Make your own free website on Tripod.com

Dawa za 'Safe plan' zaleta utata

l Inatengenezwa wapi, ni kitendawili

Na Getrude Madembwe

UTATA umejitokeza juu ya nchi inayotengeneza vidonge vya uzazi wa mpango vinavyojulikana kama "Safe Plan".

Wakati taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya kupitia kitengo chake cha Bodi ya Dawa nchini inadai dawa hiyo hutengenezwa nchini Afrika Kusini, kipeperushi kilichotolewa na Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na masuala ya utoaji wa huduma ya uzazi wa mpango(Population Services International(PSI), kinasema vidonge hivyo vinatengenezwa Marekani (USA).

Kufuatia Wizara ya Afya nchini kutofautiana na PSI kuhusu nchi husika, inayotengeneza dawa hiyo, kuna uwezekano mkubwa ikaleta madhara kwa watumiaji.

Kwa mujibu wa uchunguzi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu Benedict, ya Ndanda, Mtwara, Sista B. Shnell(OSB) pamoja na mambo mengine, Desemba 27, 2000, aliiandikia Wizara ya Afya akiomba impatie ufafanuzi juu dawa hiyo.

Katika barua yake alitaka kujua madhara yawezayo kumpata mtumiaji.

Uchunguzi umebaini kuwa, majibu ya Wizara ya Afya katika barua yake hospitalini hapo yenye kumbukumbu No. HEP/60/13/VOL.XVI/480 ya Januari 4, 2001(nakala tunayo), Wizara ilifafanua kuwa dawa inazalishwa katika maabara ijulikanayo kama Wyeth Laboratories ya nchini Afrika Kusini.

Ukabaini kuwa kipeperushi kimeandika kuwa dawa hiyo inazalishwa na imesajiliwa na taasisi ya Wyeth Laboratories ya Marekani(USA).

Pia, wakati barua ya Wizara inadai dawa hiyo inatokana na mchanganyiko wa "Norgestrel USP 0.3mg" na "Ethinyl Estradiol USP 0.0306mg", kipeperushi kinaonesha kuwa, ni mchanganyiko wa "DUOFEM" na" Ferrous Fumarate".

Akizungumzia hoja zilizo katika kipeperushi hicho cha PSI kinachoeleza kuwa dawa hiyo inazalishwa na taasisi ya Wyeth Laboratories, ya Marekani(USA), Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Uhai nchini (Pro- life-TANZANIA), Bw. Emil Hagamu amesema maelezo ya kipeperushi hicho kuwa dawa hiyo ina madhara kwa watumiaji, ni ya kweli na wala si uzushi kama kipeperushi kinavyodai.

Kipeperushi kinakanusha madai ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya watu juu ya madhara ya dawa hiyo kwa watumiaji wake wambao ni wanawake katika kupnga uzazi.

Baadhi ya madhara hayo yanayodaiwa kuwa katika dawa hiyo ni pamoja na vidonge hivyo vya uzazi wa mpango kujikusanya katika mfuko wa uzazi na kuharibu baadhi ya viungo vya uzazi, kusababisha mwanamke kuwa tasa na kusababisha kansa.

Madai mengine juu ya dawa hiyo ni kuwa inasababisha mwanamke kuzaa watoto walemavu, kuwa ni lazima kupumzika kutumia vidonge hivyo vya uzazi wa mpango baada ya kuvitumia kwa muda mrefu na kwamba, husababisha mwanamke kutokwa na maji katika viungo vyake vya uzazi na kuwashwa.

Mengine, ni dawa hiyo kudaiwa kupunguza au kuongeza uzito wa mwanamke. Hata hivyo, katika kipengele hiki, kipeperushi kinakiri hali hiyo bila kujua kuwa kupungua au kuongezeka uzito kwa sababu ya dawa, ni moja ya athari mbaya

Hagamu alisisitiza, "Mwanamke anayetumia vidonge vya uzazi anaweza kuchelewa kupata mtoto na hii inatokana na mvurugiko wa siku zake za hedhi au kuwa tasa daima".

Alisema anashangazwa na PSI kwa kuwa hawaelezi waziwazi madhara ya dawa hiyo na kwamba hali hiyo ispodhibitiwa, itazidi kuiathiri vibaya jamii.

Alisema PSI wanachoeleza kama madhara ya dawa hiyo, ni maumivu ya kichwa, kupumua kwa shida, kizunguzungu na kutoona vizuri. Mengine ni maumivu ya miguu na kiuno, pamoja na kulainika matiti.

Mwenyekiti huyo wa Pro-Life-TANZANIA, aliwahimiza wanawake kutoitumia dawa hiyo kwa madai kuwa ina madhara makubwa tofauti na maelezo yaliyopo katika kipeperushi hicho.

"Unajua watu wanapougua malaria, humeza Chroloquine na baadhi ya watu hupata madhara ya kuwashwa au hata kuchoshwa mwili sasa iweje hiyo ya uzazi ambayo haiponyeshi kitu chochote? Alihoji Hagamu.

Makanisa na vikundi mbalimbali vya dini, vimekuwa vikikemea vikali matumizi ya dawa ya kupanga uzazi kwa kuwa inaathiri afya za watumiaji na pia, inakiuka maadili ya Kimungu kwa kuwa inachochea vitendo vya uasherati na uzinzi vinavyoongeza mimba zisizotarajiwa na watoto wa mitaani sambamba na kuenea kwa UKIMWI.

Kanisa linasisitiza jamii kutumia uzazi wa mpango kwa njia ya asili ambayo ni ya uhakika, haina madhara na wala haigharimu.

Awatoroka Polisi na kubusu picha ya Mkapa mahakama imsamehe

Na Makubo Haruni, Tarime

RHOBI Masiko Mahende(42), mkazi wa kijiji cha Nyankunguru wilayani Tarime, amefanya kituko mahakamani baada ya kuwatoroka askari polisi, kuvuka kizimba na kuchukua picha ya Rais Mkapa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime nyuma ya hakimu na kisha kuibusu akiiomba imsamehe.

Tukio hilo lililoshuhudiwa na KIONGOZI mahakamani hapo Jumanne iliyopita, liliwaacha katika butwaa waliohudhuria mahakamani hapo akiwamo Hakimu wa Mahakama hiyo, Zablon Gesase aliyekuwa akiendesha kesi mbalimbali.

Katika tukio hilo lililomfanya hakimu huyo atulie kwa mshangao na kushuhudia kinachoendelea, Mahende anayekabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, alinyanyuka mahakamani hapo akiwaacha watuhumiwa wenzake ambao alikuwa katikati yao, akawapita askari polisi kumi na wawili waliokuwa wamewapeleka mahabusu mahakamani hapo, akapita kizimba hadi nyuma ya hakimu ilipokuwa picha hiyo.

Mtuhumiwa baada ya kuifikia, aliitoa picha hiyo ya Rais iliyokuwa ukutani, akaanza kuiomba radhi imsamehe makosa yake yaliyomfikisha mahakamani hapo na hivyo, kumfanya awe huru.

"Eee! Baba nisamehe! Baba Nisamehe! Baba nisamehe," alisema huku ameshikilia picha hiyo na watu wakimtazama.

Baada ya kumuomba radhi Rais Mkapa kupitia picha yake katika mahakama hiyo, askari polisi walimnyang’anya picha na kumuondoa nyuma ya hakimu, kisha wakampeleka rumande.

Baada ya tukio hilo la aina yake, hakimu huyo Gesase aliendelea na mahakama na kutomchukulia hatua zaidi kwa madai kuwa alimuonea huruma mtuhumiwa kwa kuwa alifanya hivyo kwa nia ya kuomba radhi na dua.

Rhobi Matiko Mahende anakabiliwa na kesi ya unyang’anyi kwa kutumia silaha ambapo ilidaiwa kuwa Januari 17, mwaka huu, alitumia silaha kumpora Mkurugenzi wa hoteli ya Kibacho ya mjini hapa, Bw. Matiko Kibacho, jumla ya shilingi 8,600,000.

Vitu vingine alivyodaiwa kupora Bw. Mahende akiwa mlinzi wa Bw. Kibacho ni pamoja na suti mbili, redio kaseti moja, sanduku moja na taulo moja vyote vikiwa na thamani ya shilingi 190,000/=.

Hakimu huyo Zablon Gesase ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 7, mwaka huu itakapotajwa.

Watoto waandamana kwa kukosa misaada ya OCC

l Wamlilia Mchungaji wakimdai

Na Leocardia Moswery

BAADHI ya watoto wa Mbagala, Dar-Es-Salaam, wameandamana katika Kanisa la Pentekoste la Mbagala, wakidai kupatiwa misaada iliyotolewa na taasisi ya Operation Christmas Child, kama wengine walivyoipata hivi karibuni.

katika tukio hilo la katikati ya juma lililopita, watoto hao wenye umri wa kati ya miaka mitano na kumi,walidai na wao wanataka wapewe misaada sawa na ile waliyopata wengine.

"Tunataka na sisi hizo zawadi mlizowapatia wenzetu" "Mbona sisi hatupati" walisikika wakidai na huku wengine wakisema, "Mchungjai tupatie na sisi".

Hatua ya watoto hao imekuja baada ya taasisi hiyo ya kutoka nchini Uholanzi, kugawa msaada kwa watoto wenye umri kati ya miaka 2 na 14 kupitia Kanisa la Pentekoste ambapo watoto wapatao 405, walipatiwa zawadi mbalimbali zikiwemo nguo na madaftari.

Misaada hiyo iliyowasilishwa na Mchungaji wa kanisa la Pentekoste, Mtalis Charles kwa niaba ya taasisi hiyo akisaidiwa na Mchungaji wa kanisa hilo la Mbagala, Dismas Makassa.

Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi sababu ya watoto hao kuandamana kanisani kwake, Mchungaji Makassa alisema kuwa, "Watoto wameandamana baada ya kukosa zawadi kwa sababu wazazi wao hawakuwa wameandikisha majina yao eti kwa madai kuwa waliogopa kubadilishwa dini".

Mchungaji Makassa alisema kuwa, baadhi ya wazazi na hata taasisi nyingine za dini wamekuwa wakihofia kuwa pengine misaada ya taasisi hiyo imekuwa na lengo la kuwashawishi na kuwavuta watu kubadilisha dini.

Alifafanua kuwa taasisi hiyo yenye makao yake makuu nchini Uholanzi, ilitoa misaada kwa baadhi ya nchi zanazoendelea barani Afrika ili kuwasaidia watoto kutokana na misaada hiyo iliyotolewa na watoto wenzao.

Mchungaji Makassa alikanusha tuhuma za utoaji huo wa misaada kuhusika na ushawishi wa kubadili madhehebu.

Alihoji, "Mbona Kanisa Katoliki linatoa misaada sana, je nani alishawasikia wakishawishi watu kubadili dini. Sasa itakuwaje sisi tuwarubuni?"

Uzinduzi wa mipango ya taasisi hiyo kugawa misaada nchini, ulifanyika hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es-salaam, Luteni Yusuf Makamba, hivi karibuni jijini Dar-Es-Salaam.

Hata hivyo, taasisi hiyo ya Oparation Christmas Child, imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya viongzi wa dini wanaodai kuwa, inawarubni watoto na wazazi ili wabadili dini.

BAADA YA KUWAKAMATA WANAHARAKATI...

Wasomi Chuo Kikuu wawaponda polisi

lWasema walishindwa kusoma Kiingereza, wakaamua kuwasomba

Na Dalphina Rubyema

KITENDO cha polisi kuwakamata wanaharakati waliokuwa wanapeleka ujumbe kwa maafisa na mashirika ya fedha duniani, kimepondwa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam, wakidai kilitokana na polisi hao kushindwa Kiingereza kilichotumika na hivyo, kutojua yaliyokuwa yameandikwa.

Februari 23, mwaka huu, askari Polisi jijini Dar-Es-Salaam, waliwakamata wanaharakati kadha waliokuwa wakipeleka ujumbe kwa maafisa wa mashirika ya fedha duniani (IMF na Benki ya Dunia), uliokuwa umeandikwa katika mabango.

Katibu Mkuu wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam(DARUSO), Bw. Mkili Gervas, aliyasema hayo katika mazungumzo yake na KIONGOZI jijini Dar-Es-Salaam hivi karibuni.

Alisema kuwa, kitendo cha polisi kuwakamata wanaharakati hao, kinaonesha dhahiri namna polisi wasivyokuwa na elimu ya kujua hata mambo muhimu ya kuiondoa nchi katika mikono ya ukandamizwaji na mataifa makubwa yakiwamo mashirika ya kimataifa ya fedha.

"Wanaharakati hao walikuwa wanapeleka ujumbe mzito na muhimu kwa maafisa wa mashirika hayo (World Bank na IMF)tena kwa faida ya Watanzania wote. Kitendo cha polisi kuwazuia, kinadhihirisha wazi polisi wa Kitanzania hawakusoma vizuri na wengi hawajui mambo muhimu ya kupigania kwa maslahi ya nchi," alisema Katibu Mkuu huyo Wa DARUSO na kuongezea,

"Bahati mbaya ujumbe huo uliandikwa kwa Kiingereza na hii ni lugha ambayo ni mzigo kwa polisi wengi nchini."

Katika kuondokana na hali hiyo aliyoiita ya kuburuzwa na polisi, Bw. Gervais ameishauri serikali iwape elimu ya kutosha askari hao juu ya haki zao, wananchi na hata wao wenyewe kujua hali halisi ya nchi na mipaka yao ya utendaji kazi.

"Pamoja na Profesa Maina (wa Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam) kujitolea kuwafundisha polisi wote wa Tanzania juu ya haki za binadamu, bado hawaelewi kabisa na serikali inatambua kuwa polisi hawakusoma ipasavyo lakini, bado inawakumbatia. Muda umefika sasa tunataka polisi wasomi ndani ya nchi yetu," alisema Bw. Gervais.

Februari 23 mwaka huu kikundi cha wanaharakati kikiwa kimebeba mabango, kiliandamana kuelekea katika Hoteli ya Sheraton ya jijini, ambako ulikuwa unafanyika mkutano baina ya Marais wa nchi za Afrika na Maafisa wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa(IMF).

Hata hivyo kabla wanaharakati hao hawajafanikisha ujumbe wao kwa wahusika ,polisi waliwazuia kwa kuwasambaratisha na baadhi yao kukamatwa. Kitendo hicho kililaaniwa na watu wengi akiwemo Rais wa Tanzania Benjamin William Mkapa aliyesema haoni kosa la wanaharakati hao kwa kuwa wana uhuru wa kutoa maoni yao.

Hospitali ya binafsi yalaumiwa

Na Mwandishi Wetu, Tarime

WAFANYAKAZI kadhaa wa hospitali ya kibinafsi ya Dr. H. Winani Health Center ya mjini Tarime, wameilalamikia hospitali hiyo kwa kuwacheleweshea malipo yao kwa zaidi ya miezi kumi.

Wafanyakazi hao wa ngazi tofauti waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wamesema uongozi wa hospitali hiyo umejenga tabia ya kuwacheleweshea mishahara kwa kuwalipa kwa awamu(mzunguko) hali waliyosema imewafanya kila mmoja kubuni njia nyingine za kuwawezesha kuendesha maisha mjini hapa.

Wamesema badala ya kuwalipa mishahara kwa wakati, mkurugenzi wa hospitali hiyo, amekuwa akitumia pesa yao kwa ajili ya kusomeshea watoto nje ya nchi na kujenga kituo kingine cha afya katika maeneo ya Nyamongo wilayani hapa.

"Tunajua watasingizia kuwa hakuna pesa lakini za kujengea hospitali ya Nyamongo na kusomesha watoto nje, zinatoka wapi kama sio hizi tunazohangaikia?" alihoji mmoja wa wafanyakazi hao na kuongeza, " Kama wanaona hospitali haiwezi kujiendesha, wafunge au wapunguze wafanyakazi kuliko kutesana bure."

Mfanyakazi mwingine alidokeza kuwa wafanyakazi wanaoacha kazi katika hospitali zao wamekuwa hawalipwi haki zao ikiwa ni pamoja na malipo ya NSSF.

Afisa Utumishi wa Hospitali hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake, aliwashangaza waandishi wa habari alipoulizwa juu ya madai hayo na kuving’akia vyombo vya habari kuwa vina upendeleo kwa kuwa haviandiki madhaifu ya serikali bali yale ya miradi ya watu binafsi pekee.

"Mbona hospitali na miradi ya serikali hamfuatilii lakini miradi ya watu binafsi tu, ndiyo mnaisakama.

Kwanza watu wanalipwa mishahara na wala sijui kama wapo wanaodai. Hata hivyo ngoja gazeti litoke tumuone huyo aliyesema hayo, atueleze."

Alipoulizwa na wandishi kwanini anajenga chuki na kwamba labda ni kwa kuwa yeye ni afisa na hivyo analipwa ndiyo maana hazingatii kujua kama watumishi wenzake wanalipwa, alikaa kimya na kusema, "msubirini Mkurugenzi mwenyewe."

Mkurugenzi huyo ambaye pia ni Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Winani, alisema madai hayo hayana ukweli wowote bali yanalenga kumharibia jina kwa kuwa wengine wanazusha mambo baada ya kukiuka taratibu na kusimamishwa kazi.

"Mishahara tunalipa kila mwezi isipokuwa mara nyingine tunachelewa. Kama tungekuwa hatuwalipi kabisa kwa mwaka mzima, si wangekuwa wamekufa."

Dk. Winani alishangazwa na madai hayo na kusema gharama anazutumia kufanya mambo yaliyotajwa na wafanyakzi wake kuwa yanasababisha wasilipwe kwa wakati muafaka, zinatokana na eneo lake la machimbo ya dhahabu alilokodisha kwa Wazungu raia wa Australia pamoja na mkopo alioupata toka kampuni ya East African Gold Mine.

"Nilikuwa na eneo langu la dhahabu huko Nyamongo nikawapa Wazungu(Waaustralia) kwa makubaliano ya kunilipa kwa kila miezi mitatu, Dola 2500. Hizo ndizo natumia kutengenezea mambo yangu," alisema na kuongeza, "Pia nilipata mkopo wa Dola 146,000 toka kampuni ya East African Gold Mine ambazo ninalipa kwa makato ya mauzo ya dhahabu. Hizi ndizo ninasomeshea watoto wangu, Sabiba na Moisa."

Dk. Winani alidokeza kuwa hospitali yake ina mpango wa kuwapunguza wafanyakazi hao toka 30 waliopo, hadi kufikia 13 na kwamba, katika zoezi hizo atazingatia taratibu na haki zote kwa kila atakayeguswa.

Kanisa la Presibyterian latumia milioni 23.6/= kujenga madarasa saba

l Lawasimika wachungaji, mzee wa kwanza Tanzania

Na Ndechingio Charles, Morogoro

KANISA la Presibyterian la mjini Morogoro, limetumia jumla ya shilingi milioni 23.6 za Kitanzania katika ujenzi wa vyumba saba vya madarasa katika shule ya seminari ya Great faith, iliyopo Kihonda wilayani hapa.

Mchungaji wa kanisa hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kanisa la Umisionari la nchini Korea, hapa Tanzania, Young Lee, amesema ujenzi huo ambao ni wa awamu ya kwanza, ulianza mwezi Machi mwaka juzi na kukamilika mwezi uliopita.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa seminari hiyo, alisema seminari ya Great Faith, inatarajiwa kufunguliwa rasmi kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza ifikapo mwezi Januari, 2001.

Alisema, awamu ya pili ya ujenzi wa shule hiyo, itahusisha ujenzi wa vyumba vya maabara, kompyuta, mabweni, nyumba za watumishi na madarasa ya ziada na kwamba, baada ya ujenzi kukamilika, shule hiyo ya seminari itapanua utoaji wa elimu hadi kidato cha sita.

Akizindua shule hiyo, Mchungaji Shin toka nchini Korea, alisema Watanzania wana wajibu wa kutunza vizuri shule zote zinazojengwa kwa misaada ya wafadhili mbalimbali toka nje ya nchi.

Alisema Watanzania hawana budi kutambua kuwa wahisani hawawezi kuondoka na majengo waliyojenga kwenye ardhi ya Tanzania hivyo, waitilie mkazo rasilimali hizo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

"Mfano mzuri ni shule hii iliyojengwa kwa msaada wa Wamisionari wa Korea. Hii siyo ya Korea, itabaki kuwa ya Watanzania na hata Mchungaji Lee, akimaliza muda wake, hawezi kurejea Korea na hii shule, ataiacha hapa hapa," alibainisha Mchungaji Shin.

Alisema Kanisa hilo litaendelea na mpango wake wa kuongeza majengo katika shule hiyo ili kuboresha zaidi elimu nchini hapa.

Wakati huo huo: Kanisa la Misionari la Korea (Korea Mission Church), limemsimika Andrew Mhilu, kuwa Mchungaji wa kwanza Mtanzania, wa kanisa hilo nchini hapa na Ibrahim Kalanje, kuwa mzee wa Kwanza wa kanisa.

Ibada maalumu ya kuwasimika viongozi hao, ilifanyika katika Kanisa Kuu la Presibyterian la mjini Morogoro, ambapo pia wainjilisti wengine wanne walipewa vibali vya kuhubiri nchini.

Wainjilisti hao ni Patrick Hosa, Robert Mkumbukwa, Raphael Sanga na Augustino Malulumila. Miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo, ni Askofu Dudley Mageni wa kanisa la Anglikana katika Dayosisi ya Morogoro, aliyetoa wito kwa watumishi hao wa Mungu waliosimikwa kuzithamini kazi walizopewa na kutoa mafundisho sahihi ya Kimungu kwa waamini wao.

Wengine ni Mchungaji wa kanisa hilo, Profesa Sebastian Rutahoile, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania(CCT) mkoani Morogoro, Bibi Penina Mkuchu, na waamini wengine wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo mjini hapa.

Wasabato wasema machafuko ni matokeo ya kukosa uamifu

Na Vick Peter

MACHUNGAJI Joshua Malongo wa kanisa la SDA Temeke, amesema kuwa machafuko yaliyotokea hivi karibuni baina ya wafuasi wa serikali na wafuasi wa CUF, yasingetokea kama watu wangekuwa waaminifu kwa Mungu.

Hayo aliyasema katika mkutano wa Injili, uliyofanyika Tabata Kimanga, jijini Dar-Es-Salaam, kwa takribani wiki tatu zilizopita ambapo kilele chake kilikuwa Jumapili iliyopita.

Mchungaji Malongo alisema kuwa watu wamejivua uaminifu wao kwa Mungu na badala yake, uaminifu wao wameuelekeza katika malengo yao binafsi ambayo alisema, yanaweza kuhatarishda amani kwa taifa.

Aliendelea kusema kuwa wanadamu wamekuwa wakisisitiza amani lakini amani wanayoizungumzia hawaijui kwani inawezekana kabisa kubwa amani inayozungumzwa duniani si amani ya kweli na kwamba ndiyo maana kunakuwapo na machafuko ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali duniani.

Alisema amani ya kweli inakuwepo na kupatikana endapo tu, wanadamu watayafuata ayatakayo Mungu na kuyatimiza.

Hayo aliyasema kufuatia machafuko yaliyotokea kati ya Januari 26 na 27, mwaka huu ambapo watu wapatao 23 walifriki dunia na wengine kadhaa, kujeruhiwa katika mapambano baina ya polisi waliokuwa wakizuia maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Wananchi(CUF).

Katika mkutano huo wa Injili, kulikuwa na huduma ya matibabu kwa wagonjwa mbalimbali yaliyotolewa bure kwa wagonjwa waliojitolea kama njia mojawapo ya kuonesha namna Mungu anavyofanya kazi kati ya wanadamu.

Fundisheni mema yanayokwenda na wakati - Wito

Na Leocardia Moswery

MONSINYORI Deogratius Mbiku, amewataka walimu wa dini nchini, kufundisha masomo yanayokwenda na wakati lakini yasiyopotosha maadili ya Kanisa ili yaweze kuwasadia zaidi vijana katika maisha.

Monsinyori Mbiku alisema kuwa ni wajibu wa kila mwalimu kutafakari vema na kuwafundisha vijana nchini kwa kadiri ya mahitaji ya sasa.

Alihimiza kuwa mafunzo na mahitaji hayo, hayana budi kuzingatia zaidi kulinda maadili ya jamii na hivyo kutimiza mapenzi ya Mungu huku vijana wakipata unafuu wa maisha kutokana na masomo wanayopata.

Alikuwa akizungumza mwishoni mwa juma lililopita katika semina ya Katekesi ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, iliyofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar-Es-Salaam.

Monsinyori Mbiku alisema, "Ni juu ya kila mwalimu kutafakari na kuwafundisha vijana kadiri ya mahitaji yao ili vijana wetu waendelee kuwa hapa Tanzania".

Alihimiza nia ya kuwataka walimu kusisitiza mila na desturi za Mtanzania yakiwamo matumizi mazuri ya vyombo vya asili vya mawasiliano zikiwamo michezo kama ngoma, ngonjera, methali na vitendawili.

Alitaka walimu waoneshe kwamba wako watu wanaopenda kupotosha mila na tamaduni za jamii kwa makusudi bila kujali athari zake kwa Taifa.

Semina hiyo iliandaliwa na Mkurugenzi wa Mafundisho ya Dini katika shule za sekondari zilizopo ndani ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre Joe Prabu.

Vijana awaliohudhuria walisema kwa niaba ya wenzao kuwa baadhi ya walimu wamekuwa kikwazo kwao kwa kuwa hawatoi mifano bora inayogusa maisha ya mwanafunzi.

Uovu wa kisiasa, usalama ni dalili za ujio wa Yesu - Wasabato

l Wasikitishwa majambazi kuwavua abiria nguo

Na Elizabeth Steven

MATUKIO mabaya ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kiutamaduni yanayotokea ulimwenguni, yameelezwa kama dalili za kukaribia kwa siku za kurudi Yesu baada ya watu kutomtii Mungu.

Mhubiri Emmanuel Ibrahimu, wa kanisa la Waadventista Wasabato la Mabibo jijini Dar-Es-Salaam, aliyasema hayo katika ibada ya Jumapili iliyopita iliyofanyika kanisani hapo.

Ibrahimu ambaye ni Mhasibu wa kanisa hilo, alisema vitendo vya uovu vinavyozidi kuibuka kwa kasi vimetokana na wanadamu kuhusudisha mambo ya kidunia kuliko maadili ya Mungu hali aliyosema ni hatari kimwili na kiroho kwa jamii ya wanadamu.

Akitoa mfano wa unyama unavyozidi kuongezeka katika jamii, Mhubiri Ibrahimu alisema siku hizi bila kujali utu, hata majambazi wamekuwa wakiyateka magari na kuwaamuru abiria wote kuvua nguo zao na kubaki uchi bila kuzingatia mahusiano ya kiukoo yaliyopo baina ya abiria hao aidha kaka, dada, baba au mama.

Alisema unyama huo umewafanya majambazi kudiriki hata kufanya mapenzi na baadhi ya abiria waliowateka bila hata kujali mahusiano ya wahusika na akasema hali hiyo, inadhalilisha na kufedhesha utu wa jamii iwe kwa mtenda, au mtendewa.

Alitoa mfano wa tukio moja ambalo majambazi baada ya kuwalazimisha abiria kuvua nguo zao zote, waliamumuru anayejijua ana ukimwi ajitokeze na mmoja aliyefanya hivyo, hakuguswa kimaumbile. " Vitendo hivyo ni vya aibu na vya kusiskitisha na si vema kuvifumbia macho," alisema Mhubiri huyo.

Alisema matatizo kama migogoro ya kisiasa na kijamii ikiwa ni pamoja na vtendo haramu vya utoaji mimba, havina budi kuonewa aibu na kila mwenye akili timamu na mapenzi mema kwa jamii ya binadamu na kwa Mungu pia.

'Father Franswaa' aiacha Radio Tumaini

l Katibu wa MAC ashika usukani

BAADA ya kufanya umisionari kwa njia ya radio na video akileta hamasa jijini Dar-Es-salaam, Padre Jean-Galtier Francois, ameiaga Radio Tumaini baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Taasisi ya OCIC- Missionary Service iliyopo Vatican, anaripoti John P. Mbonde.

Kufuatia hatua hiyo, Katibu wa Kamati ya Kuhamasisha Roho ya Umisonari(MAC), Esther Chilambo, ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Radio na Video Tumaini Dar-Es-Salaam, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam.

Kabla ya uteuzi na uhamisho wake, Padre Francois ndiye alikuwa katika nafasi hiyo ya ukurugenzi.

Ilifahamika katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika katika ukumbi wa Parokia ya Mtakatifu Yosef, jijini dar-Es-Salaam, Februari 27, 2001 kuwa, uteuzi wa Padre Francois utaanza Januari 2002. Hata hivyo amekabidhi madaraka na Mama Chilambo ameanza uteuzi wake.

Padre Francois ndiye muasisi wa Video Tumaini Agosti 15, 1993 na ameanzisha Radio Tumaini Februari 3, 1994.

Anaacha uongozi wa radio hiyo zikiwa ni siku chache, kabla haijazindua mkondo wa pili(Tumaini Two), utakaorusha matangazo kwa saa 24 kwa lugha za Kiingereza na Kifaransa. Utachukua vipindi toka Radio Canada International, Radio Netherland International, Deutche Welle, Radio Swiss International, na Radio France International. Utarusha matangazo katika masafa ya 105.9Mhz.

OCIC- Misionary Service, ni taasisi inayojishughulisha kusaidia uanzishaji na uendelezaji wa radio, televissheni, huduma ya video na mitandao ya mawasiliano ya kompyuta miongoni mwa makanisa na taasisi zake katika nchi za Afrika, Asia, M arekani ya Kati na Kusini, pamoja na Ulaya Mashariki.

Huyasaidia makanisa na taasisi zake kupata vifaa vya mawasiliano na fedha za kuanz a na kutoa mafunzo na huduma nyingine ili kufanikisha mawasiliano hayo.

Akitangaza uteuzi wa Mkurugenzi mpya wa Radio Tumaini, Askofu Msaidizi wa Jimbo katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini alimwelezea Esther Chilambo aliyekuwa akifanyakazi katika Tume ya Mipango katika Ofisi ya Rais, kuwa ni mchapakazi na mwenye kujitolea katika uinjilishaji.

Mhashamu Kilaini alimkabidhi picha ya Utatu Mtakatifu iliyosanifiwa huko Ulaya ikiwa ni ishara ya kuhimiza umuhimu wa kuhubiri Neno la Mungu kwa njia ya radio na video. Alisema jimbo lina imani kuwa kwa neema za Mungu, shughuli za Radio Tumaini zitazidi kuboreka zaidi chini ya uongozi mpya.

Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa MAC, Padre Joseph Healey, alimpongeza Mama Chilambo na akasema kuwa, wana MAC wanampongeza kwa kuteuliwa na kukubali kushika jukumu hilo.

Ilifahamika pia kuwa imeundwa Kamatiya Ushauri itakayoongozwa na mapadre wawili ili kuimarisha utendaji wa radio hiyo.

Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA), Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam na Mjumbe wa MAC, Mama Perpetua Mashele, alimpongeza Mama Chilambo kwa kushika wadhifa huo na kumuombea mafanikio zaidi.

Hii imekuwa changamoto kubwa iliyowatia hamasa WAWATA katika kudhihirisha umuhimu wa mwanamke katika jamii.

Wapentekoste wasali kuomba viongozi wasiwe waharibifu

Na Josephs Sabinus

KANISA La Pentekoste Tanzania(KLPT), usharika wa Kekomachungwa jijini Dar-Es-Salaam, limefanya maombi maalumu kuliombea taifa la Tanzania liwe na viongozi wanaojitolea kwa nchi na Kanisa na kuepuka uharibifu na kutokujali matatizo ya jamii.

Katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani hapo, Mchungaji Luther Shumbi wa usharika huo pia aliongoza maombi maalumu ili Mungu awaepushie wanajamii vitendo vya ukahaba na ujambazi ili waokolewe.

Waliziombea wizara na halmashauri ziboreshe huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na afya, maji, shule na barabara na kuwaondoa Watanzania katika umaskini.

Mhubiri katika ibada hiyo, Bw. Bosco Kisioli, alisema Kanisa liko hatarini kutokana na jamii kukumbwa na mabadiliko yanayokwenda na wakati katika sekta za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na kwamba hali hiyo imesababisha wenye imani duni kushindwa kwenda sambamba na mabadiliko hayo kiimani.

Alisema kutokana na udhaifu wa aliowaelezea kuwa wameegesha vidole kwenye kona za imani, shetani amepata nguvu za kuzishambulia familia za Kikristo ili hata imani kidogo iliyopo, iondoke.

"Hiyo ndiyo hali halisi ya Kanisa; linapoteza utukufu wake kwa kuwa watu wanataka wafanye mambo wenyewe bila kumshirikisha Mungu; wanasahau kuwa Mungu mwenyewe anasema nitakulinda."Naye Bibi Eudia Shumbi, aliyafananisha matendo na mtama na akasema, mtama mweupe yaani matendo mema yanayolinda maadili ya ki-Mungu, hayapaswi kuchanganywa na yale aliyoyaita mtama mwekundu.