Make your own free website on Tripod.com

Msitumie uhuru kujitafuna wenyewe - Askofu

Na Leocardia Moswery

"...Tunaishi katika ulimwengu wa kujitafuta na kujitafuna; pia, kwa kukumbatia yenye kutishia maisha na hasa, ya wale ambao hawajazaliwa bado na kukatisha kuishi pale mtu anapochoka na uwepo wake hapa duniani,"

"...Tunaishi katika ulimwengu wa kujitafuta na kujitafuna; pia, kwa kukumbatia yenye kutishia maisha na hasa, ya wale ambao hawajazaliwa bado na kukatisha kuishi pale mtu anapochoka na uwepo wake hapa duniani,"

Hayo yalisemwa hivi karibuni jijini Dar-Es-Salaam, wakati Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Mhashamu Paul Ruzoka, alipokuwa akifunga Mkutano wa Kitaifa wa Tume hiyo, uliofanyika katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala.

Alisema kwa kujificha chini ya mwavuli wa uhuru wa mtu kujiamria mambo yake, heshima kwa uhai wa watu imetoweka na kwamba hali hii, ni kinyume na imani ya Kanisa inayodhihirisha namna Yesu Kristo alivyowazawadia wanandamu maisha ya uzima kutokana na kifo chake msalabani.

Akilaumu juu ya kutoweka kwa heshima ya uhai, Askofu Ruzoka alitoa mfano akisema, "...Uholanzi imepitisha sheria ya kumsaidia mtu ambaye hataki tena kuendelea kuishi kwa kumpatia dawa ya ‘usingizi wa milele’(Euthanasia) katika kichaka cha uhuru wa mtu kujiamria mambo yake mwenyewe. Hili linakwenda kinyume na imani ya dini..."

Mhashamu Ruzoka ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, alisema kitendo cha mtu kuchoka kuishi duniani akaamua kujiondoa kwa kujiua, au hata kuwaua ambao hawajazaliwa, ni matokeo ya ukosefu wa upendo na kuwapo kwa uoga wa maisha katika kubeba misalaba.

"Palipo na upendo, hapana uoga; maana upendo kamili hufukuza uoga wote. Mtu mwenye uoga hajakamilika bado katika upendo, kwani uoga huhusika na adhabu.(1Yoh. 4.18).

Alisema kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mtandao wa mawasiliano, matukio ya maazimio ya mauaji ya wengine na hata vitendo vya kujiua, yamekuwa yakiigwa kirahisi bila jamii kuyachuja na hivyo, kuzidi kuenea katika jamii.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Haki na Amani, alisema pia kuwa, hali ngumu ya maisha katika jamii imetokana na jamii kujenga kasumba ya kunyang’anyana vipato miongoni mwa washika madau na kuwaacha watu wa chini katika hali mbaya zaidi.

"Ipo hali ngumu ya maisha kutokana na ‘kunyang’anyana kasungura’ kati ya wenye nafasi (washikadau) na kumwacha asiye nacho katika hali mbaya zaidi wakati ndiyo walengwa. Ubinafsi unakithiri," alisema.

Akizungumzia kazi za Tume yake, Askofu Ruzoka alisema, ni kupandikiza chachu ya uadilifu katika kutimiza wajibu na kuleta haki sawa kwa wote. Alisema kwa sasa Magereza siyo mahali pa kumrudi mfungwa kama ilivyokusudiwa kwa njia ya adhabu aliyopewa, bali pa udhalili kwa sababu ya huduma hafifu na ukosefu wa uadilifu.

Alisema kufuatia hali hiyo, Kanisa halina budi kujihusisha kikamilifu kuwahudumia wafungwa na mahabusu kwa kuwatembelea na kusali nao na pia, kuwapunguzia kwa huduma za kimwili na kiroho. Alisema inabidi Kanisa liendelee kuvishawishi vyombo vya dola kuanzisha adhabu nyingine kwa wenye makosa madogo na wenye kukaribia kumaliza vifungo vyao. Hii pia, itasaidia kuondoa msongamano wa wafungwa magerezani.

Alisema Tume haina budi kuwa karibu na Mahakama kwa kuwa ndicho chombo kinachosimamia haki na akashauri kuwapa mafundisho ya mara kwa mara zikiwemo semina mbalimbali, watendaji wa mahakama wakiwamo makarani na wasajiri wa Mahakama ambao, wakati mwingine wanaweza kutumika kukanyaga haki za watu.

Wanaosoma Seminari bila lengo la upadre ni wezi -Askofu Mkude

Na Ndechongio Charles, Morogoro

ASKOFU Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro amesema wanafunzi wanaosoma katika shule za seminari za Kanisa hilo pasipokuwa na lengo la kuwa watumishi wa Kanisa, ni wezi wa taaluma inayotolewa na Seminari hizo.

Akihubiri katika ibada ya Jumapili ya Mchungaji Mwema iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Patrisi mjini Morogoro, Askofu Mkude alisema pamoja na matatizo wanayokumbana nayo, wanafunzi wa seminari wanatakiwa kuwa na moyo wenye nia moja ya kumtumikia Mungu.

Alisema seminari za Kanisa hazitakiwi kufanywa mahali pa maficho ya wanafunzi wanaohitaji kufanikiwa kielimu tu, pasipo kutoa maslahi kwa Kanisa na watu aliosema wanahitaji viongozi imara na walioelimika.

"Mtu akishindwa kuufikia upadre iwe ni bahati mbaya kama ambavyo iliwatokea wenzetu lakini asiwe amedhamiria kushindwa kwani anaziba nafasi za wengine wenye nia safi ya kuwa watumishi wema wa Mungu," alisema .

Aidha, alitoa changamoto kwa wanaoshindwa kuufikia utumishi wa Kanisa uliotarajiwa, kuwa waaminifu na waadilifu katika maeneo mengine wanakobahatika kupewa dhamana za kijamii ili kutimiza lengo la Kanisa la kujenga jamii adilifu.

"Pia tunaandaa viongozi wa baadaye kwani taifa linahitaji watu wasomi ili kuhimili ushindani uliopo duniani katika nyanja mbalimbali kulingana na mabadiliko yaliyopo hivyo wanaoshindwa upadre, watekeleze hilo".

Katika Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na wanafunzi wa Seminari ya Mtakatifu Petro ya Morogoro, Askofu Mkude aliipongeza seminari hiyo kwa kushika nafasi ya nane kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.

Viongozi wa dini

ikosoeni serikali inapoboronga - Dk. Omari

Na Dalphina Rubyema

SERIKALI imesema kuwa inaheshimu ushauri na mawazo yanayotolewa na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini na hivyo wasikate tamaa wala kuchoka kuikosoa inapoonekana kwenda kinyume.

Tamko hilo lililotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Omari Ali Juma, wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichowaandalia viongozi wa dini nyumbani kwake.

Katika hafla hiyo ya hivi karibuni, Dk. Omari aliwataka viongozi hao wa dini kujiona kuwa wana mchango mkubwa serikalini na kwamba ushauri na nasaha wanazozitoa kila mara, ni muhimu.

Alisema viongozi hao hawana budi kutojisikia wala kudhani kuwa serikali inapuuza maoni na ushauri wao. "Serikali inathamini sana mawazo na ushauri wenu hivyo, msikate tamaa kuendelea kuishauri na kuikosoa pale inapoonekana kwenda kinyume" alisema Dk. Omari.

Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya kidini nchini wamekuwa mstari wa mbele kuishauri na kuikosoa serikali pale inapoonekana kwenda kinyume.

Katika tukio la hivi karibuni Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Umoja wa Kikristo Tanzania (CCT), walitoa tamko juu ya hali ya kisiasa nchini kufuatia vurugu zilizotokana na maandamano yaliyofanywa na Chama cha Wananchi (CUF) Januari 27 mwaka huu baada ya kuzuiliwa na Jeshi la Polisi.

Kama haitoshi Mabaraza hayo yaliandaa kongamano la siku moja lililohusu hali ya kisiasa nchini lililohusisha viongozi wa dini wenyewe, viongozi wa vyama vya siasa, wabunge na wawakilishi wa serikali.

Hata hivyo, wakati mwingine viongozi wa kidini wamekuwa wakisakamwa na viongozi wa serikali wanapozungumzia mambo yanayohusu dosari za uongozi katika serikali na madai ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi ya viongozi hao wa kisiasa, ni kwamba wanaingilia mambo ya siasa.

Hata hivyo viongozi ambao wamekuwa wakiwasakama viongozi wa kidini kwa madai hayo, hawasemi wala kufafanua kuwa siasa inaanzia wapi na dini inaanzia wapi na kuishia wapi.

Waamini wa Songea wahimizwa kuwajibika

Na Mwandishi Wetu, Songea

WITO huo umetolewa na Padre Paulo Chiwangu Kongocha, Paroko wa Kanisa Kuu la Songea ambaye pia ni dekano wa sehemu hiyo inayozunguka mji wa Songea. Padre Chiwango alitoa wito huo katika ibada ya jumapili hivi karibuni katika kanisa la Matogoro, alipoitembelea parokia hiyo.

Akihubiri wakati wa misa Padre Chiwangu alisema kwamba Yesu mfufuka aliimarisha imani ya mitume wake hususan Tomaso akiwaeleza maandiko matakatifu, aliwataka waumini kujenga mazoea ya kusoma maandiko matakatifu ili kuimarisha imani yao hasa katika mazingira ya leo. Aliwataka waamini wa parokia ya Matogoro kuonyesha imani komavu kwa kumtolea Mwenyezi Mungu Sadaka kwani sadaka anayotoa mkristo hasa jumapili ni alama yake ya kumshukuru Mungu kwa baraka na neema alizopata juma zima pia ni alama ya kumwomba Mwenyezi Mungu baraka kwa kazi za juma linalofuata. Nani atamshukuru jirani yake kwa kumpa sarafu ya shilingi ishirini alihoji padre huyo.

Akizungumza kuhusu zaka Padre Chiwangu alinukuu waraka maalumu wa Askofu mkuu Mhashamu Nobert Mtega wa jimbo hilo la Songea uliotolewa kwa waamini wote wa Jimbo hilo mwaka 1999. Katika waraka huo Askofu Mkuu aliwataka waamini wote jimboni kutoa sadaka, asante kwa huduma takatifu na kutoa zaka zao kwa wakulima kufikia shilingi elfu moja na kususitiza kwamba wafanyakazi watoe asilimia kumi ya mshahara wa mwezi mmoja. Akielezea kidogo historia ya ukristo katika Jimbo hilo alisema Wamisionari wa awali walipofika kuhubiri Injili waliwakuta wazee wetu katika hali duni sana kimaisha hivyo Wamisionari waliomba msaada kwao ili siyo tu kujenga majengo mbalimbali bali pia kuwasaidia wananchi katika mahitaji yao kama vile nguo, chakula chumvi na mengineyo. Wazee wetu walikuwa kama watoto wachanga katika imani. Kumbe sasa tumepiga hatua katika maendeleo na Wamisionari hawako tena ni sisi wenyewe Kanisa mahalia.

Hata hivi padre huyo aliwapongeza wafanyakazi wachache wanaotoa zaka yao kikamilifu kila mwaka akawataka wakristo wafanyakazi wa Matogoro na Songea mjini kuiga mfano huo mzuri kutoa fungo la kumi la mshahara kwani kiwango hichokina msingi kutoka maandiko Mtakatifu . akimaliza mahubiri yake alisema ni vema kuweka akiba benki kama CRDB au NBC kwa matumizi muhimu ya maisha lakini yesu anatuambia kuweka akiba au hazina mbinguni akiba ya maisha ya milele.

Wasabato kuhubiri kwa setilaiti

Na Bilhah Massaro

KANISA Kuu la Waadventisti Wasabato lililopo Magomeni katika mkoa wa Dar-Es-Salaam, kwa ushirikiano na makanisa mengine ya Kisabato nchini, limeandaa Mpango wa Kuongoa Roho kwa njia ya setelaiti.

Mratibu wa Mkuu wa Mpango huo katika kanisa hilo, Bw. Godfrey Jonathan, katika mazungumzo na KIONGOZi ofisini kwake mwishoni mwa juma lililopita, alisema kuwa, viongozi na waamini wa makanisa mbalimbali nchini, wanaalikwa kushiriki katika mahubiri hayo yanayojulikana kwa jina la AFRICA FOR CHRIST 2001.

Katika mkutano huo wa kimataifa utakaofanyika jijini Mwanza kuanzia Juni 16 hadi Julai 7, mwaka huu, walio katika makanisa ya mbali na jiji hilo, watapata mahubiri hayo kwa njia ya setelaite na hivyo, kuyashiriki wakiwa katika makanisa yao ya nyumbani.

Alisema ingawa mahubiri yatatolewa kwa lugha ya Kiingereza, kutakuwa na wakalimani tofauti kwa ajili ya kuwahudumia watu wa mataifa mbalimbali.

Tayari mikutano kadhaa ya maandalizi ya mkutano wa kitaifa, imekwishaanza katika makanisa mbalimbali ya Kisabato jijini Dar-Es-Salaam yakiwamo ya; Temeke, Mwenge, Ubungo -External na hata katika kanisa hilo la Magomeni.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, mahubiri hayo yataangozwa na Mwinjilisti Jere Petzer wa hapa barani Afrika na unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa Idara ya Mawasiliano ya Kanisa hilo toka Makao Makuu ya Kanisa Duniani pamoja na vikundi mbalimba vya uimbaji.

"Mkutano huu ni maalumu kwa ajili ya Afrika na baadhi ya vielelezo vyake vitakuwa na sura za Waafrika," alisema.

"Kabla ya mahubiri kuanza, kutakuwa na vipindi mbalimbali. Katika kipindi cha Afya Yako, baadhi ya wagonjwa tunatarajia watapatiwa matibabu bure... na kwaya za hapa Tanzania zitatumbuiza," alisema.

Hata hivyo, alisema huduma ya afya itatolewa kwa makanisa yatakayopata huduma hiyo ya mahubiri.

"Kila mkoa utatoa kwaya moja isipokuwa Dar-Es-salaam, ambao utatoa kwaya tatu," alidokeza Bw. Jonathan na kuzitaja kwaya za jijini Dar-Es-Salaam kuwa ni Magomeni SDA Choir,Temeke Mass Choir na manzese SDA Choir.

Soko Huria limeathiri uhakika wa chakula-CARITAS

Na Pelagia Gasper

SHIRIKA la Misaada lililo chini ya Kanisa Katoliki(CARITAS), tawi la Tanzania, limekiri kwamba Sera za Urekebishaji wa Uchumi na Soko Huria zimeathiri vipengele kadhaa vya uhakika wa chakula nchini.

Akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake mwanzoni mwa wiki, Mratibu wa kitengo cha Maafa kilicho chini ya CARITAS-Tanzania, Bw. Castor Kalemera, alisema kuwa si hivyo tu bali yamo mambo mbalimbali yanayochangia sera hizo kuzidi kuathiri uhakika wa chakula na kupambana na majanga yakiwemo umaskini, elimu, duni kwa wakulima na ukosefu wa mvua za uhakika.

Amesema kutokana na hali hiyo, mazao yanayolimwa na wakulima walio wengi hivi sasa mashambani si ya kuinua hali ya uchumi wa nchi bali ni ya kuongeza pato la Taifa.

"Uchumi wa nchi unazidi kudidimia lakini mapato ya nchi yanaongezeka ambapo kilimo kinacholimwa kwa sasa ni cha biashara ya pesa taslimu," alifafanua Mratibu huyo.

Aliendelea kusema kuwa, kupungua kwa mazao ya kilimo kumeanza rasmi miaka ya 80 ambapo soko huria liliigia ulingoni na kuwafanya wakulima waanze kuuza mazao yao kwa wanunuzi ambao hujipangia bei wanayoipenda wao wenyewe tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Bw. Kalemera alirejea mwaka 1967 wakati wa Azimio la Arusha ambapo kilimo cha Tanzania kilikuwa na hali nzuri ambapo maendeleo ya nchi yaliridhisha kwani mazao yaliyokuwa yanalimwa ni mazao ya kukuza uchumi wa nchi tofauti na sasa.

Akayataja mazao hayo yaliyokuwa yakilimwa nyakati hizo kuwa ni pamoja na Pamba, Mkonge, Pareto, Kahawa na Korosho.

Hata hivyo, Bw. Kalemera amesema miundombinu ya njia za usafirishaji husababisha upungufu wa chakula na hata njaa katika baadhi ya maeneo ya nchi, nazo zimechangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo kutokana na barabara kuwa mbovu.

Naye Msaidizi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam, Profesa Dk Marjorie Mbilinyi, amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na taasisi hiyo kwa mkoa wa shinyanga umeonesha kuwa tatizo la uhakika wa upatikanaji wa chakula ni tata.

Ameshauri kuwa sera mbalimbali zinazopitishwa ziangalie hali ya Watanzania itakuwaje hapo baadaye.

Mwanza wajadili sera za Kichungaji

Na James Marenga, Mwanza

JIMBO Kuu Katoliki la Mwanza, limefanya kikao chake cha nne cha Sinodi kinacholenga katika kutayarisha sera za kichungaji zitakazoliongoza katika milenia ya tatu.

Kikao hicho ambacho ni mfululizo wa vikao sita, kilizungumzia hati ya mawasiliano na kazi za kichungaji ambayo ilifafanuliwa na Askofu Anthony Banzi wa Jimbo la Tanga, aliyewaelezea wajumbe dhana nzima ya mawasiliano ya kisasa na ikihusishwa na kazi za kichungaji.

Hati nyingine iliyojadiliwa, ni ile ya Liturujia iliyofafanuliwa na Padre John Dekkers wa Shirika la Wamisionari wa Afrika. Katika hati hii, wajumbe walifafanuliwa sura mbalimbali za hati hizo zikiwemo zile za sakramenti na visakramenti, sala za Kanisa, Mwaka wa Liturujia, Muziki Mtakatifu na sanaa na vifaa vya Kanisa.

Katika matayarisho hayo, hati 16 za Mtaguso wa Pili wa Vatikani zinachambuliwa kama muongozo katika upatikanaji wa sera muafaka za kichungaji zitakazoongoza jimbo hilo.

Hadi kumalizika kwa kikao hicho, jumla ya hati sita zimekuwa zimekwisha chambuliwa ikiwa ni pamoja na Utume wa Walei, Malezi ya Kikristo, Ufunuo (Neno la Mungu), mawasiliano, furaha na matumaini (uchumi wa Kanisa), na Liturujia.

Katika kikao hicho, wanajimbo wameingia katika hatua muhimu ya Sinodi ambapo sasa wameanza kutayarisha sera.

Padre Nicholaus Segeja, alielekeza namna ya kuchambua na kuchanganua uwekaji wa sera hizo ambazo baadaye zitapigiwa kura ili kupata sera rasmi zitakazoongoza jimbo.

Kikao hicho cha Sinodi kilifanyika katika Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria, Nyegezi na kuhudhuriwa na wajumbe wapatao 200, akiwemo Askofu Mkuu Anthony Mayalla, Askofu Anthony Banzi wa Tanga, mapadre, walei na watawa wa kike na wa kiume kutoka katika parokia zote za jimbo hilo.

Kikao hicho kilifanyika kuanzia Aprili 24 hadi 26, mwaka huu.

...Msabato akemea wanaopotosha Biblia

Na Elizabeth Steven

MHUBIRI mmoja wa Kanisa la Waadventisti Wasabato amesema maisha ya utakatifu mbinguni yanahitaji kufanyiwa mazoezi tangu duniani na kwamba inashangaza watu wengi kuitafsiri na kufundisha vibaya juu ya Biblia.

Mwinjilisti huyo Melchizedeck Maingu, aliyasema hayo katika siku ya kumi (Jumanne iliyopita) ya Mkutano wa Maandalizi ya Mkutano mkubwa wa Setilaiti unaotarajiwa kufanyika mjini Mwanza Juni mwaka huu.

Katika mkutano huo uliofanyika tangu Aprili 29 na kumalizika Mei 12, mwaka huu katika Kanisa la Wasabato lililopo Kurasini, Mwinjilisti Maingu alisema tafsiri mbaya za Biblia na mafundisho batili, yamekuwa yakichangia jamii kupotoka kiimani na akashauri wahubiri wafanyekazi ya Mungu kwa usahihi.

"Ingawa watu wengi wanahitaji na kutamani ufalme wa mbinguni kila mtu anahitaji kufanya maandalizi na mazoezi duniani ... Tatizo ni kwamba Biblia watu wengi wanaitafsiri vibaya na kuifundisha visivyo," alisema.

Akizungumzia umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo, Mwinjilisti huyo alisema ni makosa kuuchukulia Ubatizo kama sherehe ya kuvaa, kula, kunywa na kuingia majini pekee bali, kujiunganisha na Yesu katika maisha.

"Wengine siku ya Ubatizo ndiyo wanayotumia kwa kuonesha ufahari na ulevi hata wengine sasa wanatafuta Ubatizo kwa mkumbo tu. Hawajui kuwa anayekubali kuzaliwa mara ya pili; matunda ya uamuzi wake ni kuzaliwa kwa maji na roho," alisema.

Aliwataka Wakristo kuutumia Ubatizo kuleta mabadiliko katika maisha na hivyo, kuondokana na ufisadi na mambo ya uhalifu yanayoiangamiza dunia kwani ndio ishara ya kufa na kufufuka pamoja na Yesu (Yoh:3:22; Mark 1.9-12 na Mt.2:37-38).

Mkutano wa namna hii kwa ajili ya maandalizi ya mahubiri ya kimataifa kwa njia ya Setilaiti tayari jiji la Dar-Es-Salaam umekwishafanyika katika makanisa ya Magomeni Temeke, Mwenge na Ubungo External.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana nje ya mahubiri hayo, mwaka 1997 mahubiri ya Setelaiti yalifanyika Kumas nchini Ghana, 1998 Marekani, 1999 Soweto, Afrika Kusini na Mwaka 2000, yalifanyika huko Port Elizabeth, Afrika Kusini. Mwezi Juni mwaka huu, yanatarajiwa kufanyika jijini Mwanza, Tanzania.

Parokia ya Kibakwe yalilia amani, msamaha

Na Damasus Mtalaze, Kibakwe

"KAENEZENI ukweli kuhusu Kristo popote muendapo bila kuhofu juu ya chochote.

Lolote alilolifanya Mungu, ni jema na hakuna awezaye kukanusha ukweli huo. Amani ninyi kwa ninyi ni kitu chema zaidi na abishaye, atafute kilicho chema zaidi ya amani duniani".

Hayo yalisemwa katika ibada ya hivi karibuni na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kibakwe, iliyopo katika Jimbo Katoliki la Dodoma, Padre Agusto Serafini

"Uwe na utajiri na mali nyingi, au cheo kikubwa; bila amani, hivyo vyote kwako havina faida," alisema.

Akawauliza waamini waliofurika kanisani kuwa, endapo watapoteza amani watapata au watajivunia nini hapa duniani lakini aksisitiza kuwa yapo mengi juu ya amani ingawa mengine hayakuandikwa.

"Mwanadamu unapokuwa ndani ya amani, Mungu naye anakupa maisha mapya ili ueneze amani hiyo kwa wote watakaoitaka amani," alisema.

Alizidi kufafanua kuwa siku zote Mungu humpa Roho ya Uhai, mtu yeyote anayeeneza amani rohoni na mwilini kwa kuwa mtu hawezi kuwa na amani bila kumtegemea Mungu amwongoze.

Padre Serafine alisema mwanadamu alitaka akose amani alipotaka kujichukulia madaraka toka kwa Mwenyezi Mungu.

Akitoa mifano zaidi juu ya amani, Padre huyo alisema kuwa, kila wakati Yesu alipowatokea mitume wake, kitu cha kwanza kusema ilikuwa, "Amani iwe kwenu".

Akasema salamu hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaongezea wanadamu uhai wa kukaa ndani yake wakimtegemea.

Alisema mtu anapokosa amani, anakuwa anaivunja salamu ya Kristo na akanukuu Biblia akisema, "Biblia inasema mti wa uzima ni Kristo na mti wa mauti ni dhambi," alisema na kuongeza, "Wa heri wale wanaomwamini bila kuona ishara."

Paroko huyo Msaidizi alihimiza kusameheana akisema, "Samehaneni, kuweni na amani kama Mungu alivyopenda... Ili tumpendeze Mungu na sisi tuokolewe Siku ya Mwisho, ni lazima tupendane na kusameheana," alisema.

Misereor yaisaidia WID

Na Leocardia Moswery

ILI kusukuma gurudumu la maendeleo ya akina mama, Shirika la Miserieor la nchini Ujerumani, limetoa msaada wa gari aina ya PAJERO kwa kitengo cha Maendeleo ya Akina Mama (WID) kilichoko chini ya Shirika la Misaada la CARITAS, tawi la Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mratibu wa WID Taifa Bi. Oliva Kinabo, wakati wa warsha ya siku nne juu ya tathmini na mipango ya baadaye ya WID, inasema kuwa gari hilo thamani yake ni shilingi milioni 18.

"Kitengo cha WID kimepata msaada wa gari lenye thamani ya milioni 18 na litatusaidia katika kuboresha maendeleo ya wanawake katika majimbo mbalimbali," alisema Bi. Kinabo.

Awali katika ibada ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) na kuwahusisha waratibu wa WID jimboni, Mwenyekiti wa CARITAS Taifa, Mhashamu Agapiti Ndorobo, aliwataka washiriki hao kuzingatia kuwa njia pekee ya kuwasaidia watu wasiojiweza ni kupunguza ukali wa maisha na kufanya kazi kwa bidii.

Mhashamu Askofu Ndorobo alisema kwa kuzingatia hali ngumu ya maisha, jamii haina budi kufanya kazi kwa pamoja.

"Tunaelewa hali halisi ya jamii yetu kwa hiyo inatupasa kufanya kazi kwa pamoja ili kupunguza ukali wa maisha pamoja na kuwasaidia wengine wasiojiweza" alisema Mhashamu Ndorobo.

Katika kutekeleza kazi zao ipasavyo, mhashamu Ndorobo aliwataka washiriki wa warsha hiyo kuwa mstari wa mbele katika kutetea amani na haki kwa kumshirikisha Mungu ili aweze kuwasaidia na kuwajalia upendano katika kazi zao.

BAADA YA MATUKI KADHA YA MAUAJI...

Igalula kwawa eneo la Kimisionari

Damas Masanja, Tabora

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, limekitangaza kijiji cha Igalula kilichopo katika Wilaya ya Tabora Vijijini, kuwa eneo la Kimisionari, kufuatia matukio kadhaa ya imani ambayo yamekuwa yakitendeka kijijini hapo. Imefahamika.

Akihubiri katika ibada iliyofanyika kijijini hapo hivi karibuni, Paroko wa Parokia ya Ipuli, Padre Leons Maziku, alisema uamuzi wa kukifanya kijiji hicho kuwa eneo la kimisionari tangu Machi Mwaka huu, umefikiwa na Uongozi wa Jimbo baada ya matukio mazito kadhaa yaliyotokea hapo yakitishia kuvuruga imani ikiwa ni pamoja na mauaji ya viongozi wa Kanisa.

Alisema waamini wa kigango hicho kwa sasa wanapata misaada na mahitaji ya kiroho kwa kufuata taratibu za kimisionari na michango yao itakuwa ni kuimarisha mioyo na imani zao.

Padre Maziku aliuomba uongozi wa serikali ya Kijiji, Kata na Tarafa ya Igalula, kuisoma vizuri na kuielewa Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa mtu kuabudu na kuamini dini anayoitaka mradi havunji sheria.

Hivi karibuni serikali ya Kijiji cha Igalula, ilifungua machimbo ya moramu ya kutengenezea barabara katikati ya kiwanja kinachomilikiwa kihalali na kisheria na Kanisa Katoliki Jimbo la Tabora. Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na maelfu ya waamini wa vigango mbalimbali vya Parokia ya Ipuli wakiwamo watawa wa kike na wa kiume.

Ibada ilikuwa mahususi kwa ajili ya kuwapa pole, kuwatia moyo na kuwafariji Wakristo wa Igalula kufuatia vifo vya makatekista Joseph Bundala na Valentine waliouawa kikatili na watu wasiojulikana mwishoni mwa mwaka jana.

Awali kabla ya ibada, Mwenyekiti wa Kigango hicho ambacho kilikuwa Parokia miaka 30 iliyopita, Bibi Stela Maricel, alisoma taarifa fupi ya kigango iliyosema kuwa, pamoja na vitisho, waamini katika kijiji hicho, hawatarudi nyuma katika imani Katoliki.

Alisisitiza umuhimu wa wana-Kanisa wote kushiriki kwa nguvu zao zote kutetea haki za wanyonge kama ilivyo asili ya Kanisa.

Wakati huo huo: Padre Maziku amesema kila Mkatoliki na Mkristo yeyote anawajibu mkubwa wa kushiriki kulinda ukweli, maadili mema na upendo kwa ajili ya majirani kwani endapo watalegalega, kwa kushindwa kutetea haki za binadamu, halitakuwa na tofauti na taasisi za kibinafsi (NGOs).

Alikuwa anahubiri katika ibada ya Jumatatu ya Pasaka iliyofanyika katika Shule ya Msingi ya Igalula.

Pamoja na mambo mengine, ibada hiyo ilikuwa ya kuwaombea na kuwakumbuka marehemu Padre Colonel Shija aliyekuwa Paroko wa mwisho wa Parokia ya Igalula, Maktekista Joseph Bundala, Nicodemus Joseph na Petro Valentine.

Mwinjilisti Mkenya ataka Watanzania wampokee Mungu

Na Joyce Joliga, TIME

MCHUNGAJI Charles Kababu wa Machakosi nchini Kenya, amewashauri Watanzania kuachana na mambo yanayopingana na mapenzi ya Mungu na badala yake, waamke na kumgeukia na kumtumaini ili mambo yao yaende sawa.

Aliyasema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya watu waliokusanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe jijini Dar-Es-Salaam, Mchungaji Charles alisema hakuna haja ya watu kuendelea kuishi maisha yanayomchukiza Mungu.

Mchungaji huyo alikuwa jijini Dar-Es-Salaam kwa ajili ya kuwaombea watu wenye matatizo mbalimbali.

"Hakuna haja ya kuendelea kuishi maisha yanayomchukiza Mungu, maisha yenye mateso na badala yake ni bora tuishi maisha ambayo yanampendeza Mungu na kuacha kufanya dhambi kama kusema uongo, kuzini, ushirikina na wizi", alisema Mchungaji Charles.

Wachngaji Charles na Pastol Onesmo Ndegi waliwaombea maelfu ya watu waliofurika uwanjani hapo waliokuwa na magonjwa na matatizo mbalimbali.

Baadhi ya wagonjwa ambao waliombea na kupona kabisa ambao majina yao hayakuweza kufahamika mara moja walipanda jukwaani na kuwaelezea watu waliokuwepo uwanjani hapo magonjwa ambayo yalikuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu ukiwemo ugonjwa wa uvimbe wa tumbo Kifua na Nimonia

Aidha, Mchungaji Charles na Pastor Onesmo waliahidi kufanya mikutano kadha katika jiji la Dar-Es-Salaam kama Mwenge, Masaki, Tegeta.

Kama una gari, elimu, kazi...

Na Margareth Charles, TIME

MKURUGENZI wa Life Ministry, Mchungaji Ignatius Nyaga, amesema kuwa mafanikio yoyote mazuri ya duniani bila Yesu, ni kazi bure kwani hayamfikishi mtu mbinguni.

Aliyasema hayo wakati wa ibada iliyofanyika katika Kanisa la Africa Inland Church, Usharika wa Magomeni Jumapili iliyopita.

"Ukipata elimu nzuri, kazi nzuri, mke ama mume na utajiri bila Yesu, ni sawa na sifuri," alisema Mchungaji Nyanga.

Aidha, Mchungaji huyo amewataka waamini kuanza na kumaliza vizuri safari yao ya duniani ili kila mmoja awe kati ya wale wanaojiandikisha kwenda mbinguni.

"Katika makanisa yetu leo, kuna watu tunaowakumbuka ambao walianza vizuri na kumaliza vizuri safari yao ya duniani, wengine walianza lakini hawakuimaliza, vizuri," alisema.

Alisema kumaliza safari inahitaji mtu kuianza akiwa amemkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake.

Wakati huo huo: Mchungaji Nyaga aliwafananisha wale wasio okoka kuwa ni sawa na wanariadha wanaokimbilia kandokando ya uwanja huku wakiwambia wanariadha wanaokimbia kwenye sehemu za uwanja zinazotakiwa, waongeze mbio wakati wao hawakimbii.