tu, wakimaliza, waambie; Mungu awabariki. ...najua lengo lao kuu ni kukuvuta uingie kwenye kanisa lao," alisema.

Alisema, wakatoliki hawana budi kuyaamini yaliyoandikwa katika Maandiko Matakatifu (Biblia); pamoja na mapokeo sahihi yanayofundishwa na Kanisa badala ya kutumia muda wao kusikiliza porojo zisizo na msingi zitolewazo na watu wanaodhani wanajua kumbe hawajui.

Akizungumzia unywaji pombe, Padre Musala alisema kuwa, unywaji pombe unaweza kuwa mbaya endapo tu, utatumika vibaya. " kunywa pombe inaweza kuwa dhambi au isiwe dhambi..." alisema.

Alisema, kabla ya kuamua kunywa au kutokunywa pombe, inabidi kuangalia madhara yake kwa familia na jamii.

"Unakuta familia nyingine zinakosa mahitaji ya lazima kwa sababu baba au mama analewa au; alifukuzwa kazi baada ya kushindwa kufika kazini kwa ulevi. Hiyo ni dhambi," alisema.

Aliongeza, "Unakuta mtu aliyeoa anaenda baa kwa ajili ya kunywa na kutuliza akili, lakini baada ya kunywa, anaanza kumtamani mhudumu wa baa na hatimaye, anazini na kuvunja Agano la Ndoa. Hapo ndipo unywaji wa pombe unakuwa ni dhambi."

Hata hivyo, alisisitiza kuwa, kuacha kunywa hakuna cha kukosa bali kunaongeza faida kiafya, kisaikolojia na kiuchumi.

Askofu wa Pentekoste afichua siri ya makanisa ya nyumbani

l Asema mengi ni ya kitapeli, yanalihujumu taifa

Na Neema Dawson

ASKOFU Andrew Joel wa Kanisa la Pentekoste; Mungu Mmoja wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, amesema baadhi ya makanisa yanayoendeshwa katika nyumba za kuishi watu, yanaendesha hujuma katika nchi kwa kisingizio cha Neno la Mungu.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar-Es-salaam.

Alisema mfumuko mkubwa wa makanisa hapa nchini na hususan katika wilaya ya Same, umesababisha kuwapo mengine yanayosajiliwa bila maandalizi kamili ya kiroho na badala yake, yanatumika kama mwamvuli wa kuficha biashara haramu na hujuma za watu dhidi ya taifa.

Alisema, makanisa hayo ambayo mengi huendeshwa katika nyumba za watu, hufanya shughuli za kibiashara na mambo ya dunia kwa kushirikiana na watu wengine wa nje ya nchi ili kufanikisha biashsra yao kupitia mgongo wa jina la Kanisa.

"Sasa yanaanzishwa makanisa mengi ya kitapeli.

Inabidi Serikali iwe makini na ichunguze kwanza kabla ya kutoa kibali cha kuendesha Kanisa au NGOs yoyote.

Inasikitisha sana maana wanapoomba, wanajitahidi kuonesha kuwa wanafuata taratibu zote sahihi lakini wanapopewa, wanaamua kuwashirikisha hata watu wa nje ya nchi kuyafanya makanisa hayo kama kitega uchumi," alisema.

Alisema, akiwa mmoja wa viongozi wa kiroho katika jamii, anasikitishwa na wanaotumia majina ya "Kanisa" kuidanganya jamii pamoja na Mungu ili kuwapendeza watu wa nje ya nchi na kujineemesha wenyewe.

Alisema viongozi wa kiroho kwa ngazi zote, hawana budi kuwa mfano bora wa mawazo, maneno, imani na matendo yao ili jamii ijifunze toka kwao badala ya kuifanyia jamii hujuma.

Askofu huyo alizidi kulaumu kuwa, wapo wachungaji na viongozi wengine wa kiroho waliovaa ngozi ya kondoo kumbe ni mbwa mwitu ambao huwaombea vibali watu toka nje ya nchi ili waje kufundisha Neno la Mungu.

Akasema, watu hao wanapofika nchini, hushirikiana nao kufanya biashara badala ya kuhubiri Injili.

Alifafanua kuwa, watu hao mara nyingi huihujumu nchi kwa kufanya biashara ya kusafirisha nyara za Serikali, na madini mbalimbali hali inayoangamiza uchumi wa taifa kwa kulikosesha mapato.

"Makanisa yanayofanyia ibada nyumbani, inabidi yachunguzwe.

Iweje nyumba ya kuishi ibadilishwe na kufanywa kanisa?" alihoji na kuongeza kuwa, kwa kuwa Serikali hutoa viwanja kwa jamii kujenga makanisa yao, ni vema nafasi hiyo ikatumika vizuri badala ya kutumia nyumba za watu binafsi ambazo huachwa pindi malengo binafsi ya waanzilishi hao yanapokamilika.

Alitoa mfano wa Mchungaji mmoja wa Kanisa lake (hakumtaja) ambaye aligundulika kufanya biashara ya kitapeli kwa jamii.

Askofu Joeli alisema kuwa, baada ya kumuonya na kumtaka aachane na mtindo huo, Mchungaji huyo aliamua kujitenga na kuanzisha kanisa lake ambalo alikuwa akiliendeshea nyumbani.

Alitoa wito kwa viongozi wote wa kiroho kuwa mfano bora wa maadili katika jamii kwa kuwa jamii na Serikali inawatazamia kuwa mfano bora.

Lilian Foundation yataka walemavu watunzwe vema

Na Mwandihi Wetu

WAZAZI wametakiwa kutowabagua na kuwaona watoto wenye ulemavu kama mkosi badala yake, wawathamini na kuwapatia haki zote na mahitaji.

Ushauri huo ulitolewa kwa pamoja hivi karibuni wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Lilian Foundation, Bw. Geert Dollevoet na mmoja wa wafuatiliaji wa shirika hilo, Bi. Nel Van Manen, walipozungumza na gazeti hili jijini Dar-Es-salaam.

Akizungumza kwa nyakati tofauti juu ya hali ya wazazi kuwapuuza ha wengine kuwatelekeza watoto walemavu, Mratibu wa kitaifa wa shirika hilo nchini Bi. Betty Mwaluli, aliwataka wazazi wenye watoto wa namna hiyo kutowaficha nyumbani bali wawasaidie na wanaposhindwa, waombe jamii iwasaidie kuwalea kwa mapenzi ya Kimungu.

Alisema wazazi hao hawana budi kuuliza kama maimboni kwao kuna waratibun wa Lilian Foundation au walijulishe shirika la Misaada la kimataifa la Kanisa katoliki (CARITAS), kwa msaada.

Viongozi hao wa Lilian Foundation, walisisitiza kuwa, lengo la shirika hilo ni kuwahamasisha wazazi ili watambue na kutimiza wajibu wao wa kuwahudumia watoto wao wote bila ubaguzi wa rangi, jinsia wala maumbile (ulemavu).

Wakifafanua mintarafu urendaji wa shirika hilo, walisema kazi yake kubwa ni kupokea na kufanya tafiti za kuaini kama kweli wanaooma misaada katika shirika hilo, wanastahili.

"Kwa mfano hapa Tanzania, ninahakikisha maombi yote ya misaada kabla hayajaenda Uholanzi (makao makuu), wanahakikiwa na kuthibitishwa kuwa kweli," alisema Bibi Mwaluli.

Alisema kazi hiyo inahitaji upendo kwa watoto wote kwani ni ya kujitolea na haina ujira wowote. Aliongeza kuwa, waratibu wengi wa majimbo, ni lazima watoke kwenye mashirika ya kitawa au yasiyo ya kiserikali

Bw. Dollevoet alisema, "Tunasaidia watoto na vijana wenye ulemavu tangu umri mdogo hadi miaka 25 ili baadaye, washiriki katika maendeleo yao na ya jamii."

Hata hivyo, walisema shirika lao halitoi msaada mkubwa kwa mtoto bali wanasaidia kuchangia pale ambapo mzazi ameshindwa. Pia, walisema shirika hubeba jukumu zima la kumlea na kumsaidia mtoto mlemavu kama itathibitika wazi kuwa wazazi hawana uwezo kabisa.

Waliitaja misaada inayotolewa na Lilian Foundation kwa ni pamoja na kuwalipia watoto ada za shule, gharama za hospitali, vifaa kama baiskeli za walemavu, magongo na viatu maalumu kwa ajili ya walemavu.

Lilian Foundation hufanya kazi kupitia kwa waratibu wake waluiopo katika nchi mbalimbali ambao ni kiungo muhimu baina ya wafuatiliaji na makao makuu.

Kazi za waratibu wa kitaifa katika nchi zao ni kuandaa bajeti ya ofisi ya kitaifa, taarifa za fedha na kuandaa mikutano, semina na warsha mbalimbali kwa ajili ya waratibu wa majimbo.

Shirika la Lilian Foundation lilianzishwa mwaka 1980 huko Indonesia. Mwanzilishi wajke, Liliane, alipata ulemavu kutokana na ugonjwa wa polio. alianzisha ili kuwapatia elimu ya haki zao, walemavu.

Shirika hilo hadi sasa linafanya kazi katika nchi 12 zinazoendelea duniani. Lina wahisani wapatao 65,000, waratibu 500 na watoto 25,000 wanaosaidiwa na kunufaika na misaada yake.

Parokia ya Kawe yapongezwa kwa maendeleo

l Kardinali Pengo kuzindua nyumba ya mapadre

Na Neema Dawson

WAKATI waamini wa Parokia ya Kawe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, wamepongezwa kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba ya mapadre, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, anatarajiwa kufungua nyumba hiyo Oktoba 6, mwaka huu.

Paroko wa Parokia ya Kawe Padre Judas Shayo, alisema hivi karibuni kuwa nyumba hiyo iliyokwisha tumia shilingi milioni 80, imejengwa kwa nguvu za waamini wa parokia hiyo.

Akitoa pongezi kwa waamini wa parokia hiyo kwa moyo wao wa kujiletea maendeleo na kuifanya kwa moyo kazi ya Mungu, paroko huyo alisema kuwa, baadhi ya waamini walichangia vifaa vya ujenzi, pesa na wengine nguvu na ushauri wao ambao ulifanikisha ujenzi wa nyumba hiyo ya kisasa.

Aliongeza kwa kusema kuwa parokia ya Kawe ni miongoni mwa Parokia kubwa zilizo katika jimbo Kuu la Dar na ilikuwa haina nyumba ya mapadre ambayo imejengwa na parokia bali iliyokuwepo ambayo ni ndogo sana ilijengwa kwa ajili ya katekista wakati parokia hiyo ilipokuwa kigango cha mtakatifu Petro Oysterbay; na tangu ilipokuwa parokia ilikuwa haijajengwa nyumba na mapadre waliendelea kutumia nyumba hiyo ndogo ambayo ilikuwa siyo imara.

"Nawashukuru waamini walipokaa na kufikiria kujenga nyumba imara ya mapadre na kuanza ujenzi Januari 1997; tena kwa nguvu zao wenyewe bila kupata wafadhili kutoka nchi za nje," alisema.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika akiwapo Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya nyumba hiyo Bw. Lucas Chogo, alisema kuwa ushirikiano baina ya waamini wa parokia hiyo na Kanisa parokiani hapo, ndio uliofanikisha kukamilika kwa ujenzi huo.

Viongozi hao kwa pamoja waliwataka waamini hao kuendelea na moyo huo wa Kikristo ili kulitegemeza Kanisa lao.

Aidha, paroko huyo aliwataka waamini kujiandaa katika Siku ya Mavuno ambayo ni kwa ajili ya kumtolea Mungu shukrani kwa yote aliyowatendea wanadamu.

Nyumba hiyo ya mapadre wanne, ina jiko, stoo, chumba cha mapumziko, choo, bafu na ukumbi wa mikutano.

Viongozi mbalimbali wa Kanisa, wamekuwa wakihimiza jamii kutumia nguvu zao za hali na mali, katika kujiletea maendeleo yao binafsi, kanisa na taifa kwa jumla kuliko kukaa na kusubili kila kitu kusaidiwa na wafadhaili.

Moyo wa kujitolea kulitegemeza Kanisa mahalia, hauna bu di kuigwa na kuungwa mkono kivitendo, na waamini wa parokia na sehemu nyingine.

Kudai haki bila wajibu ni wazimu- Profesa

Na Meryna Chillonji, DSJ

"MTU mwenye kuua nafsi moja kwa kuinyima haki, ni sawa na aliyeua watu wote duniani na mtu aliyeihaisha nafsi moja kwa kuitendea haki, ni sawa na kuwahaisha watu wote ulimwenguni."

Mbunge wa Kibiti, Profesa Juma Mikidadi, aliyasema hayo wakati akizungumza katika semina ya siku moja ya wanawake iliyofanyika katika ukumbi wa Korea jijini Dar-Es-Salaam.

Semina hiyo iliandaliwa na Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilichopo jijini Dar-Es-Salaam chini ya Mkurugenzi wake, Bw. Mohamed Shakiba.

Mbunge huyo alisema, haki haina budi kuhimizwa katika jamii kwa kuwa kadiri inavyoongezeka katika jamii, ndivyo uwajibikaji pia unaopaswa kuongezeka.

Alisema, hakuna haki bila wajibu na kwamba, wajibu bila haki ni utumwa. "Kudai haki bila wajibu ni wehu," alisema.

Katika semina hiyo, Profesa Zubeda toka Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam, aliwataka wanawake kujijengea elimu na ari ya kujikomba kwani ukombozi wao, unategemea juhudi zao wenyewe.

Aliitaka jamii kuzingatia kuwa wanawake ni wanajamii walio sawa na watu wengine hivyo, wanahitaji kupewa haki zote wanazostahili binadamu, wajibu na majukumu katika jamii.

Alisema, wanawake hawana budi kujikwamua kiuchumi na kuendelezwa kielimu kwa kuwa ndio kiini cha jamii.

Profesa huyo alisema, kumuendeleza mwanamke mmoja ni sawa na kuielimisha jamii nzima. "... mwanamke mmoja akiharibikiwa, jamii nzima itakuwa imeharibikiwa," alisema.

Parokia ya Mwananyamala yaanzisha shule ya kompyuta

Na Eric Samba

PAROKIA ya Mt. Martin De Pores Mwanyamala, katika Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, imeanzisha shule ya kompyuta kwa ajili ya watu wote.

Paroko wa Parokia hiyo, Padre Priscus Jumamosi, alisema katika mazungumzo yake na gazeti ili wiki iliyopita kuwa, shule hiyo imeanzishwa kwa msaada wa shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia elimu ya kompyuta Tanzania (Computer Literacy for Secondary School Trust Fund).

Alisema, lengo la kuanzishwa shule hiyo ni kuwapa fursa waamini na wakazi wa eneo la Mwananyamala jijini Dar-Es-salaa, kwenda sambamba na mahitaji ya elimu ya sasa katika karne ya sayansi na teknolojia.

Lengo lingine ni kuwapatia nafasi ya kupata ujuzi wa kutumia kompyuta; na kuwapa ajira, wenye ufundi wa kutengeneza kompyuta kwa kujiajiri wenyewe kwa kushughulikia vifaa vya elektroniki.

Alilitaja lengo lingine kuwa ni pamoja na kuwapa nafasi wafanyakazi ili kuongeza ujuzi wao na hivyo, kuboresha utendaji kazi wao.

Padre Jumamosi alisema sababu kubwa ya kufanya hivyo, ni kuzingatia kuwa, kwa sasa teknolojia ya kompyuta ndiyo inayotumika sana katika ofisi mbalimbali.

Alitoa mwito kwa wananchi mbalimbali kujitokeza kwa wingi ili kujipatia elimu hiyo muhimu ambayo inatolewa kwa gharama nafuu.

Alisema shule hiyo inatarajiwa kufunguliwa rasmi na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, hivi karibuni.

Parokia ya Mwanyamala ni parokia ya kwanza katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, kuwa na shule ya namna hiyo ili kuonesha jinsi inavyojali na kuwajibika kujibu maswali yanayoibuka kutokana na usomaji alama za nyakati.

Inayo shule ya ufundi inayotoa elimu ya ushonaji , na shule ya awali kwa ajili ya watoto wadogo.

Catholic Publishers yawashukuru wafadhili

l Yatuma rambirambi kwa wafadhili waliofiwa masista

Na Josephs Sabinus

IDARA ya Habari na Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) inayolea kampuni ya Catholic Publishers LTD (CPL), wamiliki na waendeshaji wa gazeti la la KIONGOZI, imewashukuru Masista wa Shirika la Mtakatifu Petro Klaveri, kwa kusaidia kiufadhili kuendesha shughuli za gazeti hilo.

Katibu Mtendaji wa idara hiyo, Padre Raphael Kilumanga, amesema analishukuru shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Roma, kwa msaada wake wa hivi karibuni kuliwezesha gazeti la KIONGOZI kuboresha shughuli zake.

Katika mazungumzo ya hivi karibuni na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Padre Kilumanga alisema kuwa, kwa niaba Idara ya Habari na Mawasiliano, amefurahishwa na msaada huo uliotolewa kupitia Nyumba ya Masista wa St. Peter Claver ya Fribourg, Uswisi, na kuahidi kuutumia vema msaada huo kwa malengo yaliyousudiwa.Ametoa wito kwa wafadhili wengine popote walipo, kuiga mfano wa shirika hilo katika kuisaidia idara hiyo pamoja na gazeti la KIONGOZI linaloinjilisha kwa njia ya habari.

Wakati huo huo: Padre Kilumanga ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa CPL, ametuma salamu za rambirambi kwa Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa St. Peter Claver, kwa kufiwa masista watatu hivi karibuni.Amesema, Marehemu hao Marcella, Sista Virginia na Sista Rosaria, wameacha pengo kubwa katika shirika hilo na kwa wote wenye mapenzi mema duniani.

Hata hivyo, amesema kuwa, ili kutukuza utumishi bora wa marehemu hao katika kazi za Mungu, wote wenye mapenzi mema hawana budi kuiga mfano wa utumishi wao bora na kuwaombea ili Mwenyezi Mungu awapokee katika Ufalme wake.

Matibabu asilia waiomba Serikali iwafadhili

Na Maryam Salumu, DSJ

CHAMA cha Utafiti wa Magonjwa Sugu na Tiba Asilia, nchini Tanzania, kimeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya, kukifadhili ili kiwasomeshe wanachama wake katika vyuo mbalimbali vya uganga.

Washiriki wa Mkutano Maalumu wa chama hicho kitaifa uliofanyika juma lililopita katika Shule ya msingi Buguruni, jijini Dar-Es-Salaam, pia wameitaka Wizara ya Afya kuwasaidia kupata misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia upatikanaji wa nyenzo za kazi ili kuboresha shughuli zao.

Akisoma risala ya chama hicho katika mkutano huo maalumu, Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Shaka Mohamed, alisema, chama chake kinaiomba Serikali kukifadhili kimasomo ili wanachama wake watoe huduma bora zaidi na zinazokwenda na wakati.

Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo, Dk. David Wiketye, alisema kuwa, ipo haja kubwa ya wanachama wa chama hicho, kupata mafunzo ya kisasa kwa kuwa, baadhi ya madaktari bingwa kutoka hospitali mbalimbali nchini, wanaiba utaalam wao na kuutumia kwa njia ya kisasa.

"...Vitengo vya utafiti vya dawa asilia, vimekuwa vikipora fani yetu kwa kutuibia utaalamu na kuukuza zaidi," alisema.

Naye Dk. Kigeli Bashabi, katika mkutano huo aliiomba Serikali kuona uwezekano wa kufungua chuo rasmi kwa ajili ya tiba asilia ili kuwapa wanachama uwezekano wa kujiendeleza kitaaluma ikiwa ni pamoja na kushirikiana na kubadilishana utaalamu na madaktari bingwa.

Chama cha Utafiti wa Magonjwa Sugu na Tiba Asilia Tanzania, kipo katika baadhi ya mikoa ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Arusha, Morogoro, Dar-Es-Salaam, Tanga, Pwani na Tabora.

Kinajihusisha na utoaji wa tiba asilia kwa magonjwa sugu kama kisukari, pumu, magonjwa ya akili, shinikizo la damu, Saratani (kansa), vidonda vya tumbo na meno.

Waanglikana Mara wazisaidia chakula koo zinazopigana Tarime

Na Christopher Gamaina, Tarime

KANISA la Kianglikana katika Dayosisi ya Mara lenye makao yake mjini Musoma, limetoa msaada wa magunia 100 ya chakula kwa vijiji vitano vilivyoathirika na mapigano ya koo na koo katika Tarafa ya Inchungu Wilayani Tarime.

Taarifa zilizopatika hivi karibuni kutoka uongozi wa Kanisa hilo mjini hapa, zimesema msaada huo umefautia athari zilizotokea katika mapigano ya koo za Wanchari na Walenchoka, mwanzoni kwa Julai na Agosti, mwaka huu.

Vijiji vilivyonufaika na msaada huo wa Kanisa la Anglikani ni, Korotambe, Kubiterere, Kyongera, Nyabirongo na Nyamhonda.

Vijiji hivyo vilikabiliwa na mapigano makali na hakuna sababu zinazoelezwa wazi kuwa ndizo zilizosababisha mapigano hayo.

Mapigano yalisababisha watu kadhaa kupoteza maisha, kuteketezwa kwa mashamba, kuchomwa maghala ya chakula na kufungwakwa shule mbalimbal.

Watu zaidi ya 1000 walipoteza makazi yao na wengine kukimbilia eneo la Motemorabu nchini Kenya.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Paschael Mabiti, aliliamuru Jeshi la Polisi wilayani humo, kuwakamata waandishi wa habari waliokuwa wanafuatilia chanzo na athari za mapigano hayo ili kuihabarisha jamii.

Mchungaji wa Kanisa hilo mjini hapa, Jacob Robert, aliyeongoza mgao huo uliosimamiwa na Richard Hamza kutoka Musoma, alisema, msaada huo wa magunia 100 ya udaga na mtama, ulifikia katika kijiji cha Kubiterere.

Msaada huo uliothibitishwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwema, wilayani hapa, Bw. Paulo Maisori, uligawanywa kwa wananchi hao kwa utaratibu kwamba familia kubwa, ndiyo iliyopata fungu kubwa.

Akihubiri kwa wanavijiji hao wakati zoezi la mgao wa msaada huo likiendelea, Mchungaj Jacob, aliwahimiza kupendana, kuheshimiana na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo bila kujali tofauti za koo, dini wala siasa.

Aliwashauri wasio na dini kujiunga katika madhehebu wanayoyapenda ili kuyajua mafundisho na mapenzi ya Mungu.

Alisema, hali hiyo itasaidia kuishi kwa amani na kutokomeza uhasama baina yao.