Mauaji Tanzania ni kutokujua demokrasia - Kanisa Katoliki

l‘Busara zitumike kuliko jazba, vyombo vya dola vifunzwe kuzingatia utu’

lLasisitiza kuwa, kuhitilafiana kisiasa si uasi wala uadui

Na Mwandishi Wetu

KANISA Katoliki nchini Tanzania, limelaani mauaji yaliyotokea hivi karibuni kufuatia maandamano ya chama cha CUF, yaliyozuiliwa na Serikali na kusema kuwa, hayo ni matokeo ya kutokujua vema demokrasia ya vyama vingi.

Katika taarifa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),iliyosainiwa na Rais wake, Askofu Severine NiweMugizi juu ya hali ya sasa nchini, maaskofu Wakatoliki nchini wamesema baada ya mkutano wao uliomalizika jana(Ijumaa) kuwa, mauaji hayo yametokana na sababu mbalimbali zikiwamo hisia mbaya za kihistoria, kutoaminiana na kutokujua mambo yanavyokwenda.

Viongozi hao wa kiroho wamesema hali ya kutokujua mwenendo halisi wa demokrasia ya vyama vingi, imesababisha jamii kudhani kimakosa kuwa, kuhitilafiana katika jambo la kisiasa, ni uasi au uadui.

Katika tamko la mkutano wao wa kawaida wa Kamati Tendaji ya TEC, uliofanyika Februari 21 hadi 23,mwaka huu, wamesisitiza wahusika wa pande zote katika migogoro ya kisiasa nchini, kuzingatia rai ya viongozi wa dini kwa serikali na vyama vya upinzani kufanya mazungumzo ya pamoja ili kujadili namna ya kurejesha maelewano na kuondoa tafauti zilizopo.

" Katika kutafuta maelewano, makundi mbalimbali yahusishwe kwani yana haki na wajibu huo katika jamii. Swala la kujenga nchi yetu ya Tanzania kwa utulivu na amani linawahusu wananchi wote," inasema sehemu ya tamko hilo na kuongeza

"...watu wasiongozwe kwa jazba bali busara itumike kwa wakati wote wanaposhughulikia masuala amabayo ni ya kisiasa na yale yanayoweza kuhatarisha amani...vyombo vya dola vielimishwe vizuri na kufundishwa mbinu za kisasa za kushughulikia ghasia na machafuko wakizingatia utu na ungwana wa raia."

Januari 26 na 27, mwaka huu, takribani watu 23 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika ghasia zilizoibuka baada ya wafuasi wa Chama cha Wananchi(CUF), kufanya maandamano yaliyozuiliwa na serikali.

Kwa ufafanuzi zaidi , soma tamko rasmi kama lilivyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ambalo tumelichapa kama lilivyo Uk. 10

Abiria wenye Suti, 'moka' wagomea stendi ya Tarime

lWasafirishaji waitupia lawama Halmashauri

lVibanda vya soko navyo vyawa choo

Josephs Sabinus Na Christopher Gamaina, Tarime

ABIRIA wanaovalia "viwalo" zikiwamo gauni, viatu na suti za gharama, kwa muda mrefu wamekuwa wakigomea kutumia kituo kikuu cha mabasi cha mjini Tarime kutokana na matope yanayojaa kituoni hata baada ya mvua ya dakika chache kunyesha.

Hali hiyo imewafanya wafanyabiashara na wasafirishaji mjini hapa kuvunja taratibu kwa kuwatafuta abiria mitaani kabla hawajafika kituoni.

Wananchi kadha wakiwamo baadhi ya wasafirishaji na wafanyabiashara waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti mjini hapa hivi karibuni, wameitupia lawama Halmashuri ya Wilaya ya Tarime kwa kutofanyia matengenezo kituo hicho kikuu.

Walisema licha ya kukusanya ushuru kwa magari yanayotumia kituo hicho na wafanyabiashara nyingine wa kati ya shilingi 500 na 2000/=, halmashauri hiyo imekuwa haizingatii uboreshaji wa huduma katika wilaya hiyo.

Walisema hali hiyo imewalazimisha kutoroka stendi na kufukazana mitaani ili kupakia abiria waliogoma kuingia stendi kwa kukwepa matope.

Walibainisha kuwa kimsingi hawaifurahii hali hiyo kwa kuwa ni kero kwa abiria na hatari kwa watumiaji wengine wa barabara lakini inabidi wafanye hivyo kwa kuwa biashara yao sio y a kupamba stendi kwa magari yasiyopata abiria.

"Halmashauri wanajali mno kukusanya mapato kuliko kuboresha huduma. Unadhani nani atakubali kuingiza moka au suti yake kwenye tope namna hiyo?" alisema Nyamseti Mantago, dereva wa "kipanya" kimoja kinachofanya safari zake kati ya Musoma na Tarime.

Dereva mmoja wa "Peugeot" inayofanya safari kati ya Tarime Mjini na Sirari, ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema, "Hii stendi yetu inatisha mno. Tatizo ni kwamba, wao(halmashauri) wanajali kujineemesha maofisini kwa kununulia magari ya kifahari lakini huduma kwa watu wao, hawakumbuki."

Naye Mfanyabiashara mwingine maarufu mjini hapa, John Rutente, alisema kuwa, ingawa halmashauri inayo magari, mitaro na maeneo mbalimbali ni machafu kutokana na magari hayo kutofanya kazi hizo, badala yake, yanafanya kazi za kibinafsi.

Kanisa kufungua Bima ya Wajawazito kwa wananchi

Na Peter Dominic

BODI ya Afya Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, ipo mbioni kuanzisha BIMA ya Afya kwa akina mama wajawazito ambapo watatakiwa kujiunga na bima hiyo toka hatua ya mwanzo ya ujauzito.

Akifungua semina ya siku moja ya kujadili mpango huo, Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Mhashamu Method Kilaini, aliwataka akinamama kuunga mpango huo kwa kulipia taratibu bima zao kama njia ya kujiandaa kujifungua katika mazingira na hali bora.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Afya Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Dk. Brigid Corrigan, lengo la semina hiyo iliyowahusisha wafanyakazi wa zahanati 13 zilizo chini ya bodi hiyo, ni kujadili Bima ya afya kwa akinamama ili waelewe mabadiliko yaliyopo katika sekta ya afya na kuwa na mahusiano mazuri na serikali.

Semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), hivi karibuni, pia ililenga kutathmini takwimu za zahanati tangu mwaka jana ili kujua mahitaji ya baadaye.

Askofu Kilaini alisema kuwa, huduma hiyo licha ya kusaidia kuimarisha vituo hivyo vya afya jimboni ikishirikiana na serikali, pia itawezesha akinamama kuwa na uhakika wa kujifungua katika mazingira mazuri ya kiuchumi na hivyo, kupata huduma bora anazostahili mzazi.

"Inasikitisha kuona bado kuna akinamama wanaozalia nje ya hospitali kwa kukosa shilingi 5000. Uzazi bora ni muhimu na tunatakiwa kufanya kazi na ili kusaidia kuzuia mtu asiugue, akinamama wewe tayari kulipia bima taratibu kabla ya kujifungua." Alisema.

Aliwataka wafanyakazi wa vituo hivyo kutumia lugha nzuri kuwabembeleza wagonjwa wanaowapowapokea na kuwatibu.

Alisema hali hiyo ni muhimu kwa kuwa asilimia 50 ya matibabu ya mgonjwa, huchangiwa pia na lugha nzuri na upendo apatavyo toka kwa waangalizi wake.

"Asiye na huruma kwa mgonjwa hafai hata kama ana taaluma. Hyuyo anaharibu sifa ya kituo. Lazima wote tujitahidi kutoa huduma bora kwa kutumia ulimi wetu," alisema.

Kamishna wa Jiji la Dar-Es-Salaam, aliyekuwa Mwakilishi wa Serikali katika semina hiyo, Dk. Mtasiwa, aliupongeza utaratibu huo wa kulipa BIMA ya Afya kwa vile umelenga kuwasaidia watu wasio na uwezo.

"Watu hawana uwezo wa kulipa pesa kwa mpigo; na haya ni maamuzi mazuri. Serikali itajitahidi kuufuatilia mpango hu na hatimaye, kuutumia," alisema.

Aidha, alizisifu huduma zinazotolewa na Kanisa na akasema kuwa, Serikali inaridhika nazo na kuzipongeza.

"Asilimia kubwa ya malalamiko, yapo upande wa Serikali siyo Kanisa," alisisitiza na kuongeza Serikali ipo tayari kusaidia juhudi za Kanisa zinapokwama.

Akitoa mada katika Semina hiyo, mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo ya Afya,Padre Vic Missiaen alisema, malengo ya awali ya miaka mitano yaliyoandaliwa na Bodi, yameonesha kuwa upo uwezekano wa kuanzisha bima ya afya ambayo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, itaanzia kwa akinamama wajawazito.

"Tumepata uzoefu wa kutosha. Hata serikali imeanza kutoa huduma kwa wafanyakazi wake. Sisi kama Kanisa, tuna uwezo wa kutoa Bima kwa wananchi ingawa kwa upande wa Dar. tutaanza na Bima ya akina mama," alisema

Mpango huo wa Bima upo kwenye mpango wa uzazi salama toka Baraza la Maskofu wa Italia na unadhaminiwa na Shirika la Madaktari wa Italia(CUAMM) na hapa nchini, mpango huo wa Bima na uzazi salama, unaratibiwa na Dk. Guido.

MIGAWANYIKO YA KIDINI NDANI YA VYAMA VYA SIASA...

Pengo atoboa Siri

lAsema vyama vyote, viongozi wa dini wamo

lAtahadharisha kuwa mkorogano unazua ‘vibwetere’

Na Mwandishi Wetu

MWADHAMA Polycarp Kardinali Pengo, amesema si halali kukisakama na kukipakazia chama cha CUF pekee mintarafu minong’ono ya Watanzania wengi kuhusu udini katika siasa unaotishia kuvunja umoja wa Watanzania kwa kuwa vyama vyote vya siasa vinahusika na hata baadhi ya viongozi wa dini.

Katika Ibada ya Jumamosi iliyopita iliyoandaliwa na Wanawake Wakatoliki Tanzania, Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam,(WAWATA), Pengo ambaye ni Askofu Mkuu wa jimbo alisema kuwa ingawa minong’ono ya migawanyiko ya kidini imekuwa ikisakama CUF peke yake, ni dhahiri ipo katika vyama vyote vya kisiasa nchini.

Alisema, "Kuendesha mijadala ya kisiasa ndani ya misikiti kama vile hata makanisani, ni udini usiokubalika katika taifa la Tanzania."

Aliongeza, "Lakini vilevile viongozi wa dini kuruhusu watumike kwenye mihadhara ya kisiasa kama vile kwenye majukwaa ya kampeni za uchaguzi ni udini wenye madhara yaleyale ya kuchanganya dini na siasa."

Kardinali Pengo alibainisha kuwa moja ya madhara ya kuchanganya dini na siasa, ni hatari ya kufanya kufuru ya kuhalalisha maovu ya kibinadamu kwa kutumia mamlaka ya Mwenyezi Mungu.

Alisema mara nyingi matokeo ya kufuru ya namna hiyo yamedhihirika katika historia ya binadamu kwa watu kuuawa kwa jina la Mungu hali kinachotetewa ni maslahi binafsi ya wanadamu.

Aliwataka wanasiasa nchini kujiepusha na udini udini wa aina yoyote katika harakati zao za kisiasa.

Alisistiza kuwa homilia yake haikihusu chama cha CUF peke yake bali vyama vyote vya siasa nchini.

"Mara ngapi nimesikia minong’ono ya migawanyiko ya kidini hata ndani ya chama kimoja cha siasa hata ndani ya chama kimoja cha siasa kama vile CCM?.

Minong’ono siyo tu ya mgawanyiko kati ya Waislamu na Wakristo, lakini pia, kati ya Wakatoliki, Walutheri, Waanglikana n.k. Migawanyo ya aina hiyo, haiashirii amani," alisema.

Kwa ufafanuzi zaidi na mengine, soma homilia kamili kama ilivyotolewa na Kardinali Pengo ambayo tumeichapa kama ilivyo Uk.7

DC, Mchungaji wataka mahakimu wasiwe 'Pilato'

lWataka pia mahakama zisilaumiwe ovyo

Na Mwandishi Wetu, Tarime

MCHUNGAJI Chris Kateti wa Kanisa la Menonite la mjini Tarime, ameungana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Paschal Mabiti kutumia Biblia kuwaasa wanasheria wakiwamo mahakimu na majaji kutokuwa "Pilato" kwa kutowatia hatiani watuhumiwa wasio na makosa kutokana na shinikizo la rushwa.

Walikuwa wakizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Duniani yaliyofanyika kiwilaya katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime. Mada kuu ilikuwa WAJIBU WA MAHAKAMA KWA UMMA.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi wa dini mbalimbali, mahakimu wa mahakama za mwanzo , makarani na mahakimu wote wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Mkuu wa Wilaya, Bw. Mabiti, alivihimiza vikundi vya dini kutumia imani zao za kiroho kutatua matatizo yao badala ya kuyapeleka katika vyombo vya sheria.

"Unajua si vema masuala ya dini yaingiliwe na dola. Hivi kwanini waamini mkasuluhishwe na watu wa mataifa?" alihoji.

Alivitaka vyombo vya sheria kusimama kidete katika misingi ya haki bila upendeleo wala uoga.

Wakifafanua kwa nyakati tofauti, viongozi hao walisema, vyombo vya sheria havipaswi kuwa kama Pilato kwa kuwa licha ya kumuona Yesu hana kosa, alikubali kumtia hatiani kutokana na shinikizo alilolipata toka kwa watu aliowaita, wapambe.

Walisema katika ulimwerngu wa sasa, wapambe ni watoa rushwa wakiwamo matajiri wanaojaribu kununua haki za watu hata kwa magunia ya sukari, ndugu au ukoo wa wanasheria wanaotaka kutumia nafasi za ndugu zao kupora haki za wengine.

"Mahakimu wasiyumbishwe na wapambe hao. Wafanye kazi bila kuangalia sura, vyeo wala utajiri wa mtu kwa kuwa kazi hiyo, wanaifanya kumwakilisha Mungu," alisema Mchungaji Kateti na kuongeza kuwa, kwa kuwa haki ya mtu hutoka kwa Mungu, basi ni kinyume cha maadili ya Kimungu kwa mwandamu yeyote kuipokonya.

Alisema vyombo vya sheria havina budi kusimama kidete kuona kwamba kila mtu anapata haki yake.

Kiongozi huyo wa kiroho alisema bila sheria, haitawezekana kwa wanadamu kutambua kosa au jema wanalolifanya .

Mchungaji Kateti aliilaumu tabia ya baadhi ya watu kutumia dini zao kuapa mahakamani lakini akasema, "Cha kushangaza, wanapofika mahakamani, huanza kuporomosha uongo kama kinanda," alisema na kuongeza, "hao wanastahili adhabu kwa sababu hata Biblia inasema Mungu hadhihakiwi."

Katika sherehe hizo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Nichodemus Kurwijila, alisema ili vyombo vya sheria vitoe haki, jamii haina budi kuvipa ushirikiano kwa kutoa malalamiko na ushahidi wa kweli.

Alisema malalamiko mengi yanayoelekezwa kwa vyombo vya sheria, kwa sehemu kubwa yamekuwa yakichangiwa na jamii yenyewe kutotoa ushirikiano.

"Kama umma utaleta yasiyo ya haki; ukatoa malalamiko na ushahidi usio wa kweli, malalamiko kuwa vyombo vya sheria havitoi haki hayataisha," alitahadharisha.

Mashirika yatakiwa kuwahusisha wakazi katika miradi yao

Na Getrude Madembwe

MASHIRIKA na vikundi mbalimbali vya ndani na nje ya nchi vinavyotaka kuanzisha miradi, wameshauriwa kuwahusisha watu na maeneo husika kabla na wakati wa kuendeleza miradi hiyo ili isife.

Hoja hiyo ni moja ya masuala muhimu yaliyozungumziwa katika warsha iliyoandaliwa na taasisi ya Human Resources Management and Personnel Cooperation.

Warsha hiyo ya siku tatu iliyofanyika na kumalizika hivi karibuni jijini Nairobi, Kenya, ililihusisha shirika la moja wa maendeleo la nchini Ujerumani (AGEH), pamoja na wajumbe wa Mabaraza ya Maaskofu ya Afrika Mashariki na Kati (AMECEA).

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kurejea nchini toka katika warsha hiyo nchini Kenya, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Pius Rutechura, alisema sababu ya kuwahusisha wakazi wa maeneo husika ni kufanikisha na kushirikiana vizuri na watendaji wa shirika hilo la AGEH pindi wanapokuja kufanya kazi zozote au kuanzisha miradi.

Alisema wahusika wanaotaka kufanya jambo lolote ni bora wawashirikishe watu wa maeneo hayo ili watu watambue kuwa miradi inayoanzishwa, inaanzishwa kwa ajili yao.

Akitoa mfano wa kauli hiyo, Padre Rutechura alisema, "Kama Caritas wanataka kuchimba kisima mahali fulani kwa ajili ya maji, hawana budi kuwafahamisha watu walioko maeneo hayo ili wakitunze kisima hicho kwani wao ndio wanaokitumia".

Aidha, alisema kuwa kabla ya wahusika hao hawajaanzisha mradi wowote, ni vizuri wakapata maoni kutoka kwa watu wanaoenda kuwafanyia jambo hilo ili kuepuka kuanzisha mradi ambao hauna manufaa kwa watu husika.

Pia, alisema wanaofanyiwa miradi hiyo, hawana budi kuwa na ushirikiano mzuri na watendaji hao ili kufanikisha zoezi hilo.

AGEH ni shirika lililoundwa mwaka 1959 nchini Ujerumani na linaendeshwa kote ulimwenguni. Shirika hilo hupeleka watendaji wake sehemu mbalimbali za ulimwengu ikiwemo Tanzania.

SHDEPHA+ Wataka UKIMWI usiwe ulaji

Na Dalphina Rubyema

IMEELEZWA kuwa suala la kutokomezwa kwa ugonjwa wa UKIMWI hapa duniani bado ni kitendawili kwani baadhi ya watu na mashirika wanachukulia kama sehemu ya kujipatia ulaji na ajira.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Afya ya Maendeleo kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (SHDEPHA+)kitaifa, Bw. Joseph Katto wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake hivi karibuni.

Alisema watu wanaofanya kazi katika mashirika na miradi ya kupambana na UKIMWI wanaomba kila kukicha dawa ya ugonjwa huu isipatikane na wengine kutoa takwimu zisizo sahihi kwa mataifa mbalimbali kwa nia ya kuendeleza miradi hii lengo likiwa ni kutaka kuendelea kujineemesha.

"Ehe! Hawa watu wanaona dawa ya UKIMWI ikipatikana kitumbua chao wanaona kitakuwa kimemwagikiwa mchanga, kazi yao ni kuwatumia waathirika kujinufaisha wenyewe bila kuwasaidia kwenye masuala ya (care and treatment)’ matunzo na matibabu, alisema bwana Katto.

Vile vile mwenyekiti huyo ameitaka Serikali na jamii kwa ujumla kutambua kuwa kuendelea kuwashauri watu wenye Virus vya UKIMWI kuishi kwa matumaini bila kuwapatia matunzo na matibabu (Care & Treatment) hakutasaidia kupunguza kasi ya uognjwa huo.

‘Unatuambia wenye Virus vya UKIMWI tuishi kwa matumaini bila kutupa Care and Treatment kuishi kwa matumaini ni pamoja na kutupatia care and treatment bwana siyo blaa blaa’ alisema Bwana Katto.

Alisema kuwashauri watu wapime damu na wakishabainika kuwa na Virus vya UKIMWI uwashauri kuwa waishi kwa matumaini bila msaada mwingine ni sawa na kuwakatisha tamaa ya maisha.

‘Hivi lengo la kupima ni kutaka kupata idadi ya waathirika kama ni hivyo kuna haja gani ya mtu kujitolea hadharani na kujitangaza kuwa na virusi, bila faida yoyote kwanini asikae kimya bila kujiweka wazi, inakatisha tamaa!’ alisema.

Aliongeza ‘Waathirika lazima watiwe moyo kwa kuwapatia dawa za kuwaongezea muda siyo kuwachukulia kama watu wa kufa kesho’ alisema.

Mchungaji wa KKKT ahimiza upendo baina ya makanisa

Na Elizabeth Steven

MCHUNGAJI mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), amewataka waamini wa kanisa lake, kuimarisha upendo baina yao na Wakristo na waamini wengine ili kuimarisha amani.

Mchungaji huyo Kheri Mwakabonga wa KKKT usharika wa Tabata katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, alitoa wito huo Jumapili iliyopita wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika usharikani hapo.

Alisema kuwa, kwa kuwa Mungu anayeaminiwa ni mmoja ambaye ni Yesu Kristo Masihi, jamii haina budi kuondoa tofauti zote za kimadhehebu ili kufikia mapatano zaidi kama yaliyojitokeza na kuimarisha urafiki na uhusiano baina ya Walutheri na Wamoraviani.

"Walutheri zamani tulikuwa hatupatani na wenzetu Wamoraviani. Alipo Mmoraviani, Mlutheri huwezi kumpata; hayupo kabisa na alipo Mlutheri, Mmoraviani hawezi kufika. Siku hizi mambo ni mazuri kabisa. Tofauti zetu zote tumeziweka kando na sasa tunashirikiana vizuri kwa sababu tunayemuamini ni Mungu mmoja," alisema.

Alisema sasa ni wakati muafaka kila mmoja kuwa na upendo wa dhati kwa mwenzie na kuupiga vita upendo wa kinafiki.

Alisema endapo kila mmoja atatumia juhudi zake zote katika kumpenda jirani yake kwa dhati, ni dhahiri upendo wake atakuwa ameutoa hata kwa Mungu.

Aidha, alishauri jamii ya walutheri kuepuka tabia ya kwenda kanisani kwa siku za matatizo pekee na zile za kupokea Chakula cha Bwana, kwa kuwa jambo hilo si utaratibu wa kanisa.

Alisema haimpendezi Mungu , kumkumbuka siku pekee unazopata matatizo na kumsahau ukimtupa kando shida zako zinapoisha.

Mchungaji Mwakabonga amewahimiza waamini kupokea chakula cha Bwana wakiwa katika hali ya usafi wa kiroho badala ya kugeuza kama mkumbo au mtindo.

UNICEF kuchunguza zaidi matatizo ya watoto, vijana

Na Leocardia Moswery

SHIRIKA la kimataifa la kuhudumia akinamama na watoto(UNICEF), kupitia kitengo chake cha UKIMWI na Stadi za Maisha nchini, limesema kwa kushirikiana na Serikali, limeandaa mpango madhubuti wa kuwasaidia watoto na vijana kwa kuchunguza na kujua zaidi matatizo yao.

Mkurugenzi wa kitengo hicho, nchini Tanzania, Bw. Richard Maballa, ameliambia gazeti hili katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake katikati ya juma kuwa, kitengo chake kimeandaa mpango huo wa miaka mitano kwa lengo la kuwasaidia na kuwaendeleza watoto.

Alisema wanatarajia kutembelea wilaya nane zikiwamo zinazoathirika na wakimbizi na kuzingatia watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwaendeleza.

Alizitaja wilaya hizo kuwa ni Ngara, Iringa Mijini, Mafia na Kisarawe.

Nyingine ni Magu, Musoma Vijijini, Temeke na Masasi.

"Tunataka waeleze wanataka UNICEF iwasaidie kwa kuwafanyia nini," alisema.

Maballa alisema baada ya ziara ya kutembelea wilaya hizo na kupata maoni na hisia hzo, mpango huo utaanza mara moja.

Mkurugenzi huyo amedokeza kuwa kitengo chake kinaandaa semina ya stadi za maisha jijini Dar-Es-Salaam, hususan katika wilaya ya Temeke yenye vijana wengi.

Jumamosi hii Bw. Maballa anakutana na vijana wa AMREF ili kujadili namna na sababu za kuenea kwa kasi ya UKIMWI na baadaye, atakutana na vikundi vya UVIKIUTA na kile cha akinamama cha KIYODESU, vyote vya Mbagala jijini dar-Es-Salaam.

Mama alia kumsaka mwana pekee

Na Mwandishi Wetu, Tarime

MWANAMKE mmoja mjini hapa, Mreba Mtani maarufu kwa jina la Mama Riziki, amehaha akilia kumsaka mwanae wa pekee Riziki Mkisi(28)ambaye hadi sasa hajui alipo.

Mama huyu anayeishi mjini Tarime kwa kusomba maji katika hoteli kadha, amesema kutokana na ugumu wa maisha, anaomba popote alipo, mwanae huyo wa pekee ambaye ni mvulana, atumie njia yoyote wawasiliane na ikibidi arudi nyumbani tokea alipo sasa.

Amesema tangu baba mdogo wake, Isack Muhoni, alipomchukua nyumbani Bunda kuja Tarime mwaka 1988, hawajawasiliana kwa njia yoyote na hajui kama yu hai hadi sasa na kwamba hajui yupo wapi.

Amesema anaishi katika Mtaa wa Starehe mjini hapa. Anuani yake ni, Mama Riziki, S.L.P 95. Tarime.

Simu namba 028-2690032.

Juhudi za kupata picha ya kijana huyo, hazikufanikiwa.

Waanglikana wawakumbusha matajiri jambo muhimu

Na Neema Dawson

KANISA la Anglikana, Dayosisi ya Dar-Es-Slaam, limewakumbusha matajirikutokuwa mithili ya mbegu za mpanzi zilizoanguka kwenye miamba na miiba, bali watumie mali zao kuendeleza utukufu wa Mungu.

Mchungaji wa kanisa hilo, Canon Eliya Mtokambali, alitoa ushauri huo mwishoni mwa juma wakati akihubiri katika kanisa la mtakatifu Nikolaus lililopo Ilala jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema jamii nzima wakiwamo matajiri, hawana budi kutamani kuwa mfano halisi wa mbegu za mpanzi zilizoanguka kwenye udongo mzuri ulorutubishwa; zilizomea vizuri na kutoa matunda bora.

Alisema matajiri hawapaswi kutumia mali walizo nazo kama kigezo cha kumuweka Mungu kando na badala yake, wazitumie kama kichocheo cha kuboresha mahusiano yao.

Akiwafananisha matajiri wanaomuweka Mungu kando na mbegu zilizoanguka kwenye miiba, alisema watu hao wameng’ang’ania mno mali na kwamba inashangaza kuona wanashindwa kutumia walau muda kidogo kumshukuru Mungu.

Vifo vya ajali vyawa tishio Mara

Na Samson Chacha, Tarime

WATU sita wamefariki wilayani Tarime katika mkoa wa Mara katika matukio matukio manne tofauti ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Katika moja ya ajali hizo ambazo si kawaida kutokea wilayani hapa kwa kipindi kifupi namna hiyo, Bhoke Matiko Weisiko(38), wa kijiji cha Sabasaba, Februari 5, mwaka huu aligongwa na gari dogo aina ya Toyota lenye namba za usajili TZD 9831 katika eneo la daraja la Msati na kufariki papo hapo. Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Bw. Chacha Mwita.

Februari 14, saa 12 jioni, Mkami Maranya Waiguti(32), Mwise Waisaki(22), aliyekuwa kondakta na dereva wa gari namba ARU 351, Bw. John Mtatiro(25)walifariki dunia baaada ya gari walilokuwa wakisafiria toka Musoma kwenda Sirari kupata ajali eneo la kasino kilomita 20 toka mjini hapa.

Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Mama Susy Peter Mganda na Mwita Marwa. Marehemu wote ni wakazi wa Sirari wilayani hapa.

Katika tukio la Februari 15, mwanafunzi wa wa darasa la pili katika shule ya msingi Rebu, Winnie Mwita Sasita, alifariki baada ya kugongwa na gari la abiria namba TZN 486, iliyokuwa ikiendeshwa na John Maiko.

Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema mwanafunzi huyo msichana alikuwa na unga alipojaribu kuvuka barabara.

Mwanafunzi wa shule ya Msingi Kemakorere, Mwita Mohere(10), alifariki baada ya kujaribu kuruka toka katika gari TZ 41307 lililokuwa ikiendeshwa na Mwita Kisiri wa Mugumu, huku likiwa katika mwendo. Baada ya tukio gari hilo halikusimama.

Wakati huo huo: Matinde Ryoba Nyahiri(28), wa kijiji cha Nkende wilayani hapa, aliyekuwa akiishi katika jengo moja maarufu mjini hapa kwa jina la Kiseru C, Februari 17, mwaka huu alifariki wakati amelela na mpenzi wake aliyejulikana kwa jina la David Nyanyusa.

Hadi sasa sababu za kifo chake hazijajulikana na polisi wilayani hapa bado wanaendelea na uchunguzi.

Uhaba wa magari na uchache wa askari polisi wa Kikosi cha Usalama barabarani wilayani hapa, vimechangi kuzuka kwa ajali kwa kuwa waliopo hawawezi kumudu kufuatilia magari na watumiaji wengine wa barabarani wanaokiuka taratibu.