Make your own free website on Tripod.com

NCCR wataka viongozi wa dini wasinyanyaswe

l Wasema penye dosari, lazima dini ziseme

l Wadai anayepinga ukweli huo, hajui maana ya dini

Na Getrude Madembwe

CHAMA cha siasa cha NCCR-Mageuzi, kimelaumu vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali na vikundi vya dini, kuwalaumu viongozi wengine wa dini kutokana nakukosoa katika misingi ya uwazi na ukweli linapotokea kosa katika jamii.

KATIBU Mwenezi wa chama hicho, Bw. Joseph Selasini alisema katika mazungumzo yake na KIONGOZI yalipo Makao Makuu ya chama jijini, Dar-Es-Salaam katikati ya juma kuwa, kitendo cha kutaka kuwawekea mipaka viongozi wa dini katika kazi zao za kutangaza Neno la Mungu na kudumisha amani, ni kuwanyima haki zao na kuwalazimisha kutowajibika katika jamii kitu ambacho ni kinyume na mwito wao wa kufanya kazi ya Mungu.

Selasini alisema viongozi wa dini ni raia wenye haki sawa katika nchi hivyo, kuwazuia kutoa michango yao ya mawazo na kuzungumzia mambo ya msingi nchini mwao, ni kutowatendea haki na kutokujua maana halisi ya dini.

Baadhi ya wanasiasa na viongozi kadha wa kidini, aidha kwa kutokujua walifanyalo au kwa chuki za kibinafsi, wamekuwa wakiwalaumu na hata wengine kudiriki kuwaombea dua baya, viongozi wa vikundi vya dini wanaokuwa wakweli na kukosoa jamii bila unafiki juu ya makosa yanayojitokeza na kutoa angalisho la Kimungu.

"Unajua viongozi wa dini waliapa kutenda na kutetea yaliyo mema; sasa kwa nini wakae kimya wakati wanaona mambo yanakwenda vibaya?" alihoji Selasini na kuongeza,

"Kiongozi yeyote wa kidini anayekaa kimya huku vitendo vinavyofanywa siyo vizuri, na wengine(viongozi wa dini)

kuviunga mkono, huyo hafai kabisa kwa kuwa hataki waamini wawe katika hali ya usalama, amani na upendo."

Akisisitiza kauli yake, Selasini alitoa mfano kuwa iwapo kiongozi wa kidini ameona hali iliyopo katika nchi si nzuri akasema ili viongozi wa kisiasa wapatane na kuondoa chuki miongoni mwao kisha akatokea muumini wa madhehebu yoyote na kusema kuwa kiongozi huyu na serikali ni kitu kimoja, basi mtu huyo hafai kwa kuwa upeo wake wa kuelewa mambo ni finyu.

"Sasa kiongozi wa dini anasema tupatane; halafu mtu mwingine anakuja na kusema eti huyu na serikali ni kitu kimoja; kweli mtu huyo anafaa?" alihoji.

Alisema inashangaza kuwaona viongozi aidha wa kisiasa au kidini kuitisha mikutano na badala ya kuzungumzia mambo ya vyama au vikundi vyao vya dini kwa lengo la kuimarisha upendo na mshikamano, wanaanza kuwadharau na kuwahubiria viongozi wa vikundi vingine vya dini na akasema huko ni kutojua umuhimu na majukumu yao.

Selasini alisema hali hiyo isipopingwa na hata kudhibitiwa na jamii nzima yenye mapenzi mema ya kimungu kwa taifa, italiangamiza taifa na kulipeleka pabaya kutokana na mgawanyiko wanaoujenga miongoni mwa jamii hali ambayo ni hatari kimwili na kiroho.

"Kama dini au chama kimeamua kufanya mkutano wowote; wawe na kauli nzuri na siyo kuanza kuwatukana viongozi wengine wa kidini au wa chama kwani wakifanya hivyo, utakuwa ni uchochezi na tutaipoteza amani hii tuliyonayo," alionya Selasini.

Hivi karibuni gazeti moja litolewalo kila siku nchini kwa lugha ya Kiswahili, liliripoti kuwa Jumapili iliyopita, Waislamu wa madhehebu mbalimbali jijini Dar-Es-Salaam, walisoma dua maalumu ya kumlaani Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, pamoja na serikali eti kwa madai kuwa wanawakandamiza Waislamu. Hatua hiyo imelaumiwa na wakazi wengi wa jijini wakiwamo baadhi ya Waislamu ambao hawakutaka majina yao yatajwe.

Mhadhara huo uliofanyika katika viwanja vya Jangwani, na uliongozwa na Sheikh Rico.

Apigwa risasi kwa kukaidi kucheza zeze kilioni

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Mwanamke Magreth Owino (27) wa kijiji cha Rwang’enyi kata ya Nyamtinga wilayani Tarime, anaendelea kuuguza jeraha baada ya kupigwa risasi kwa kukaidi kucheza zeze kilioni.

Kwa mujibu wa binamu wa Bibi Owino, Bw.Jumanne Hassan, mkazi wa kijiji cha Omoche, katika tarafa ya Nyancha, tangu kutokea kwa tukio hilo, Oktoba mwaka jana, bado hali ya majeruhi ni mbaya na kwamba bado anasumbuliwa na maumivu makali.

Jumanne alisema tukio hilo lilitokea usiku wakati umati wa waombolezaji walipokuwa wakicheza muziki katika matanga kufuatia kifo cha Kadogo Tenga.

Alisema wakati wanaendelea kucheza, kaka wa marehemu, Bw. Leonard Tenga, alijitokeza na kuwaamuru wanawake wote waliokuwa kilioni hapa kuungana kucheza zeze(ngoma ya asili).

"Wengine akiwamo Mama Magreth wakagoma kwa kuwa waliona haiwezekani wacheze wamechanganyika na vijana wao" alisema Jumanne na kuongeza, "... kuona hivyo jamaa(Lenard), aliingia kwa hasira chumbani kwake na mara katoka na bastola akaanza kufyatua risasi ovyoovyo ambapo ya nne ndiyo ilimpiga."

Alisema baada ya kupigwa risasi hiyo katika bega la kulia na kuvunja mfupa alipelekwa katika hospitali binafsi ya RAO(RAO Hospital) aliposhonwa bila kutolewa risasi ambayo bado ilikuwa mkononi.

Jumanne aliendelea kueleza kuwa baada ya kuona hali ya majeruhi inazidi kuwa mbaya,walimhamishia katika Hospitali ya Shirati iliyopo wilayani Tarime na kwamba atatolewa risasi baada ya jeraha kupona.

Alisema ili kukwepa kugundulika kazini kwake katika Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Mwanza, badala ya kuandikisha jina la Leonard Tenga, katika kituo cha polisi cha Mjini Tarime, mtuhumiwa aliandikisha jina la Wiva Tenga.

Habari zilizopatikana toka hospitali ya Wilaya ya Tarime, zinasema kaimu mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Albogust Kululetela, amekwisha toa kibali cha kumpeleka Bibi Owino katika Hospitali ya Bugando ya jijini Mwanza.

250 kuhudhuria mkutano wa AMECEA Tanzania

Na Mwandishi Wetu

KATI ya wajumbe 250 kutoka nchi mbalimbali, wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi za Afrika Mashariki na Kati(AMECEA-2002) unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2002.

Katika kufanikisha mkutano huo unaotarajiwa kufanyika jijini Dar-Es-Salaam, katikati ya Mwaka 2002, Maaskofu Wakatoliki Tanzania, wametoa wito kwa waamini kote nchini kulipokea jukumu hili kama heshima kwa Kanisa la Tanzania na hivyo, kuchangia kwa hali na mali kuufanikisha mkutano huo.

Katika Mkutano wao wa 37 wa Kamati Tendaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), uliofanyika Kurasini jijini Dar-Es-Salaam, kati ya Februari 21 na 23, mwaka huu chini ya Rais wa TEC, Mhashamu Severine NiweMugizi, maaskofu walisisitiza ukweli kuwa kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania, ni neema na heshima kwa Wakatoliki nchini na taifa kwa jumla.

Katika mkutano huo wa Kamati Tendaji ambao kwa kawaida huhudhuriwa na Maaskofu Wenyeviti wa idara mbalimbali za TEC, jumla ya shilingi 1,435,000, zilichangwa ili kuunga mkono juhudi za ufanikishaji wa mkutano huo ambao maandalizi yake yanaendelea.

Mwandishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Raphael Kilumanga, alisisitiza haja ya Wakatoliki na Watanzania wote kujionea ufahari kufuatia mkutano huo kufanyika nchini.

"Wakristo Watanzania hatuna budi kujua kuwa hii ni hadhi na heshima ya pekee kwa Tanzania tuliyotupiwa kama mpira wa kutafutia goli la ushindi," alisema Padre Kilumanga na kuongeza,

"Ilikuwa kama mazoea mkutano huo kufanyika katika nchi nyingine lakini sasa, ni heshima kwa Watanzania. Inabidi kila mmoja ajivunie na kutumia juhudi zake zote kuufanikisha kwa kuwa sasa mataifa kote ulimwenguni yanatuangalia tutanya nini kizuri."

Padre Kilumanga alisisitiza kuwa, ili kuufanikisha mkutano huo, mioyo ya ukarimu haina budi kuimarishwa zaidi miongoni mwa jamii ya Wakristo na Watanzania wote kwa jumla.

Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya nchi za Afrika Mashariki na Kati, unazihusisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia, Sudan, Malawi, Ethiopia na Eritrea na ulianzishwa nchini Tanzania mwaka 1961.

Kufanyika kwa mkutano wake nchini mwaka 2002, ni historia ya pekee katika karne na milenia mpya.

... Hatutaogopa kukemea uovu - Kanisa Katoliki

Na Elizabeth Steven

KIONGOZI mmoja wa kanisa Katoliki nchini, amesema kanisa halitaogopa kushikilia msimamo wake wa kukemea vitendo haramu vya utoaji mimba, uzinzi na uasherati eti kwa lengo la kuwa na wafuasi wengi zaidi.

Padre Aloyce Ngitu, aliyasema hayo Jumapili iliyopita wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika katika kanisa la Mwenyeheri Anuarite la Makuburi katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Alisema baadhi ya watu wenye imani duni na wanaotetea vitendo viovu kama utoaji mimba, ndoa za watu wa jinsia moja pamoja na matumizi ya mipira ya kiume, wamekuwa wakikimbia kanisa kwa kuwa wanashindwa kumudu taratibu hizo zinazoendana na maadili ya Kimungu.

Alisema wengine wasiojua walifanyalo, wamekuwa wakihama dhehebu kwa madai kuwa hayaponyi lakini wanashindwa kujua kuwa anayeponya ni Mungu na si vinginevyo.

Padre Ngitu alisistiza kuwa kamwe Kanisa halitasita kuendelea na msimamo wake wa kutoa mafunzo sahihi ya maadili na kukemea maadili yanapokiukwa na kuwataka waamini wote kuwa imara kupambana na vishawishi vyote.

"Ni muhimu kila mmoja kuishi kuzingatia kuishi katika imani thabiti. Lazima mjue kuwa ni dhambi kukubali na kuviruhusu vishawishi vinginevyo vishawishi hivyo havitaisha na tutakuwa navyo hadi kuingia kaburini," alisema.

Mbunge wa CCM awachachamalia wanaozuia wanasiasa kusali

Na Neema Dawson

MBUNGE wa Wanawake kwa Viti Maalumu(CCM), Bi. Rhoda Khatano, amewashangaa wanaowastajabia wanasiasa wanapojihusisha na masuala ya kiroho kwa kuwa katika ufalme wa Mungu, hakuna ubaguzi wa kisiasa.

Alisema inashangaza kwa baadhi ya wanajamii kuwachukulia viongozi wa kiserikali na wanasiasa kama watu wasiostahili kuabudu na kujihusisha na mambo ya kiroho.

Akizungumza katika kanisa la Tanzania Assemblies of God(TAG) la Mikocheni B. jijini Dar-Es-Salaam, alipoalikwa na Wanawake Watumishi wa Kristo(WWK).

Katika sherehe za umoja huo zilizofanyika kanisani hapo, mbunge huyo alisema,

"Inashangaza sana kuona watu wanavyotuchukulia vibaya sisi wanasiasa wanapotuona makanisani utafikiri sisi hatuna madhehebu na wala hatustahili kumjua Mungu"Katika sherehe hizo, WWK walionesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na wanawake na pia, wajibu wa mwanamke Mkristo katika kanisa la Mungu.

Aliwafananisha wanawake na meli mpya inayofanyakazi vema kwa kuwa vifaa vyake bado vipya na imara na hivyo, wana mchango katika kuliendeleza Kanisa popote ulimwenguni.

Bibi Khatano alisema wanawake ni mfano bora wa taa ambayo pindi inapowashwa , haina budi kuachwa ili aingaze.

"Sasa taa ukiiwasha na kuifunika, huwezi kuona kabisa lazima uiweke wazi iangaze. Na ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kila siku," alisema.

Katika sherehe hizo, Mchungaji wa kanisa hilo la TAG, Ilala, Titus Mkama, aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kuliendeleza kanisa na pia, kuwa walezi na washauri wazuri kwa watoto.

Alisema dunia iliyo nje ya kanisa, haina maadili mema ya kijamii na ki-Mungu na kwamba njia pekee ya kuliondoa tatizo hilo ni kuwajenga watoto na kuwaelekeza katika kujua maadili mema huku wakijenga utamaduni wa kujishughulisha na masuala ya Kanisa kwa karibu.

Sherehe hizo zilizohudhuriwa pia na Kiongozi wa TAG, Mikocheni B, Getrude Rwakatale, zilihudhuriwa pia na baadhi ya wanawake toka Umoja wa Makanisa toka Mombasa nchini Kenya, Bibi Aida Bruno na Neli Kigendu.

Wakati huo huo: Katika ibada ya Jumapili iliyopita, Mchungaji Julius Lugendo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), usharika wa Kariakoo katika D ayosisi ya Mashariki na Pwani, amewataka wakristo kudumu katika imani wanapokumbwa na matatizo yakiwamo magonjwa badala ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji ambako hujihusisha na imani za kishirikina.

""Mateso kama magonjwa yasiwafanye kupokea ushauri usiofaa kama ule wa kupoteza pesa kwenda kupiga ramli kwa waganga wa kienyeji. Yesu ndiye anayeweza kutibu magonjwa hayo yote endapo utamkiri na kumuamini katika maisha yako," alisema Mchungaji Lugendo.

Mwenyekiti wa kijiji awachinjia Waislamu ng'ombe watatu

Neema Dawson na Leocardia Moswery, Mkuranga

MWENYEKITI wa kijiji cha Kipara wilayani Mkuranga katika mkoa wa Pwani, Bw.Choba M.Bariko, amechinja ng’ombe watatu na kuwagawia nyama ya bure, wakazi wa vijiji vya Kipara, Kiberewele na Kichangani ambao ni Waislamu.

Jumatano iliyopita gazeti hili liliwashuhudia baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wakiwa katika makundi mbalimbali wakitoka kupata mgao huo ambapo kila mmoja wa wakazi wa vijijini hivyo, anayejulika kuwa muumini wa dini ya Kiislamu, alipata takriban kilo moja ya nyama.

Katika mgao huo, familia yenye watu wengi ilijipatia kiasi kikubwa cha nyama; hali hiyo ilitokana na baadhi yao kutumia mwanya wa kuwa na watoto wengi kujipatia mizigo ya nyama baada ya kurudia kiujanjaujanja.

Wandishi walipomuuliza Mwenyekiti huyo wa kijiji sababu ya kufanya hivyo, alisema kuwa ni kufuatana na mafundisho ya dini yao ya Kiislamu juu ya kutoa sadaka hasa katika kipindi cha sikukuu kama hiyo ya Idd -El Haji.

"Katika siku kama hizi, ni lazima utoe au uchinje kama sadaka kwa Mungu. Lakini kama hauna, haulazimishwi," alisema Mwenyekiti huyo Bw.Choba.

Bw. Choba alisema alifanya ugawaji wa nyama hiyo katika misikiti na vitongoji vya vijiji hivyo.

Msichague viongozi kwa sura - Mchungaji

Na Neema Dawson

MCHUNGAJI George Mrekano wa Chuo cha Biblia cha St. Marks cha Buguruni jijini Dar-Es-Salaam, amewataka Wakristo kuwachagua viongozi watakaowafikisha katika kilele cha maendeleo kutokana na uwajibikaji wao.

Aliyasema hayo katika ibada ya uchaguzi wa viongozi wa Kanisa la Kianglikana la Mtakatifu Mariamu iliyofanyika Jumapili iliyopita baada ya uongozi uliopita kumaliza kipindi cha miaka miwili.

Mchungaji huyo alisdema kikanisa, hata ambao hawakuchaguliwa katika uchaguzi huo ni viongozi kwa kuwa ushirikiano na ushauri wao ni muhimu ili viongozi hao wafanikishe majukumu yao kwa jamii.

"Kiongozi yeyote anachaguliwa kwa uwezo wa Mungu na Mungu huyohuyo ndiye anayetuandalia. Kiongozi hachaguliwi kwa kuangalia sura bali kwa kuzingatia uwajibikaji," alisema.

Waliochaguliwa ni pamoja na Katibu wa Mtaa, George Chambo, Mshauri wa Kristo Shembarankene, Mweka Hazina, Anna Leiy na atakayekuwa Mshauri wa Mchungaji, ni Theodor Marito pamoja na viongozi kumi wa mitaa kumi waliosimikwa Jumapili iliyopita.

Wakati huo huo: Mchungaji Julius Lugendo,amewataka waamini wa Kikristo, kutoogopa kutengwa na jamii wakati wa juhudi zao za kutimiza mapenzi ya Mungu.

Alisema hayo katika mahubiri yaliyoandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Kariakoo ambapo mchungaji huyo alialikwa kuhubiri hivi karibuni.

Wakatoliki wahimizwa kujiunga katika jumuiya

Na Vick Peter

WAKATOLIKI wametakiwa kuelewa umuhimu wa kujiunga na jumuiya ndogondogo za Kikristo kwani ndiyo njia pekee inayoweza kuwaweka karibu zaidi na kanisa hasa wakati wa uhitaji wa huduma za kiroho.

Akizungumza wakati wa ibada iliyofanyika hivi karibuni, Paroko wa Parokia ya Chang’ombe, Padre Andrea Komba, alisema kuwa inakuwa vigumu kwa mtu ambaye hayupo katika jumuiya yoyote kupata msaada kwa wakati muafaka kufuatia taratibu zilizowekwa na uongozi wa Kanisa kwamba, ni lazima mtu apitie kwenye jumuiya ndogondogo ili aweze kusaidiwa.

Alisema kuwaingawa mtu anaweza kuwa muumini mzuri kwa kanisa fulani lakini, endapo hayupo katika jumuiya mojawapo ya waamini hususani jumuiya ndogondogo za Kikristo, inakuwa vigumu kwa Kanisa kumsaidia hasa wakati wa mahitaji ya huduma za kiroho.

Padre Komba alisema jumuiya ndogondogo zilianzishwa kwa lengo la kuwaweka waamini karibu zaidi na Kanisa lakini, inashangaza kusikia kwamba wapo waamini ambao bado hawajajiunga na jumuiya hizo.

Alisema kuwa tatizo kubwa ni baadhi ya waamini kusubiri hadi wanapoona wanahitaji huduma au wana tatizo ndipo huanza kuhangaika.

Aidha aliwataka waamini kuelewa kuwa, inakuwa vigumu kwa Kanisa kumsaidia mtu ambaye si mmoja katika jumuiya hizo kwani wao wanapokea maombi kupitia jumuiya anayotoka mhitaji huduma anatoka.

Padre Komba aliwataka waamini wajiunge mara moja na jumuiya hizo ili yasijetokea matatizo hasa wakati wa uhitaji wa huduma ya kiroho.

Kinanda cha TEC sasa chadai laki1.8/=

Na Leocardia Moswery

BAADA ya Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu askofu Aloycius Balina, kuchangia shilingi 100,000/= sasa kinanda cha kanisa la TEC, bado kinadai shilingi 183,835 ili kufikia kiasi cha pesa zinazohitajika kukinunua.

Kufuatia mchango huo wa Askofu Balina, sasa zimepatikana shilingi 216,165 kati ya 400,000 zilizokuwa zinahitajika awali ili kukamilisha malipo ya kinanda kinachogharimu shilingi 600,000.

Akitoa taarifa ya mchango huo mwishoni mwa juma, "Paroko" wa Kanisa la TEC, Padre Elias Msemwa, alisema kuwa baada ya mchango huo wa Askofu B ika shilingi 183,835 na kwamba juhudi za makusudi za hali na mali za waamini, hazinabudi kuongezwa ili kufanikisha lengo hilo.

Padre Msemwa ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Elimu wa TEC na Kaimu Katibu Mtendaji wa Idara ya Kichungaji, aliwataka waamini wengine wa ngqzi zote kuiga mfano wa kujitolea kuchangia kinanda hicho kama alivyofanya Askofu Balina.

Alisema katika kufanikisha mambo yanayohusu shughuli za kanisa, si vema kuchangia huku ukizingatia unatoka katika parokia au jimbo gani kwa kuwa Kanisa ni moja Katoliki na Injili inayotangazwa ni ya Yesu Kristo mmoja.

Nusu ya walioingia sekondari Ulanga, walishindwa darasa la saba

Na Ndechongio Charles, Morogoro

ZAIDI ya asilimia 50 ya wasichana waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, walishindwa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Bw. Halfani Hidda, inaonesha kuwa, katika kipindi hicho, jumla ya wasichana 268 walichaguliwa kwenda sekondari pasipo kufaulu.

Imefafanua kuwa mwaka 1998, wasichana waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza bila kufaulu ni 117 na mwaka 1999 walipungua hadi kufikia 12. Mwaka jana waliongezeka 139.

Hidda alisema katika taarifa kuwa wilaya hulazimika kufanya hivyo kutokana na wasichana wengi kutofikia kiwango cha kufaulu ambacho ni alama 61 kati ya 150 ili kutosheleza mahitaji ya wasichana katika shule za sekondari ambayo katika miaka 3 iliyopita, walikuwa 524.

Takwimu zinaonesha kuwa wasichana waliofaulu mitihani ya darasa la Saba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ni 259 sawa na asilimia 7.5 ya wasichana 3438 waliofanya mitihani.

Taarifa imeongeza kuwa hali hiyo imeathiri kiwango cha taaluma katika shule za sekondari za Mwaya na Igota wilayani Ulanga ambazo zimekuwa zikichukuwa wanafunzi wenye alama hadi 34 kati ya 150.

Wakati huo huo: zaidi ya asilimia 40 ya wanafunzi wa shule za msingi wilayani Kilombero katika mkoa wa Morogoro huacha shule kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafunzi kupata mimba.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Bw. Kahale, imezitaja sababu nyingine kuwa ni ufugaji wa kuhamahama, wanafunzi kujihusisha na kazi za kilimo na uvuvi wa samaki.

"Wastani wa wanafunzi 15 hawahudhurii masomo katika shule za msingi na hii ni picha halisi inayoonesha kukithiri kwa utoro katika shule za msingi wilayani Kilombero," inaeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa katika mkutano maalumu uliojadili maendeleo ya elimu mkoani Morogoro hivi karibuni.

Kwa mujibu wa maelezo hayo idadi ya wanafunzi 3501 waliohitimu elimu ya msingi wilayani humo mwaka jana ni pungufu kwa asilimia 40.5 ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 1994 ambao walistahili kuhitimu darasa la saba mwaka jana.

Hata hivyo wilaya ya Kilombero imeanza kutumia sheria ndogo kuwabana wanafunzi watoro ili kuongeza kiwango cha mahudhurio shuleni kutoka asilimia 85 za sasa hadi kufikia asilimia 90 katika kipindi cha miezi 3 ijayo.

Umaskini unatokana na vijana kuwaachia wazee vijiji

Na Joseph Sabinus

VIJANA wa kati ya miaka 10 na 35, wameelezwa kuwa wanachangia umaskini katika jamii kwa kuwa badala ya kuzalisha mali vijijini, wanakimbilia mijini na kuwaachia vijiji wazee wasio na uwezo wa kuzalisha.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Same, Mhashamu Jacob Koda, aliyasema hayo wakati akizungumza katika siku ya kwanza ya semina ya mapadre, masista, watawa na walezi wa Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki wa Sekondari na Vyuo Tanzania (TYCS) toka majimboni iliyofanyika juma lililopita katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala, jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema kufuatia vijana wenye nguvu za uzalishaji mali kukimbilia mijini na kuwaacha wazee vijijini, umaskini, uhalifu na ukosefu wa huduma bora za kijamii, vimekuwa vikishamiri hata katika maeneo ya vijijini.

"Vijijini pamekuwa sehemu ya umaskini mkubwa na huduma duni kwa kuwa wasomi, wafanyabiashara na wenye ujuzi, wamekimbilia mijini," alisema na kuongeza "Sasa vijijini kuna vijana wa darasa la saba na wazee waliostaafu."

Alisema hali hiyo inasikitisha kwa kuwa imeshababisha hata vijijini kuongezeka uhalifu kama wizi, umalaya, utoaji mimba na wimbi la umasikini uliokithiri.

Alitaka uimarishwe ushirikiano wa malezi endelevu baina ya familia, shule na Kanisa. "Ni muhimu kuwapa vijana mafunzo ya kiroho kwa vipindi vyote baada ya shule ya msingi. Kijana akiachwa baada ya malezi hayo tu, ni rahisi kushawishiwa akaingia hata ulokole bila hata uchaguzi wowote; ndiyo maana wanafunzi wengi wa vyuo vikuu ni walokole," alisema Askofu Koda na kuongeza, "Na hii, inachangiwa pia na hofu ya masomo."

Askofu Koda alimpongeza Mlezi wa TYCS Taifa, Padre Lucas Mzuanda kwa kuandaa semina hiyo aliyosema ni muhimu katika kuwafanya walezi kujua wajibu na umuhimu wa malezi yao kwa Kanisa.

Mlezi wa TYCS Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre Joe Prub, alisema kwa kuwa vijana hujifunza zaidi kwa mifano na matendo waonayo, ni vema walezi wakawa mifano bora ya kuigwa.

Mlezi wa TYCS tawi la Tanga Technical School, jimboni Tanga, Mwalimu Yordan Sanga alisema, "Jamii itafute uwezekano wa kutumia sheria za mila ili kuzuia uzinzi na uasherati."

Mshauri na Mlezi wa TYCS jimboni Singida Padre Raphael Madinda, alisema wahusika wa upokeaji bidhaa za nje, hawana budi kuachana na tamaa ya pesa ili wasipokee na kuingiza nchini bidhaa zenye madhara wa jamii kimwili na kiroho.

"Wengine wanafahamu mambo haya yana madhara lakini kwa tamaa ya fedha na mali lakini, wanakubali kuyaleta nchini. Inabidi tuwape changamoto mpaka wakubali kuwa, wanaangazima jamii," alisema.

Padre Kangalawe awa Monsinyori

Na Mwandishi Wetu

BABA Mtakatifu, Yohane apaulo wa Pili, amemtunuku hadhi ya Monsinyori, katibu wa Idara ya Liturjia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Julian Kangalawe.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana toka kwa Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura, katika hati maalumu ya Januari 26, mwaka huu toka Ofisi za Vatican, ambayo KIONGOZI liliishuhudia,Papa amemuweka Padre Kangalawe kuwa miongoni mwa wakapilani(wasaidizi) wake na kwamba kwa heshima hiyo, ana hadhi ya Umonsinyori.

Barua ya Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Mkuu Luigi Pezzuto, kwa katibu Mkuu wa TEC, kumjulisha hatua hiyo ilikuwa hivi,"Mheshimiwa Mpendwa Padre,Ninayo heshima kukutumia nakala ya hati inayotoka ofisi ya waziri wa nchi wa vatican, inayohusu heshima ya kapilani wa papa kwa hadhi ya Umonsinyori, anayotunukiwa Mheshimiwa padre Julian Kangalawe,Katibu Mtendaji wa Tume ya Liturjia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania."

Monsinyori ni hadhi anayopewa Padre katika Kanisa Katoliki na Baba Mtakatifu kama shukurani baada ya kuridhishwa na utumishi bora kwa Kanisa.

Huku akishangiliwa na wafanyakazi mbalimbali wa TEC wakati katibu Mkuu akiwatambulisha juu ya hatua hiyo Alhamisi iliyopia, Padre Kangalawe(sasa Monsinyori), alisema, "...Unapokuwa naibu askofu, unakuwa monsinyori hadi unapoachia wadhifa huo lakini, kwa uteuzi na waraka rasmi wa Baba Mtakatifu, unakuwa monsinyori hadi mwisho wa maisha yako".

Akaongeza, "Ninawashukuru kwa kuwa ushirikiano na upendo wenu ndivyo vimenifanya hata ikaonekana ninafaa kupewa hadhi hii."

Mchungaji ataka vijana wajiunge kuweka na kukopa

Na Elizabeth Steven

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), limesema ili kukabiliana na tatizo la ajira, vijana hawana budi kuanzisha miradi na kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali vikiwamo vya kuweka na kukopa.

Mchungaji Mika Katale wa KKKT usharika wa Buguruni, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar-Es-Salaam.

Hata hivyo Mchungaji Mika alisema kwa kuwa tatizo hili si la vijana peke yao, jamii nzima haina budi kuona kuwa inafanya kila linalowezekana, kujiunga katika vikundi na miradi mbalimbali ya uzalishaji mali.

Alihadharisha kuwa endapo wanajamii kila mmoja kwa nafasi yake hawatajenga tabia ya kutaka kuaminika na kuamini wengine, bado itakuwa vigumu kufikia mafanikio kwa kuwa bado wataendelea kuhofu kujiingiza katika vikundi ambavyo hatima yake huwa haina mafanikio yoyote ikiwa ni pamoja na vikundi vya biashara ndogondogo kama "mamantilie."

Alisema hali ya kutoaminiana pia imechangia kwa kiasi kikubwa, jamii kutojiunga katika vikundi hivyo.

"Watu wengi si kwamba hawapendi kujiunga katika vyama kama hivi vya kuweka na kukopa, tatizo ni kasumba iliyopo ndani ya mioyo yao; ya kutoaminiana na hali hiyo kila mtu anapaswa kuiweka kando. Endapo watu wataaminiana, maisha yataboreka zaidi," alisema.

Wakati huo huo: Mchungaji Mika amewalaumu wanajamii wanaokalia kuvilaumu vyombo vya kutetea haki za binadamu kwa madai kuwa havifanyi kazi kama inavyotakiwa na badala yake, amewataka kujua kuwa kila kikundi hufanya kazi kulingana na uwezo na taratibu zake na pia, kwa kuzingatia kuwa hakivunji shertia za nchi.

Mahenge wampoteza Padre

Na Padre Chrysantus Ndaga, Mahenge

JIMBO la Mahenge limempoteza tena mmoja wa wachungaji wake, Padre Jonas Mayombo aliyefariki Februari 26, mwaka huu, huko Kwiro na kuzikwa Februari 27, mwaka huu huko Ifakara, Jimboni Mahenge.

Kifo cha Padre Mayombo kinaendeleza wimbi la majonzi lililotanda jimboni Mahenge katika kipindi cha miezi sita. Mwezi Agosti mwaka jana, Jimbo Katoliki la Mahenge lilimpoteza Sista Regina Chamtwa na kufuatiwa na kifo cha Sista Sixta Kahise, mwezi Oktoba mwaka jana. Wote walizikwa Itete.

Katika misa ya mazishi iliyoongozwa na Askofu wa jimbo, Mhashamu Agapit Ndorobo, na kuhudhuriwa na mapadre zaidi ya 50 na mamia ya waamini toka ndani na nje ya jimbo, Askofu alisema maisha ya mwanadamu yanafanana na ua ambalo asubuhi huchanua na jioni hunyauka.

"Tulikuwa tumepanga naye mipango mingi; mmojawapo ukiwa kujenga Kanisa. Sasa pengo hilo litajazwa na nani! Hata hivyo lazima tukubali maneno ya Ayubu kwamba, Mungu aliyetupatia Padre Mayombo, ndiye aliyemwita," alisema.

Alimwelezea padre Mayombo kama ni padre mtii aliyekuwa tayari kutumwa popote, na kwamba daima alitafuta ushauri. Aidha Baba Askofu aliwaomba Mapadre na waamini wote kuiombea Roho ya padre Mayombo kusudi iweze kupata rehema kwa Mungu na kupumzika kwa amani.

Padre Jonas Mayombo ni mtoto wa pili katika familia ya watoto tisa ya wazazi Aloyce Mayombo na Bonifacia Kingumwile alizaliwa tarehe 10-12-1948 huko Ifinga Baada ya masomo yake ya shule ya msingi aliamua kujiunga na seminari ya Kasita mwaka 1962, nia yake ya kuwa padre ilimpeleka katika seminari kuu za Kibosho na Kipalapala ambapo hatimaye alipata daraja takatifu ya Upadre tarehe 27-8-1775.

Padre Mayombo alifanya kazi katika parokia za Ifakara, Kilombero na Kisawasawa kabla ya kwenda Roma Italia kwa masomo ya juu ya Liturjia aliporudi alifanya kazi katika parokia za Igota na Kwiro hadi alipofariki.

Bradha Matthias Gotz OSB mwaka 1913- 2001

MEI 2, 1913 Bradha Matthias Gotz OSB, alizaliwa katika kijiji cha Tauberrettersheim, katika tarafa ya Ochsenfurt na kufariki Januari 3, 2001 katika Hospitali ya Bumbuli akiwa na miaka 88.

Katika ubatizo alipewa jina la Josef. Aliishi katika familia iliyojaliwa watoto wanane.

Wazazi wake Michael na Adelheid walikuwa wakulima. Nacho kilimo kilijenga maisha yake yote mpaka ndani ya tabia yake. Baada ya kumaliza shule ya msingi (1920-1926), alijiunga na Trade School ya Abasia ya Munsterschwarzach.

Mwaka 1930, aliweka nadhiri za muda na mwaka 1934 aliweka nadhiri za daima.

Alihudhuria shule ya kilimo huko St. ottilien. mwisho wa mwaka 1934, alitumwa aende Misioni ya Abasia ya Ndanda. Ufundi wake wa kilimo ulimsaidia sana katika miaka ya kazi yake.

Kwanza, alifanya kazi ya kilimo hapa Ndanda (1936), baadaye Nyangao (1937). Toka 1937 mpaka 1949, alisimamia kilimo na ufugaji katika prokura yetu huko Kurasini/Dar-Es-Salaam.

Wakati wa Vita Kuu ya Pili, alihamishwa afanye kazi huko Ifakara na Kwiro (1942-1946).

Mwaka 1949 alirudi Ndanda na kujaliwa kutimiza ndoto yake ya kuanzisha shule ya kilimo ili kuwaingiza wakulima vijana katika kilimo cha siku hizi. Aliendesha shule hii kwa muda wa miaka kumi.

Mwaka 1959 aliitwa afanye kazi katika seminari ndogo ya Namupa ili kuwaingiza wanafunzi katika ufundi na kilimo cha bustani na mashamba. Wanafunzi hao walitazamiwa baada ya kuwekwa padre katika parokia mbalimbali, kuwasimamia kazi ya bustani na mashamba ili kuwapa wanaparokia nafasi ya kujitosheleza kuhusu matumizi ya parokiani.

Kwa wengi, mawazo ya Bradha Matthias yalikuwa mawazo ya kigeni kabisa. Kwa maoni yake, alitangulia wakati ujao. Lakini, ufundi wake ulitakiwa mahali pengine pia. Kwa hiyo, alifuata mwito wa kwenda Sakharani katika eneo la Usambara ili kuendesha kazi ya kilimo.

Usambara ni eneo linalitofautiana sana na hali ya Kusini ya Tanzania. Pale, wajibu wake ulimshughulisha hasa na kilimo na miti ya Kwinini na kahawa.

Aliona hatari ya kukata miti ovyo. Kwa hiyo, alianza kupanda miti kwa maelfu. Alipanda miti ya Macadamia na kujaribu kupata soko la kuiuza.

Baadaye, alianza kutimiza ndoto nyingine yaani kupanda shamba la mizabibu ili kutengeneza divai. Hapo, alitoa nguvu nyingi kwa sababu alilazimishwa kujaribu mara kwa mara, na kubadili mizabibu mara nyingi mpaka alipofanikiwa kupata shina moja ambalo liliweza kusitawi katika milima ya Usambara.

Aliona kwamba nguvu zake zilianza kudhoofika. Kuwa hiyo, alikubali msaidizi kwa moyo mchangamfu. Bradha Celestini wa Ndanda, alifurahi kupelekwa Sakharani ili kumsaidia mzee Bradha Matthias.

Sehemu ya mwisho wa mwaka 2000, alipata operesheni ya Prostata katika hospitali ya KCMC ya Moshi. Alirudi na kupata nguvu yake tena lakini, Mungu aliamua kwa njia yake na kumwita mtumishi wake afurahie raha ya milele huko mbinguni.

Mhashamu Askofu wa Tanga, Anthony Banzi, alisimamia misa ya wafu na mazishi yake karibu na kikanisa cha Sakharani.

Astarehe katika amani ya Kristu Mfufuka

Imetolewa na Abate Siegfried na watawa, Abasia ya Ndanda na kuidhinishwa na Askofu wa Jimbo katoliki la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi