Tafuteni kwanza vyanzo vya matatizo- Askofu

Na Pd. Ayoub Mwampela, Mbeya

MHASHAMU Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Kanisa Katoliki la Mbeya, amesema matatizo katika jamii hayatakwisha endapo jamii haitatumia nguvu, akili, mali, na muda wake kutafuta vyanzo vya matatizo badala ya kuhangaikia kutatua matatizo kijuu juu yanayojitokeza.

Mhashamu Chengula, aliyasema hayo katika Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu lililofanyika katika siku ya Jumapili ya Pentekoste parokiani Songwe, jimboni humo.

Alisema, kabla ya kutatua tatizo lolote, jamii husika haina budi kuchunguza na kubaini chanzo au kiini cha tatizo hilo na kukiondoa kabisa.

Katika ibada hiyo ya Juni 3, mwaka huu, Mhashamu Chengula alisema, "Jitihada ya namna hiyo(kujua chanzo cha tatizo) si tu kwamba itasaidia kulijua tatizo zima, bali pia itasaidia katika kulipatia tiba bora na ya moja kwa moja".

Akifafanua zaidi, Askofu Chengula alitoa mfano akisema, "Huwezi kujenga hospitali kwa nia ya kuwatibu wagonjwa tu bila kuyashughulikia yanayowafanya watu waugue,".

Aliongeza, "...na huwezi kusema unamsaidia maskini, bila kulitupia macho lile linalomfanya mtu huyo awe maskini".

Aliwaasa Wakristo kuonesha alama za uwepo wa Roho Mtakatifu katika Kanisa kwa kudumisha amani na upendo katika jamii.

Alitoa changamoto kwa vijana kujua kuwa, ni wakati wao sasa kujitokeza kwa wingi ili kumtumikia Mungu na Taifa lake kwa kufuata wito wa Upadre na Utawa.

Akisisitiza hilo, Askofu Chengula aliwakumbusha vijana kujiwekea malengo na dira zitakazowaongoza kufikia hatima ya maamuzi na malengo yao wawapo shuleni.

Naye Paroko wa Parokia ya Songwe, Padre Anselm Mwakasagule, katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari hizi, alisema mawazo ya Mhashamu Chengula, yamekuja wakati muafaka ambapo jamii ya Wakristo na Watanzania kwa jumla, wanakumbwa na matatizo ya mara kwa mara.

Alisema hali hiyo inatokana na jamii kutochimbua, kujua, wala kuondoa vyanzo vya matatizo hayo.

Alisema, endapo vijana watazingatia ushauri wa Askofu, vijana wanaochanganyikiwa kutokana na ugumu wa maisha baada ya kukosa ajira, watapungua.

Rushwa na UKIMWI ni mapacha; hawatakufa kama...'

Na Damasus Mtalaze, Kibakwe

KIONGOZI mmoja wa Kanisa Katoliki nchini, amesema rushwa na UKIMWI, ni matatizo mapacha ambayo hayatakoma endapo jamii haitayaona kama adui na hivyo, kunuia kupambana nayo kwa dhati.

Kiongozi huyo ambaye ni Paroko wa Parokia ya Kibakwe katika Jimbo Katoliki la Dodoma, Padre Leonard Amadori, pia aliwataka viongozi wa serikali na vyama vya siasa wawapo majukwaani, wazingatie kuzungumza athari za UKIMWI katika jamii na namna ya kupambana nao.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili ya Pentekoste ambayo huadhimishwa na Kanisa Katoliki Duniani kote kutimiza siku 50, baada ya Ufufuko wa Yesu, Padre Amadori alisema upo uwezekano wa kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la rushwa lakini, sio kuliondoa kabisa.

"Kuondoa kabisa tatizo la rushwa ni kitu kisichowezekana kwa sababu imekwisha jijengea mizizi imara ingawa inawezekana kulipunguza hata kufikia asilimia 99," alisema na kuongeza kuwa, usugu wa rushwa katika jamii unatokana na utovu wa maadili na siyo suala la mishahara midogo kama wengi wanavyodai.

Padre Amadori alisema tatizo hili la utovu wa maadili aliloliita ugonjwa, linatokana na ubinafsi miongoni mwa jamii ambao unashamiri kwa kasi.

"Rushwa ni dhambi, mpokeaji na mtoa rushwa; wote ni wadhambi... Mdhambi ni yule anayeng’ang’ania kuitumikia dhambi siku zote," alisema na kuongeza,

"Wizi, ujambazi, ushirikina, umalaya na utoaji mimba, mbona vinazidi kushamiri katika jamii yetu? Kwanini viwe vitu vya kawaida nchini vikiongozwa na ndugu yao rushwa?"

Akifafanua mintarafu UKIMWI, aliitaka jamii kupuuza kauli za kipumbavu kuwa KUFA NI KUFA TU au UKIMWI NI AJALI KAZINI zinazotolewa na baadhi ya watu wanaoishi kwa kuabudu tendo la ngono.

"Msiathirike na maneno hayo ya kipumbavu...Kifo cha UKIMWI ni kifo cha aibu kwa jamii na mtu yeyote anayeendekeza ufuska, ni muuaji. Ufumbuzi wa pekee na wa haraka kwa suala hili lililobeba kifo mbele yake, ni YESU".

Aliongeza, "Hata nyie viongozi wa serikali na vyama vya siasa mliohudhuria ibada hii, kemeeni UKIMWI mnapokuwa majukwaani siku zote".

Aliitaka jamii kushirikana katika kukemea matendo yote yanayochangia kuwepo kwa matatizo ya rushwa na UKIMWI huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Aliwataka Wakristo kumpa nafasi Roho Mtakatifu katika mioyo yao ili kuepuka tabia ya kuwa Wakristo wa nje, bila kujali undani wa nafsi zao.

"Sisi ni Wakristo ambao siku zote huhudhuria makanisani kuongea na Mungu lakini, kwanini hatutaki kubadilika? Ni dhahiri Roho Mtakatifu hajapewa nafasi katika mioyo yetu," alisema.

Mchungaji wa EAGT aeleza uchumba wa sasa ulivyo mbovu

Na Rose Romani, TIME

MCHUNGAJI, Philemon Fili wa kanisa la Evangelism Assemblies of God Tanzania (EAGT), amewataka vijana ambao hawajaoa na wale ambao hawajaolewa, kuzingatia ukweli kuwa uchumba ni kipindi cha kuzoeana na kujuana kitabia na sio kujuana kimwili.

Aliwataka vijana kujua na kutofautisha vipindi vya ndoa na vipindi vya uchumba na akafafanua kuwa kipindi cha uchumba sio kipindi cha kukutana katika tendo la ndoa bali tendo hilo ni halali ndoa kamili inaposhuhudiwa kanisani na mbele za Mungu.

Alikuwa akizungumza hivi karibuni katika kambi ya vijana wa Kanisa hilo, iliyofanyika katika kanisa la EAGT, Sinza jijini Dar-Es-Salaam.

Amewashangaa vijana wanaochagua wachumba kwa kuzingatia vigezo vya mali na vipato vya wachumba badala ya kuomba Mungu awasaidie kumpata mchumba mwenye tabia njema huku wakizingatia kuwa kuoa au kuolewa, ni mpango wa Mungu.

Mchungaji huyo alisema kuwa, hali ya uchu wa tendo la ndoa kabla ya kuoa au kuolewa, ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Alibainisha kuwa, uchumba sahihi ni ule unaodumu kwa muda wa kutosha ili kuwapa nafasi wachumba kujuana wazi kitabia na siyo kimwili.

Alisema ndoa inayozingatia mali, sura na kipato cha mmoja wa wahusika, haifai kwa kuwa ina hatari ya kubomoka muda mfupi licha ya kuwa siku ya ndoa ilifana machoni pa watu.

Mchungaji Fili aliwaasa vijana kuwa na subira huku wakidumu katika maombi ili Mungu awachagulie wachumba wenye kuwafaa katika maisha.

Wanawake wamwibia mwenzao baada ya kujifungulia kwenye treni

l Walimsaidia akajifungua vema kisha wakajilipa wenyewe

l Wambakizia 6000/= zimsaidie yeye na mwanae

Na Damasius Mtalaze, Singida

YALIYOTABIRIWA katika Maandiko Matakatifu kuhusu siku za mwisho kuwa watu watapenda fedha kuliko watu wao, yametimia kwa Mama Juliana Mathias wa kijijini Siuyu, wilayani Singida Vijijiini.

Mama huyo, baada ya kusaidiwa na wanawake wenzake ili ajifungue, walifanikiwa naye akajifungulia kwenye treni, kisha bila haya wala huruma, wanawake hao, walitoweka na pesa za mzazi na kumuacha akihangaika na mtoto mchanga hospitalini.

Mama huyo alizungumza na mwandishi wa habari hizi siku chache baada ya tukio hilo, akiwa katika Hospitali ya Mt. Gasper De Buffalo, iliyopo Itigi, alikolazwa katika kitanda namba 13 jengo linalojulikana kwa jina la MEDICAL B.

Alisema kuwa, siku hiyo alikuwa anatokea Kigoma anakoishi kikazi na mmewe akielekea nyumbani kwa wazazi wake wilayani Singida. Hii, ni baada ya kuchukua likizo ya uzazi huku siku za kujifungua kwake zikiwa zimekaribia kabisa.

Alisema, "Tarehe 3, mwezi huu(Juni), niliondoka Kigoma kuelekea nyumbani kwa wazazi kule kijijini Siuyu. Nilikuwa na hali ya ujauzito. Wakati huo, mimi na mme wangu tulikuwa tayari tumepiga simu kuwa wazazi kule Singida ili wamtume mtu wa kunipokea Stesheni(Itigi) kwa kuwa nilikuwa peke yangu."

"Nilipofika njiani, nilianza kujisikia hali ya kuumwa uchungu wa uzazi," akaendelea kusimulia, "Katika behewa nililokuwa (Daraja la Kwanza; kulala), kulikuwa na wanawake wenzangu watatu.

Hata mimi sasa, hofu yangu ya kuteseka na kuhangaika kwa mambo ya uzazi, haikuwa kubwa maana nilijua lolote litakalotokea, nitasaidiwa; si kuna wanawake wenzangu!"

"Mambo yalizidi kukaribia hadi wakati wenyewe wa kujifungua ulipofika. Hapo mambo yalikuwa magumu hata nikasahau kila kitu nilichokuwa nacho.

Bahati nzuri, wale akina mama walinisaidia sana katika hali hiyo na mimi ninashukuru Mungu nimejifungua salama salimini humo humo ndani ya treni; tena bila tatizo lolote," akasema.

Akaendelea kuelezea yaliyomsibu, "Nilipofika Stesheni ya Itigi, niliteremka na wale akinamama waliendelea kunisaidia kiungwana hadi nilipofika chini huku wakionesha huruma na upendo juu yangu."

Anasema baada ya kuteremka toka ndani ya treni akiwa na akinamama wale, alikutana na mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Salome Mathias, aliyekuja kumpokea stesheni.

"Baada ya akina mama wale kunisaidia kuteremka mimi na kichanga changu, nilimwambia Salome anipe kibegi changu kilichokuwa na shilingi 66,000..."

Huku akiwa na mtoto wake mchanga hospitalini hapo, mama huyo alisema kuwa, lengo la kuagiza mkoba huo lilikuwa kumuwezesha kutoa walau fedha kidogo za soda ili kuwashukuru akinamama wale kwa wema waliomtendea.

Akaendelea, "Waliposikia nimemwambia mdogo wangu anipe mkoba ule uliokuwa na hela niwape asante, waligoma kabisa wakisema,

"Asante mama acha tu! Tumekusaidia tu!" "Hapana mama fedha za nini; sisi tumekusaidia kama wazazi wenzako. Baki nazo tu" "siku nyingine na wewe utamsaidia mwingine."

Mama huyo aliongeza kuwa, alipoona hali ile, aliongeza shukurani kwao huku akiamini kuwa miongoni mwa watu wema, hao nao wamo.

Alisema anawashukuru zaidi hasa anapozingatia namna watu wa siku hizi watu wanavyothamini fedha kuliko utu.

"Nilipofika hapa (hospitali), sasa nikamwomba mdogo wangu anipe kile kibegi kidogo ili nimpe fedha ya kutafutia chakula na nyumba ya kulala wageni kwa ajili yake."

Mama huyo anasema, baada ya Salome kumpa kibegi kile, alishituka kuona badala ya kuwa na shilingi 66,000, sasa zilikuwamo shilingi 6,000 pekee.

"...Hapo ndipo nilipogundua kuwa wale akina mama wameniibia fedha yangu yote shilingi 60,000 na kunibakishia shilingi 6000.

Alibaini kuwa kumbe ndiyo maana walikuwa wanakataa nisiwape chochote ili asigundue hila zao.

"Maskini kumbe walijua wamekwisha jichukulia wenyewe," alisema.

Alizidi kulalamika kuwa pesa iliyobaki, ilikuwa kidogo na isingeweza kumsaidia yeye kama mzazi na matumizi ya mtoto mchanga hapo hospitalini.

Pia, alisema kiasi walichombakizia kilikuwa kidogo hasa ukizingatia kuwa Salome naye alizitegemea.

Alisema kwamba, pia alibaini kuwa saa yake ya mkononi pia ilikuwa imechukuliwa sambamba na fedha hizo (Shilingi 60,000).

Juu ya akina mama hao waliovalia ngozi ya kondoo juu ya sura zao kumbe ni nyoka wenye sumu kali, alisema ingawa anawashukuru kwa kusaidia kujifungua salama ndani ya treni, wakuwa wamemtesa sana.

Alisisitiza kuwa, alikuwa anateseka na mwanae wakiwa hospitalini pamoja na mdogo wake, Salome kwani shilingi 6,000 walizombakizia, hazikuwa zinatosha.

"Namshukuru Mungu kunifikisha katika hali ya kujifungua salama na pia, ninawashukuru wale wanawakw wenzangu kwa yote waliyonitendea na katoto kangu kachanga, Mungu mwenyewe ndiye anajua namna atakavyonilipia," alisema.

Akitoa wito kwa akinamama hao waliomfanyia wema kisha wakaugeuza kuwa ukatili usiopimika, Mama Juliana alisema, "Watu wawe na msaada wenye upendo na huruma ya dhati; siyo kuchanganya na tamaa".

Alisema anawaombea roho wa shetani awatoke ili wanapowasaidia wanaohitaji msaada wao, wasiwasaidie huku wakitawaliwa na tamaa.

Salome (mdogo wake), alisema mkasa wa dada yake ni mkubwa lakini, anamshukuru Mungu kwa kila jambo. "Tunawashukuru wote waliotusaidia kwa hali na mali toka hali ya ufu hadi uzima... Tunamshukuru Mungu kwa yote kwani huu ni uwezo wake," alisema.

Hadi tunapokea taarifa hii toka Singida kwa njia ya posta, mama huyo na mtoto wake mchanga walikuwa wameruhusiwa kutoka hospitalini.

Wanawake wanaoringa wanakwamisha maendeleo ya familia - Mch. Rwakatare

l Ataka waonee uchungu mali za familia

Na Neema Dawson

MCHUNGUAJI Getrude Rwakatare wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), amewashauri wanawake wenye tabia ya maringo, kuachana nayo na badala yake, wajishughulishe kiuchumi ili kujiletea maendeleo katika familia badala ya kutegemea kupewa kila kitu na waume zao.

Aliyasema hayo wakati wa Kongamano la Wanawake wa Afrika Mashariki lililofanyika katika kanisa hilo lililopo Mikocheni B, jijini Dar-Es-Salaam na kuhudhuriwa wa Wanawake kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, Kenya na Uganda.

"Wanawake wengi hawapendi kujishughulisha na shughuli yoyote hata biashara badala yake, wanakaa tu kusubiri pesa kutoka kwa waume zao...Wengine wanabaki kuringia sura zao wakidhani zitawasaidia...," alisema.

Mchungaji Rwakatare alisema katika karne hii, wanawake wengi wamekuwa wanaachwa na waume zao si kwa sababu hawapendwi, bali kutokana na hali ya kipato duni katika familia.

Alisema hali hiyo duni kiuchumi, inawafanya baadhi ya wanaume wawaone wanawake kama mizigo katika familia zao.

Alisema, ili kuwe na amani na maendeleo katika familia, kila mmoja mke na mume hana budi kuuthamini uwepo wa mwenzie katika ndoa yao na hivyo, kuheshimiana.

"Mwanaume ni Rais ndani ya nyumba na anafuatiwa na Waziri Mkuu ambaye ni mwanamke. Hivyo, lazima Waziri Mkuu amheshimu Rais na Rais amheshimu Waziri Mkuu. Hata katika familia, lazima mume na mke waheshimiane," alisema.

Aliongeza kuwa, wanawake hawana budi kuepuka mambo yanayowaathiri waume zao ikiwa ni pamoja na kiburi, hasira, dharau na manung’uniko kwani vitu hivyo visipoondolewa, ni hatari kwa maisha ya ndoa.

Aliilaumu tabia ya baadhi ya wanaume kudhani kuwa suluhisho sahihi la migogoro katika ndoa, ni kuachana na mke.

"Je, ni halali kumwacha mke wako kwa sababu yoyote?" alihoji na kuongeza kuwa dawa bora ni mijadala ya mara kwa mara na kila mmoja kukiri kosa lake na hivyo kuondoa tofauti zao.

Naye Erick Samba, anaripoti kuwa, Mchungaji Rwakatare katika Kongamano hilo, amesema wanawake hawana budi kuwa walinzi wa mali za familia na kuwa waangalizi wazuri wa mali za waume zao ili wawaamini na kuwa wazi juu ya mishahara waipatayo.

Aliwataka wanaume kuwaonesha upendo wake zao kwa kuwa karibu nao kila inapowezekana na hata kuwanunulia zawadi mbalimbali kadiri wanavyozipata.

"...Ukiwa safarini kitu kizuri unachopata, mpelekee mama utagusa moyo wake na kuwa na amani nyumbani," alisema.

Aliwataka wenye wazazi walio hai, wawatunze vema na kwamba hali hiyo, itawaongezea baraka za Mungu.

Katika Kongamano hilo Mchungaji Rwakatare aliwaita mbele baadhi ya watu waliokuwa pale pamoja na wazazi wao waliotunzwa vizuri na kuonekana kama ndugu.

Kongamano hilo la wiki nzima liliandialiwa na kanisa la Tanzania Assemblies of God, Mikocheni B na kuhudhuriwa na watu toka madhehebu mbalimbali ya Kikristo jijini Dar-Es-Salaam.

WAWATA Njombe waanzisha mradi wa vikapu

Na Getrude Madembwe

Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Jimbo la Njombe wameanzisha mradi wa kusuka vikapu kwa akina mama wanaoishi vijijini kwa lengo la kuwasaidia akinamama hao kuinua vipato vyao kwa njia nyingine badala ya kutegemea kilimo pekee.

Msimamizi wa Miradi ya WAWATA jimboni humo, Bi. Dafrosa Mgimba, alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na gazeti hili jijini Dar-Es-salaam.

Alisema wameanzisha mradi huo kwa ushirikiano na shirika moja lisilo la kiserikali la AMKA ambalo ndilo watafutaji wa masoko nje ya nchi.

"Shirika la AMKA ndilo linalotutafutia masoko kwa kutuletea order kutoka nchi za nje kama vile Japan, China na nchi nyingine," alisema.

Bi. Mgimba aliyekuwa safarini kuelekea Arusha katika maonesho ya bidhaa za mikono yaliyotarajiwa kufanyika Juni 9-16, mwaka huu ambayo yalitarajiwa kuwahusisha wote wanaoshirikiana na shirika hilo la jijini Dar-Es-Salaam.

"Unajaua watu wa nje wanazipenda hizi rangi za asili na hata upatikanaji wake siyo mgumu sana," alidokeza.

Bi. Mgimba alisema shughuli za ufumaji wa vikapu haziathiri kilimo chao kwa kuwa hufanyika kati ya miezi ya Mei hadi Septemba wakati ambao kiangazi huwa kimepunguza shughuli za kilimo.

Alisema mradi huo unawashirikisha wanafunzi wa kike wanaosoma na kwamba katika kipindi cha mapumziko au kipindi cha sanaa WAWATA huwatembelea wanafunzi hao na kuwafundisha jinsi ya kutengeneza vikapu hivyo.

Alisema pesa wanazopata akina mama hao wa WAWATA, huwasaidia kuwasomesha watoto wao badala ya kuwaachia jukumu hilo wanaume wao pekee.

'Umoja wa kitaifa uanzie katika familia'

Na Elizabeth Steven

WAKRISTO wote wamehimizwa kushirikiana na kuleta umoja miongoni mwao ikiwa ni pamoja na kushughulikia mambo yenye manufaa.

Ushauri huo ulitolewa Jumapili iliyopita na Padre Paul Njoka, wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu jijini Dar-Es-Salaam.

Katika mahubiri hayo, Padre Njoka alisema kuwa, umoja wa kitaifa ambao umekuwa ukisisitizwa na wanajamii wakiwamo viongozi mbalimbali wa kidini, kisiasa na kiserikali, hauna budi kuanzia katika ngazi ya familia badala ya kukazania tu umoja wa kitaifa na kimataifa kabla ya kuimarisha umoja wa kifamilia.

"...Tunataka umoja wa kitaifa uanzie katika familia zetu na kama kweli tunautaka, basi tuanzie hukohuko kwenye familia hadi ngazi ya kimataifa," alisema.

Aidha, Padre Njoka aliwataka Wakatoliki kuzingatia umuhimu wa kufanya "Ishara ya Msalaba" kama kitambulisho cha imani Katoliki, kinga na njia ya kuwaongoza katika maisha yao.

Alisema, Wakatoliki hawana budi kutoogopa macho ya watu wala kuona aibu na badala yake, waitumie Ishara hiyo kila mahali wanapokuwa na kila wanapokumbwa na vishawishi.

"...hata tunapoingia ndani ya basi, tufanye ishara ya msalaba; tunapotoka tufanye ishara ya msalaba na hata mahali popote tunapopatwa na vishawishi, tusisite kufanya ishara ya msalaba," alisema Padre Njoka.

Jumapili hiyo, Wakatoliki kote duniani, walisherehekea Siku ya Utatu Mtakatifu yaani; Mungu mmoja katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Hananasifu wanufaika na Jubilei Kuu

Na Pelagia Gasper

KASI ya ongezeko la waamini kupokea Sakramenti ya Ndoa katika Parokia ya Mt. Anna Hananasifu, katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, ni matunda ya maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo duniani; amesema Padre Daudi.

Akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake katikati ya juma, Padre Ndelacho Daudi ambaye ni Paroko wa parokia hiyo, alisema ongezeko hilo ni matunda ya jubilei hiyo iliyofikia kilele chake Januari 6, 2001.

Alisema waamini wake wametambua umuhimu wao kubadilika kiroho na hivyo, kuanza maisha mapya yanayoendana na maadili ya Ki-mungu.

Alisema anawapongeza waamini hao na kuwaombea wazidi kuiva na kudumu katika imani.

Padre Daudi alisema kabla ya maadhimisho hayo, waamini wengi hawakushiriki sakramenti kadhaa kutokana na kufungwa na vikwazo lakini tangu kipindi cha jubilei, wengi wamebadili mtindo wao wa maisha na kujitokeza kupata sakramenti mbalimbali za Kanisa.

Alisema wengi wao walikuwa wakiishi kinyumba bila sakramenti na kwamba hali hiyo iliwafanya waone aibu kujitokeza katika mambo ya kikanisa.

"Kwa kiasi kikubwa ambacho hata mimi sikukitarajia, jubilei imeleta mafanikio makubwa kiroho... waliofunga ndoa wameongezeka mno.

Hata waliokuwa na matatizo, wameelekeza shida zao kwa Mungu na sasa wameanza kushiriki Sakramnti ya Upatanisho," alisema.

Aliongeza kuwa, sababu nyingine ya waamini kuyapa mwitikio maadhimisho ya Jubilei Kuu parokiani, ni kitendo cha Askofu Method Kilaini kuwasimika viongozi wa ngazi mbalimbali tangu jumuiya hadi parokia.

Alisema kitendo cha Askofu Kilaini kuchimba msingi kwa ajili ya upanuzi wa kanisa lao, kilchangia ongezeko la imani kwa waamini wake na akawataka waiboreshe siku hadi siku.

Padre Daudi alidokeza kuwa, fedha kwa ajili ya upanuzi wa kanisa hilo, zimetokana na waamini wenyewe pamoja na wafadhili wa ndani na nje ya parokia.

Aliwahimiza kudumisha moyo wa kujitolea ili kusaidia na kufanikisha shughuli za kikanisa.

Upanuzi huo ukikamilika, kanisa hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua waamini 1000 badala ya 400 wa sasa.

Parokia ya Hananasif inazo Jumuiya Ndogondogo za Kikristo 25. Haina vigango.

'Mkinuniana ndani ya nyumba, hamfanikiwi ng'o!'

Na Rose Romani, TIME

"NDANI ya nyumba pakiwepo fitina, ugomvi, kutoelewana na masengenyo, mjue Mungu hayupo kati yenu na kamwe hamtapata mafanikio".

Hayo yalisemwa na Mchungaji Erick Mrindoko wa Kanisa la Waadventisti Wasabato la jijini Dar-Es-Salaam, alipowatembelea waamini wa kanisa hilo eneo la Kimara-Resort kwa lengo la kuwafundisha jinsi ya kukaa na familia.

Alisema anasikitishwa na vitendo vya chuki na ugomvi vinavyofanyika siku hizi katika familia nyingi.

"Baadhi ya familia zetu neno upendo limekuwa msamiati kwani halipewi uzito. Hakuna upendo hata kati ya baba na mama. Mama hamjali baba na hata baba hamjali mama. Hii inatokana na kutothaminiana kwao," alisema.

Aliongeza kuwa, kutokana na upendo kutokuwepo ndani ya familia, ndoa nyingi zimevunjika na watoto kuishi katika maisha ya shida huku wakikosa malezi bora.

"Mama wewe umeshindwa kumtunza mumeo kumpa mapenzi mazuri na kumwonesha upendo wa dhati, je, wewe unategemea akimpata atakayempatia anavyovitaka atamwacha?" alihoji.

Aliwashauri wanawake wawapende na kuwatunza waume zao kwani wao wenyewe wanaweza kuwa sababu tosha ya kuchangia kuvunjika au kudumu kwa ndoa.

Alisema ili kudumisha upendo katika familia, kila mmoja katika ndoa, hana budi amuone mwenzake kuwa ni wa thamani kuliko yeye.

Alisema inasikitisha kuona wanadamu wanakuwa wagumu kuyatii mafundisho ya Kanisa na kwamba hali hiyo, ndiyo inachangia matatizo hayo katika familia nyingi.

"Kanisa limekuwa likisisitiza jamii kuepukana na matendo maovu yafanywayo hapa duniani lakini, binadamu tumekuwa wagumu kubadilika na kujirekebisha," alisema.

Aliwakumbusha wanandoa mintarafu ahadi walizotoa kanisani siku ya ndoa yao.

Akakumbushia kuwa, siku hiyo kila mmoja aliahidi kumpenda na kumsaidia mwenzake kwa wakati wote; wa raha na shida.

"Wewe mwanamke, mtii mumeo kwa yote na mume umpende mkeo. Pakiwepo na upendo; Mungu akiwa ndani ya familia zetu, shetani hatapata nafasi ya kuwaingilia," alisema.

255 wavuna walichopanda Dar

l Paroko awataka wasipoteze

Na Mwandishi Wetu

WAAMINI wa Kanisa Katoliki jijini Dar-Es-Salaam, ndugu, jamaa na marafiki zao, Jumapili iliyopita walifurika katika Kanisa la St. Maurus- Kurasini, kushudia na kuwashangilia vijana waliopata Sakramenti ya Komunio ya Kwanza.

Siku hiyo, Paroko wa Parokia hiyo iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre Mieczyslaw Kijaczek, alitoa sakramenti hiyo kwa vijana wapatao 255 waliofaulu mafunzo yao ya mambo ya Kanisa.

Katika ibada hiyo, Padre Kijaczek, aliwataka vijana waliopokea Komunio ya Kwanza, kudumisha heshima ya maisha yao ya kibinadamu huku wakizingatia na kuuheshimu Umungu wa Yesu Kristo.

Alisema njia pekee ya kufanya hivyo, ni kudumu katika kupokea Ekaristi Takatifu katika hali ya neema, badala ya kuipokea katika hali ya dhambi hali ambayo ni hatari.

Alisema ni vema wakawaza, kusema na kutenda kama yasemavyo mafundisho ya ki-Katoliki ili kuepuka uwezekano wa kuwa wasaliti wa imani. Alisema hali ya usaliti wa imani ni hatari na inaweza baadaye ikawaliza machozi.

"Msipojitahidi kutunza neema ya Mungu, baadaye mnaweza kulia machozi na endapo mtafanya yanayofundhiwa, furaha ya leo itadumu na kuwa ya manufaa kwa Kanisa na jamii," alisema.Paroko huyo wa Kurasini.

Aliwapongeza wazazi, walezi na walimu wa watoto waliohitimu mafunzo hayo kwa kuwalea na hatimaye kuwawezesha watoto hao kupata sakramenti hiyo.

Katika sherehe hizo zilizotawaliwa na shamrashamra mbalimbali, Padre Kijaczek aliwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo na kupokea sakramenti hiyo pamoja na rozali.

Kulikuwa na watumbuizaji wa ngoma za asili, matarumbeta, kikundi cha bendi ya muziki wa mapipa, pamoja na watumbuizaji na washangiliaji binafsi.

SAHIHISHO

Katika uk.10 wa toleo lililopita, chini ya habari WAAMINI WA MBAGALA WATUMIA NGUVU KUJILETEA MAENDELEO, tulitaja kimakosa kuwa mchango parokiani Mbagala, ulikuwa kwa ajili ya ujenzi wa kanisa jipya. Usahihi ni kwamba, mchango huo ni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Huduma za jamii, Kizuiani, jijini Dar-Es-Salaam.

Wananchi wataka serikali iingilie mgogoro na kampuni ya madini

Na Gimonge Haruni, Tarime

WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu katika vijiji vya Gamburu Nyamwaga, Nyangoto, Kewanja na Kerende; vinavyoizunguka migodi ya Nyabigena na Nyabirama, wilayani Tarime, wameiomba serikali kuingilia kati mgogoro baina yao na kampuni ya utafiti na uchimbaji dhahabu ya Afrika Mashariki Gold Mines(AMGM) LTD.

Wamesema AMGM imewasababishia hasara iliyowaletea umaskini huku ikidai kuwa inafanya utafiti ambapo sasa ni mwaka wa nane hawajaona mafanikio yoyote.

Wamesema kwa kipindi chote hicho, AMGM haijawalipa fidia ya mashimo yao ya machimbo ya dhahabu wala mazao yao jambo walilodai ni wizi na utapeli.

Katibu wa wachimbaji hao, Bw. Kirigiti Sasi, alizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni baada ya kufanyika mikutano miwili tofauti katika maeneo ya Nyabikondo na Kewanja.

Alisema wananchi wamesononeshwa na taarifa zinazotolewa na AMGM kuwa inawanufaisha kwa kuwaboreshea huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na afya, elimu na mawasiliano.

Amesema maneno hayo si kweli kwa vile AMGM imeanza utafiti wake mwaka 1994 hadi 1997 kampuni ilipoandika barua ya kusimamisha kufanya shughuli za maendeleo katika vijiji hivyo.(nakala tunayo).

Walidai AMGM imekataa kutoa malipo baada ya serikali kutathimini mazao ya wakulima wa eneo la migodi fedha ambazo zilikuwa zaidi ya milioni 480 na wachimbaji wengine wamekufa wakisubiri fidia yao.

Katika mkutano wa pili uliofanyika hivi karibuni na uliowashirikisha wananchi na kampuni ya AMGM, wachimbaji hao walitoa siku tatu kwa kampuni hiyo kulipa fidia kwa wadai.

Walisema kinyume na kufanya hivyo, wachimbaji na wenye mazao ndani ya migodi hiyo wangerudi kufanyakazi katika maeneo yao.

Hadi tunakwenda mitamboni, hakuna taarifa zaidi tulizopata juu ya suala hili.

Kauli hiyo imefuatia Mwenyekiti wa AMGM, Bw. Jeffer Stawati, kusema kuwa kampuni yake haitalipa mazao ya wakulima na kuongeza kuwa utafiti uliofanywa na AMGM, umeonesha kuwa eneo la Nyabigena halina dhahabu na hivyo, kampuni hailitaki.

Alisema AMGM itatumia sehemu uliopo mgodi wa Nyabirama Gold Mines ambao alidai, walau una dhahabu kidogo."Mimi siwezi kulipa fidia yoyote labda serikali iyalipe," alidai Jeffer bila kufafanua.

Bw. Jeffer Stawati amefafanua kuwa atalipa sehemu ndogo ambayo waliitumia kufanya utafiti na kuzua zogo kubwa kwa wale waliofyekewa miti na mashamba.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja ambaye alidai ni mmoja wa wananchi waliathirika na shughuli za AMGM, Bw. Marwa Sasi, alisema, "Tunataka atulipe mashamba na mashimo yetu aliyofukia ndipo aondoke".

Mkuu wa Wilaya ya Tarime Bw. Pascal Mabiti, hakupatikana kuzungumzia suala hilo lakini awali, aliwataka wananchi kuwa na subira ili ufumbuzi wa suala lao utafutwe.

Mtenda dhambi ni mtumwa- Kauli

Na Bilhah Massoro

MWINJILISTI David Mwakwenda wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), amesema kila mtenda dhambi hana budi kujihesabu miongoni mwa watumwa.

Aliyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa "Matendo Makuu ya Mungu" uliofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Mbezi Beach Christian Center, jijini Dar-Es-Salaam.

"Watendao dhambi wote ni watumwa wa dhambi bila kujijiua" alisema.

Mwinjilisti huyo alisema ulevi, uzinzi, ukahaba, na matumizi ya dawa za kulevya, ndivyo vitu vinavyo waharibu watu katika ulimwengu huu.

Alisema anawashangaa vijana wanaotenda dhambi kwa madai kuwa, wanakwenda na wakati na akasema watu wa namna hiyo, hawajui kuwa kwenda na wakati ni kumpokea Yesu katika mioyo yao.

"Hata uwe na nyumba na gari nzuri bila kumpokea, Yesu ni kazi bure," alisema.

Mwinjilisti Mwakwenda alisema vijana hawana budi kujua na kuzingatia ukweli kwa, uzima wa milele haupatikani kwa kwenda shule, bali kwa njia ya kumwamini Yesu na kumtumikia.

Aliwataka wanaofikiri kuwa juhudi za kutafuta uzima wa milele ni kuchanganyikiwa, waamini kuwa hali hiyo inatokana na hali ya kutotenda dhambi na kumwamini Yesu katika maisha yao.

Wakati huo huo: Watoto wadogo wa Wavumbuzi(Adventure) wa Kanisa la Wasabato la Magomeni wamewaalika watoto yatima wa Kituo cha Kurasini jijini Dar-Es-Salaam, katika siku maalumu waliyoiandaa kwa ajili yao.

Pamoja na sherehe hiyo iliyofanyika hivi karibuni, watoto hao walipata zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na misaada ya nguo na viatu.

Akizungumza katika sherehe hizo, mmoja wa wazee wa kanisa, Daudi Uze, alisema watoto yatima hawana budi kujiona sawa na watoto wengine hivyo, kujijengea msimamo wa maisha na kwamba, Mungu atawasaidia.

"Mpango wa Mungu kuwasaidia watu haulengi kwa watoto fulani fulani, ni kwa wote na hivyo, watoto wote mnapaswa kumwabudu Mungu kwa kila jambo," alisema.

Akizungumza kwa niaba ya yatima wenzake, mtoto Leonard alisema wameridhishwa na ukarimu waliooneshwa na watoto wa "Adventure" na akawashukuru pamoja na uongozi wao mzima.

Msikubali kuugua kwa uchafu - Ushauri

Na Elizabeth Steven

JAMII imetakiwa kutoruhusu kusumbuliwa na magonjwa yatokanayo na uchafu wa mazingira, kwa kuwa magonjwa hayo yanaweza kuepukika na yapo chini ya uwezo wa watu kuyadhibiti.

Hayo yalisemwa katika ibada ya Jumapili iliyopita, wakati Padre Ireneus Mbahulila wa Parokia ya Makuburi, katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, alipokuwa akihubiri katika ibada iliyofanyika parokiani hapo.

Alisema magonjwa yanayotokana na uchafu wa mazingira toka viwandani na majumbani, yanaweza kuepukika endapo jamii itatumia juhudi katika kupambana na kuondoa uchafu katika mazingira.

Aliongeza kuwa juhudi hizo zitafanikiwa endapo tu, jamii itaepuka kasumba ya kuwategemea watumishi wa serikali na idara husika katika masuala ya usafi, kushughulikia jukumu hilo kwani ni wajibu wa kila mtu na madhara yake hayachagui mtu wa kuathirika, bali huidhuru jamii nzima.

"Tumepewa akili na hekima wa kuweza kupambana mambo mengi ukiwamo uchafu huo. "Ni ajabu sana kumuona mtu anatupa takataka nje tena barabarani eti kwa sababu tu anajua wapo watu wanaofagia," alisema Padre Mbahulila.

Alisema kutokana na upendo wake Mungu, amempa kila binadamu akili na hekima ya kumwezesha kufahamu mema na mabaya.

Pia, aliwataka kuachana na malimwengu ambayo alisema hayana maana wala faida isipokuwa, upendo.

Alisema mtu yeyote ambaye hatumii iipasavyo akili pamoja na hekima kamwe matendo yake huwa si mema, maana mtu huyo huwa haongezwi na Roho bali huongozwa na dhambi yenyewe ambayo imemtawala.

Aliwataka waamini kutambua na kuamini kuwa wanaongozwa na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa makini na mafundisho yanayotolewa na watu mbalimbali juu ya imani kwani, vikundi vingine, hupotosha badala ya kufundisha imani ya kweli.

Aliwataka waamini wa Parokia hiyo kufahamu kuwa kunyakuliwa kwao kutatokana na kuishikadiri ya imani yao.

Aidha, aliwahimiza wakiri kwamba ni wakati wao sasa kuamini kuwa wanaongozwa na Roho Mtakatifu.

Watoto wa miaka tisa wachangia ujenzi wa kanisa

Na Wilhelm Mpangile, Morogoro

WATOTO wa kati ya miaka 9 na 15 wa Parokia ya Mtakatifu Maria, MODECO katika Jimbo Katoliki la Morogoro, wamechanga shilingi 43,530 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa.

Mchango wa watoto hao ni matunda ya wito wa Padre Josephat Msongore , aliyeshauri kuwapo kwa misa maalumu kwa ajili ya watoto hao kutumia vipawa vyao kulichangia kanisa. Misa hiyo ilifanyika siku ya Jumapili ya Pentekoste katika kanisa jipya ili watoto hao walione kwa karibu.

Katika mahubiri yake, Padre Msongore aliwashauri vijana kutambua maana kamili ya vipaji vya Roho Mtakatifu na namna ya kuviishi na kuvitumia katika kulitumikia Kanisa.

Alisema tangu utoto wao, vijana hawana budi kujenga mahusiano bora baina yao na Kanisa, wazazi, walezi na vijana wenzao kwa kuwa watii, wenye huruma na wenye moyo wa kujitolea katika kulitumikia Kanisa na jamii kwa jumla.

Mlezi huyo wa kiroho aliwahimiza vijana kuwa na utaratibu mzuri katika maisha ikiwa ni pamoja na kushiriki sala kwa pamoja, kutambua na kuthamini maana ya adhimisho la Ekaristi Takatifu.

Katika misa hiyo iliyohudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Walei wa parokini na masista ambao ni walezi wa vijana hao katika mafundisho ya dini, Katibu wa Halmashauri Walei parokiani hapo Bibi Lucy Senzighe, aliupongeza uhamasishaji uliopelekea watoto hao kulichangia Kanisa kwa kadri ya uwezo wao.

Alisema, "Tukitimiza maagizo ya viongozi wetu wa kiroho, tunaweza kufanikisha mambo mengi likiwamo hilo la mchango wa ujenzi wa kanisa."

Aliwapongeza wazazi waliowawezesha watoto wao kuwakilisha michango ikiwa ni njia ya kuitikia wito wa Padre Msongore kuwafunza vijana kulitegemeza Kanisa tangu wakiwa wadogo.

Wizara yataka wanaopuuza UKIMWI, wapuuzwe

Na Getrude Madembwe

MKURUGENZI Msaidizi wa Kitengo cha Jinsia katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Bw. Mohamed Ally, amewataka wahitimu wa kozi ya Uhazili na jamii kwa jumla, kuwapuuza wanaodai kuwa, kuugua UKIMWI ni sawa na ajali kazini.

Aliyasema hayo katika mahafali ya wahitimu wa kozi ya Uhazili yaliyofanyika katika ukumbi wa Msimbazi Centre, jijini Dar-Es-Salaam, juma lililopita.

Alitahadharisha kuwa, endapo wahitimu hao hawatakuwa miongoni mwa watu wanaochangia kupambana na UKIMWI eti wakafanyia kazi hoja potofu kuwa UKIMWI ni ajali kazini, ipo hatari wakaangamia wakiwa bado vijana.

"Ugonjwa bado upo na hauna kinga wala tiba; sasa ukiupata, ujue umekwenda na hakuna cha msalia Mtume," alisema.

Ally aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri katika Wizara hiyo, Dk. Asha Rose Migiro, aliwataka wahitimu kukumbuka kitu UKIMWI kila wanapoingia katika majaribu na vishawishi vya kushiriki vitendo vya ufuska.

"Jamani naomba mjiepushe na kila tabia ambayo inachochea maambukizi ya ugonjwa huu...msiridhike na elimu mliyonayo. Yule asiyependa kujisomea, ajue ni mtu mfu," alisema.

Aliwahimiza kutotumaini kupata ajira serikalini bali wajue kuwa, elimu sharti itumike kuboresha maisha yao ikiwa ni pamoja na kujiajiri wenyewe.

Aliwahimiza kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili wajileteemaendeleo.

Akijibu risala ya wahitimu hao walioomba chuo kiongeze idadi ya kompyuta, Mkurugenzi wa Msimbazi Center, Padre Benedict Shayo, alisema kuwa chuo kinatarajia kuongeza kompyuta ili zikidhi mahitaji.

Alisema licha ya kutoa mafunzo ya kompyuta, chuo hicho kina mpango pia wa kutoa huduma za E-Mail, internet, karakana ya magari na huduma nyingine zitakazomsaidia Mtanzania kujipatia ujuzi kwa gharama nafuu.

"Jengeni tabia ya kufikiri mara mbili. Elimu hii mnayoipata hapa hamuwezi kuipata tena na wala haiwezi kujirudia mara mbili. Pia, kuweni watu wa nidhamu mahali popote mtakapo kwenda," aliasa.

Dumuni katika imani sahihi -Wito

Julius Njolle na Gerald Chami, Morogoro

WAAMINI wa Kanisa Katoliki wamehimizwa kudumu katika imani na kuyapuuza yote yenye muelekeo wa kuabudu miungu bandia.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padre Ricardo Maria, wakati akiongoza Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Mt. Patris, katika Jimbo Katoliki la Morogoro.

Padre Ricardo alisema kila Mkristo hususan Mkatoliki, ana wajibu kumpenda na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa roho na kweli huku akitumia uwezo na vipawa alivyojaliwa, kulitangaza Neno la Mungu.

Aliongeza kuwa, Wakristo wanapaswa kufahamu kuwa Mungu yupo na hivyo, hawana budi kumwabudu na kumtukuza daima.

Pia, amewahimiza Wakristo kuepuka kupenda na kuviabudu vito vya thamani huku wakimsahau Mungu.

Aliwataka kuachana mara moja na tabia hiyo na badala yake, watumie nguvu zao kumrudia Mungu kwa kushiriki matendo yaliyo ndani ya mapenzi yake.

Wakati huo huo: Naibu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Monsinyori Stanslaus Daki, ametoa wito kwa vijana kutumia elimu na nguvu zao kulinda maadili ya jamii.

Habari zilizopatikana mjini Morogoro hivi karibuni zimesema kuwa Monsinyori Daki alisema kuwa, wanaoendelea kutumia elimu na nguvu zao kuiga tamaduni za kigeni, wanapotosha maadili ya Kitanzania.

Amesema ni vema vijana Watanzania wakafuata mafundisho na maadili wanayopata toka kwa wazazi na walezi ili kutenda mambo yanayoliendeleza Kanisa, taifa na jamii kwa jumla.

Monsinyori Daki ameilaumu tabia ya baadhi ya wazazi kutotimiza wajibu wao katika familia hali inayochangia upotofu wa maadili kwa watoto.

Katika tukio jingine: Padre Joseph Msongore wa Kanisa la Mt. Maria, MODECO mjini Morogoro, amewataka Wakristo kuwa na umoja katika kufanya mambo yanayompendeza Mungu.

Alisema hayo wakati akihubiri kwenye Misa Takatifu ya kusherehekea Utatu Mtakatifu.

Padre Msongore alisema Wakristo ni mali ya Mungu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na hivyo, wanapaswa kuwa wamoja katika kufurahia mema ya duniani na pia, kukemea maovu yanayofanyika.

Alisema matatizo mengi yanayoikumba dunia, yanasababishwa na jamii kukiuka Amri za Mungu kwa makusudi.

Akaongeza kuwa jamii mbalimbali zimekuwa zikishindwa kuona mema hali ilowafanya kutokutenda yanayo mpendeza Mungu, bali yanayozifurahisha nyoyo zao.

Naye Jane Kibona, anaripoti kutoka Morogoro kuwa: Mchungaji Christopher Samuel wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Bungo, mkoani hapa, amewataka Wakristo kuepuka na Ubatizo batili na badala yake, watambue kuwa Ubatizo halisi ni ule wa maji na Utatu Mtakatifu.

Alisema hayo wakati akihubiri katika ibada ya hivi karibuni kanisani hapo juu ya Utatu Mtakatifu.

Katika Ibada hiyo, Mchungaji samuel aliwahimiza Wakristo kuachana na mawazo potofu ya kibinadamu na badala yake, wamtegemee Mungu katika nafsi zake Tatu yaani: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Kanisa lazidi kupoteza mapadre

l Yumo padre aliyewahi kupigwa risasi na majambazi,akalemaa

l Mwingine ni Naibu Askofu, RC amkumbuka

Pd Chrysantus Ndaga, Mahenge na Wandishi Wetu Mikoani

JIMBO Katoliki la Mahenge limempoteza mmoja wa mapadre, aliyekuwa Paroko wa Mtimbira, Padre Barnabas Mahunja na kumfanya kuwa padre wa pili kufariki jimboni humo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Alifariki ghafla parokiani kwake, Mei 31, mwaka huu. Padre mwingine ni Marehemu Jonas Mayombo, aliyefariki Februari 26.

Habari toka parokiani Mtimbara alikoishi Padre Mahunja, zinasema, alfajiri ya Mei 31, aliteremka toka ghorofani kilipo chumba chake na kumuamsha Frateri Oscar Kaziyareli aliyepo parokiani hapo katika Mwaka wa Kichungaji.

Zinasema marehemu alimuomba Frateri Oscar ampeleke katika kituo cha afya takribani mita 500 hivi toka parokiani kwa kuwa alijisikia vibaya.

Zinaongeza kuwa, alifariki mara tu baada ya kufika kituoni. Mwili wake ulisafirishwa hadi Ifakara kwa mazishi yaliyofanyika Juni 4, mwaka huu.

Akiongoza Misa ya Mazishi iliyohudhuriwa na mapadre zaidi ya 60, watawa na waamini toka ndani na nje ya jimbo, Naibu Askofu wa Jimbo la Mahenge, Monsinyori Mdai, aliwaomba waombolezaji kuupokea msiba huo kwa imani.

"Mungu ametupatia ujumbe kutokana na kifo cha Padre Mahunja kwamba, maisha yetu ni ya kupita tu, hapa duniani na daima tujiweke tayari. ...Mungu amependa kumuita kwake kwa maisha bora ya baadaye".

Alisema ingawa jimbo linajiuliza maswali mengi ikiwa ni pamoja na nani wa kuziba nafasi ilizoachwa na Marehemu, waamini wote hawana budi kumuombea kwa Mungu kutokana na namna alivyokuwa mkarimu katika kutumia vipawa vyake kwa ajili ya wengine. "... Mwenyezi Mungu naye amrudishie kwa ukarimu," alisema.

Akitoa rambi rambi kwa niaba ya Umoja wa Makanisa, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Ulanga Kilombelo, Abel Mwambungu, alisema waamini wanapaswa kupokea kifo kama njia pekee ya kumfikia Mungu.

Marehemu ni wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto kumi wa Thomas Mahunja (marehemu) na Mama Afra Shinyaka.

Alizaliwa Oktoba 7, 1954 huko Uponera, Mahenge ambako alipatia elimu ya msingi na kisha kujiunga na shule ya Kati ya Kwiro hadi Darasa la Nane.

Mwaka 1974, alijiunga na Seminari ya Kasita na kisha, akajiunga na Seminari za Kibosho na Kipalapala. Alipata Daraja Takatifu ya Ushemasi mwaka 1981 na Desemba 19, 1981, alipewa Daraja Takatifu ya Upadre huko Kwiro, Mahenge.

Alianzia kazi parokiani Ifakara akiwa Paroko Msaidizi kwa miaka minne. Kisha, alikwenda kufundisha katika Keminari Kuu ya Segerea mwaka 1986.

Mwaka 1987, alienda Roma kwa masomo zaidi ya Teolojia juu ya Mafumbo ya Imani ambako alifaulu na kutunukiwa Shahada ya Udaktari katika Kanisa.

Alirudi na kuendelea kufundisha katika Seminari Kuu ya Segerea tangu mwaka 1991 hadi 1999 aliporudi jimboni na kuwa Paroko wa Mtimbiraalipotumikia Kanisa hadi mauti yanamfika.

Hadi kifo chake, pia alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadre Wazalendo wa Jimbo la Mahenge (UMAWAMA), Mkuu wa Tarafa ya Itete na mmoja wa Wajumbe wa Halmshauri Kuu ya Jimbo na pia, alikuwa mmoja wa wakufunzi wa Teolojia kwa walei.

Padre Mwingine aliyeaga dunia, ni Francis Greef (81), Mmisionari wa Shirika la Mapadre wa Roho Mtakatifu, aliyefariki Mei 21, 2001. Aliwahi kufanya kazi katika Jimbo Katoliki la Moshi tangu mwaka 1948 hadi 1992.

Mhashamu Amedeus Msarikie wa jimbo hilo, ndiye aliyeongoza Misa ya Mazishi akishirikiana na Maaskofu Wastaafu, Mhashamu Denis V. Durniny (Arusha), na Mhashamu Bernad Ngawiliau (Zanzibar). Mapadre 57 wa majimbo ya Arusha na Moshi, watawa na waamini mbalimbali, walihudhuria mazishi hayo.

Wakati wa mahubiri, Mhashamu Msarikie alisema kuwa, Injili ya Mtakatifu Luka, 17:7-10, inaelezea kama utumishi wa Hayati Padre Greef, ulivyokuwa.

Alisema marehemu alifanya yaliyotakiwa kwa umakini na hata baada ya utumishi wake, hakusubiri kupongezwa wala shukurani kwani alijua dhahiri kuwa ni wajibu wake kama mtumishi wa Kristo.

Wakati wa uhai wake, Padre Greef aliwahudumia kwa upendo vijana wenye shida mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwalipia ada, baadhi yao na wengine kuwapa malezi bora ya Kikristo.

Marehemu alizaliwa huko Mount Carnel, Pennsylvania Marekani, Machi 14, 1920. Baada ya elimu yake ya msingi, alijiunga na seminari ndogo na kisha Seminari Kuu ya Shirika la Mapadre wa Roho Mtakatifu huko Marekani.

Aliweka Nadhari za Kwanza za Utawa, Agosti 15, 1942. Alipadrishwa Juni 1947. Baada ya Upadrisho, alitumwa Vikariati ya Kilimanjaro kama Mmisionari.

Mwaka 1948, aliwasili Moshi na kufundisha Seminari Ndogo ya St. James, Kilema-Chini hadi mwaka 1950.

Kati ya 1962 na 1996, alifanya kazi za uchungaji Parokiani Kishimundu, kisha Narumu na Mbosho. Mwaka 1967, aliteuliwa kuwa Paroko wa Mbosho hadi mwaka 1992.

Novemba 1991, alipigwa risasi na majambazi na baada ya miezi sita alipona lakini, akabakia mlemavu hadi kifo chake. Mwaka 1992, alihamia jimboni Arusha.

Naye James Marenga anaripoti kutoka Mwanza kuwa, Kanisa limempoteza Naibu Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Padre Hilary Mfungo, aliyefariki Mei 30, 2001 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Marehemu alizaliwa Januari 14, 1938 katika kijiji cha Bumere, Mwibara. Alibatizwa Januari 14, 1951, seminarini Nyegezi na kupewa Kipaimara parokiani Nyegezi mwaka 1952.

Alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Kasuguti na Kagunguli mwaka 1948 hadi mwaka 1950. Alijiunga na Seminari ya Nyegezi mwaka 1951 - 1962 alipohitimu Kidato cha Sita.

Aliendelea na masomo ya Falsafa, Teolojia na Malezi ya Upadre toka mwaka 1963 hadi 1968 katika seminari ya Mt. Paulo Kipalapala, Tabora.

Desemba 22, 1968 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre katika Parokia ya Kibara na Mhashamu Renatus Butibubage, aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Mwanza wakati ule.

Marehemu Padre Mfungo alifanyakazi katika parokia za Kome toka mwaka 1969 hadi 1971 na Parokia ya Nyalubele mwaka 197I hadi 1980.

Mwaka 1981 hadi 1985, alifanya kazi seminarini Nyegezi akiwa Mhasibu na kisha, akalitumikia Kanisa katika Parokia ya Itira toka mwaka 1985-1990.

Mwaka 1991 hadi 1992, alikuwa India kwa masomo ya Kiroho (spirituality)na kisha akarejea nyumbani na kufanya kazi katika Parokia ya Magu tangu mwaka 1992-1994.

Aliteuliwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC) mwaka 1994 hadi 1997. Baadaye, alirejea jimboni na kuwa Paroko wa Nyambiti tangu mwaka 1997 hadi mwisho wa uhai wake.

Akiwa parokiani Nyambiti, aliteuliwa kuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Julai 1, 1999.

Ibada ya Misa kumuombea marehemu, ilifanyika katika Kanisa Kuu la Epiphania Bugando na kuongozwa na Askofu Mkuu Anthony Mayala akiwa na wahashamu Justine Samba wa Jimbo Katoliki la Musoma na Askofu Aloisius Balina wa Jimbo la Shinyanga.

Wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Askofu Mstaafu, Fortunatus Lukanima wa Arusha pamoja na mapadre kutoka katika majimbo ya Mwanza, Shinyanga, Musoma, Bukoba, Rulenge na Geita.

Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Steven Mashishanga ambaye katika salamu zake, alisema marehemu atakumbukwa kama kiongozi aliyekuwa kiunganishi baina ya Serikali mkoani hapo, na Kanisa.

Alisema sifa za marehemu kiutendaji, alizipata muda mfupi tu baada ya kuwa Mkuu wa Mkoa huo. Alitoa shilingi 50,000 kama rambirambi kutoka katika ofisi yake.

Naye Mhashamu Mayalla alisema kuwepo kwa mapadre, maaskofu na hata mkuu wa mkoa pamoja na umati wa waamini, ni ishara wazi ya utumishi bora wa Padre Mfungo.

Salamu za rambirambi kutoka TEC, ziliwasilishwa na Padre Nicolaus Segeja kwa niaba ya Katibu Mkuu.

Padre Segeja alisema kuwa, TEC watamkumbuka Padre Mfungo kwa kazi yake nzuri aliyoifanya alipokuwa TEC.

Baada ya Misa hiyo ilifuatia ibada ya mazishi iliyofanyika katika Seminari Ndogo ya Maria Mtakatifu Nyegezi, Mwanza na kuongozwa na Askofu Samba. Alizikwa katika makaburi ya mapadre yaliyopo seminarini hapo.

Kanisa pia limempoteza Padre Gerald Taylor, M.AFR.

Alizaliwa Sunderland Uingereza, Octoba 13, 1919, Alipata Daraja ya Upadre Juni 6, 1949. T

Tangu 1960 - 1996 alikuwa Mhadhiri wa Sheria za Kanisa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala na Peramiho.

Idadi kubwa ya Maaskofu na Mapadre nchini Tanzania, walikuwa wanafunzi wake.

Akiwa Kipalapala alifanya kazi ya Uchungaji kwa iliyokuwa Kambi ya Wakimbizi Pangale, Jimboni Tabora. Alishughulikia pia mashauri mbalimbali ya ndoa na kuyafanyia utatuzi. Aliandika vitabu na makala mbalimbali hasa kuhusu Sakramenti ya Ndoa katika Sheria za Kanisa.

Padre Taylor alikuwa pia Mshauri wa Kiroho kwa Masista wa mabinti wa Maria,Masista wa Mama Theresa, Mtakatifu Anna Tabora, pia kwa Nyumba ya Masista CDNK Kipalapala Seminari.

Padre Gerald (Gerry) Taylor alifariki Juni 2, 2001 na kuzikwa huko Nairobi Juni 6, 2001 ambako alipelekwa kwa matibabu. Padre Taylor amekuwa mkazi wa Kipalapala kwa miaka 40.

WAPUMZIKE KWA AMANI

AMINA