Make your own free website on Tripod.com

Mali za Idd Simba kupigwa mnada?

lAskofu aeleza sababu ya Rais Mkapa kusikitika

Peter Dominic na Dalphina Rubyema

WAKATI Askofu amempongeza Idd Simba kwa kujiuzulu, kiongozi mwingine wa kidini amesema Bunge likibaini kuwa alitumia vibaya madaraka, litaifishe mali zake na kuzipiga mnada kama mwenyewe hatakubali kufidia hasara.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti mwishoni mwa juma jijini Dar es Salaam juu ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Idd Simba.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Same, Mhashamu Jacob Koda, alisema kujiuzulu kwa Bw. Simba ni ushujaa unaoonesha kukomaa kisiasa hali inayolinda umoja wa kitaifa.

Naye Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Monsinyori Julian Kangalawe, alisema kwa vile Bunge linaendelea kufuatilia suala hilo, ikithibitika kuwa Waziri Simba alitumia vibaya madaraka yake, basi awajibishwe kisheria kwa kulipa na kufidia hasara aliyolisababishia taifa.

"Ikishindikana kulipa, Serikali itaifishe mali zake na kuziuza, mali aliyoifirisi itakuwa imelipwa," alisema.

Monsinyori Kangalawe alimshauri Idd Simba kutumia ustaarabu wa kukubali kulipa na kufidia hasara kama alivyotumia ustaarabu wa kujiuzulu. Aliishauri Serikali kutodanganyika kumshtaki Simba kwani itajiingiza katika upotezaji wa pesa zaidi katika kushugulikia kesi.

"Akifungwa Serikali itatumia pesa nyingi kumtunza isitoshe ana pesa nyingi, akifunguliwa mashtaka ataweka mawakili wanaoweza kumuwezesha kushinda kesi.

Dawa ni kukubali kulipa mwenyewe ama mali zake kupigwa mnada," alisema Monsinyori Kangalawe.

Akielezea kitendo cha Rais Mkapa kusikitishwa na kujiuzulu kwa Waziri huyo, Mhashamu Koda, alisema ilikuwa halali kwa Rais kufanya hivyo kutokana na ubinadamu kwa kuwa amefanya naye kazi kwa muda mrefu.

"Pamoja na Waziri Simba kujiuzulu, nafsi yake ilimsuta kwa kitendo hicho. Hata hivyo, Rais alisikitika ili kulinda umoja wa kitaifa siyo kwamba alisikitika ili kutetea vitendo vya rushwa," alisema Askofu Koda.

Askofu huyo pia alikielezea kitendo cha Rais Mkapa kuendelea kumshikilia Idd Simba kuiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri wa Viwanda unaoendelea nchini Quatar kuwa amefanya hivyo kwa vile alikwishamteua muda mrefu kabla ya kashfa kumkumba.

"Tunataka kujenga taifa moja, binadamu si mkamilifu, siyo rahisi kutambua tatizo la kila mtu lakini tunapotambua udhaifu wetu, tujirekebishe," alisema.

Kujiuzulu kwa Waziri huyo wa Viwanda na Biashara, kumekuja kutokana na hoja iliyoibuliwa Bungeni na Mbunge wa Jimbo la Kwela (CCM) aliyetaka wizara hiyo ifafanue namna ilivyotoa vibali vya uagizaji wa sukari.

Idd Simba alijiuzulu wadhifa wake juma lililopita baada ya hoja yake kufikishwa bungeni ili kujadiliwa.

'Wasiofikiwa na vyombo vya habari wakumbukwe'

Na Eric Samba

MAASKOFU wa Kanisa Katoliki kutoka sehemu mbalimbali duniani walio hudhuria Sinodi huko Roma, wameyataka mataifa ya Magharibi kuzikumbuka sehemu ambazo hazifikiwi na vyombo vya habari.

Akizungumza na KIONGOZI mwishoni mwa juma katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Mhashamu Norbert Mtega, alisema katika Sinodi hiyo ilibainika kuwa sehemu zenye matatizo mbalimbali zimesahaulika.

Mhashamu Mtega ambaye alikuwa miongoni mwa maaskofu hao, alisema maaskofu hao walibaini kuwa, kutokana na ukosefu wa mawasiliano na huduma katika maeneo hayo, makundi mbalimbali ya watu wanakufa kwa njaa na ukosefu wa dawa.

Alisema katika Sinodi hiyo, Maaskofu hao walizungumzia suala la kimaendeleo ambapo walirudia tena wito wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, wa kupunguza mzigo wa deni la nje kwa mataifa maskini, kulinda haki za binadamu hasa haki ya uhuru wa kidini.

Aidha, waliwataka vijana kuwa makini ili kutohusishwa katika vurugu za kikabila na vitendo vya rushwa.

Maaskofu hao vile vile wamewataka viongozi wa kisiasa na kiuchumi kushughulikia zaidi mambo yenye manufaa kwa watu wote.

Mhashamu Mtega alisema kuwa Maaskofu hao kwa nia moja wanaungana kwa dhati na viongozi hao kutafuta haki na amani.

Katika Sinodi hiyo iliyohudhuriwa na maaskofu 50 toka barani Afrika, Tanzania iliwakilishwa na maaskofu wawili ambao ni Askofu Mkuu Norbert Mtega na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Muhashamu Josaphat Lebulu.

Wakatoliki kutunga sala kuombea ukimwi?

Na Eric Samba

WASHIRIKI wa mkutano wa mwaka juu ya UKIMWI kutoka Majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini, wameshauriwa kutunga sala maalum kwa ajili ya kuwaombea watu walioathirika na ugonjwa huo.

Ushauri huo ulitolewa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ,Padre Pius Rutechura wakati akifungua mkutano huo uliomalizika katikati ya wiki katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) jijini Dar es Salaam.

Alisema licha ya kuwepo na sala za kuwaombea wagonjwa lakini si vibaya ikiwepo sala maalum kwaajili ya kuwaombea waathiriki hao wa UKIMWI.

Vile vile Katibu Mkuu huyo aliwataka washiriki wa mkutano huo kujipatia mbinu mpya kila mara za utendaji ili kuleta tofauti ya mtazamo, fikra na matendo.

Alisema wakati umefika sasa kutoka kwenye nadhari na kwenda kwenye kutenda ili kuleta tofauti.

"Lazima tujifunze mbinu mpya katika kukabiliana na magonjwa na mabalaa mengine," alisema.

Alisema badala ya kujibu mapigo ni lazima kufundisha maadili na akahoji ni majimbo mangapi wanahusika kufundisha ujinsia wa binadamu na jinsi ya kupambana na UKIMWI?

Alisema ni lazima kuzama kwenye kila kitu na kukijua kwa undani badala ya kukalia maelezo ya jumla.

"Tusikalie kusema tubadili tabia. We unafikiri kubadili tabia ni kitu rahisi, kutoka mtu mwovu kuwa mwema. Wangapi tabia zetu si nzuri lakini tunashindwa kuzibadili," alisema.

Aliongeza, "inabidi tuondokane na mawazo finyu juu ya tatizo hili na kuna haja ya kujifunza toka kwa wengine."

Aliwataka kuwa na uhusiano mwema na Halmashauri za Wilaya katika mipango yao bila kusubiri kualikwa vinginevyo wataachwa nje.

Akifunga mkutano huo,Mwanzilishi wa kitengo cha UKIMWI ambacho kipo chini ya Idara ya Afya TEC,Muhashamu Methodius Kilaini,aliwataka washiriki hao kutoa elimu juu ya ugonjwa huo, kwani hata baada ya miaka 2000 ya Ukristo bado Injili inahubiriwa pamoja na kuwa watu wanatenda dhambi.

Muhashamu Kilaini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Fedha katika Baraza la Baaskofu Katoliki Tanzania na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, pamoja na kwamba watu wameisha sikia ugonjwa huo,wanatakiwa kupigana nao kwa kila njia badala ya kujenga mawazo ya kusema kwamba hiyo ni kazi ya mtu ama kikundi fulani.

"Huenda watu wamesikia lakini kinacho takiwa ni kufanya hiyo vita iwe yao wenyewe na waseme ‘hata sisi inabidi tuhusike,’"alisema na kuongeza kuwa si lazima kuwa na fedha ili kuendesha shughuli zao bali hata kwa kuhamasisha.

Nao wajumbe wa mkutano huo walipendekeza kitengo cha kudhibiti UKIMWI ngazi ya taifa kiimarishwe kwa kuongezewa nguvukazi ili kitoe miongozo sawia majimboni itakayorahisha utendaji na ufanisi, na kisiwe chini ya Idara ya Afya tu.

Pia walipendekeza Kanisa Katoliki litumie fursa, rasilimali na muundo wake kutoa elimu na habari juu ya tatizo hili, ikiwa ni pamoja na kuacha waratibu wakae kwenye nafasi zao ili kuendeleza miradi.

Aidha walitaka Tamko la Maaskofu juu ya UKIMWI la mwaka 1987 lipelekwe tena majimboni hadi jumuiya ndogo ndogo ili kuamsha tena ari ya kupambana na ugonjwa huo.

Katika mkutano huo wajumbe walipokea taarifa za majimbo na kubadilishana uzoefu na kuelimishana juu ya mambo wafanyayo majimboni kwao.

Pia walipewa uzoefu toka Anglikana na utafiti juu ya Kitengo cha Kudhibiti UKIMWI TEC lililofanywa na wataalam, Dk. Tengio Urio na Dk. Callista Simbakalila.

Mkutano huo wa siku tatu ulihudhuriwa na Waratibu wa miradi ya UKIMWI, Makatibu wa Afya na wawakilishi wa mashirika na taasisi zinazopiga vita UKIMWI toka majimbo ya Kanisa Katoliki nchini.

Watanzania kueneza Neno la Mungu Kongo

Na Anthony Ngonyani

VIONGOZI wa dini mbalimbali nchini wamejitokeza na kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) Joseph Kabila wa kwenda kuwekeza nchini mwake.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini, Theodehe Mugalu wa Muhingu wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni nyumbani kwake jijini Dar-es-salaam.

Balozi Mugalu amesema viongozi wa dini walimfuata baada ya wito huo ili kujua ni jinsi gani wanaweza kwenda nchini humo na kueneza neno la Mungu kwa wananchi ambao wamekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa miaka nane sasa.

Amesema makundi ya viongozi wa dini yamekuwa yakienda Kongo na kurudi bila matatizo.

"Wananchi wa DRC wamemkabidhi Mungu maisha yao , wanaamini Mungu atakuja na wamejiweka tayari kwa ajili ya kumpokea"alisema.

Amesema wito huo wa Rais Kabila pia umepokelewa na wafanyabiashara wengi kwani wamejitokeza na kwenda kuwekeza nchini humo na makampuni zaidi ya 50 yamejitokeza .

Hata hivyo Balozi huyo alisema kuwa nchi yake inakabiliwa na tatizo la mawasiliano sehemu kwani nyingi hazina mawasiliano mazuri ikiwa ni pamoja na ukosefu wa barabara nzuri na simu.

Aidha ameongeza kusema kuwa wananchi pamoja na wageni wanalazimika kutumia usafiri wa ndege kwa safari zao za ndani na nje ya nchi kwani barabara zimeharibika kutokana na vita ya muda mrefu.

Amesema mpaka hivi tayari Shirika la ndege Tanzania (ATC) na kampuni na Taqwa linalotoa huduma ya usafiri kwa mabasi, hutoa huduma zake nchini humo.

Rais Joseph Kabila alitoa wito wa makampuni na mashirika mbalimbali toka nchini Tanzania kwenda kuwekeza nchini mwake wakati akizungumza na Wafanyabiashara katika Hoteli ya Royal Palm jijini Dar-es-Salaam, wakati wa ziara yake nchini Tanzania miezi michache iliyopita.

Wakristo watakiwa kuvipokea, kuvitumia vyama vya kitume

 

Na Peter Dominic

WAKRISTO wametakiwa kuvipokea na kuvithamini vyama vya kitume ili kuimarisha imani yao katika ukristo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa rejio Maria Kanda ya Chang‘ombe ,Bi.Modesta Kyamuhangire wakati akitoa nasaha zake kwenye sherehe za uzinduzi wa Regio Maria, ikiwa ni tawi (Precidia) ya kwanza ya kigango cha Mipeko Paraokia ya Vikindu.

Akizungumza katika sherehe hizo zilizofanyika Jumapili iliyopita katika kigango cha Mipeko, Mwenyekiti huyo alisema, kila Mkristo anatakiwa kujiunga na chama chochote cha kitume kama njia rahisi ya kuimarisha imani yake badala ya kukaa na ukristo bila kuutangaza.

"Kuwa mkristo bila matendo imani imekufa, chama cha kitume kinaimarisha imani", alisema na kuongeza "tunapata Utakatifu kwa kueneza Utakatifu".

Vile vile Bi.Kyamuhangire aliwataka vijana na watu wengine katika jamii kujiunga na chama hicho na kusiwe na hofu ya kusema kuwa Redio Maria ina kazi nyingi za kuchosha. "Hofu kama hii inapunguza vijana katika chama hicho" alisema Mwenyekiti huyo wa Kanda ya Chang’ombe.

Akizungumza kwa niaba ya Paroko wa parokia ya Vikindu, Sista Maria Elizabeth aliwataka Wanarejio wasichoke kwa mchango wao ambao ni kiini cha upendo na nuru ya kurejesha imani na kuleta umoja katika jamii.

Alisema Wanarejio wamekuwa wakikumbana na matatizo mengi katika utendaji wao, akasisitiza matatizo usiwe msingi wa kukata tamaa.

Katika uzinduzi huo wa Rejio Maria uliofanyika katika kigango hicho wanachama wapya 12 waliweka ahadi zao.

Ibada ya uzinduzi huo iliendeshwa na Paroko Msaidizi wa parokia ya Vikindu ,Padre John Karukappily Kigango cha Mipeku kilifinguliwa mwezi Januari 6 mwaka huu.

Msienzi Watakatifu na kumsahau Yesu-Wito

lMwananyamala wafunga ‘ndoa poa’

Na Eric Samba

WAAMINI wa Kanisa Katoliki nchini wametakiwa wasimsahau Yesu na kukalia kuenzi watakatifu kwani yeye ndiye msingi wa watakatifu hao.

Wito umetolewa hivi karibuni na Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturjia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Monsinyori Julian Kangalawe, katika nasaha zake kwa wanajumuiya ya Mtakatifu Yuda Tadei, Mtoni Sabasaba, parokia ya Kurasini Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Alisema umaana wa Yuda Tadei au Mtakatifu yeyote unatokana na kuwezeshwa na Yesu hivyo watu lazima wamwombe tu awaombee kwa Yesu.

"Msimuenzi Yuda Tadei na kumsahau Yesu. Hiyo itakuwa kama mtu aliyeoa mke na kuwasahau wazazi wazaa chema," alisema.

Alisema maisha ya wakristo hayana budi kujisimika kwenye jumuiya ndogo ndogo na kuwa chanzo cha maadili mema.

"Ukristo wa kweli lazima uingie ndani ya maisha yetu, bila hivyo ni ukristo bandia ambao ndani yake Yesu hayumo," alisema.

Alisema wale walio ndani ya Yesu hawahitaji sheria yoyote kuwaongoza kwani wanaye Roho Mtakatifu na hawahitaji karatasi katika sala.

Naye Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Bw. Ethelbetus Hebuka, alisema kuwa katika kuadhimisha sikukuu hiyo walifanya matendo ya huruma kwa kutoa misaada kwa vituo vya Yatima Group na Scadet vinavyohudumia watoto yatima.

Wanajumuiya hao walitoa mchango wa Sh. 10,000 kwa ajili ya mabenchi ya kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambalo limepanuliwa hivi karibuni kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa AMECEA mwaka 2002 ambao unafanyika hapa Tanzania.

Wakati huo huo: Parokia ya Mwananyamala katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wameadhimisha siku ya somo wao Mt. Martin de Pores kwa kufunga ‘ndoa poa’.

Akitoa nasaha zake kwa wanandoa hao, paroko wa parokia hiyo, Padre Pricus Jumamosi, aliwataka wawe makini bila ubinafsi ambao unachangia kuvunja ndoa siku hizi.

"Ubinafsi wa kusema huyu simpendi tena, huyu kachoka, huyu hang’ai tena ni hatari sana," alisema.

Alisema kwa kuwa wameamua kunyoosha maisha yao wasitarajie maisha ya mteremko bali kuna vishawishi na majaribu makubwa toka kwa Shetani.

"Muwe waangalifu Shetani anaweza kuwajaribu. Nanyi mtaanza kusema mbona tumeishi wote miaka kumi vizuri tu, shida inatoka wapi?" alisema na kuongeza kuwa ni lazima kila mmoja wa aache makandokando yake na kuishi maisha safi ya ndoa. Katika siku hiyo jumla ya ndoa 15 za gharama nafuu zilibarikiwa ambapo wote kwa pamoja walifanyia shereha ya jumla parokiani hapo.

Pamoja na sherehe ya mtakatifu somo, parokia ya Mwananyamala pia ilikuwa ianatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.

Watakiwa kuwaombea wototo wenzao

Na Dalphina Rubyema

WATOTO kote nchini wametakiwa kuwaombea watoto wenzao duniani wanaoteswa katika mazingira magumu ya vita na magonjwa.

Rai hiyo ilitolewa na Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme Tabata,Padre Albinus Tesha wakati akitoa nasaha katika Siku Kuu ya Utoto Mtakatifu parokiani hapo,sherehe zilizofanyika Jumamosi iliyopita .

Padre Tesha alisema kuwa pamoja na mambo mangine,watoto hao katika sala zao hawanabudi kuwaombea watoto wenzao ambao wanateseka katika baadhi ya nchi dunia kwa kukosa amani kutokana na vita na maradhi mbalimbali.

"Sala zenu mnazo sali muwaombee wale watoto wanao teseka katika mazingira ya vita,wanaoumwa magonjwa na njaa ,mkifanya hivyo mtakuwa mnashiriki nao katika mateso yao na mnakuwa mnawapatia faraja"alisema Padre Tesha.

Vile vile Paroko huyo aliwataka watoto hao wa Utoto Mtakatifu kuishi kwa upendo na kufanya matendo mazuri yatakayoweza kuwahamasisha watoto wengine na kufuata njia zao.

Aliwataka wazingatie kuwa Utoto Mtakatifu ni moja wapo ya utume hivyo wayatakatifuze mazingira wanayoishi ikiwa ni pamoja na kuwa na mapenzi kwa jirani zao.

"Takatifuzeni mazingira mnayo kaa kwanza,siyo mkaishi huko kwa kupigana, kutukananapamoja na kupora huko kwenu na shuleni ,mkifanya uovu huo,hapo mazingira yenu yatakuwa hayamtamanishi Kristo,jengeni mazingira yatakayo mvutia Kristo na hapo mtakuwa mnatekeleza kazi ya Umisionari"alisema.

Mbali na hayo ,Padre Tesha vile vile aliwashauri watoto hao kumtolea Mungu sadaka ya pekee kwa kuacha kuangalia vipindi vya michezo ya kuigiza katika Televisheni na badala yake watumie muda huo katika kusali na kumuomba Mungu.

"Mpeni Mungu sadaka ya pekee kwa kuacha kuangali michezo kwenye TV ukiwemo ule wa Tausi,wewe wakati wa michezo huo ukifika,ondoka na nendeni kusali na kumuomba Mungu"alisema.

Waamini watakiwa kuwa makini

Na Christopher Gaimaina, Tarime

WAAMINI wa Madhehebu mbalimbali ya dini nchini,wametakiwa kuwa makini na waangalifu kwa kile wanachosema na kukiwazia wakati wanapokuwa wanasali kwa nia ya kumuomba Mwenyezi Mungu.

Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Tarime katika Jimbo Katoliki la Musoma,Padre Methew Burra wakati akitoa mahubiri katika Misa Takatifu Jumapili iliyopita.

Padre Burra alisema maneno anayo tamka mtu anapokuwa anasali ,humwonyesha Mwenyezi Mungu kilichopo ndani ya moyo wa mtu huyo na msimamo wake katika maisha ya Kikristo.

Vile vile Paroko aliwataka watu kuepukana na usafi wanje wa miili yao kwa mavazi safi na kauli nzuri wakati ndani ya mioyo yao kumejaa uchafu wa chuki ,uzinzi ,udhalimu,uongo,wivu na uchoyo.

BAKITA kuwapiga msasa waandishi

Na Neema Dawson

KUTOKANA na kuibuka kwa matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili kwa vyombo vya habari nchini , Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) linatarajia kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya matumizi fasaha ya lugha hiyo.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni,Mchunguzi wa Lugha BAKITA,Bw. Mbigili Marcus alisema kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikitumia maneno ya mitaani ambayo siyo kiswahili fasaha katika kulenga kuielimisha jamii.

Alisema kuwa vyombo vya habari vinatakiwa kuangalia kwa makini matumizi ya lugha fasaha ya Kiswahili katika utoaji habari na kumekuwapo na vyombo ambavyo vinatumia maneno yanayolenga upande mmoja wa vijana na upande wa wazee wanashindwa kabisa kuyaelewa baadhi ya maneno yanayotumiwa katika vyombo hivyo.

‘’Kuna habari ambazo ukizisoma zinakuwa haziko katika mtiririko mzuri na unaoeleweka , sisi Baraza la Kiswahili la Taifa kazi yetu kubwa ni kuhakikisha jamii ya watanzania wengi wanatumia lugha ya kiswahili vizuri na vyombo vya habari vinakuwa makini kwenye matumizi ya hiyo, si kutumia maneno yanayoibuka kama lugha sahihi"alisema.

Alisema kuwa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ambayo yanatarajia kufanyika Novemba mwaka huu yatalenga kuwaelimisha kuandika na kutumia lugha fasaha , maadili na matumizi ya lugha kwa mujibu wa watu wa rika tofauti.

"Vile vile yatalenga kuonyesha matatizo ya kisarufi kwa vyombo vingi vya habari , makosa ya mara kwa mara katika vyombo vya habari, na dhima ya vyombo vya habari katika ukuzaji wa lugha"alisema.

Aidha Bw, Mbigili alisema BAKITA imekuwa ikitoa tuzo mara kwa mara kwa vyombo vya habari vinavyoandika habari kwa kutumia lugha ya kiswahili fasaha.

Kanisa lapania maendeleo Kisarawe

Na Josephs Sabinus

WAKATI Kardinali Pengo, amepania kuinua parokia zilizo nyuma kimaendeleo, Novemba 18, 2001, Askofu Method Kilaini wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, atazindua mchango kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kisarawe.

Kwa mujibu wa Mhashamu Kilaini ambaye ni Askofu Msaidizi wa Jimbo, uzinduzi wa mchango huo katika Parokia Katoliki ya Kisarawe jimboni humo, ni sehemu ya mpango wa Kardinali Pengo ambaye ni Askofu Mkuu, kuendeleza parokia zote jimboni kwake kimwili na kiroho.

Katika mazungumzo na KIONGOZI mwishoni mwa juma, Mhashamu Kilaini alisema kuwa, Kanisa limepania kuwahudumia watu wa maeneo hayo kimwili na kiroho na tayari baadhi ya masista wamekwisha kwenda Kisarawe kwa ajili ya huduma. Alisema, tayari masista wa KOLTOLENGO wa Italia, wamekwisha anzisha konventi pamoja na shule ya awali kwa ajili ya watoto wa eneo hilo.

"Licha ya masista wa Mtakatifu Tereza kuwa huko kwa shughuli za maendeleo na miradi ya kiafya, upo mpango wa kuwaleta masista wengine kutoka Musoma na Sumbawanga ili kuchangia kufanikiwa kwa lengo hilo," alisema.

Mhashamu Kilaini alitoa wito kwa waamini na wakazi wote wa Kisarawe kujitoa kuchangia na kulisaidia kanisa katika juhudi zake kuleta maendeleo katika eneo lao.

Alifafanua kuwa, huduma zitakazotolewa na Kanisa zikiwamo za elimu na afya, hazitakuwa na ubaguzi wa wowote na hivyo, ni jukumu la wakazi wote kujitolea kufanikisha na hatimaye kunufaika na mpango huo wa Kanisa.

Alizitaja baadhi ya parokia ambazo Kardinali Pengo amenuia kuzinyanyua kimaendeleo kuwa ni pamoja na Kisarawe, Mlandizi, Mkuranga, Kilimahewa na Mafia.

Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki (Caritas-Tanzania), limekuwa likijitahidi kuinua hali za wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa misaada na mikopo kwa vikundi vya akinamama na kuwasaidia wenye shida mbalimbali.

Waamini na wote wenye mapenzi mema, hawana budi kuunga mkono kwa hali na mali juhudi za Kanisa katika kuinua hali za watu kimwili na kiroho.

Vyuo vya uandishi vyaambiwa visitegemee ada kujiendesha

 

Na Neema Dawson

WAMILIKI wa vyuo wametakiwa kutotegemea ada za wanafunzi na badala yake, waunde mfuko maalumu kuwasaidia wanafunzi wasio weza kulipa ada.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Hanzuruni Mungula, wakati wa mahafari ya kwanza ya wahitimu wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha TIME lichopo jijini Dar es Salaam yaliyofanyika katika ukumbi wa Msimbazi Center.

Katika mahafari hayo ambayo wahitimu 92 walihitimu mafunzo, naibu Meya hyo alisema, kuzorota kwa elimu ya vyuo mbalimbali nchini, kunatokana na vyuo hivyo kutegemea ada za wanafunzi pekee kama vyanzo vya mapato yake.

Alisema hali hiyo, inachangia gharama kuwa kubwa katika kujiunga na vyuo hivyo.

Alibainisha kuwa, gharama zinapokuwa juu, vijana wengi hushindwa kujiunga na vyuo hivyo hata kama wana sifa na vipaji vya kuendelezwa katika fani husika.

Alisema kuwa ubora wa chuo upo ndani ya ufanisi wa kazi za wahitimu na huonekana wahitimu hao wanapoanza kuyaonesha matunda yao mbele ya jamii inayowazunguka.

Aidha Mstahiki Meya huyo aliwataka wazazi kuwa macho na kujifunza kuuliza umri wa vyuo wanapoona matangazo yanayoeleza kuomba wanafunzi kujiunga na kozi mbalimbali za vyuo hivyo .

‘’Chuo kama kweli kinatoa elimu, ujuzi na maarifa kuhusu taaluma ya uandishi; na kama kweli wanafunzi wake walisoma na sio kupita tu na kugawiwa vyeti, wahitimu wake watakuwa ni tangazo tosha kwa jamii", alisema. Aidha, aliwahimiza wahitimu kujenga utamaduni wa kutembelea vijijini ili kukusanya habari mbalimbali za kijamii badala ya kuishia mijini pekee. Alisema, watu waishio vijijini wanahitaji msaada toka kwa wanahabari hivyo, ni wajibu wa wanahabari hao kuwa karibu na vijiji.

Naye Mlezi wa chuo hicho , Bw. Idd Simba, alisema chuo kina upungufu wa majengo kama maktaba, vifaa kama mashine za uchapaji, mashine za kisasa za usafishaji na uchapaji wa picha.

Alisema matatizo mengine yanayokikabili chuo hicho ni pamoja na ukosefu wa studio kwa ajili ya mafunzo ya utangazaji wa redio na Televisheni. ambavyo ni muhimu kwa chuo chochote cha uandishi wa habari .

Alitoa wito kwa wazazi na watu binafsi kujitokeza kukifadhili chuo hicho ili kuondoa mapungufu hayo badala ya kukaa kimya kusubiri wafadhili kutoka nje ya nchi.