Hatuna sheria ya kuwapima UKIMWI maharusi - Kanisa Katoliki

l Wamoraviani wafurahishwa na uamuzi huo

l Yadaiwa hali hiyo itazidi kuua badala ya kuponya

Na Mwandishi Wetu

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, limesema halina mpango wa kuweka sheria ya kuwabana maharusi kupima UKIMWI kabla ya ndoa kwa kuwa hali hiyo itaongeza matatizo zaidi.

Hayo ni miongoni mwa maazimio ya mkutano wa pamoja wa mapadre wote wanaofanya kazi na majukumu mbalimbali ya kichungaji katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, uliofanyika Jumatano iliyopita katika ukumbi wa Msimbazi jijini Dar-Es-Salaam.

Mkutano huo uliohudhuriwa na mapadre wapatao 71, uliongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini na kuhudhuriwa pia na Askofu Mkuu wa Jimbo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Katibu wa Askofu wa Jimbo, Padre Andrew Luanda, ameliambia KIONGOZI ofisini kwake kuwa mkutano huo wa mapadre wa jimbo umefikia uamuzi huo baada ya kuangalia kwa makini na kuona kuwa kwa sasa hatua hiyo ina athari nyingi mbaya kuliko faida.

Padre Luanda alizitaja baadhi ya sababu za umuhimu wa Kanisa jimboni kutofanya hivyo, kuwa ni pamoja na ukweli kuwa katika Sheria za Kanisa, haipo sheria inayowalazimisha wanandoa watarajiwa kupimwa UKIMWI kabla ya ndoa yao. "Kwanza hakuna sheria ya kuwazuia wagonjwa kufunga ndoa", alisema.

Mawazo ya Katibu huyo wa Askofu, yalifanana na ya Mchungaji wa Kanisa la Moravian Tanzania, Ushirika wa Kekomachungwa katika Wilaya ya Mashariki, Jimbo la Kusini, Salatieli Mwakamyanda ambaye awali alisema kuwa kuwalazimisha wanaotaka kufunga ndoa kupimwa UKIMWI, kutawafanya waamini kulikimbia Kanisa kwa kuogopa kupimwa na hali hiyo, itachangia kuwepo kwa utitiri wa "ndoa bubu."

"Hii itafanya watu wakusanyane haraka haraka na wengine waache kabisa mambo ya Kanisa na hili wazo la kuwapima sijui linatoka wapi. Cha msingi hapa ni kuwafundisha wanajamii waujue vema ugonjwa wa UKIMWI" alisema Mchungaji Mwakamyanda na kuongeza, "Mimi napinga sana wazo la kuwalazimisha watu kupimwa UKIMWI eti ndipo wafunge ndoa."

Naye Padre Luanda alisema, "Kanisa linachosisitiza ni watu kuishi katika uadilifu. Hata hivyo, kwa watu walioamua wenyewe kupima, Kanisa haliwazuii; wanaruhusiwa hata jimbo lina kituo chake cha mambo ya UKIMWI, kipo Chang’ombe kinaitwa PASADA. Lakini, wazo la kuwalazimisha kupima, ni hatari mno. Mwenye roho nyepesi anaweza hata kujiua," alisema.

Akifafanua zaidi, Padre Luanda alisema kuwa, kitendo cha kuwalazimisha watarajiwa wa ndoa kupima, kitasababisha hata ambao wana vizuizi vingine vya ndoa, jamii iwatazame kwa mawazo kuwa ni wagonjwa wa UKIMWI.

"Hata ukizuiliwa kwa suala lingine usifunge ndoa, jamii itachukulia tu kuwa una UKIMWI na hii itasababisha hata wengine kujiua bure," alisema.

Aliongeza kuwa ni mapema mno kwa jimbo kuweka sheria hiyo kwa kuwa hata vitendea kazi havitoshi. Alisema hata idadi ya vituo vya kupimia UKIMWI vilivyopo, haiwiani na idadi wala mahitaji yatakayo kuwapo endapo sheria hii itatumika.

Tume ya Haki na Amani yasambaza kitabu cha haki kwa wafungwa

l Dar waombwa kuwachangia wafungwa sabuni, kandambili.

l Waambiwa hata wao ni watoto wa Mungu

Peter Dominic na Josephss Sabinus

TUME ya Haki na Amani ya Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki (CPT), imechapisha na kusambaza kitabu kwa wafungwa kitakachosaidia jamii na wafungwa wenyewe kuelewa haki zao.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Katibu wa Tume hiyo, Padre Vic Missiaen, zimesema kitabu hicho kinachoitwa HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA TANZANIA BARA, kina lengo la kuifanya Tume hiyo, serikali na jamii nyingine wakiwamo wafungwa na uongozi wa magereza kushirikiana katika kubuni mbinu za kuboresha na kurekebisha haki za wafungwa.

Padre Vic alisema mwishoni mwa juma kuwa hali ya mfungwa kutambua haki yake, ni pamoja na kumfanya atambue makosa yake na kuyajutia ili pindi amalizapo adhabu, ajirekebishe kitabia katika maisha yake.

"Hata mfungwa ni mtoto wa Mungu na lazima aheshimike na utu wake na kuyatambua makosa yake kwa kuwa magereza siyo sehemu ya mateso ila ni ya kumsaidia mkosefu ajirekebishe na kuisaidia jamii" alisema.

Habari zaidi zilizopatikana, zilisema nakala 1500 zilikabidhiwa kwa Kamishna Mkuu wa Magereza nchini, Bw. Onel E. Malisa , na kuna habari kuwa kitagawanywa katika magereza mbalimbali kwa kadiri ya mahitaji ya wafungwa na pia, baadhi ya viongozi mbalimbali wa Serikali, wamekwisha pata nakala za kitabu hiki yakiwamo Makao Makuu ya Magereza.

Wafungwa mbalimbali katika magereza nchini, watapata fursa ya kusoma kitabu hicho kwa kadiri ya taratibu za gereza husika.

Katika mazungumzo na gazeti hili, Padre Vic, alisema lengo la kumfanya mfungwa atambue haki zake si kumpa uhuru wa kufanya vurugu na kukiuka taratibu, bali ni kumfanya ajifunze na kutambua kuwa magereza siyo mahali pa kukaa na kujifunza ubaya bali kuirekebisha jamii.

Alitoa wito kwa viongozi mbalimbali wa dini, jamii na wahusika mbalimbali, kushirikiana vema na Jeshi la Magereza katika kuwahudumia wafungwa kimaadili na kusaidia kutoa huduma nyingine muhimu kwa wafungwa kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Katika kitabu hicho kilichoandaliwa chini ya Mwenyekiti wa Tume ya haki na Amani ya baraza la Maaskofu katoliki tanzania(TEC), Askofu Paul Ruzoka, katika Dibaji yake kamishna Mkuu wa Magereza Bw. Onel E. Malisa, amezishukuru taasisi mbalimbali za kidini kwa mchango wao wa kujenga maadili na kufundisha dini kwenye magereza na misaada mingine ya kibinadamu kama dawa za tiba.

"... nafarijika kupewa heshima ya kuandika dibaji ya kijitabu hiki kilichoandaliwa na kanisa katoliki kwa nia ya kuelimisha umma kuhusu dhana na shughuli za Magereza, " inasema sehemu ya dibaji ya kitabu hicho chenye kurasa 50.

Wakati huo huo: Chama cha Wanataaluma Wakatoliki(CPT), kimewaomba Wakristo katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, kuchangia zawadi mbalimbali ili kuwasaidia wafungwa katika magereza jimboni humo.

Kwa mujibu wa barua ya chama hicho kwa maporoko jimboni humo yenye Kumb. Na. CPT/J&P/L./00/25 ya Machi 9, mwaka huu iliyosainiwa na mshauri wa CPT, Padre Vic Missianen na Mwenyekiti , Bw. Agapit Meiseyeki ambayo nakala yake imetumwa kwa Askofu Mkuu wa Jimbo na Mkurugenzi wa Utume wa Walei imesema, zawadi hizo ziwasilishwe wiki mbili baada ya Sikukuu ya Pasaka tayari kwa kuwafikia wafungwa mwishoni mwa mwezi Mei.

"Kutokana na uzoefu wa mwaka jana, mahitaji muhimu kwa wafungwa ni sabuni za kufulia na kuogea, miswaki na dawa zake pamoja na kandambili," inasema barua hiyo ambayo nakala yake tunayo.

BAADA YA KUPATA KANSA YA KIBOFU, ASKARI MSTAAFU WA POLISI ALIA...

Naumia jamani nateseka !!

l Hivi sasa anaishi magengeni

l Amefanyiwa operesheni mara nne

l Analilia kumuona Mkapa amueleze matatizo yake

l Anasema vita ya Amini imechangia 'kumuua'

Na Neema Dawson, Mkuranga

"Naumia! Naumia mie jamani! Nateseka nateseka!!" analia Bw. Abdul A. Mchotika(52), ambaye ni Mstaafu wa Jeshi la Polisi aliyekuwa namba C.133 na cheo cha Koplo. Mchotika alikuwa katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU).

Anaendelea, "Tatizo linalonisumbua na ambalo lilikuwa linanitesa hadi sasa, ni kukosa haja ndogo baada ya kibofu cha mkojo kuziba. Hiyo niliigundua kwa kuwa nikienda kujisaidia, inashindikana kabisa na kinachotoka, ni kimkojo kidogo tu. mkojo unaobaki ulikuwa unaniumiza sana."

Bw. Mchotika ambaye kwa sasa anaishi katika magenge eneo la Kongowe Wilayani Mkuranga katika mkoa wa Pwani, anasema alipoamua kupimwa hospitalini, baada ya kuridhika na mateso aliyokuwa akiyapata wakati anakojoa, iligundulika kuwa alikuwa akiteswa na kansa ya kibofu cha mkojo.

Anasema kansa hiyo ya kibofu imemsababishia kufanyiwa upasuaji mara nne tofauti katika hospitali ya KCMC.

Gazeti hili lilipomkuta magengeni na kumtaka watembelee nyumbani kwake ili lijionee mazingira anayoishi na hata kuzungumza kwa hali ya kuelewana zaidi kutokana na kelele zilizokuwapo gengeni, Bw. Mchotika alisema,

"Hapa uliponikuta, ndipo ninaposhinda na ndipo ninapolala. Sina nyumba, vyombo, kitanda wala shuka. Hiki ni Kigunia changu ninachotandika na kulala hapa kwenye mbao, sina mtu wa kunisaidia hata mahali pa kulala; nifanyeje!" anasema.

Akitokwa na machozi ya mara kwa mara wakati wa mazungumzo yake na gazeti hili, Bw. Mchotika anasema hapo anapoishi katika genge la Kongowe, mvua na jua vyote huishia kwake licha ya kuwa amefanya kazi serikalini kwa muda mrefu na hajapata mafao yake.

Anasema kutokana na hali yake ya kiafya na kukosa mafao yake licha ya kufuatilia kwa takriban miaka 14, vinamfanya ashindwe kufanya kazi yoyote ya kumuingizia kipato na hivyo, kumpa riziki.

"Unadhani mimi sina nguvu za kuweza kulima? Nguvu ninazo lakini, haya maradhi niliyo nayo, yananishambulia na kunitesa mno. Ninateseka sana. Ndiyo maana ninashindwa hata kwa kuwa miguu yangu yote imeoza; ona nilivyovimba."

"Sina matatibu ninayopata ya kutuliza maumivu ya vidonda vya miguu zaidi ya kuvifunga vidonda hivi na matambala hayo ninayofunika, ndiyo kumbe yanavifanya vizidi kuoza zaidi."

Akisimulia namna kansa hiyo ya kibofu cha mkojo inavyomuathiri hata kumsababishia pia matatizo ya kuvimba miguu, Bw. Mchotika anasema kuwa, hali hiyo imemuathiri miguu.

Anasema baada ya kufanyiwa upasuaji, madaktari walimtahadharisha kuwa angeathirika.

Anaongeza kuwa kweli kama alivyotahadharishwa, miguu na vidole vyote vilianza kuvimba na baadaye, uvimbe huo ulirukia kwenye miguu na kuwa matende na wakati wote huo alikuwa anajisaidia kwa kutumia mpira.

Aliendelea kuathirika kutokana na kutotimiza masharti ya daktari wake ya kutosimama kwa muda mrefu.

"Kwa kuwa, nilikuwa kazini Moshi, nilimpa barua mkuu wangu wa kazi(RPC). Barua hiyo ilikuwa imetoka kwa daktari wangu ambaye alikuwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya KCMC Moshi Dk. J. Lester Eshleman.

Haya ni mambo ya kijeshi Huyo RPC hakutaka kunisikiliza wala kunisaidia. (Hamtaji jina wala mwaka) na niliendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na kwenye maumivu na mateso kwelikweli.

Bwana Mchotika alisema kuwa kusema kweli, matatizo yake pia yanachangiwa na ndugu zake kumkimbia baada ya kukumbwa na matatizo.

Ingawa alikuwa Muislamu aliona bora aweze kuwa karibu na marafiki wa kiroho waliomfariji kwa kiasi kikubwa kwani Wakristo wa madhehebu ya Waadventista Wasabato (SDA) wa Kongowe, walikuwa karibu wakimpa moyo wa uvumilivu.

Anasema, Wa-SDA hao na walimsaidia kwa nauli ya kumsafirisha hadi KCMC, Moshi kwa matibabu tena baada ya njia ya mkojo kuziba.

Anasema alitibiwa na kurejea jijini Dar-Es-Salaam. Hivi sasa, kwa kiasi fulani Bw. Mchotika anaangaliwa na rafiki yake, Bw Stamil Twaha Kamilaga.

"Nikikumbuka nilivyokuwa mzima anafanya kazi mwenyewe; chakula najinunulia; nguo, pesa nazipangia bajeti mwenyewe lakini; maradhi yaliyonipata nimekuwa ombaomba. Sina pa kulala; chakula ninakosa na kubaki ninaomba Mungu tu. Kwa kweli maisha ninayoishi si maisha, bali ni kusukuma siku tu ninasubiri kifo" akasema kwa uchungu.

Mchotika ambaye ni mstaafu wa serikali alisema kuwa amefuatilia mafao yake kwa muda mrefu bila mafanikio na amekuwa akizungushwa bila kusaidiwa ingawa afya yake ni mbaya.

Mchotika alisema, kutokana na hali ya mahangaiko anayopata kwa maradhi yake na hata usumbufu uliomsibu kwa miaka 14, bila kupata mafao yake, anaomba yeyote mwenye mapenzi mema amsaidie aonane na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa.

Anasema hali inaweza kumsaidia kwani watendaji wote wa ngazi za chini alipopita, wameshindwa kumsaidia ili apate haki zake.

"Ninachoomba ni Mkapa aingilie kati suala langu; atoe msukumo zaidi ili Wizara ya Mambo ya Ndani inilipe mafao yangu kwa kuwa sasa ni miaka 14 tangu nilipostaafu polisi kutokana na matatizo ya kiafya."

Anadai Wizara imekuwa ikimzungusha kwa madai kwamba faili lenye kumbukumbu zake, ni miongoni mwa mafaili yaliyoungua moto wakati jengo la Wizara ya Mambo ya ndani lilipoteketezwa na moto mwaka 1988.

"Ninaomba Rais aingilie kati ili anisaidie katika suala hili kusudi nilipwe mafao yangu kwa sababu mimi mwenyewe kumbukumbu zote ninazo lakini, kinachonikatisha tamaa ni pale ninapokwenda wizarani halafu ninaambiwa kwamba faili lako limeungua moto na kuambiwa eti nifanya subira.

Sasa ninashangaa maana subira hiyo inakuwa haina jibu lolote mpaka leo hii. Je, hii ni kwa wote ambao mafaili yao yameungua moto au ni mimi peke yangu tu?" alihoji kwa huzuni.

Anazidi kulalalimika kuwa kutokana na yeye kustaafu kutokana na matatizo ya kiafya, kumcheleweshea malipo ya mafao ni hatua inayozidi kumuathiri sana kwani hadi sasa, anakabiliwa na matatizo mengi mno.

"Ninaishi maisha yaliyojaa dhiki sana kwani mpaka sasa ninaweza kukaa kwa njaa siku na siku mpaka atoke msamaria mwema anipe pesa au anikaribishe nyumbani kwake nikale.

Bw. Mchotika ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Lindi, anaongeza kulalama kuwa endapo hakutokea mtu kama huyo, siku hiyo atashinda au kulala na njaa kwani anaona aibu kubwa kwa umri wake(52), kutoka ndani na kuwa ombaomba.

Amchotika alizaliwa mwaka 1949 na alipofikisha umri wa miaka 21 alioa mke. Mwaka 1970, alijuunga na Wizara ya Mambo ya Ndani kama mhudumu wa Ofisi kazi ambayo aliendelea nayo mpaka mwaka 1971 alipokuwa mtumishi katika kikosi cha Bandari Mtwara "Marine Police Unit" akiwa mpishi kwenye meli iliyojulikana kwa jina la RAFIKI No.6.

Mwaka 1972 alichaguliwa kwenda kuchukua mafunzo katika Chuo Cha Polisi, Moshi. Alimaliza mafunzo hayo mwaka 1978.

Baada ya kumaliza mafunzo hayo, alipelekwa mkoani Ruvuma kuanza kazi ya uaskari Polisi.

Baada ya nchi hii kuvamiwa na Nduli Iddi Amini mwaka 1978 walichaguliwa wapiganaji kwenda kupigana vita hiyo.

Bw. Mchotika alikuwa ni miongoni mwa askari waliochaguliwa kwenda kupambana na Iddi Amini.

Ni huko alikoanzia kupata matatizo hayo akiwa vitani nchini Uganda katika kambi ya Ohima.

Anasema, hapo ndipo afya yake ilipoanza kudhoofika na kupelekea umaskini alionao mpaka leo.

Ana watoto wawili ambao anakiri mwenyewe kuwa amewatelekeza wote tangu 1978 alivyoenda vitani na sasa familia yake(watoto na mke), inaishi asikokujua nchini Msumbuji.

Pia anakiri kwa masikitiko kuwa, hana mawasiliano nao tangu kutengana kwao na huko vitani, alienda kama askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU)

Anaomba yeyote mwenye mapenzi mema, kwa huruma na uwezo wake, amsaidie. Anapatikana magengeni, Kongowe wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani maeneo ya mpaka na manispaa ya Temeke, jijini Dar-Es-Salaam.

Mchungaji achukizwa na wanaouza majeneza

lAwashangaa wanaovaa dhahabu huku familia zinakufa kwa njaa

Na Elizabeth Steven

MCHUNGAJI mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), amesema hakuna anachochukizwa nacho na kumkera katika maisha yake, kama wafanyabishara ya majeneza kumtaka mnunuzi arudi tena.

Mchungaji huyo Heri Mwakabonga, wa KKKT usharika wa Mabibo jijini Dar-Es-Salaam, aliyasema hayo wakati akihubiri kanisani kwake katika ibada ya Jumapili iliyopita.

Alisema hapendezwi na kitendo cha kuambiwa "karibu tena " kwa kuwa kinaashiria wafanyabiashara hao wanaombea wenzao wafe ili wao wauze majeneza.

"Hakuna kitu kinachonichefua na kuniudhi katika maisha yangu, kama watu wanaochonga majeneza pale Muhimbili. Unapoenda kununua jeneza na kuondoka, eti wao wanakuambia karibu tena. Je, mimi nikaribie kwa ajili ya kuwanunulia wenzangu majeneza na kuwazika au...?" alihoji kwa mshangao.

Katika mahubiri yake siku hiyo, Mchungaji Mwakabonga alisema mapigano yanayoendelea nchini Israel baina ya Wapalestina na Waisrael, ni dalili kwamba huenda ikatokea Vita Kuu ya Tatu.

Alisema mapigano hayo yatakwisha pale tu, Yesu Kristo atakaporudi na akadai kuwa, huenda hata wanaopigana si maadui bali wana undugu baina yao.

Wakati huo huo: Mchungaji Mwakabonga ameilaumu tabia inayofanywa na baadhi ya akinamama kuendekeza kuvaa pete za dhahabu vidole vyote na kujivisha mavazi yenye thamani kubwa huku familia zao zikihangaika na hata kushinda au kulala na njaa.

Alisema mara nyingi tabia ya kuvaa mipete vidole vyote vya mikono, inafanywa na wakazi wa visiwani wanaoamini kuwa kwa kufanya hivyo, huvaa majini ambayo huwalinda nyumbani na katika ofisi zao.

"Wengine utamuona amevaa mipete ya dhahabu katika vidole vyao; ya maelfu na maelfu ya pesa na nguo za gharama ya juu na hata anatumia pesa nyingi kujisafisha safisha na marembo mengine lakini, nyumbani kwake ukifika utakuta familia yake inahangaika tu hata wakati mwingine, kulala na kushinda njaa," alisema kwa mshangao.

"Ukienda Zanzibar ukiona mwanamke anamipete ya dhahabu imejaa mkononi, ujue hayo ni majini ambayo wanaamini yanawalinda nyumbani mpaka ofisini lakini sisi wa Bara, tunaona kama urembo kumbe wenzetu kule wana maana yao," aliongeza.

Aidha, amewakemea makondakta wa magari ya abiria yanayojulikana kama daladala kwa kuitana "wanga" wanapomuona mwenzao akiwa nyuma au mbele yao na akadai kuwa, pamoja na kuwaita hivyo wenzao, wajue haipendezi hata wao wanapoitwa hivyo.

WAWATA Tarime wawashauri wanawake wenzao

Na Christopher Gamaina, Tarime

AKINAmama wa madhehebu mbalimbali, wameshauriwa kujiunga na kushiriki katika shughuli zinazojitokeza makanisani pamoja na kuanzisha vikundi ili waweze kujiendeleza vema katika shughuli za kiroho na kimwili wakisaidiana katika raha na taabu.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA), Parokia ya Tarime, katika Jimbo katoliki la Musoma, Bi. Elizabeth S. Makuti wakati alipokuwa akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake hivi karibuni.

Alisema kujiunga katika vikundi kama hivyo vya akina mama, kutawawezesha kuwa na umoja zaidi katika kuzalisha mali, kusaidiana katika matatizo na kufanya kwa ushirikiano kazi za Kanisa.

Akitoa mfano wa mradi wa WAWATA ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa na manufaa kwa wanachama wake, Bi. Makuti alisema ulianza mwaka 1987 ukishughulikia kilimo cha mahindi na ufuta.

Nyingine ni ushonaji, ususi, ufinyanzi, kutalizi, mapishi, malezi ya watoto na kutoa semina juu ya namna ya kumlea mama mjamzito, anayenyonyesha, mzee na familia kwa jumla.

"Tuna mgahawa ulioanza 1990 na duka la kuuzuia bidhaa tunazotengeneza wenyewe," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema mradi huo ni kwa ajili ya kuwawezesha akina mama kushiriki shughuli za kiroho kama mafungo, kufarijiana katika matatizo kadha, na kutoa chochote kwa wasiojiweza; pamoja na kuinua hali ya maisha ya akina mama na familia kwa ujumla.

Alieleza kuwa WAWATA hutoa semina juu ya Biblia, washiriki hutembeleana na kuhamasisha waamini katika jumuiya juu ya malezi ya vijana wao na ugonjwa wa Ukimwi pamoja na maradhi sugu kwa watoto na jinsi ya kujikinga, dalili na namna ya kumlea mgonjwa.

"Tunatoa semina kwa vijana wa sekondari na vyuo na wahitimu wa darasa la saba na ili wasijihusishe na uzinzi, ulevi na utumiaji wa madawa ya kulevya na kushiriki kikamilifu katika imani ya dini zao," alisema.

Hata hivyo alisema duka la WAWATA hivi sasa linakabiriwa na upungufu wa wateja kutokana na wingi wa maduka mjini hapa.

Aliwataka waamini kujua kuwa ni wajibu wao kulinyanyua duka hilo kwa kununua bidhaa zake kwani ni mali yao kama Wakristo Wakatoliki.

Alisema kutokana na shughuli hizo za WAWATA akina mama hupata mgao wa pesa, hununua mazao kwa bei nafuu na vifaa vya WAWATA, pia, hupata elimu kuwawezesha kuboresha maisha ya familia zao.

"Kwa kipindi hiki, tunatarajia kuanzisha mpango kabambe wa kuzidi kuboresha zaidi miradi yetu pamoja na huduma za kiroho na kimwili," alisema.

Wanaobaka, hawajui sheria ya ubakaji ilivyo - Hakimu

Na Vick Peter

HAKIMU wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Joseph Kayombo, ameishauri Serikali kuanzisha kazi maalumu kwa wanaume itakayoelimisha madhara ya ubakaji kwa kuwa wanaume wengi hawaelewi sheria ya ubakaji ilivyo.

Ushauri huo ameutoa mahakamani hapo wakati alipokuwa akisikiliza moja ya kesi za ubakaji iliyokuwa inamkabili Idd Abdalah(18) aliyefikishwa mahakamani hapo kwa kumbaka msichana wa miaka 15, Machi 13, mwaka huu.

Hakimu Kayombo amesema wengi wa wanaume wanaobaka huwa wanakuwa hawaelewi vizuri sheria ya kubaka ilivyo ndio maana vitendo vya ubakaji vinaongezeka siku hadi siku.

Aliendelea kusema kuwa, kwa kuwaelimisha wanaume wanaofanya vitendo vya ubakaji, tatizo la ubakaji linaweza kupungua au kutoweka kabisa.

"Naona serikali ikianzisha kozi maalumu kuhusu tatizo la ubakaji, tatizo hili linaweza kupungua kama siyo kuisha kabisa."

Alisema kama tatizo hili halitatatuliwa mapema, vitendo vya ubakaji vitazidi kuongezeka na wanaume wengi hasa vijana, watakuwa wanaathirika kwa kiasi fulani.

Aliendelea kuwa, haina budi kueleweka kwa wanaume kuwa, kitendo cha kufikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka hasa kumbaka msichana chini ya miaka 18 hata kama mlikubaliana ikiwa si kwa idhini ya wazazi, ni lazima hukumu ya miaka 30 itolewe kama adhabu.

"Kwa muda mrefu tumekuwa tukipokea kesi za kubaka na malalamiko yamekuwa yakitolewa na wazazi au walezi. Inabidi sisi kama mahakama, tuyapokee na kuyafanyia kazi na ikithibitika kuwa ni kweli, lazima adhabu kali itolewe," alisema.

Hakimu Kayombo aliamua kutoa somo hilo kwa wasikilizaji waliokuwa mahakamani hapo kama njia moja wapo ya kuwasaidia wanaofanya vitendo hivyo kuachana navyo.

Idd Abdallah(18) alifikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kubaka.

Mbele ya Hakimu Joseph Kayombo, Mwendesha Mashitaka, James Kasusura alidai kuwa, mtuhumiwa alifanya kosa hilo Machi 7, mwaka huu saa 3.00 usiku katika maeneo ya Temeke Mikoroshini kwa kumbaka msichana wa miaka 15.

Mtuhumiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini na kesi hiyyo imeahirishwa hadi Machi 27, mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena.

Mchungaji ashauri jamii kujiweka tayari

Na Leocardia Moswery

MCHUNGAJI Amani Dilunga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), usharika wa Mbagala katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, amesema njia sahihi ya kumfikia Mungu si kupata Sakramenti tu na kuzipuuzia bali ni kujiweka tayari wakati wote kumpokea Mungu.

Mchungaji Dilunga aliyasema hayo wakati akihubiri katika Ibada ya Jumapili iliyopita katika kanisa la KKKT, usharika wa Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema kosa ambalo wanadamu wamekuwa walikifanya, ni kukazania kuomba vitu na mali za duniani pekee badala ya kumuomba Mungu akufanikishe kuufikia ufalme wa mbinguni.

Alisema wengi wameelekeza juhudi zao katika maombi ya kupata mume, mke, mtoto, mali na vitu vingine badala ya kukazania neema za Mungu.

"Shida yetu, tunakazania sana kuomba kuwa sina mume, sina mke, ooh! Sina nyumba na kadhalika. Lakini tunasahau kuwa hivyo vyote ni mali ya ulimwenguni tu." Alisisitiza Mchungaji Dilunga.

Mchungaji huyo wa KKKT alisema hivi sasa ulimwengu umebadilika na kuelekea pabaya kutokana na wanajamii kukazania na kuthamini masuala ya starehe na anasa zaidi kuliko kutafuta mapenzi ya Mungu.

Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikichangia vifo mbalimbali kutokana na magonjwa ya zinaa na vifo vinavyotokana na uhalifu wa wanadamu.

Alisema kuwa zamani vifo vilitokea kwa nadra tofauti na ilivyo hali ya sasa ambapo watu wanakufa kwa wingi mithili ya ndege.

Aliwataka waamini wake kujiuliza kuwa wakati huu wa Kwaresima wanaomba vitu gani na akawataka waepuke tabia ya usengenyaji na kuzingatia kuomba yanayompendeza Mungu hasa katika kipindi hiki cha Mfungo ambacho ni sahihi kwa kuelekea mbinguni.

"Ni lazima tukae na kujiuliza kuwa Yesu anakwenda msalabani nasi tupo nyuma yake. Chukua maombi yako na umkabidhi Yesu kwa imani," alisema.

Wakati huo huo: Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania(TEC), Padre Pius Rutechura, alisema inashangaza kuona jamii ya watu inashangilia zaidi goli katika mchezo kuliko namna wanavyoshangilia utukufu wa Mungu. Padre Rutechura aliyasema hayo Jumapili iliyopita wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika katika kanisa dogo la TEC.

Alisema hadi sasa, bado kiasi cha nyuso kung’aa kanisani kwa furaha, hakijafikiwa na waamini wengi na akawataka kila mmoja kujitoa kwa nguvu zote kumshangilia Mungu.

Demokrasia Makini wasema Serikali haikujiandaa kwa vyama vingi

Na Gabriel Mduma

MUASISI wa chama cha siasa kilichopata usajili wa muda cha Demokrasia Makini, Profesa Leonard Shayo, amesema urasimu uliopo Tanzania wa kuanzisha vyama vya siasa, ni kielelezo kuwa serikali haikujindaa vema kwa sera ya vyama vingi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar-Es-Salaam, Profesa Shayo alisema endapo urasimu huu utaachiwa uendelee, nguvu ya upinzani itatoweka nchini jambo litakaloiwezesha CCM kuwa na nguvu siku zote.

"Mimi nazungumzia vyama vya siasa ambavyo vina miaka mingi vinahangaikia usajili wa kudumu, sizungumzii Demokrasia Makini pekee. Ukweli ni kuwa, kama kusingekuwa na urasimu wa kuvipatia usajili wa kudumu tungekuwa na mabadiliko ya uongozi" alisema na kuitaka serikali kuondoa woga inapofanya usajili.

Alisema chama cha Demokarasia Makini, kilishakamilisha hatua zote muhimu za kukiwezesha kupata usajili huo ikiwa ni pamoja kuwa na wanachama 200 katika kila mkoa katika mikoa 10 ya Tanzania bara na Visiwani.

"Nashangaa Msajili wa Vyama (George Liundi), hajafika katika mikoa hiyo kuhakiki kama sheria inavyosema licha ya kuahidi kufanya hivyo," alisema Profesa Shayo.

Aliongeza kuwa, Msajili aliwaandikia barua ya kufanya uhakiki katika mikoa hiyo wakianzia na Arusha lakini jambo la kushangaza, uongozi wa chama hicho ulikwenda Arusha kumsubiri kama barua yake ilivyosema lakini hakutokea.

Profesa Shayo alisema kitendo cha Msajili huyo kuzunguka na viongozi wa chama husika katika mikoa waliyokuwa na wanachama wasiopungua 200 ni kigumu hasa ukizingatia kuwa uwezo wa vyama hivi kifedha ni mdogo wa kuwawezesha kuzunguka katika mikoa yote.

Alisema urasimu huu ungekuwa na nafuu kubwa endapo serikali ingekuwa inatoa fungu maalumu kwa vyama hivyo kuweza kuzunguka na Msajili kuhakiki badala ya fungu hilo kutolewa katika Ofisi ya Msajili pekee.

Hata hivyo Prof. Shayo alipendekeza kuwa kutokana na uwezo duni wa vyama hivi kuweza kuzunguka mikoani na msajili kuhakiki, ni vyema akazunguka mwenyewe katika mikoa hiyo bila ya kushirikisha viongozi wakuu kwa vile katika mikoa hiyo, zipo ofisi za vyama hivyo na viongozi watakaoweza kuwaulizia.

Pia Profesa Shayo aliwataka Watanzania kuondokana na dhana potofu kuwa vyama vya siasa vipo kwa manufaa ya viongozi wake tu kifedha badala yake, aliwataka kuvipa misaada ya hali na mali ili vistawi kwani vyama hivyo ndivyo vitakavyotoa mchango wa kuibadilisha jamii ya Watanzania.

SUALA LA KUBINAFSISHA MASOKO.....

MUMADA washikilia msimamo; hawataki

l Asiyesafisha soko, kufikishwa polisi, au kufukuzwa sokoni?

Dalphina Rubyema na Getrude Madembwe

CHAMA cha Wafanyabiashara ya Masoko Mkoani Dar-Es-Salaam(MUMADA), kinazidi kushikilia msimamo wake wa kupinga suala la ubinafsishaji wa masomo kama ilivyoangizwa hapo awali na Tume ya Jiji.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu wa MUMsADA, Bw. Hemed Panzi, katika mkutano wa wafanyabiashara uliofanyika hivi karibuni sokoni Tandika katika Manispaa ya Temeke, mkoani Dar-Es-Salaam.

Bw. Panzi ambaye alikuwa mmoja wa wageni waalikwa katika mkutano huo, alisema kuwa kama manispaa zimeshindwa kuendeleza masoko hayo, ni bora wayakabidhi mikononi mwa wafanyabiashara wenyewe badala ya kuyabinafsisha kwa watu wengine.

"Watukabidhi sisi wafanyabiashara tutajua namna ya kuyaendesha kwani tunaelewa fika matatizo ya masoko hayo... lakini, kutuambia kuwa wayabinafsishe kwa watu binafsi au kampuni, sisi hatuko tayari" alisema.

Pia, ameitaka serikali kutambua umuhimu wa wafanyabiashara ndogondogo kama wa masoko badala ya kuwavua utu wao.

"Tunavuliwa hata thamani ya kufanyabiashara. Serikali itambue kuwa sisi hatutofautiani. Biashara yetu ingawa ni ndogo, ipo katika saizi ya biashara," alisema.

Wakati huo huo: Wafanyabiashara hao wameitaka Manispaa ya Temeke kufanya ukarabati sokoni hapo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma ya choo badala ya kukusanya ushuru na kuingia "mitini".

Wito huo umefuatia taarifa ya utendaji kutoka kwa Mwenyekiti wa Soko kuwa soko hilo, halina choo. Hali hiyo ilidaiwa kuwa unyimwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji kwa wafanyabiashara.

Aidha, ilipendekezwa kuwa mfanyabiashara yeyote atakayebainika kukiuka sheria za usafi, afukuzwe toka katika eneo lake.

Wajumbe wawili Bw. Mohamed Abdalah na Bw. Masenge S. Masenge, walitoa pendekezo kuwa mtu huyo afukuzwe na mjumbe mmoja Bw. Issa Bendera alipendekeza kuwa mtu huyo apelekwe polisi.

Akitoa salamu zake katika mkutano huo, Diwani wa kata ya Tandika Bw. Salehe Msoka, alisema bajeti ya Manispaa, imelipa kipaumbele suala la ukarabati wa masoko mbalimbali ya Manispaa likiwemo la Tandika.

Bw. Msoka aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisema kulingana na bajeti soko hilo, litafanyiwa ukarabati wa vyoo, barabara pamoja na kuwekewa mifereji ya kutoa maji machafu na kujengewa uzio.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Tandika Bw. Anzamen Samweli Manzari, amewataka wafanyabiashara hao kuunda kikundi maalumu cha ulinzi(sungusungu) kitakachosaidia kuimarisha ulinzi.

Tumieni Upadre wenu kuwasaidia waathirika wa UKIMWI- Wito

Na Mwandishi Wetu, Njombe

"TUMIENI Upadre wenu kuwasaidia walioathirika kwa UKIMWI, mkiwaonesha upendo wenu huku mnazingatia kwamba, jamii ina matumaini kwa Mungu."

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Utume wa Walei katika Jimbo Katoliki la Njombe, Padre James Chaula, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne ya ushauri nasaha kwa waathirika na wasio waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI.

Mafunzo hayo yaliyowahusisha mapadre wa Kanisa Katoliki jimboni Njombe, yalitolewa na wataalamu wa afya kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kudhaminiwa na Kanisa katoliki jimboni humo.

Jumla ya mapadre 12 wa Kanisa Katoliki jimboni humo, walihitimu mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika kituo cha Nazareth cha mjini hapa.

Walifundishwa mambo kadha juu ya UKIMWI ikiwa ni pamoja na historia ya ugonjwa huo mkoani Iringa na duniani kote.

Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi huyo wa Utume wa Walei jimboni, aliwataka mapadre hao kuifanya ipasavyo, kazi ya kutoa ushauri nasaha kwa walioathirika na wasioathirika na UKIMWI ili kutoa matumaini kwa waathirika na kuionesha jamii namna ya kujiepusha na janga la ugonjwa huu.

Alisema mapadre wote hawana budi kuzingatia zaidi kuwa wao ni wakombozi wa jamii kuhusu janga la ugonjwa huo.

Habari zilizopatikana toka kwa Mratibu wa Kitengo cha kupambana na UKIMWI jimboni humo, Padre Chrispin Mligo, zinasema mapadre hao watatoa huduma yao kwa wananchi wote wanaoishi katika katika parokia zao bila ubaguzi wa kidini wala kimadhehebu.

Wafungwa Waanglikana wakosa Injili

Na Neema Dawson

KANISA la Kianglikana katika Dayosisi ya Dar-Es-Salaam, halijatoa huduma ya kiroho kwa wafungwa waliopo katika magereza ya dayosisi hiyo kwa takriban miezi mitatu sasa kutokana na kifo cha mchungaji aliyekuwa akishughulikia magereza hiyo.

Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zimesema kutokana na kifo cha Mchungaji Canon Leonard Kamunga miezi mitatu iliyopita, Kanisa hilo la Kianglikana halijaanza kutoa huduma ya Injili kwa wafungwa wa eneo lake kutokana na kukosekana kwa mchungaji mingine mwenye sifa za kuhudumia wafungwa.

Uongozi wa Kanisa la Kianglikana, dayosisi ya Dar-Es-salaam, umekirik kuwapo kwa hali hiyo na kusema unashughulikia kupata ufumbuzi wake.

Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi hiyo, , Mchungaji Canon Eliya Mtokambali, alisema kuwa kanisa linafahamu hali hiyo na linashughulikia ufumbuzi wake unaoonekana kuwa mgumu kutokana na ukweli kuwa siyo mchungaji yeyote anaweza kutoa huduma ya kiroho kwa wafungwa.

Alisema wafungwa wanahitaji mchungaji mwenye uzoefu wa hali ya juu kwa kuwa tabia zao zimekwisha athirika kutokana na makosa ambayo wamekuwa wakiyafanya kabla ya vifungo na hata kutokana na maisha waliyo nayo sasa katika magereza.

"Unajua hawa wafungwa wanakuwa wameathirika kisaikolojia hivyo, wanahitaji mchungaji mwepesi wa kumsoma mtu na kumuelewa. Mwenye huruma na upendo wa kuwaona wafungwa kuwa sawa na yeye bila kuwa na hasira dhidi yao," alisema Canon Mtokambali.

Alisema hii ni kutokana na ukweli kuwa wakati mwingine wafungwa hata katika mafundisho wengine hutoa maneno yasiyofaa hivyo wanahaitaji uvumuilivu wa kutosha.

Aliongeza kuwa, kanisa lake haliwezi kukaa kimya kwa kuwa linafahamu umuhimu wa kuwainjilisha wafungwa ili kila mmoja atambue makosa yake na kuyajutia rohoni mwake. Aliongeza kuwa hali hiyo inawasaidia wafungwa kubadili tabia wanapomaliza adhabu zao.

"Tunatoa Sakramenti za Ubatizo kwa wafungwa na tunawasisitiza wachungaji wa madhehebu mengine ambao tayari wana vibali vya serikali, kuhakikisha kuwa hawakosi kutoa huduma hizo gerezani, " alisema Canon Mtokambali.

Kwa kawaida, ili kiongozi yeyote apate nafasi ya kuhubiri kwa wafungwa, ni lazima yeye na kanisa lake, watume maombi maalumu serikalini na kukubaliwa. Hii ni kwakuwa magereza ni sehemu nyeti zinazohitaji ulinzi na usalama wa kutosha.

Kama Yesu, nae alitoa sauti kuu, akakata roho

Na Mwandishi Wetu

"Tulimzoea Ndugu Vincenzo kwani hakuwa na makuu na alipenda kuongea na kila mtu. Ingawa alikuwa na mwili wa kutisha, hatukumuogopa maana alikuwa mpole. Ingawa alikuwa mzee, hatukutegemea kuwa leo tutamuaga na kumzika."

"Jumapili tulishtushwa. Aliletwa kutoka Mlali na alilazwa katika Hospitali ya Mikocheni(Dar-Es-Salaam). Jumatatu tulimkuta hana ufahamu, anavuta pumzi kwa shida, madaktari na wauguzi wakajaribu kumsaidia.

Lakini usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano, alikohoa na kutapika. Saa 9, alikohoa kwa sauti kubwa.

Ndugu Steven aliyekesha karibu naye na wauguzi walistuka kwa sauti ile ya mshindo. Ilikuwa sauti yake ya mwisho duniani. Akakata roho kama Yesu Msalabani mnamo saa 9 mchana."

Maneno ya huzuni yalisemwa na Ndugu Donat Moeller, wakati wa homilia ya mazishi ya Ndugu Vicenzo Gherardini, yaliyofanyika Msimbazi jijini Dar-Es-Salaam, Machi 10, 2001.

Alifariki Machi 7, 2001, kwa ugonjwa wa kiharusi wa muda mfupi.

Tangu mwaka 1999, marehemu alikuwa katika Kituo cha Mafunzo ya Kiroho, Mbagala jijini Dar-Es-Salaam kama Mshauri na Muungamishi.

Kwa muda mrefu, alikuwa mwanashirika wa Jumuiya ya FOKOLARI, shirika (Movement) la kutafakari na kuishi Injili katika jumuiya Ndogondogo.

Mazishi yalihudhuriwa na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Balozi wa Vatican nchini, Mhashamu Askofu Mkuu, Luigi Pezzuto, mapadre, masista, wawakilishi toka Dodoma, Mahenge, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimisionari nchini.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polyacarp Kardinali Pengo ambaye aliongoza misa ya mazishi, alisema upungufu wa wamisionari nchini, haupaswi kuwafanya wamisionari waliopo kujiona wako ugenini bali wajue na kujiona kuwa wako nyumbani kwao na kwamba Padre Vincenzo hakuzikwa ugenini bali nyumbani pake.

Alisisitiza kuwa hata kama huko Ulaya wanakotoka wamisionari, ni wachache na wanazidi kupungua, bado ni muhimu nchini na wanahitajika kwa kiasi kikubwa.

"Hata kama mumebaki watano, tunaomba mbaki na watatu; wawili mtuletee. umuhimu wa wamisionari bado ni mkubwa kwa Watanzania," alisema Kardinali Pengo.

Provinsiali wa Wakapuchini nchini tanzania, BeatusKinyaia, aliwashukuru wote walioshiriki katika msiba huo na akaomba ushirikiano wa namna hiyo, uimarishwe zaidi katika jamii.

Naye Provinsiali wa TOSKANA Ndugu Stephen alisema, "Na sisi tumefarijika kuona Ndugu huyu, amekufa na kuzikwa nyumbani kama alivyosema Kardinali."

"Mwaka 1924 Padre Vincent, alizaliwa jijini Roma, Italia na Yesu alimwita mara ya kwanza katika ubatizo, akamshirikisha katika kifo chake, na hatimaye kufufuka kwake", alisema Ndugu Donat na kuongeza alijiunga na Ndugu Wakapuchini akiwa na miaka 25.

Aliingia Provinsya ya Florence akafuata hatua za malezi na.mwaka 1952 aliweka nadhiri za maisha na baadaye mwaka 1956,akapewa Daraja ya Upadre na kufanya kazi ya uchungaji kama Mshauri wa vijana waliofungwa gerezani na pia, alikuwa Mshauri wa Idara ya Papa(ONARMO).

Mwaka 1968, alitumwa Tanzania kama Mmisionari.Tangu mwaka 1963, Idara ya papa ya kueneza Injili, iliwakabidhi Wakapuchini wa Provinsya ya Toskana eneo la Mpwapwa jimboni Dodoma.

Aliwahi kuwa paroko wa Kibakwe na Mlali na kisha akaanzisha parokia ya Rudi.

Mara nyingi marehemu alipenda kusisitiza kuwa KUWA MKAPUCHINI MAANA YAKE KUISHI NA YESU, KUMSHUHUDIA YESU SIYOKUENDESHA PAROKIA TU.

1984 hadi 1991, alikuwa mhudumu katika nyumba ya novisiati Kasita, Mahenge. pia alikaa Morogoro akiwa Mshauri wa Wafransisko Wasekulari kitaifa. Tangu mwaka 1993, alichaguliwa kuwa mhudumu wa

Ndugu Wakapuchini katika eneo la mpwapwa na alikaa Mlali katika kituo cha watoto wenye ulemavu kwa mika miaka 3.

Aidha mwaka 1996 hadi 1999 alihudumia masista wa Mtakatifu Klara, yaani Waklara mafukara ambao ni shirika la pili la Mtakatifu Fransisko wanaoishi huko Ruhuwiko, Songea.

APUMZIKE KWA AMANI AMINA