BAADA YA KUSHAMBULIWA, MAREKANI YATAKIWA KUJIULIZA

Kwa nini magaidi hawapigi Ujerumani, Ufaransa, Uingereza?

Na Mwandishi Wetu

MAREKANI imeshauriwa kujitafiti na kujiuliza sababu ya kushambuliwa kwake kigaidi huku mataifa mengine makubwa kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yakiwa hayahusishwi katika mashambulizi.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Monsinyori Deogratias Mbiku, wa Kanisa Katoliki, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam.

Monsinyori Mbiku alikuwa akitoa mada katika semina kwa Wanaume Wakatoliki wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Msimbazi, jijini Dar-es-Salaam.

Alisema, kwa kufanya hivyo, taifa hilo litabaini palipo na dosari zake na kuzirekebisha na kwamba, hali hiyo itaboresha uhusiano wake na mataifa mengi kama yalivyo mafundisho ya Kanisa.

Mwaka 1998, Balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya, zililipuliwa kwa mabomu na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200, wakati Septemba 11, mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi na Kituo cha Biashara ya Kimataifa nchini Marekani, vilishambuliwa kwa ndege za Marekani zilizotekwa na magaidi. Shambulizi hili limesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Monsinyori Mbiku alisema, kulipiza kisasi dhidi ya maadui wa nchi hiyo (magaidi), ikisaidiwa na nchi nyingine washirika wake, si

Inatoka Uk. 1

dawa ya kuondoa matatizo ya ugaidi duniani bali ni hatua ambayo itasababisha hatari ya kuzidisha uhasama na hivyo, kusababisha maafa zaidi.

"Jiulize na waulize kwanini mnatupiga? Watakwambia hiki hatupendi kinatuumiza. Hapo, utagundua kumbe hiki hawakipendi. Hapo sasa mwafaka utatafutwa ili kuwanufaisha wote...Wajiulize kwanini hawapigi Ujerumani, au Ufaransa; au Uingereza na mataifa makubwa mengine?" aliuliza.

Aliongeza, "Jamii nzima lazima ijiulize kuwa, kama tunataka usalama,

Je, tunaonesha sura ya Mungu kwa kuwa na uhusiano mwema na wenzetu?"

Aliendelea kuwa, suala la usalama na amani duniani, halina budi kujengwa tangu mioyoni mwa watu vinginevyo, hata kama ulinzi wa kijeshi utaimarishwa, hautasaidia kitu.

"Haitoshi tu kusema nitampiga, atakiona; yule si mwendawazimu hata kama ana kosa lakini kuna sababu iliyowasukuma kufanya hivyo," alisema na kuongeza lazima kukaa na maadui meza moja kwa upendo na kuzungumza badala ya kuendeleza mlolongo wa uovu.

"Kama unataka amani tenda haki, vinginevyo ni kujidanganya," alisema Monsinyori Mbiku na kuongeza kuwa ni lazima haki itendeke hata kama anayenyimwa haki ni mnyonge kiasi gani kwani ipo siku atalipuka na kusababisha maafa makubwa.

Aidha, aliwataka wanasemina kuamka na kuchangamka katika kuijua imani yao kwa kujisomea Neno la Mungu na kuishi maisha safi ya ndoa wakifuata mafundisho ya Kanisa kwa kuiishi Injili ya Kristo."Kujitafiti na kujifikiria ni kwa nini mwenzio kakutendea hivi au vile ili kuboresha uhusiano kati yenu, ndiyo kugeuza shavu la pili, na ninyi fanyianeni hivyo," alisema.

Pia, aliwataka kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kuliendeleza Kanisa kimwili na kiroho badala ya kusubiri mapadre na maaskofu.

Wanasemina hao waliomba Kanisa Katoliki kuwa na mpango endelevu wa kufundisha Neno la Mungu ili lizame katika mioyo ya watu na kuwabadilisha katika maisha yao.

Baba Mtakatifu abariki kigango kuwa Parokia Dar

l Kardinali Pengo,Paroko wasema

ni bahati ya pekee

Janeth Kavira na Jenifa Benedicto, DSJ

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, ametoa baraka maalumu kwa Kigango cha Luhanga kilichopo katika Parokia Katoliki ya Makuburi jijini Dar-es-Salaam, kwa ajili ya maandalizi ya kuwa parokia.

Baraka za Kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, zilitolewa kupitia kwa Padre Janes, aliyekuwa mjini Roma Italia hivi karibuni aambaye aliomba baraka za Baba Mtakatifu kwa ajili ya kigango hicho kinachotarajiwa kuwa parokia.

Wakizungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, na paroko wa Parokia ya Makuburi, Padre Geraldo Derksen, walisema jijini wiki iliyopita kuwa, wamefurahishwa na maneno ya baraka aliyoyatoa kwa kigango hicho kwa njia ya barua.

Katika mazungumzo yake, Kardinali Pengo alisema kuwa, ameshangazwa na kufurahishwa juu ya hatua hiyo kwani hakuwa na taarifa ya juhudi za kigango hicho kutafuta baraka za baba Mtakatifu.

"...hata niliposikia kuwa wamepewa barua ya baraka na Baba Mtakatifu, nilifurahi nikashangazwa mpaka nikawauliza, mmeiiba wapi hiyo," alisema Kardinali Pengo kwa furaha.

Alikipongeza kigango hicho na kuwapa changamoto ya kujitolea kwa hali na mali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

KIONGOZI lilipotaka kujua ni lini kigango hicho kitakuwa parokia, kardinali Pengo alisema, "Mimi sina kipingamizi kwani wana Luhanga wamekwishapata baraka toka kwa Baba Mtakatifu hivyo, hakuna wa kupinga".

Kardinali Pengo alisisitiza juhudi za waamini na wote wenye mapenzi mema ili kukamilisha ujenzi wa nyumba ya mapadre.

Alisema, juhudi hizo zitafanikisha kuondoa tatizo la upungufu wa huduma ya mapadre, uliopo katika parokia ya Makuburi. Alisema, kinyume na juhudi za kujitolea kwa hali na mali za waamini, ipo hatari ya muda mwingi kupita huku kigango cha Luhanga kikiitwa Parokia tarajiwa.

Paroko wa Parokia hiyo, Padre Geraldo, alisema kuwa, baraka hizo za Baba Mtakatifu, zimetolewa kwa watu wote wakiwamo walemavu, wazee, watoto, vijana na hata wagomvi wote wamebarikiwa. "Baba Mtakatifu habagui mtu. Baraka zake anazitoa kwa watu wote," alisema Padre Geraldo.

Kigango hicho kilizinduliwa Oktoba 22, mwaka jana, kwa Misa Takatifu iliyoongozwa na Padre Geraldo Derksen. Kabla kigango hakijapata jengo la muda, kilikuwa kikitumia maturubai yaliyowekwa Jumamosi na kuondolewa baada ya ibada ya Jumapili.

Hivi karibuni kigango hicho kilifanya uchaguzi wa viongozi wake. Bw. Bruno Hinju, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti alikuwa Bw.Lawrance Masawe.

Simon Dolongo alipata nafsi ya Ukatibu, Bibi Anna Kambona, alikuwa Katibu Msaidizi na Richard Bantulaki, akawa Mweka Hazina.

Pia, ziliteuliwa Kamati mbili; ya Litrujia na Kamati ya Maendeleo ambazo zinafanya kazi kwa kushirikiana na Kamati Tendaji ya Kigango.

Kigango cha Luhanga kina jumuiya 34 na kanda 5 ambazo ni Mabibo A, Mabibo B, Luhanga, Minyonyoni na Mji Mpya. Kina waamini 8,568 walio katika makundi tofauti.

Kuna familia 572 zenye ndoa na familia 856, zisizo na ndoa. Vijana ni 5140, wazee 428 na walemavu 257.

Hata hivyo, habari zaidi zilizopatikana toka kigangoni hapo zinasema, Kamati Tendaji inashirikiana na Kamati za Kanda kuhakikisha familia zisizo na ndoa , zinapata sakramenti hiyo.

Tangu kuanzishwa kwa kigango, takribani Ndoa 40 zimefungwa na watoto wapatao 190, wamebatizwa. Vijana 65 wamepata Sakramenti ya Kipaimara na watoto wasiopungua 100, wanatarajiwa kupata Komunyo ya Kwanza, hivi karibuni.

Walezi wa kiroho katika kigango hicho ni Padre Geraldo Darksen, Padre Erineus Mbahulila na Padre George Sai.

Padre wa DRC awaasa Watanzania kuepuka mapigano

l Asema kama hawajui ubaya, waende Burundi, Kongo na Rwanda

l Asema mwenyewe alishakimbia mara saba

Na Mwandishi Wetu

PADRE mmoja wa Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Kongo (DRC), amewahimiza Watanzania kukumbatia amani kwani machafuko katika nchi ni hatari na yamekwisha mfanya akimbie jimboni kwake mara saba ili kujisalimisha.

Padre huyo raia wa Ubelgiji, Edgard Declercq, aliyefanya kazi za kichungaji nchini DRC nchi ambayo imetawaliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1958 hadi 1999, aliyasema hayo wakati akizungumza na KIONGOZI jijini Dar-es-Salaam, mwishoni mwa juma.

Alisema, Serikali na Watanzania kwa jumla, hawana budi kuwa makini na watu wote wanaofanya majaribio ya kuvuruga

Inatoka Uk. 5

amani kwa kile alichokiita, kutumiwa na watu wa nje.

Alisema, Watanzania wenye mawazo finyu na mipango ya kuvuruga amani, hawana budi kwenda katika nchi za Rwanda, Burundi na DRC ili waone hasara za vurugu katika nchi zenye vita.

Alisema watu wa namna hiyo ambao tayari wameanza kujitokeza ni vizuri wakadhibitiwa mapema ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza endapo wataachwa kwa muda mrefu na kudhani kwamba wanayofanya yanavumilika na yanaweza kukubalika katika jamii.

"Dumisheni amani na utulivu; hawa watu ambao wanaanza kujitokeza kuvuruga amani ni vizuri wakadhibitiwe mapema," alisema Padre Declercq.

Alisema kwa kuwa watu hao wanatumiwa na watu wa nje kwa malengo yao wasionewe aibu hata kama watatumia mgongo wa dini kwa kuwa vurugu zinapotokea, huathiri watu wote bila kubagua.

Padre Declercq (77), kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Bukavu nchini DRC, alisema katika miaka 41 aliyokaa nchini DRC, amepitia machungu mengi yaliyotokana na vurugu za kivita nchini humo hali iliyomfanya akimbie mara saba na kurejea baada ya hali kutulia.

Alisema kutokana na hali hiyo, alilazimika yeye binafsi kukimbia na kuacha huduma ya kiroho mara tano na kisha, kutakiwa na uongozi wake kuondoka katika eneo lake mara mbili.

"Mimi mwenyewe kuna wakati wa Jubilei yangu ya Mika 50 ya Upadre, niliungama kwa waamini wangu nikawaambia wanisamehe kwa kuwa niliwafanya makosa kwani kama mchungaji sikutakiwa kukimbia na kuwaacha kondoo wakati machafuko yalipozidi lakini, wenyewe walisema, hukukimbia bali ulikimbizwa," alisema.

Alifafanua kuwa, katika vipindi vyote alivyokimbia na kuacha watu wake, mara mbili alikuwa nje ya nchi hiyo na wakati mwingine, alikimbilia maeneo ya jirani nchini humo.

KIONGOZI lilipomuuliza kama yakitokea mapigano mengine sehemu aliyopo anaweza kukimbia tena? Padre huyo alisema, "Siwezi kukimbia tena kwani hata wakati ule mara nyingine nililazimishwa na ndiyo maana roho iliniuma nikaungama kwa waamini wangu nao wakasema sikukimbia bali nilikimbizwa."

Alisema amani huko DRC ni vigumu kupatikana kwa sababu ya utajiri wa madini nchini. Alisema, utajiri huo umewafaya wanajeshi wa kigeni walioingia humo hawako tayari kutoka kwani hawahitaji hata mshahara toka katika serikali zao bali wanajilipa kwa madini na utajiri wa nchi hiyo.

Alisema hata serikali zao zinafaidika na hali ya DRC kubakia vitani ili kupata fursa ya kupora utajiri wa madini.

Kutokana na hali hiyo, Padre Declercq alisema wafanyakazi huko Mashariki mwa Kongo hawalipwi mishara na serikali. Hata hivyo, alisema, walimu wanalipwa na wazazi wa watoto kupitia michango mbalimbali.

"Hali inatisha huko. Lakini hapa kwenu nashangaa mtu unatembea kutoka hapa mpaka mahali unakokweenda bila kuona mtu anakusumbua au kukutukana. Inafurahisha,"

Alisema na kuongeza kuwa alisafiri kwa treni toka Mpanda hadi Tabora na kukaa chumba kimoja na Mwislamu mmoja ambaye waliongea vizuri na kwa upendo pamoja na kwamba walikuwa hawafahamiani.

Alisema endapo Watanzania watachezea amani iliyopo, hawana budi kujua kuwa hali kama iliyopo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, itajitokeza nchi kwao.

"Majeshi yatatoka nchi nyingine kuja kulinda huku na kupora utajiri na mali yote mliyo nayo nchini. Watanzania muwe macho," alisema.

Padre huyo ambaye hivi sasa yuko nchini kwake, baada ya kumaliza utumishi wake nchini DRC, alikuwa nchini hapa kwa muda wa miezi miwili ambapo aliendesha mafungo kwa watawa jimboni Sumbawanga akiwa njiani kurejea nyumbani Ubelgiji. Alisema yuko tayari kuja nchini kutoa huduma za namna hiyo endapo ataalikwa.

Wakristo ni waajiriwa, wadaiwa wa Mungu - Pengo

Jenifa Benedicto Na Janeth Kavira, DSJ

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema kila Mkristo ni mwajiriwa na mdaiwa wa Mungu hivyo, ni wajibu kutumia mali na uwezo wa kila mtu katika kutimiza mapenzi ya Mungu.

Kardinali Pengo aliyasema hayo Jumapili iliyopita wakati akihubiri katika Ibada aliyotoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 65 wa kigango cha Luhanga, kilichopo katika Parokia ya Makuburi, jijini Dar-es-Salaam.

Alisema Wakristo na wote wenye mapenzi mema, hawana budi kutumia mali zao kwa kusaidiana miongoni mwa jamii na kuepuka tabia ya kuthamini mali kuliko utu.

Alisema, kwa kuwa watu wote ni waajiriwa na wadaiwa wa Mungu, ni wajibu wa kila mmoja kufanya jitihada za kulipa madeni na kutimiza wajibu wake kwa Kanisa. Alisema, hii ni pamoja na kufanya yote yanayompendeza Mungu ikiwamo tabia ya kupenda kuwasaidia wenye shida.

Aliongeza kuwa, kamwe si vema kukumbatia mali huku wengine wakiteseka kwa kuwa mali ya ulimwenguni, ni mali ya kupita na ambayo haipaswi kumfanya mtu apingane na mapenzi ya Mungu.

Alisema ni wazi kuwa, Mkristo anayetimiza wajibu wake na kutumia mali aliyo nayo kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu, huwa anajiandaa kupokea maisha yenye uzima wa milele.

Aliwaasa waliopokea Sakramenti ya Kipaimara, kuishi na Roho Mtakatifu ambaye walimpokea wakati wanapokea Sakramenti hiyo.

Aliwahimiza waamini wote kujenga utamaduni wa kuombeana mema siku zote ili wote wapate kushiriki uzima wa mlele.

Katika risala yao iliyosomwa na Katibu wa Kamati ya Ibada ya Kigango, Bw. Simon Dollongo, waamini walisema kuwa, wametiwa moyo na ukubali wa ujio wa Kardinali Pengo kigangoni hapo na kwamba, wamefurahishwa na kazi ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara aliyoifanya.

Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar-es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, waamini hao waliushukuru uongozi wa jimbo kwa kuwaongezea mlezi mwingine, Padre George Sai.

Awali, parokia ya makuburi ilikuwa na mapadre wawili; Paroko, Padre Geraldo Derksen na Padre Erneus Mbahulila.

Katika risala yao, waamini hao walisema kigango hicho kinakabiliwa na tatizo la barabara na daraja kwa ajili ya magari na waenda kwa miguu hali waliyoielezea kama kikwazo cha usafiri na mawasiliano ya kuaminika hadi kigangoni.

Vyama wapinzani vyapondana vyenyewe kwa vyenyewe

l S.M.T chasema sio lazima kuipinga Serikali kwa kila kitu

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha siasa chenye usajili wa muda cha SAUTI YA MSHIKAMANO TANZANIA (S.M.T.), kimesema tofauti na matarajio, kinasikitika kuona vyama vya upinzani nchini vimeshindwa kukidhi haja za wananchi badala yake, vinang’ang’ania vurugu na migogoro isiyo na manufaa kwa wananchi.

Kaimu Makamu wa Rais Chama hicho chenye usajili mwingine wa muda tangu Agosti 22, mwaka huu, Bw. Paulus M.B. Mwanja, Naibu Katibu Mkuu, Ali Chigoma na Katibu wa Vijana wa chama hicho, Mohamed Liunde, waliyasema hayo mwishoni mwa juma wakati wakizungumza na KIONGOZI jijini Dar-es-Salaam.

Walikuwa wakifafanua mintarafu taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari yenye Kumb. Na S.MT/GEN/DSM/1/19 ya Septemba 23, mwaka huu.

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Makamu huyo wa Rais na Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Yusuf H. Kibuti, S.M.T. kimesema kuwa, licha ya kufurahi Serikali ya Tanzania kuanzisha mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi, kinashangazwa kuona kuwa, kinyume na matarajio ya mfumo huo kutumika kusukuma maendeleo ya taifa kwa kufufua uchumi, sasa vinashughulikia migogoro badala ya malengo yaliyokusudiwa.

"... Sio siri kuwa Tanzania kuna vurugu. Tulitegemea kutakuwa na amani na vyama vitaendesha shughuli kwa ushirikiano lakini sivyo. Sisi tunachohubiri ni amani, utulivu na mshikamano. Hatutaki maandamano yasiyo na maana wala hoja za jazba kwa kuwa tunajua hivyo ni vichocheo vya vurugu," alisema Bw. Mwanja katika ufafanuzi wake.

Alisema chama chake kikipata usajili wa kudumu, kitahakikisha kinaangalia kwa makini na kutumia busara kuikosoa na kuishauri Serikali penye udhaifu na ilipo sahihi na kushirikiana nayo palipo sahihi.

" Si kwamba kila kitu ambacho Serikali inafanya ni kibaya. Maeneo mengine inafanya vizuri na katika maeneo kama hayo lazima tuipongeze, maana Serikali ni yetu sote. Tuangalie na kuishauri penye udhaifu wa Serikali kama udhaifu wa wote;... tutasema sisi tunashauri mfanye hivi ili mambo yaende vizuri. Kama Serikali itang’ang’ania msimamo ambao ni kosa, wananchi wataamua katika uchaguzi. Siyo eti Serikali ifanye kosa, na sisi tufanye kosa. Kosa juu ya kosa ni maafa kwa jamii," alisema.

Chama hicho kimetoa wito kwa walalahoi nchini kuungana nacho ili kutetea na kulinda haki zao za msingi ili wawe washauri madhubuti wa Serikali katika kuinua maisha yao.

"Tunaomba kama WALALAHOI, tushirikiane kwa hali na mali katika nyanja mbalimbali kuinua na kukuza uchumi na maendeleo ya nchi yetu kwa faida ya wananchi wote ambayo hivi sasa ni tatizo kubwa katika nchi hii," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

SAUTI YA MSHIKAMANO ni chama cha siasa chenye lengo la kuwaunganisha Watanzania wote wanyonge wa jinsia zote bila ubaguzi wa rangi, kabila, dini, au hali ya mtu. Makao yake makuu yapo Kurasini, Dar-es-Salaam.

Kipo mbioni kufungua ofisi katika wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni. Pia, katika mikoa ya Pwani, Mtwara, Lindi, Mbeya, Rukwa, Dodoma, Singida, Tanga, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Pemba na Unguja-Kaskazini.

Big November Crusade yawaambia wanawake, msidanganywe kwa simu, saa

Na Mwandishi Wetu

MKUTANO Mkuu wa wa Injili(The Big November Crusade), umewahimiza wanawake kuwa makini katika maisha yao na kuepuka kudanganywa kwa simu na saa huku wakihatarisha maisha yao kiroho na kimwili.

Mchungaji Joshua Sserwada kutoka nchini Uganda, alitoa ushauri huo katika siku ya mwisho ya mkutano huo uliokuwa ukifanyika katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar-es-Salaam.

Katika Mkutano huo uliomalizika Jumapili iliyopita, Mchunguji huyo aliwataka wanawake wakatae kuhongwa saa na simu za mkononi bali waseme ‘No’ kwa imani ya mwili kwa kuwa zawadi hizo haramu, zinawapeleka katika hatari.

Alisema kuwa, kutokana na kuendekeza mambo ya dunia, mara nyingi wanajamii wakiwamo Wakristo, wamekuwa wakifanya dhambi huku wakisingizia kuwa, wanatafuta suluhisho la matatizo.

"Suluhu nyingi ziko ndani ya Kanisa. Kwa sasa watu tunahalalisha dhambi halafu tunashuhudia na kumshukuru Mungu kwa jina la dhambi," alisema Mchungaji Sserwada na kuongeza kuwa, kila mtu hana budi kujiuliza kuwa vitu alivyo navyo amevipataje.

Alisema endapo watafanya hivyo, ni dhahiri watabaini kuwa katika kuvitafuta, kulikuwa na suluhu na uongo mwingi katika maisha yao na hivyo, wajirekebisha kwa kufanya toba ya kweli.

"Huu ni wakati wa kuwa na imani sahihi ya kusema ‘No’ siyo kupokea pokea tu," alisema.

Aidha, Mchungaji huyo ametaka Wakristo kuiga mfano wa Mtume Paulo kwa kulinda imani na kupigana vita dhidi ya mambo yote yanayokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Aliwataka Wakristo kuzingatia Maandiko Matakatifu(Biblia),toka Kitabu cha 2Tim, 4:7-8, isemayo, "Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia walipenda kufunuliwa kwake."

Mkutano wa The Big November Crusade, ulianza Septemba 1, mwaka huu na kuanzia mwakani, utakuwa ukifanyika mara tatu kwa mwaka yaani Januari, Juni na Septemba.

Askofu Minde achangia ujenzi wa nyumba ya malezi

l Amteua Padre Sekere kuwa Mlezi wa Waseminaristi

Na Pd. Mwenge Deogratius, Kahama

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Kahama, katika Awamu ya Pili, Mhashamu Ludovick Minde, amechanga shilingi 1,500,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya malezi kwa waseminari wanaojiandaa kuingia seminari kuu na watakaojiunga na seminari jimboni humo.

Askofu Minde alitangaza uchangiaji huo, hivi karibuni katika kikao chake na mapadre wa jimbo hilo. Mhashamu Minde alitaka kuwashirikisha mapadre wa jimbo lake, mawazo na maoni juu ya utendaji kazi za kitume katika kipindi cha uongozi wake.

Alisema kuwa, katika uongozi wake jimboni hapo, mradi wake wa kwanza wa jimbo utakuwa ni kujenga nyumba ya malezi (Formation House) na kuwaeleza mapadre hao kuwa, alipotembelea Roma, Italia mapema mwaka huu, alionana na Mkuu wa Idara ya Uenezi wa Imani (Propaganda Fide), Mwadhama Kardinali Sepe.

Mhashamu Minde alisema kuwa, katika mazungumzo yao, mjini Roma, Kardinali Sepe alisisitiza umuhimu wa kuwa na semimari ndogo au nyumba ya malezi kwa ajili ya wanaseminari wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Aliendelea kusema kuwa, kutokana na msisitizo wa Kardinali Sepe, mapadre wawili waliokuwa ofisini humo wakati wa mazungumzo na Askofu Minde, kwa moyo wa huruma na upendo kwa Jimbo la Kahama, palepale walichangia Dola za Kimarekani 240 (sawa na Tsh 192,000)kama kianzio cha ujenzi wa nyumba hiyo.

Mapema, Askofu Minde aliwajulisha mapadre hao wa jimbo lake kuwa, zawadi yote ya fedha taslimu alizopatiwa wakati wa sherehe za kuwekwa kwake wakfu na kusimikwa kam a Askofu wa Pili wa Jimbo Katoliki la Kahama Agosti 5, mwaka huu, ameitoa kama mchango wake kwa ujenzi huo.

Wakati huo huo: Askofu Minde amemteua Padre Joseph Sekere, kuwa Mlezi wa Vijana Waseminaristi katrika Jimbo la Kahama, wanaojiandaa kujiunga na seminari kuu.

Awali, vijana hao walikuwa wanafanya mwaka wao wa malezi katika Jimbo Katoliki la Singida lakini, imefahamika kuwa kuanzia sasa Waseminaristi hao watapewa malezi jimboni Kahama.

Msichanganye migogoro ya siasa, dini - Askofu Sambano

l Aelezea hasara za vita kwa jamii

Na Mwandishi wetu

ASKOFU Mstaafu wa Kanisa la Kianglikana, Dayosisi ya Dar-es-Salaam, Basil Sambano, amesema ni hatari kuhusisha migogoro ya kisiasa na imani za kidini kwani hali hiyo husababisha madhara kwa wanajamii hata wasio husika na migogoro hiyo.

Katika hotuba aliyoitoa katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Mt. Albano Jumamosi iliyopita ili kuwaombea waathirika wa mashambulizi ya kigaidi huko New York na Washington, nchini Marekani, Septemba 11, mwaka huu, Askofu huyo mstaafu alisema kuwa katika kipindi hiki alichokiita kuwa ni cha "mpinga Kristo", endapo jamii, hususan wakristo, hawatakuwa makini kutafakari, ipo hatari jamii ikajikuta inachanganya migogoro ya kisiasa na imani za kidini hali ambayo itazua madhara makubwa.

Baada mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Marekani yaliyopelekea dunia kukumbwa na hofu na tishio la vita, maafa na machafuko, wakristo wametakiwa kuwa makini katika kutafsiri matukio mbalimbali kwani huu ni wakati wa ‘mpinga Kristo’.

"Huu ni wakati wa Mpinga Kristo, hivyo tusihusishe mifarakano ya kisiasa na imani za kidini... kila mmoja kutii mamlaka ya serikali kwani hiyo imeanzishwa na kupangwa na Mungu," alisema.

Aliongeza, "Mwogopeni Mungu, na Serikali zenu; nanyi mtakuwa salama kiroho na kijamii," alisema Askofu Sambano.

Alisema kuwa amani, mapatano na umoja baina ya watu duniani, vyote vinategemea moyo wa upendo, uvumilivu na kuheshimiana na tabia bora ya kuthamini utu kuliko vitu.

Akitumia historia kuelezea madhara ya vita toka katia Biblia Takatifu, askofu Mstaafu Sambano alisema kuwa, vita ya Majimaji, Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia, na vita dhidi ya uvamizi wa Idd Amin nchini Tanzania, havikuleta faida yoyote mbali na hasara ya upotevu wa maisha ya watu na mali.

Kutokana na hali hiyo watu wanaishi katika hofu ya kuzuka vita nyingine ya dunia wakati wowote hasa wakati huu wa mipango ya taifa la Marekani kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.

Alisema kuwa inapotokea vita, waathirika wengi huwa ni raia wasio na hatia ambao hawana cha kujilinda dhidi ya silaha nzito za kivita.

Aliwataka Wakristo kuzidisha vita ya kiroho dhidi ya maovu ambayo husababishwa na maadui wa Mungu.

"Ndugu hizi ni nyakati za mwisho. Muwe macho, ni wakati wa maangamizi ya shetani aliyeachiwa kwenda kuyadanganya mataifa," alisema.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Rais Benjamin Mkapa na mkewe Anna, Balozi Mdogo wa Marekani, Bi Wanda Nesbit, Jaji Mkuu, Barnabas Samata, viongozi wa serikali, mabalozi, viongozi wa dini na watu wenye mapenzi mema.

KKKT Kinondoni wakiri Dini imewasaidia wanafunzi shule za msingi

Na Neema Dawson

MKUU wa Jimbo la Kinondoni la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Ajuaye King’omela, amesema Elimu ya Dini kwa shule za msingi, imechangia kuwafanya wanafunzi wengi wamgeukie Mungu.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, aliyetaka kujua endapo somo hilo katika shule za msingi lina mchango wowote wa kiroho kwa wanafunzi.

Ingawa hakutoa takwimu, lakini Mchungaji King’omela alisema kuwa Jimbo la Kinondoni, linaongoza katika dayosisi yao kwa idadi kubwa ya wanafunzi waliofaulu vizuri na kupata vyeti vya somo la Dini kwa wahitimu wa elimu ya msingi kwa miaka iliyopita.

Alisema, mafanikio ya somo hilo katika shule za msingi, yanatokana na walimu wa somo hilo katika madhehebu mbalimbali ya Kikristo, kushirikiana vema na walimu katika shule lnapofundishwa.

"Inafurahisha sana maana somo hili la Neno la Mungu (Dini), limewabadilisha wanafunzi wengi waliokuwa wanakwenda katika njia potofu kutokana na wengi wao kulelewa katika mazingira mabaya na wengi kutoka katika familia zilizokata tamaa; familia zisizojali malezi ya watoto; zinawaacha wafanye hata mambo maovu bila kuwakemea," alisema.

Alionesha kuwa hadi hivi sasa, wapo baadhi ya wanafunzi Wakiislamu wanaolipenda na kuvutika na somo la Dini ya Kikristo ambao hulisoma na kuamua kulifanyia mtihani. Alisema hao, hufaulu vizuri na kupata vyeti. Alisema kuwa vyeti hivyo vilitolewa na Idara ya Elimu ya Kikristu kwa Waratibu wa Elimu ya Kikristo majimboni kwani waliotunukiwa vyeti hivyo ni wanafunzi waliosoma somo la Dini na kufaulu katika mitihani waliyoifanya bila kujali dini zao.

Alitoa mwito kwa wanafunzi kuendelea kujiunga na masomo ya Dini ili yawasaidie kumjua Mungu na kuishi kwa kadiri ya mapenzi yake. Alisema, hali hiyo itawafanya wawe watoto wema machoni pa Mungu.

Naye Meryna Chillonji, DSJ, anaripoti kuwa,

UMOJA wa Akinamama wa KKKT, Usharika wa Kariakoo katika Jimbo la Ilala (Kariakoo Lutheran Women Group), wapo nchini Kenya

Kwa wiki moja kwa Maonesho ya kazi za mikono Mwinjilisti Jema Mtinge, amesema maonesho hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa kampuni ya "Micro Interprises Support Programe (MISP)) na Skills Across Kenya (SAK).

Maonesho hayo yanahudhuriwa na nchi za Tanzania, Zambia, Malawi, Kenya na Uganda na bidhaa zinazooneshwa ni pamoja na vitenge, batiki na vikoi.

WAWATA wataka Vijana wasome, wajiajiri

Na Elizabeth steven

Vijana nchini wametakiwa kubuni miradi mbalimbali hasa ya uzalishaji kwa njia ya ajira binafsi ikiwamo ya kilimo, ufugaji na ufundi kama njia ya kuondokana na maisha tegemmezi

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mratibu wa Miradi na

Mafunzo wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam, Bibi Perpetua Mashelle, alipokuwa akiendesha semina ya vijana iliyofanyika parokiani Tabata jimboni hapo.

Alisema kuwa, wakati umefika kwa vijana kutambua kuwa wao ndio nuru ya ulimwengu na tegemeo la taifa na hivyo, hawana budi kubuni njia mbalimbali za uzalishaji mali ili wakabiliane na ugumu wa maisha katika kipindi hiki cha ukosefu wa ajira.

Bibi Mashelle alisema, kumekuwa na malalamiko yasiyo na msingi toka kwa vijana dhidi ya Serikali kuwa haitoi ajira.

Alisema, njia pekee ya kuyaondoa malalamiko hayo ni kutumia nguvu zao wenyewe kujiajiri.

"Vijana wanazo nguvu za kufanya kazi za uzalishaji mali na kujizalishia chakula ili wamudu maisha... inabidi kila kijana ajishughulishe na shughuli halali zitakazomuingizia kipato badala ya kusubiri kuajiriwa"alisema Bibi Mashelle.

Aliwakumbusha vijana kuzingatia elimu ili iwasaidie kumudu maisha yao na kuwa waamuzi wazuri katika familia zinazowaetegemea na taifa kwa jumla.

" Ni vema kabla ya kuamua kujishughulisha na kitu chochote, kijana ajitahidi kupata elimu ili imsaidie kupanga mipango kwani, bila elimu, mipangop yote ni sifuri," alisema.

Akaongeza kuwa, kijana asiyefanya juhudi za kujielimisha, ajue anajitafutia uhakika wa kuwa maskini hadi kifo.

"Ni aibu kwa kijana mwenye akili timamu na nguvu za kufanya kazi, kukaa bila kujishughulisha akitegemea misaada kutoka kwa wazazi wake wakati yeye ndiye anayetakiwa kuwasaidia," alisema.

Aliwashauri vijana kuwa na upendo wao kwa wao na kupendana bila kujali tofauti za kidini, kabila wala jinsia na badala yake, wasaidiane wanapokuwa katika manzingira magumu na kuepuka makundi mabaya.

Epukeni ndoa za majaribio mshiriki Meza ya Bwana- Ushauri

Na Maryam Salum, DSJ

MAJARIBIO ya watu kuishi katika ‘ndoa bubu’ (kimada) kwa madai ya kuchunguzana tabia, pamoja na tofauti za kimadhehebu, zimeelezwa kuwa baadhi ya vikwazo vya watu kutofunga ndoa na hivyo, kutoshiriki Meza ya Bwana.

Mchungaji Michael Kitale, wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Buguruni, Jimbo la Ilala katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, aliyasema hayo katikati ya juma lililopita wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar-es-Salaam.

Alisema tatizo la kuishi katika ndoa za majaribio na tofauti za kimadhehebu, inawafanya wanajamii wengi kubweteka na kujisahau kuwa wanaishi katika ndoa zilizo kinyume na mapenzi ya Mungu.

Mchungaji Kitale aliendelea kusema kuwa, licha ya wanajamii hao (waamini) kushiriki taratibu na shughuli kadhaa za Kanisa ikiwa ni pamoja na kuhudhuria ibada mbalimbali na kutoa sadaka, maisha ya ndoa bubu wanayoishi yanawafanya kutoshiriki Meza ya Bwana huku wengine wakisisitiza maombi kwa ajili ya vijana wao kubatizwa.

"Wengine wanadai kuwa wanakaa pamoja ili kuangaliana tabia kwanza ndipo eti baadaye wafunge ndoa. Matokeo yake, wanajisahau kabisa na hata kufikia kuzaa watoto kabla ya ndoa. Bado wazazi hao wanarudi kuwaombea vijana wao ubatizo," alisema.

Kuishi kinyumba bila kufunga ndoa iliyopata baraka za Mungu kanisani, ni kuvunja Amri ya Sita ya Mungu inayozuia kuzini.

Hata hivyo, Mchungaji Kitale alisema kuwa, tatizo la watu kutoshiriki Meza ya Bwana kutokana na kutofunga ndoa, pia lipo katika madhehebu mengine.

Aliwahimiza viongozi wa kiroho katika madhehebu mengine, kuwasisitiza waamini wao katika ibada, semina na mikutano mbalimbali ili wazingatie umuhimu wa mkristo kupokea Sakramenti ya Ndoa na hivyo, kushiriki Meza ya Bwana.

Wakati huo huo: Mchungaji Kitale amewahimiza vijana na walezi wa vijana wanaopokea Sakramenti ya Ubatizo, kushiriki kikamilifu katika semina maalum zinazotolewa na Kanisa kwa ajili yao, ili kuboresha maisha yao kiroho.

Hata Maskini, mtafuteni Mungu kwa bidii- Mch. EAGT

Na Jenifa Benedicto, DSJ

"MUNGU anawasikia watu wake wanapomwita na kumtafuta kwa bidii katika maisha yao. Hata kama ni maskini".

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mwinjilisti Samuel George, wa Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT), wakati akihubiri katika Mkutano wa Injili uliofanyika katika viwanja vya Temeke jijini Dar-es-Salaam.

Akitumia Maandiko Matakatifu toka katika kitabu cha Zaburi 34:6,

Mchungaji George alisema kuwa, ni wazi kwa mwanadamu yeyote anayemlilia Bwana kwa imani na matumaini wakati wa masumbuko na taabu mbalimbali, Mungu husikia kilio chake na kumsaidia.

Aliendelea kusema, japo watu wanaishi katika ulimwengu wa shida, ni lazima kila mmoja ajione kuwa ni mhitaji mbele za Mungu ili Mungu amsaidie.

Alisema ni vema kumwendea Mungu katika kila jambo, kwaniNi Mungu pekee aliye msaada kwa wanadamu wote.

"Unapomwendea Mungu kwa imani katika umaskini wako, atakuinua kwa sababu Mungu anaweza mambo yote," alisema.

Alisisitiza kuwa, mtu anapotaka kupokea neema za Mungu, ni lazima aimarishe kwanza imani aumbike moyoni mwake kwa kuwa siku zote Mungu anawawazia watu mambo mema na namna ya kuwasaidia.