Make your own free website on Tripod.com

Wazazi watahadharishwa kuwa makini na shule za Kimataifa

l Baadhi zadaiwa kuweka maslahi ya pesa mbele kuliko ubora wa elimu

Na. Dalphina Rubyema

WAZAZI nchini wametakiwa kuwa makini na shule za Kimataifa ambazo zinaonekana kuwa nyingi nchini kwani baadhi yake zinatoza ada kubwa ambapo elimu inayotolewa haina viwango vya Kimataifa.

Kauli hiyo ilitolewa Jumamosi iliyopita na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati alipokuwa akibariki majengo mapya ya shule ya Kimataifa ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu iliyopo Ukonga Jimboni humo.

Mwadhama Kardinali Pengo ambaye alikuwa akitoa nasaha zake mbele ya wageni waalikwa, wazazi, wafanyakazi wa shule hiyo ambayo ipo chini ya Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Jimbo Katoliki la Bukoba, alisema kuwa kinachotakiwa kufanywa na wamiliki wa shule hizo ni kujali ubora wa elimu badala ya kuweka mbele suala la pesa.

"Pamoja na hatua iliyopiga Taifa ya kuwa na shule nyingi za 'International' na nyingi zaidi zikiwa hapa Dar-Es-Salaam cha ajabu ni kwamba elimu inayotolewa katika baadhi ya shule hizo,siyo ya Kimataifa" alisema Mwadhama.

Alitoa mfano kuwa kuna baadhi ya shule zinazotoza karo ya shilingi 700,000 kwa mwaka kwa wanafunzi wa chekechea na shilingi 1,400,000 kwa wanafunzi wa shule ya Msingi lakini pamoja na ukubwa wa karo bado unakuta matokeo ya mtihani kwa shule hizi yapo nyuma kuliko hata shule za kawaida.

Vile vile Mwadhama Pengo aliendelea kutoa masikitiko yake kwa baadhi ya wazazi wanaowapeleka watoto wao nje ya nchi kwa ajili ya kupata elimu na kukimbia ile inayotolewa nchini.

" Kilio changu bado kipo pale pale, ni kitendo cha baadhi ya Watanzania kuchukua watoto wadogo kwenda kupata masomo nje ya nchi, kwa kudhania pengine huko ndiko wanakopata elimu nzuri zaidi kitu ambacho hakina ukweli ndani yake" alisema.

Alisema kufanya hivyo ni kuwanyima watoto hao uhuru na haki ya kujifunza utamaduni na mazingira ya nchi yao na badala yake wanajifunza na kuiga tamaduni za wengine.

"Si kwamba pengine nawaonea wivu watoto hao maana pengine kuna watu wanaosema mbona hata mimi nimeweza kusoma nje ya nchi, muelewe kuwa mtoto umri wake ni mdogo anatakiwa kwanza ajifunze mambo mbalimbali ya nchi yake"alisisitiza Mwadhama.

Kwa upande wa shule hiyo ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu ,Mwadhama aliwataka wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni hapo kuwa karibu kwa kufuatilia maendeleo ya shule na wanafunzi kwa ujumla.

"Shule hii pamoja na kuongozwa na Watawa lakini wazazi mpo ndani ya kamati, hivyo ni wajibu wenu kuangalia na kufuatilia maendeleo ya shule yenu, endapo matokeo ya mtihani hayatakuwa ya kuridhisha, lawama wasitupiwe watawa peke yao wala mimi na badala yake tulaumiwe sote" alisema Mwadhama.

Vile vile Mwadhama Pengo ametoa tahadhari kwa uongozi wa shule hiyo kuwa makini na watu, makampuni na mashirika na wafadhili kwani baadhi yao wanaweza kutaka kuendesha shule hiyo kadiri ya matakwa yao.

"Tusiruhusu kutafuta wafadhili ambao wanaweza kuifanya tuiuze shule yetu na utamaduni wetu, ni bora tuendeshe shule yetu kwa umasikini tulio nao kuliko kuwa na wafadhili ambao watatuwekea sheria ambazo ni kinyume na malengo yetu na utamaduni wetu" alionya Mwadhama.

Kwa mujibu wa maelezo toka kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Sr. Perpetua Muhana, majengo mapya yaliyobarikiwa na mwadhama kwa siku hiyo ni pamoja na madarasa matano na ofisi mbili ambapo gharama yake ni sh. 27,339,363/50 ambazo zimefadhiliwa na wafadhili kutoka ndani na nje ya nchi.

Shule hiyo kwa hivi sasa ina wafanfunzi wa kuanzia chekechea hadi darasa la pili na karo kwa upande wa chekechea ni shilingi 310,000 kwa mwanafunzi anayeanza shilingi 175,000 kwa yule anaye endelea na chekechea ambapo kwa upande wa shule ya msingi kama mwanafunzi alisomea pale chekechea, atatakiwa kulipa shilingi 220,000 kwa mwaka na kama ametokea nje ya pale (fresh) karo ni shilingi 350,000 kwa mwaka.

"Unajua kuna hatua tatu za wanafunzi wa chekechea,kuna wale watoto wadogo sana wenye miaka mine,hao wana darasa lao na karo yao ni shilingi 310,000 kwa mwaka. huyu kabla hajaingia darasa la kwanza, kulingana na umri wake mzazi akikubali ni lazima apitie hatua ya pili na hatimaye ya kwanza ,katika hatua hizi mbili za mwisho,karo inapungua na kuwa sh.220,000 kwa kila hatua"alisema.

Askofu aponda utabiri wa Nyota

l Adai ni mtazamo wa fikra za wanadamu

l Wanaozisoma na kuzifuata wadaiwa kuwa wafuasi wa shetani

Na Ndechongio Charles, Morogoro

WAAMINI wa madhehebu ya Kikristo mkoani Morogoro wameaswa kuacha kuishi kwa kutegemea utabiri wa nyota ambao huchapwa kwenye magazeti mbalimbali kwani ni kinyume cha maadili ya ukristo pia maandiko matakatifu ya Mungu.

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro aliitoa wito huo hivi karibuni katika mahubiri yake kwenye moja ya ibada za Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Patris mjini hapa.

Askofu Mkude alisema wakristo hawapaswi kabisa kuwa wasomaji wa nyota kwenye magazeti kwani kwa kufanya hivyo wanamaanisha kuacha kumtegemeda Mungu na badala yake kuongozwa na wanadamu kwa njia ya nyota.

"Usomaji wa nyota unamaanisha mwanadamu kumwacha Mungu na kumfuata shetani hivyo huwezi kujiita mkristo huku ukiendelea kukiuka misingi ya ukristo kwa kuendesha maisha yako ukiongozwa na nyota" alisema Askofu huyo.

Alisema wakristo wanapaswa kufahamu kuwa nyota wanazozisoma ni mtazamo wa fikra za wanadamu kama walivyo wao, hivyo si sahihi kutegemea utabiri huo.

"Maandiko Matakatifuya Biblia ya Mungu yanatukataza kuwategemea wanadamu sasa iweje leo wewe Mkristo utegemee nyota?" alihoji Askofu huyo kwa mshangao.

Askofu Mkude alisema nyakati za sasa ni nzuri na muafaka kwa wanadamu kujenga mahusiano bora na Mungu kwa kumtegemea badala ya kushinda wakisoma nyota magazetini ambazo hazina msaada wowote kimaisha.

Hata hivyo Askofu Mkude alisema wakristo kama wanadamu wengine wasome magazeti kwa maana ya kupata habari muhimu za kijamii na kujielimisha lakini si vyema wakayageuza kuwa vitabu vya ibada kwa kutafuta nyota.

Kuhusu uadilifu kazini Askofu huyo aliwataka wakristo kuwa waaminifu kama njia mojawapo ya kujenga imani kwa wananchi na jamii pia kuwa kielelezo bora katika utumishi na wachungaji wa maandiko ya Mungu.

Usomaji wa nyota katika magazeti kwa lengo la kufahamu mwelekeo wa shughuli za siku nzima limekuwa jambo la kawaida katika sehemu kubwa ya jamii ya watanzania wakiwemo waumin wa madhehebu ya kikristo kinyume na maandiko ya Biblia.

Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam kuanzisha shule ya kisasa

l Ni kumbukumbu ya Jubilei Kuu

Na Getrude Madembwe

ILI kuweka kumbukumbu ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limeamua kuanzisha shule ya Msingi itakayoitwa MILLENIUM PRIMARY SCHOOL.

Akizungumza na gezeti hili katikati ya juma ,Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya shule hiyo Padre Brian Mkude alisema kuwa shule hiyo itakuwa katika majengo ya zamani ya Mtakatifu Yosefu ambapo hapo awali ilikuwepo shule ya msingi ya Forodhani.

Padre Mkude alisema kuwa wazo la kujenga shule hiyo ilitokanana na vuguvugu la Jubilei Kuu hiyo hasa baada ya kila jimbo kutakiwa liwe na ukumbusho wa Jubilei Kuu ya mwaka 2000.

Padre Mkude ambaye ni Mkurugenzi wa Utume wa Walei Jimbo Kuu La Dar-Es-Salaam,alisema kuwa awali jimbo lake lilifikiria kujenga hospitali kama kumbukumbu ya Jubilei hiyo lakini uamzi huo haukutekelezwa kwa kuhofia kuchuku muda mrefu.

"Kwanza tulifikiri kujenga hospitali lakini tuliona kuwa hospitali ingechukua muda mrefu hivyo tukaona tujenga shule. kwa vile sehemu hiyo hapo mwanzo ilikuwa imechukuliwa na Serikali na sasa imerudishwa mikononi mwa kanisa hivyo tukaamua kuyakarabati majengo hayo" alisema.

Hata hivyo Padre Mkude alisema kuwa ukarabati huo bado haujaanza ila wanatarajia kuanza Julai mwaka huu .

Aliendelea kueleza kuwa hadi ukarabati huo kumalizika utagharimu kiasi cha shilingi milioni 12.

Aidha Padre Mkude alisema kuwa pesa hizo za ukarabati zitatokana na michango ya waamini. Kutakuwepo na matembezi ya hiari ya kuchangia pesa hizo ambayo yataanzia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu na yataongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo,Mwadhama Kardinali Pengo

Matembezi hayo ambayo yataishia kwenye kituo cha Msimbazi na kupokewa na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Luigi Pezzuto mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Padre Mkude ambaye pia ni Paroko wa parokia ya Kibangu alisema kuwa katika shule hiyo ambayo inatarajiwa kuanza mwakani itawahusisha watoto wa madhehebu mbalimbali na kila darasa litakuwa na wanafunzi 24.

"Elimu itakayotolewa itakuwa ya kisasa pia somo la kompyuta litakuwepo na hii itapunguza wimbi la watoto wadogo kupelekwa nje ya nchi kama vile Kenya, Uganda na kwingineko ambako hujifunza tamaduni za watu wa huko", alisema Padre Mkude.

Mbezi Beach yaipiga 'jeki' Bagamoyo

Na Bilhah Massaro

KIGANGO cha Mwenye Heri Maria de Mattias cha Mbezi beach kilichopo katika Parokia ya Mtongani Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam. kimetoa msaada wa vitu mbalimbali zikiwemo nguo na viatu kwa ajili ya waamini wa parokia ya Bagamoyo jimboni Morogoro.

Akizungumza na KIONGOZI katikati ya wiki,kigangoni hapo Katekista,Marino Mafunde wa Kigango hicho alisema kuwa misaada hiyo imetolewa baada ya kupokea maombi ya kusaidiwa kutoka kwenye parokia hiyo ya Bagamoyo.

baada ya kupokea ombi hilo,uongozi wa kigango ulitoa matangazo kwa waamini wake

"Tuliletewa ombi kutoka katika Parokia ya Bagamoyo ambayo ilituomba tuwachangie vifaa hivyo, nasi tukawatangazia waamini wetu kwa majuma mawili mfululizo na wao wameamua kutuletea vitu hivyo kama unavyoviona" alisema Katekista huyo huku akionyesha nguo pamoja na viatu ambavyo vilikuwa vimetolewa na waamini hao.

Alisema kuwa katika kanisa la Bagamoyo waamini ni wachache ingawa ndiko Ukristo ulikoanzia na waamini ambao huhudhuria misa huwa ni wachache.

"Ingawa Ukristo ulianza huko bado waamini ni wachache na matoleo yao hayazidi shilingi 50,000 hivyo bado ni changa na pia imezungukwa na Waislamu" alisema.

Aidha alisema michango hiyo bado haijawasilishwa katika parokia ya Bagamoyo kwa sababu wanafanya mipango ya kuwasiliana.

Wakati huo huo: Jumla ya shilingi 80,000/= zimetolewa na jumuiya ndogo ndogo nane za Parokia ya Mtongani kwa ajili ya kuwasaidia wakoma.

Katekista Marino Mafunde wa Kigango cha Maria de Mattias alisema kila jumuiya moja ilitakiwa kutoa shilingi 10,000 na zipo jumuiya 8 ambapo pesa hizo zitatumika kununua chakula na dawa kwa ajili ya kituo cha wakoma kilichopo Kigamboni.

Parokia ya Mavurunza kufanya uchaguzi mwezi ujao

Na Ferdinand Ngowi

PAROKIA mpya ya Mavurunza Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam imetangaza kufanyika kwa uchaguzi wa kamati tendaji kwa vigango vyake vinne mapema mwezi ujao ili kuruhusu uchanguzi wa kamati tendaji kamili ya Parokia kufanyika.

Akizungumza katika kikao cha viongozi wa Jumuiya ndogondogo za parokia hiyo kilichofanyika kanisani hapo Jumapili iliyopita,Makamu Mwenyekiti wa muda wa parokia Severine Ndunguru alisema vigango vyote vinne vya parokia vinatakiwa viwe vimekwishafanya uchunguzi wa viongozi wao kabla ya Julai mwaka huu.

"Tunatarajia kufanya uchaguzi wa parokia tarehe 29 Julai hivyo ni vizuri kama vigango vitakuwa vimemaliza zoezi hili kabla ya tarehe hiyo" alisema.

Hivyo Juni uwe mwezi wa uchaguzi wa vigango vyote.

Kikao hicho cha viongozi wa jumuiya kilichokuwa na Agenda tatu pia kilimshirikisha Paroko wa kwanza kwa parokia hiyo Padre Faustin Mlelwa ambaye pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la utoaji sadaka kanisani.

Padre Mlelwa alisema mtu anayetoa sadaka atoe kile kitu ambacho anasikia kinamgusa moyoni.

"Toa kitu kinachokugusa lakini usitoe chote ulichonacho ukalaza watoto njaa, utakuwa umetenda dhambi kama watoto watalala njaa" alisema.

Parokia ya Mavurunza ni parokia mpya ambayo awali ilikuwa kigango cha parokia ya Msewe iliyopo Ubungo.

Parokia hiyo ambayo ilizinduliwa rasmi Januari 6 mwaka huu na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam Mwadhama Polycarp Pengo, ina vigango vinne kikiwemo kigango cha Mavurunza ,Nzasa, Matosa na Temboni kwa Msuguri.

Sikukuu ya mavuno yaingizia parokia mamilioni ya fedha

Na Vick Peter

PAROKIA ya Mtakatifu Camilius Yombo iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam imekusanya jumla ya shilingi 2,445,550 wakati wa sikukuu ya mavuno iliyofanyika hivi karibuni parokiani hapo.

Akizungumza kwenye ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika Jumapili iliyopita kanisani hapo Padre Camilius Neuray alisema kuwa pesa hiyo imetokana na michango mbalimbali iliyotolewa na waamini wa parokia hiyo ikiwemo makusanyo ya bahasha na mauzo ya mazao mbalimbali.

Padre Camilius ambaye ni Paroko wa Parokia hiyo,alisema pesa hiyo itaisaidia kuendeleza parokia katika nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma za kiroho badala ya kuendelea kutegemea msaada toka nje.

Paroko huyo vile vile amewataka waamini wa Kigango cha Mtakatifu Karoli Lwanga Yombo Dovya ambacho kipo chini ya parokia hiyo kujitokeza kwa wingi wakati wa sikukuu za mavuno kwa kigango hicho itakayofanyika siku ya Pentekoste hapo Juni 3 mwaka huu.

Alisema michango itakayopatikana siku hiyo itatumika kuendeleza kigango hicho ikiwa ni pamoja na kutoa kiasi cha pesa kwa ajili ya kuwapa posho walimu wa dini wanaotoa huduma ya elimu ya dini katika shule zilizomo kwenye kigango hicho.

Wakati huo huo: wakristo kote nchini wametakiwa kufahamu kuwa njia ya pekee ya mtu kuishi ndani na nje ya nchi bila usumbufu,ni kuwa na alama ya upendo.

Katika mahubiri yake jumapili hiyo, Padre Camilius alisema kuwa kwa kuwa na alama hiyo ya upendo mtu anaweza kuishi mahali popote anapotaka bila kusumbuliwa.

"Mtu anapotafuta kitambulisho cha nchi isiyo ya kwake ataulizwa ni alama gani aliyonayo inayo mtofautisha na mtu mwingine na swali hili huulizwa pale pale anapokuwa anajaza fomu, vivyo hivyo Mkristo unatakiwa uwe na alama ya kukutofautisha na wengine na alama hiyo ni "upendo" alisema Padre Camilius.

Mwinjilisti akerwa walevi kuimba nyimbo za dini

Na Elizabeth Steven

MWINJILISTI Mwipile Ismail wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Tabata ameeleza kuwa anakerwa na tabia za watu kulewa pombe na kuanza kuimba nyimbo za dini.

Mwinjilisti Mwipile alieleza kukerwa kwake na tabia hiyo wakati wa ibada ya Jumapili iliyopita iliyofanyika katika usharika huo.

Alisema bila kujali mazingira halisi, watu wanapokuwa kwenye majumba ya starehe wanapokunywa pombe na kuwakolea, huanza kuimba nyimbo za dini.

"Hakuna kitu kinachonikera na kunisikitisha kama kundi la watu ama mtu mmoja kulewa pombe na kuanza kuimba nyimbo za dini ,mbaya zaidi wanaimba kwenye vilabu! kwa nini wasiimbe nyimbo zingine ambazo zinaendana na maeneo hayo?" alihoji.

Alisema kuwa tabia kama hiyo haifai katika jamii hasa kwa Wakristo ambao mara nyingi nyimbo zao zimekuwa zikiimbwa na walio wengi.

Aidha Mwinjilisti Mwipile aliwataka waamini wa kanisa hilo kuacha tabia ya kupenda kuiga mambo wasiyoyajua hasa pale weanapoona mtu ama kundi fulani linafanya kitu .

Aliwataka wawe makini katika kuchunguza na kuelewa kwa undani zaidi mambo hayo wasije wakaangukia sehemu mbaya.

"Napenda kuwatahadharisha washirika wenzangu wa Usharika huu, msipende kuiga mambo mnayoyaona yakitendwa katika jamii ,nawatahadharisha sana kuwa makini na watu hawa wanaojiita walokole usimuone mlokole kafanikiwa jambo fulani ukamuiga ,ujue utapotea".

Wakati huo huo: Mwinjilisti huyo amewataka waamini wa usharika huo kujiunga katika vikundi vya kwaya ili waweze kumwimbia bwana na kwa kufanya hivyo matatizo mbalimbali yanayowapata katika familia zao yataweza kuondoka na kama si hivyo basi yatapungua zaidi.

Watanzania watakiwa kupambana na madawa ya kulevya

Na Joicye Joliga,TIME

PADRE Benedikti Shayo wa Kanisa Katoliki ya Msimbazi Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam,amewashauri Watanzani kutafuta mbinu mbalimbali za kupambana na kutokomeza madawa ya kulevya badala ya kuendelea kuyatumia.

Padre Shayo alito ushauri huo ofisini kwake katikati ya wiki wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili

Alisema Watanzania ni lazima wakubali kuwa madawa ya kulevya ni tatizo la nchi nzima na linasababishwa na jamii yenyewe hivyo halina budi kuvaliwa njuga..

Alisema serikali haina budi kuwaelimisha wananchi wake kuhusu madhara ya kutumia madawa hayo ya kulevya na pia wananchi wenyewe wakubali kubadili tabia ya utumiaji wa madawa haya.

Wapinzani kuunda chama kimoja ni kuwapa nafasi wahujumu - Sendoro

Na Gabriel Mduma

ILI kukomaza nguvu ya upinzani nchini,imependekezwa vyama vya upinzani nchini kuungana na kuunda vyama vipatavyo vinne badala ya kuunda chama kimoja kama wengi wanavyopendekeza.

Pendekezo hilo lilitolewa na Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani ,Elinaza Sendoro wakati akizungumza na gazeti hili katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam alikokuwa akishiriki mkutano wa tisa wa kujadili hali ya kisiasa nchini ambao uliandaliwa na Mpango wa Utafiti wa Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) uliomalizika hivi karibuni chuoni hapo.

Alisema kama vyama hivyo vitaungana na kuunda chama kimoja tu nguvu ya upinzani itakufa Tanzania kwani baadhi ya viongozi wenye uchu wa madaraka watakuwa wamejipatia nafasi ya kuhujumu.

"Kama ni muungano wa upinzani basi usiwe wa kuwa na chama kimoja heri kwa kuupa nguvu kubwa upinzani, vyama vya upinzani viungane na kuwa walau vinne kuliko wanavyong’ang’ania kimoja" alisema.

Hata hivyo Askofu huyo Mstaafu alikiri kuwa utitiri wa vyama unadumaza nguvu ya upinzani.

"Kila kukicha unasikia kuna chma kipya kimesajiliwa ama kinatafuta usajili,kwakweli utitiri wa vyama nao si mzuri unadumaza upinzani,ndiyo maaana napendekeza viundwe vyama vinne tu"alisema Askofu Sendoro.

Wakati huo huo,Watafiti wa masuala ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu Cha Dar-es-Salaam wanaendelea na utafiti wa kuangalia jinsi gani taasisi za kidini zinaweza kuendeleza ama kurudisha nyuma harakati za demokrasia nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na REDET ,hadi Aprili mwaka huu ,asilimia 80 ya utafiti huo tayari ilishafanyika ambapo jumla ya maswali 3,380 yamesambazwa kwa viongozi wa kidini Bara la Visiwani.

Taarifa hiyo ya REDET ilisema kuwa maswali hayo yaliyoulizwa kwa viongozi hao wa dini yalilenga juu ya masuala ya kidini,elimu na ajira jinsi vinavyohusiana na mambo ya kisiasa.

Walei kuadhimisha siku ya Mwenye heri Bakanja

Na Mwandishi Wetu

MHASHAMU Askofu Venance Koda ambaye ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ataongoza Misa Takatifu katika kuadhimisha siku ya kutangazwa Isdore Bakanja kuwa Mwenye Heri ambaye ni Msimamizi wa Kituo cha Walei Katoliki kinachoendelea kujengwa.

Taarifa iliyotolewa na Menejimenti ya Kituo hicho kinachojulikana kwa jina la Bakanja TEC Laity Centre na kuthibitishwa na Ofisi ya Idara ya Utume wa Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania inasema kuwa maadhimisho hayo ambayo kituo hicho kinayaadhimisha kwa mara ya kwanza ,yatafanyika Mei 26 mwaka huu katika eneo la Ukonga Sitakishari Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam ambapo kituo hicho kinajengwa.

Lengo la Misa hiyo maalum mbali na kuombea amani uchaguzi wa viongozi wa Walei majimboni na kitaifa na kusali kwa ajili ya utekelezaji wa dhamira ya utendaji utume wa Walei mwaka huu vile vile ni kukabidhi shughuli ambazo zinaendelea kufanyika katika kituo hicho chini ya usimamizi wa Mwenye Heri Bakanja.

Mkristo Mlei Isdore Bakanja ,alizaliwa mwaka 1885 katika nchi ya Zaire (sasa Jamhuri ya Congo),alitangazwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mwenye Heri Aprili 25 mwaka 1994.

Katika ujana wake Mwenye Heri Bakanja alikuwa ni shahidi wa kweli wa imani ,mtenda kazi hodari,mtiifu na mwenye usafi wa moyo.

Halmashauri ya Walei Katoliki Tanzania kwa kuzingatia mchango wa pekee kiimani wa Mwenye Heri Bakanja katika kanisa Afrika na hasa ushuhuda wa maisha yake ya kueneza habari njema,walimpendekeza awe Msimamizi wa kituo hicho wazo ambalo lilikubaliwa na Maaskofu Katoliki wa Tanzania.

Kituo hicho cha Bakanja ambacho hadi sasa ujenzi wake unaendelea kwa kasi, kitakapokamilika kinatarajiwa kuwa mahali ambapo shughuli za Utume wa Walei kitaifa hasa Halmashauri Walei na vyama vya kitume zitaratibishwa. mafungo, kozi fupi ,semima na warsha kwa Walei na watu mbalimbali zitatolewa.

Aidha kituo hicho kitatoa nafasi kufanyika shughuli za maendeleo ya kanisa na jamii na kwa watu wote wenye mapenzi mema pia zitakuwepo kumbi za mikutano na matukio mengine kama sherehe na burudani huduma za chakula na malezi.

KKKT yaipongeza Serikali kwa kufuta daraja la nne

Na Elizabeth Steven

KANISA la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT) limeipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kutowapatia vyeti wanafunzi wa shule za sekondari wanapopata daraja la nne katika mitihani yao ya mwisho.

Pongezi hizo zimetolewa na Mchungaji Mika Kitale wa kanisa hilo Usharika wa Buguruni Jimbo la Ilala wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake katikati ya wiki.

Alisema uamzi huo hauna nia mbaya bali utapandisha kiwango cha elimu ya Tanzania ambayo inaelekea kushuka chini ya kiwango.

"Uamzi wa Serikali wa kutowapa wanafunzi vyeti wanapopata daraja la nne katika mitihani yao ya kumaliza elimu ya Sekondari mimi nauunga mkono na pengine nia si mbaya bali inataka kupandisha kiwango cha elimu nchini kwa kiasi fulani "alisema.

Mchungaji Kitale vile vile amewataka vijana kuondokana na dhana potofu ya kufikiri kuwa elimu ni kupata cheti na kusahau kuwa elimu ni njia mojawapo itakayowawezesha kuyamudu mazingira yanayowazunguka katika maisha yao ya baadaye.

Amewataka wanafunzi wote kuongeza bidii katika masomo yao kuepuka makundi, marafiki na mazingira ambayo yanaweza kuwashawishi kufanya mambo ambayo hayana faida kwao.

"Vijana waaache ugoigoi wa elimu ,wayaepuke makundi , marafiki na mazingira ambayo yanaweza kuwashawishi kufanya mambo ya ajabu ikiwa ni pamoja na ulevi, uvutaji bangi, pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya"alisema.

Serikali imefuta daraja la nne kwa wanafunzi wanaomaliza elimu yao ya sekondari na zoezi hili litaanza kutekelezwa mwaka kesho ambapo wanafunzi watakaomaliza kidato cha nne mwaka huu ndiyo watakuwa wa kwanza kukumbwa na balaa hilo.

Mamia wafurika kuusindikiza mwili wa Meneja wa Kituo cha Msimbazi

Na. Tom Chilala

MAMIA ya watu kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam ,walifurika katika makaburi ya Msimbazi kuusindikiza kwenye makao ya milele mwili wa aliyekuwa Meneja wa kituo cha Msimbazi. Bw. Charles Samson Beatus Lyamba.

Marehehmu Lyamba alizaliwa Desemba 26,1950 mkoani Tabora, na alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Kikatoliki Arusha mwaka 1957.

Hata hivyo alihamia katika shule ya Msingi Chumbageni Tanga ambapo alihitimu mwaka 1964

Mwaka mmoja baadaye (1965) alijiunga na Seminari ndogo ya Itaga, Tabora mwaka 1972 alihitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Pugu iliyopo nje kidogo ya jiji la Dar-es-salaam.

Alipata Shahada yake ya kwanza juu ya masuala ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya ambayo alihitimu mwaka 1974.

Baadaye alibadilisha fani yake na kujiunga na masuala ya Mawasiliano ya Anga na hatimaye akateuliwa kuwa Mwongozaji wa Usalama wa Anga (Air traffic controller) ambapo alifanya kazi hiyo kwa muda mrefu. baadaye akajiunga na kituo cha Msimbazi mpaka kifo kilipomfika saa 8 usiku Jumapili Mei 13 mwaka huu.

Marehemu ameacha watoto wane.

Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi Amina.

Wanaotumia watoto kufanya uhalifu kukiona-Wizara

Na Neema Dawson

MKURUGENZI wa Maendeleo ya Jinsia katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii Wanawake na Watoto, Bi. Edine Mangesho amesema kitengo chake kwa kushirikiana na Wizara nyingine za serikali,kitawachukulia hatua kali wazazi na walezi watakaobainika kuwatumia watoto wao kufanya vitendo vya uhalifu

Bi Mangesho alitoa kauli jijini Dar-Es-Salaam katika mahojiano na gazeti hili liliotaka kufahamu hatua ambazo kitengo chake kitawachukulia watzazi wanaotumia watoto wao katika masuala ya uhalifu.

Hivi sasa kuna uvumi kuwa kumekuwepo na baadhi ya wazazi ambao wanawatuma watoto wao kufanya vitendo vya uhalifu kama ujambazi ambapo baadhi ya watoto hukabidhiwa kwa majambazi sugu na pato linalopatika watoto hao hulikabidhi kwa wazazi wao.

Mkurugenzi huyo alikiri kuwa tetesi hizo ni za ukweli ambapo alisema kundi linalo husika zaidi ni lile la watoto yatima ambao wanakaa na walezi wao.

"Tumeishayasikia malalamiko mengi ya namna hiyo ambayo tunayapata kutoka kwa wazazi walio na upendo na huruma kwa watoto wao kuhusiana na vitendo vya baadhi ya wazazi au walezi wanaowalea watoto walio yatima kuwatumia watoto hao kama vitega uchumi kwa kuwaingizia kipato na tunashirikiana na Wizara nyingine kuweza kuwafuatilia kwa undani zaidi na kuwakamata ili tuweze kuwachukulia hatua kali za kisheria" alisema.

Vile vile Mkurugenzi huyo ameitaka jamii ielewe kuwa zipo sheria ambazo zinaweza kuwabana wazazi na walezi wanaofanya watoto vitendo vya kinyama na vya kulidhalilisha taifa na jamii nzima.

"Katika makundi ya majambazi wapo pia hata watoto ambao wanajihusisha na ujambazi, kwa kutumiwa na majambazi Sugu na baadaye kupewa ujira kidogo kutokana na mapato wanayoyapata"alisema

Aliongeza "nasisitiza kuwa wazazi na walezi ambao wanashindwa kuwapeleka watoto wao shule pindi wanapofikia umri wa kufanya hivyo na badala yake kuwatumia kufanya vitendo visivyofaa,watachukuliwa hatua kali za kisheria hivyo ni bora waache tabia hiyo mara moja".

Imani potofu chanzo cha kumsahau Mungu-Mchungaji

Na Magreth Charles, Time

IMEELEZWA kuwa miongoni mwa mambo yanayomfanya mwanadamu amsahau Mungu na kufuata mambo ya kidunia ni imani potofu hali inayo mchanganya mwanadamu huyo.

Hayo yalisemwa mwanzoni mwa wiki na Mchungaji Grace Mbise wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani,(KKKT) Dayosisi ya Mashariki - Arusha wakati akihubiri katika mkutano wa Injili unaoendelea kwenye viwanja vya Kanisa la KKKT - Kinondoni jijini Dar-Es-Salaam.

Katika kuondokana na hali hii,Mchungaji huyo ameishauri jamii kumrudia Mungu na kuachana na tamaa za kidunia ambazo mwisho wake ni kuingia katika moto wa milele.

"Sisi duniani tu wapitaji makao yetu ni mbinguni, tugeuke sasa tumrudie Mungu na tuachane na uovu wa duniani" alisema.

Alisema binadamu amejisahau hata kumpita ng’ombe na punda. wanyama wanakumbuka kurudi kwenye makazi yao.

"Binadamu amejisahau hajui kwake,anawazia ataishi duniani milele,anapitwa hata na ng’ombe na punda wanaojua vibanda vya bwana wao ,kwanini binadamu naye asigeuke sasa na kutende mema?"Alihoji Mchungaji huyo.

Aliwakumbusha wanadamu wakumbuke kuwa Mungu hana ubaguzi, haangalii sura ya mtu, dini wala madhehebu bali humjali yeyote anayelitii jina lake.