Wanaotumia dini kujinufaisha chanzo cha migogoro- Pengo

Na Eric Samba

WATU wanaofanya mambo kwa jina la Ukristo au Uislamu kwa malengo ya kibinafsi, ndio chimbuko la migogoro na mapigano ya kidini, amesema Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Aliyasema hayo Ijumaa iliyopita wakati akihubiri katika Misa ya Kufunga Mwaka kwa Wafanyakazi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), iliyofanyika katika Kanisa la Baraza hilo Kurasini, Dar es Salaam.

Kardinali Pengo ambaye pia ni Makamu Rais wa TEC na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, alionya kuwa, endapo waamini wa dini na mdhehebu mbalimbali wakiwamo Wakristo watatumia dini kwa malengo ya kibinafsi, ipo hatari ya kuibuka machafuko na mapigano ya kidini katika jamii.

Alisema mapigano mengi yanayoendelea duniani kwa sasa ni matokeo ya watu kutumia dini kwa malengo binafsi na yasiyomshirikisha Mungu.

"Kuna watu wanaoweza kufanya mambo mbali mbali kwa jina la Ukristo au Uislamu kwa lengo la kujinufaisha, hii yaweza kuwa chimbuko la mapigano ya kidini. Mkitumia dini kwa malengo ya ubinafsi hiyo itasababisha mapigano na machafuko ya kidini hata kama sio leo basi au kesho, basi siku moja yatatokea," alionya.

Aliongeza, "Ukichunguza vita inayoendelea leo ulimwenguni utagundua kuwa ama ni vita ya kidini kweli au inahusiana na dini kwa namna moja ama nyingine. Kwa hiyo, dini badala ya kuwa chanzo cha amani na utulivu imegeuzwa na sasa imekuwa inayosababisha mapigano na vurugu."

Aliwataka wakristo kuendelea kuitika wito wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kutaka wafunge na kuombea amani, ili amani iweze kutawala duniani kote.

Aliwaonya wasifanye kitu chochote wakitumia dini kwa lengo la ubinafsi kwa kuwa hatua hiyo itapanda mbegu za machafuko nchini kwa siku zijazo.

Alisema vurugu zinayoendelea huko India baina ya Wakristo na Wahindu kwa kuwatumia Waislamu kuua Wakristo, mivutano baina ya Waislamu na Wakristo huko Indonesia na vurugu zinazoendelea huko Nchi Takatifu kuwa zote zinachochewa na imani za dini.

Alisema, kwa kudhania kuwa mapigano baina ya Waislamu na Wakristo yataipa nafasi ya kupumzika, Israel inalekea kutoa kibali kwa Waislamu wenye itikadi kali ili wajenge msikiti karibu na Kanisa Kuu la Habari Njema huko Nazareti ingawa hatua hiyo inapingwa hata na Waislamu wenye msimamo wa wastani.

Alisema endapo msikiti huo utajengwa, huenda hatua hiyo ikasababisha msuguano mkubwa kwani eneo hilo liliachwa kwa ajili ya mahujaji wa Kikristo.

Alitoa mfano kuwa, ingawa vita inayoendelea huko Afghanistan ni dhidi ya ugaidi, gaidi wa kimataifa Osama bin Laden na wafuasi wake, wamefanikiwa kutumia dini kuwadanganya na kuwaaminisha baadhi ya Waislamu nchini na sehemu nyingine duniani kuamini kuwa hiyo ni vita dhidi ya Uislamu kitu ambacho si kweli.

Kardinali Pengo alisema kufuatia hila hizo, Osama na wafuasi wake wamepata wafuasi wengi wasiojua ukweli wakiwamo vijana wa nchi mbalimbali ikiwamo Indonesia, ambao wanawaunga mkono.

Chondechonde! Madereva kipindi hiki kibaya -Mwinjilisti KKKT

Na Maryam Salumu

MWINJILISTI mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amewalilia chondechonde madereva ili wazingatie kanuni za usalama barabarani na kuepusha ajali hasa wakati huu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya na pia, akawataka wanajamii kuepuka vitendo viovu.

Mwinjilisti huyo Dickson Mwimbe wa Usharika wa Buguruni katika Jimbo la Ilala, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema watu wengi wakiwamo madereva, mara nyingi wamekuwa wakiitumia vibaya Sikukuu ya Krismasi kwa kulewa na kufanya vitendo mbalimbali vinavyosababisha vifo na maafa mengine katika jamii.

Alisema ingawa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani wanasisitiza madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia kanuni za usalama barabarani, ni wajibu wa madereva hao kuwa makini zaidi na kuchukua hatua za tahadhari wanapoendesha magari yao.

Alisema uzembe wowote unaosababisha ajali na hasara ya mali na roho za watu, ni kosa ambalo halina budi kuepukwa na kila mmoja wa watumiaji wa barabara..

Alisema wazazi wawe makini kwa watoto wao wanapokuwa matembezini wakati wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ili kuepuka ajali.

Aliilaumu tabia ya baadhi ya watu kuitumia siku hiyo kwa ulevi wa kupindukia pamoja na kushiriki vitendo viovu ikiwa ni pamoja na unyang’anyi, wizi, uzinzi na uasherati.

Alisema hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa maafa katika jamii ikiwa ni pamoja na ajali mbalimbali zikiwamo za barabarani ambazo huangamiza roho za watu, kusababisha majeraha na kuharibu mali.

Desemba 25, wakristo nchini wataungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Yesu Kristo (Krismasi).

Tumieni Krismas kuitangaza imani- Rai

Na Dalphina Rubyema

WAAMINI wa Madhehebu mbalimbali ya kidini nchini hususan Wakristo wametakiwa kuipokea na kuitangaza amani iliyoletwa na Yesu Kristo, katika kipindi kizima cha Krismasi.

Hayo yalisema na Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Adam Kombo wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa juma.

Mchungaji Kombo alisema kuwa makanisa mbalimbali likiwemo KKKT yenyewe, ni lazima yapokee amani ya Yesu na kisha kuidumisha miongoni mwa jamii nzima ya Watanzania.

"Yesu alileta amani duniani, Kanisa liipokee amani yake na kuidumisha miongoni mwa jamii nzima ya Watanzania," alisema.

Alisema katika kuadhimisha Siku Kuu ya Krisimasi, sharika zote katika Daiyosisi yake zitakuwa na Ibada Kuu za maadhimisho hayo ambazo zitaanza Desemba 24 usiku hadi Desemba 26 mwaka huu.

Aliongeza kuwa, ibada zote zitakuwa na mahubiri, sala, kuombea amani, huduma za Sakramenti na mambo mengine ya kiroho.

Alisema ibada hizo, pia zitafanyika sambamba na Ubatizo wa watoto wadogo.

"Ibada za Krismasi yenyewe na Krismasi ya Pili zitaambatana na Ubatizo wa watoto wadogo ambapo baadhi ya shirika katika mkesha wa Krisimasi zitakuwa maigizo ya kuzaliwa kwa Yesu, ingawa huwa wanarudi nyuma kuangalia historia ya Biblia kuhusu mpango wa Mungu na wokonu," alisema Mchungaji Kombo.

Aliongeza, "Katika suala hilo la mpango wa Mungu na wokovu, vile vile litakuwemo suala la utabiri wa manabii wa kale kuhusu kuja kwa Masiha".

Alisema katika kukamilisha ratiba ya maadhimishao ya Krismasi, Kanisa lake litaungana na Wakristo wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo katika ibada ya pamoja itakayofanyika Desemba 26 mwaka huu katika Kanisa Katoliki la Mwenge.

Msitafute dini kufuata sherehe - Mhubiri

 

Na Mwandishi Wetu

LICHA ya kuitaka jamii kuepuka kutumia dini kama mitindo hasa wakati wa kuelekea sikukuu za kidini, mhubiri mmoja wa Kanisa la Sabato amesema familia zenye watoto ndizo zinaongoza kwa kuwa mbali na Mungu.

Mwinjilisti huyo Ernest Mkama, aliyasema hayo wakati akihubiri katika Kanisa la Sabato la Kurasini katika Mtaa wa Temeke, jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita.

Alisema, anashangazwa na tabia ya watu kufuata dini kutokana na sikukuu za dini zilizo mbele yao na kwamba hao kimaneno wanavaa dini lakini kimatendo, ni waovu.

"Watu wengi sikukuu za dini zikikaribia wanavaa dini; na kujifanya waamini wa dini hizo; hao wamezifanya dini na wanazifuata kama mtindo. Wanajidai kutaua (kufunga), lakini hawatendi kama mafundisho ya dini yanavyotaka," alisema.

Katika mahubibiri yake, Mwinjilisti Mkama alisema, familia nyingi zenye watoto ndizo zinaongoza kwa kuwa nyuma katika kumtumikia Mungu kwa kuwa muda mwingi zinautumia kuhangaikia mahitaji ya watoto wao.

Gazeti hili lilipotaka kupata ufafanuzi wa kauli hiyo, Mhubiri huyo alisema, "Simaanishi kuwa tusiwajali watoto maana hata Maandiko yanasema: Amelaaniwa asiyewajali watoto lakini ninachosisitiza ni kwamba, wazazi wawe makini ili watoto wasiwatenganishe na Mungu. Mfano wa wazi ni kwamba wazazi wengi wanatumia gharama na muda mwingi kuwasomesha watoto wao lakini sio kufanya kazi ya Mungu."

Aliendelea, "Wengine hata mtoto akitaka kitu fulani kikubwa kwa ajili ya sherehe au sikukuu yoyote, atatumia kila njia kukitafuta mpaka akipate lakini kwa Mungu, hakuna anayehangaika na ndiyo maana ingawa leo ni siku ya Sabato, wengine wako hapa lakini biashara yao ya soda kule nyumbani inaendelea."

Akizungumzia mahangaiko ya binadamu katika kipindi cha sasa, Mhubiri huyo alisema kuwa, ukosefu wa uaminifu na msimamo mbele za Mungu ndicho chanzo kikubwa cha mateso ya wanadamu.

"Shida inaendelea kuwa shida siku hadi siku; njaa inazidi kuwa njaa kwa kuwa mwanadamau amekosa uaminifu na msimamo katika kazi ya Mungu. Shida zote zinatokana na watu kushindwa kusimama katika misingi ya Bwana na badala yake, wamekalia miungu wengine," alisema.

Aliongeza kuwa, ni wajibu wa kila mmoja kujitazama kama yuko katika mstari mnyoofu kulifuata Neno la Mungu. "Kila mmoja ajiulize ni mara ngapi amepita mbele za Mungu kimwili na kiroho bila kwenda kushoto wala kulia".

KARDINALI PENGO: Wanawake tumieni uwezo wenu kuleta amani

Brigitta Nungu na Christina Joseph, Bagamoyo

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, limesema wanawake watumie asili yao ya usamehevu, huruma na upendo kuwa chimbuko la amani duniani.

Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyasema hayo

wakati wa ibada maalumu iliyoandaliwa na Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) jimboni humo. Ibada hiyo ilifanyika Bagamoyo katika Jimbo Katoliki la Morogoro, Jumamosi iliyopita kwa ajili ya kuombea amani duniani.

"Pamoja na ulimwengu kupotoka mama anaweza kuwa chimbuko la amani katika ulimwengu kwa kuwa kiasili mama ni msamehevu, hana asili ya kuua ana moyo wa huruma," alisema.

Kardinali Pengo alisema, licha ya kutetea haki, ni hatua za kuitafuta ziende sambamba na rehema, usamehevu na huruma kwa kuwa ndiyo mapaji aliyo nayo mwanamke yeyote.

Alisema endapo jamii inataka kuwa na amani na neema, ni vema ikajiombea hususan akinamama ambao wanayo nafasi kubwa ya kuunusuru ulimwengu usiendelee kupotea.

Aidha, alisema kuwa vita vingi katika dunia ya leo ni vya kidini kati ya Wakristo na Waislamu pamoja na baadhi ya madhehebu kama Wahindu ambao nao wanashambuliana kwa misingi ya dini. Katika hija hiyo, Kardinali Pengo alisema kuwa, sababu ya vita isiyokoma duniani ni kosa la kuwashirikisha wanawake katika vita na mauaji. "Mungu amewawekea akinamama moyo wa kupokea na kutunza uhai, kitendo cha kuwashirikisha katika vita vya mauaji ni kinyume na mpango wa Mungu," alisema.

Kardinali Pengo alisisitiza kuwa, ili kulinda amani, watu wote hawana budi kujenga moyo wa huruma, upendo na usamehevu. "Tusipobadili msimamo wetu, hatuwezi kumaliza vita," alisema.

Aliwahimiza wanawake na wanajamii wote kumuomba Mungu aeneze moyo kwa Wakristo ili watambue na kuzingatia kuwa, hakuna anayeweza kuua kwa misingi ya jina la Mungu.

WAWATA katika parokia zote 40 za Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita walifanya hija katika maeneo ya kihistoria kwa Wakristo huko Bagamoyo mkoani Pwani ili kuona eneo ambalo Ukristo ulianzia miaka 133 iliyopita.

Wanawake hao Wakatoliki walitembelea sehemu ambayo msalaba wa kwanza ulijengwa na makaburi ya Wamisionari ikiwa ni pamoja na kuzuru pango la Bikira Maria.

Katika hija hiyo WAWATA, walitoa kiasi cha shilingi 1 052 255 pamoja na mabati 20 kwa ajili ya ujenzi wa parokia ya Bagamoyo, ujenzi wa Kanisa Dogo la Mtakatifu Ana na wanakwaya walikabidhiwa hundi ya shilingi 300 000 kwa ajili ya sare zao.

Hii ni mara ya pili kwa WAWATA jimboni humo kufanya hija kama hiyo huko Bagamoyo toka wajiwekee utaratibu huo mwaka jana.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa WAWATA Jimbo Kuu la Dar es Salaam. utafanyika kila mwaka.

SACHITA yataka vijana waepuke UKIMWI ili waheshimike

 

Na Christopher Gamaina, Tarime

RAIS wa shirika la Okoa Watoto wa Tarime (SACHITA), Bw. Peter Mwera, amesema kujizuia vitendo vya zinaa na kuepuka maambukizi ya magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa, ni njia bora ya vijana kujijengea maisha bora ya baadaye.

Alisema hayo wakati akifungua warsha ya siku tano juu ya Mafunzo Stadi za Maisha kwa Vijana iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime Alhamisi iliyopita.

Mwera alisema kuwa, endapo vijana watavishinda vishawishi vya kufanya mapenzi kabla au nje ya ndoa, hawatapata mimba ovyo wala kuambukizwa magonwa ya zinaa ukiwamo ugonjwa wa UKIMWI na kwamba hali hiyo, itawajengea heshima mbele za Mungu na machoni pa watu.

Amewahimiza vijana kuzingatia elimu pamoja na kupiga vita mila zote potofu zinazochangia kuenea kwa UKIMWI na unyanyasaji wa kijinsia ukiwamo ukeketaji wa wanawake kwani hali hiyo huwaathiri kiafya na kisaikolojia.

Mada zitakazojadiliwa katika warsha hiyo ya siku tano iliyoandaliwa na SACHITA na kudhaminiwa na shirika la PATH- AYA la nchini Uganda, ni pamoja na kutambua mabadiliko ya maumbile katika maisha ya vijana, mila zenye madhara na mbinu za kuwafikisha vijana katika malengo sahihi ya baadaye.

Mwera alisema kuwa, katika siku ya mwisho ya warsha hiyo iliyowashirikisha vijana wa kiume na wa kike zaidi ya 70 wenye umri kati ya miaka 10 na 14, wazazi watashirikishwa ili waelewe majukumu yao katika familia.

Alisema lengo lingine la kuwahusisha wazazi katika warsha hiyo ni kujua mila zilizopitwa na wakati pamoja na mafunzo ya namna ya kuwaelimisha na kuwahamasisha vijana kuepuka tendo la ngono kabla ya ndoa.

Wakufunzi katika warsha hayo wanatoka SACHITA, PATH-AYA, asasi zisizo za kiserikali (NGOs), madhehebu mbalimbnali ya dini, na Idara za Afya na Elimu.

Heshima ya taifa ni elimu-DC

Na Dalphina Rubyema

ELIMU ndiyo nguzo pekee inayoleta heshima ya taifa popote pale duniani, amesema Mkuu wa Wilaya ya Temeke.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Temeke, Bw.Seif Mpembenwe, alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akifungua Semina ya Elimu ya Watu Wazima iliyowashirika Walimu Wakuu wa Shule za msingi katika Manispaa ya Temeke, Maafisa Watendaji Kata na waratibu wa Elimu.

Katika Semina hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mkuu huyo wa Wilaya ya Temeke alisema kuwa hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kupata mafanikio pasipo elimu ya kutosha.

"Ukitaka kitu kizuri ni lazima uwe na elimu ya kutosha, hata ukitaka mwandisi mzuri, mwalimu mzuri vyote hivyo, suala la elimu linahitajika," alisema

Katika kusisitiza suala hilo la elimu, Mpembenwe alisema kuwa, wilaya yake ina idadi kubwa ya watu wazima ambao hawajui kusoma na kunadika na kuna watoto wengi ambao hawasomi katika shule za msingi kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema katika kuonyesha jinsi gani wilaya hiyo inajali elimu, watoto wenye umri kati ya miaka 8 -15 ambao hawasomi, tayari wamekwisha orodheshwa kwa lengo la ni kuwapa haki hiyo ya elimu.

Alisema watoto hao watasoma chini ya mpango mpya wa kila mtoto kupata elimu inayofaa hususan elimu ya Msingi.

Alitoa wito kwa watendaji wake kuendeleza kwa kasi, jitihada hizo na kwamba, na zisiwe moto wa mabua.

"Natoa wito kwa watendaji wote kwamba jitihada hizi zisiwe moto wa mabua ambao una kawaida ya kusambaa na kuwaka kwa kasi sana lakini ghafla huzimika," alisema.

Mpembenwe alisema, "Maasfisa Kata tunapokuja kutembelea kata yako kuangalia shughuli mbalimbali za Maendeleo, katika ratiba yako kama haujatuwekea shughuli za Elimu ya Watu Wazima basi wewe utakuwa haujafanya kitu," alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Shirika la Kipapa kutoa misaada kwa watoto wafungwa

Na Anthony Ngonyani.

SHIRIKA la Kipapa la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wiki hii linatoa misaada kwa watoto yatima, wasiojiweza, mahabusu na watoto wa mitaani katika vituo 20 jijini Dar-es-Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi.

Mwenyekiti wa shirika hilo jimboni Dar es Salaam, Cletus Majani, ameliambia Gazeti hili kuwa, misaada hiyo inatarajiwa kusambazwa Desemba 26, mwaka huu, siku ya kumbukumbu ya watoto waliouawa kwa amri ya Mfalme Herode kwa lengo la kumuangamiza Yesu alipozaliwa miaka 2000 iliyopita mjini Jerusalemu.

Miongoni mwa misaada itakayo sambazwa na shirika hilo ni sabuni, miswaki, nguo, dawa za meno, viatu, kandambili na hata fedha taslimu.

Shirika la Kipapa la Mtoto Yesu, linaudwa na watoto kutoka parokia mbalimbali za Kanisa Katoliki kwa lengo la kuwalea katika maadili mema.

Majani alisema kuwa, kutoa misaada hiyo ni sehemu ya matendo ya huruma kwa wenzao ambao wana sida na kuwafariji kutokana na kukosa bahati ya kulelewa na mapenzi kutoka kwa wazazi wao.

Siku hiyo watoto watajigawa kulingana na parokia zao na kwenda katika vituo vya watoto yatima na wa mitaani ambapo watashinda nao toka asubuhi mpaka jioni huku wakicheza, wakiimba nyimbo na kula chakula pamoja.

Alisema katika kuhakikisha wanatoa misaada mingi iwezekanavyo kwa wenye shida, watoto hao wa shirika hilo walikuwa wakichangisha vitu mbalimbali.

Vituo vya watoto vitavyofaidika na misaada hiyo ni pamoja na Kurasini, Mburahati, Kibaha, Kibaha Kwa Mfipa, Msimbazi na Tuamoyo. Vituo vingine ni DogoDogo Centre, Ally Hassain Mwinyi, Child in The Sun, mahabusu ya watoto na misaada mingine itaelekezwa kwa watoto wagonjwa walio wodini katika hospitali za Muhimbili, Tumbi, Agha khan, Temeke, Amana, Mwananyamala, Ukonga na Kisarawe

Shirika la Kipapa Jimbo la Dar es Salaam, hutoa misaada ya namna hiyo kila mwisho wa mwaka kwa watoto wenye shida ikiwa ni sehemu ya kutekeleza matendo huruma kwa wenzao.

Sweeden yaisadia TCCIA Tarime

Na Christopher Gamaina, Tarime

SERIKALI ya Sweeden imekisaidia Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) Tawi la Tarime, vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni nane ili virahisishe mawasiliano ndani na nje ya nchi.

Balozi wa Sweeden nchini Tanzania Bw. Sten Rylander, alikabidhi vifaa hivyo kwa Mwenyekiti wa TCCIA, Bw. Steven Sanifu, alipozindua ofisi mpya ya TCCIA wilayanmi hapa hivi karibuni.

Vifaa vilivyokabidhiwa kwa Mwenyekiti huyo ni pamoja na fotokopi, mashine ya kuchapia habari mbalimbali, kompyuta, fax na mtandao wa kompyuta (internet).

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika Desemba 18, mwaka huu zilipo ofisi mpya katika mtaa wa Kenyatta mjini hapa, Balozi huyo wa Sweeden nchini alisema kuwa, pamoja na kuirahisishia mawasiliano TCCIA- Tawi la Tarime, msaada huo pia ni changamoto kwa wananchi hususan wafanya biashara na wakulima kujitokeza zaidi na kujiunga katika chama hicho.

Alisema ni vema watu wakajitokeza na kujenga tabia ya kujiendeleza katika kutumia vyombo hivyo badala ya kusubiri misaada kutoka serikalini na kwa wafadhili wa nje.

Alisema Serikali ya Sweeden ipo tayari kuisadia Tanzania na hivyo, ni wajibu wa Watanzania kutosita kutoa mawazo yao mazuri ili yatumike kujenga uchumi wa nchi yao.

Aliupongeza mshikamano na juhudi zinazofanywa na TCCIA katika kujiendeleza kiuchumi na kusema kuwa, hilo ni moja ya mambo yatakayoihamasisha Serikali ya Sweeden kuongeza misaada kwa Tanzana.

Baadhi ya viongozi walioambatana na Balozi huyo ni, Rais wa TCCIA, Bw. Elivis Musiba, Kaimu Mwenyekiti wa TCCIA Kitaifa, Bw. Julius Matiku, Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Mara Bw. Rajab Okwaju na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime Bw. Wolfom Mpulu.

400 kupoteza kazi TRC

Na Josepaht Kiboga

JUMLA ya wafanyakazi 400 wa Shirika la Reli (TRC) wanatarajiwa kupoteza kazi zao kutokana na makubaliano yaliyofikiwa ya kulibinsfsisha shirika hilo.

Akizungumza ofisini kwake hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Gregory Makula, alisema wafanyakazi hao ni wale walio ajiriwa katika vitengo tofauti katika mikoa mbalimbali nchini ambapo reli hiyo inapita.

Alisema kuwa wafanyakazi hao watapunguzwa kazi kwa awamu na mpango huo ni sehemu ya uuzaji wa mashirika mengine manne yaliyotangazwa na serikali hivi karibuni.

Katibu huyo alisema kuwa yeye binafsi haungi mkono upunguzaji wa wafanyakazi hao sambamba na uuzaji wa shirika hilo kwa madai kuwa kitu kama hicho kilishindikana nchini Uingereza kutokana na unyeti wa shirika hilo.

Alidai kuwa mbali ya hilo ameitaka serikali kufikria upya mpango wake huo kwani kwa kufanya hivyo kutawaumiza wafanyakazia hasa kufuatia sera mpya ya malipo ya uzeeni ya wafanyakazi (PPF)abmyo imepitishwa na bunge hivi karibuni.

Alisema kuwa sera hiyo ambayo inaeleza wazi kuwa watakaostaafishwa wataanza kulipwa baada ya kufika umri wa miaka 56 ambao ndio wa mtu kustaafu hata kama mtu akiwa na umri wa miaka 25, itawaathiri wastaafishwa hao.

Makula alisema kuwa jitihada zake za kuonana na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Mark Mwandosya zimegonga ukuta.

Alisema kuwa alienda na jopo la viongozi wengine wa chama hicho bungeni kuonana na waziri huyo wakati wa bunge la bajeti na kumueleza ukweli kuhusu mpango huo mpya wa NPF lakni hakuna hatua ambazo alizozichukua.

Afisa Uhusiano wa shirika hilo hakuweza kupatikana kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo.

 

Maaskofu waongoza Jubilei ya Fedha Iringa

 

Na Bro. Andrew Chimesela, Iringa

MAASKOFU wawili Wakatoliki, Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa na Mhashamu Magnus Mwalunyungu wa Tunduru- Masasi, wamewahimiza wanaoishi katika nadhiri za utawa, kuishi kiaminifu.

Wakizungumza katika sherehe za kuadhimisha Jubilei ya Fedha kwa baadhi ya mabradha wa Shirika la Moyo Usio na Doa wa Bikira Maria, maaskofu hao walisema ni vema wanaoweka nadhiri za kitawa, waishi kama wanavyotakiwa.

Sherehe hizo ambazo ziliambatana na nderemo, shangwe, vifijo, vigelegele na shamrashamra zilifanyika Desemba 8, mwaka huu katika Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu- Tosamaganga.

Siku hiyo, mabradha watatu wa Shirika la Moyo Usio na Doa wa Bikira Maria, Thadeus Mwasalla, Wilfred Msigwa na Daniel Mwinuka, waliadhimisha Miaka 25 tangu kuweka Nadhiri za Kitawa.

Pia, masista watatu wa Shirika la Teresia wa Mtoto Yesu, waliadhimisha Jubilei ya Miaka 50, wakati masista wengine watatu waliadhimisha Jubilei ya Miaka 25.

Mabradha watatu na masista 19 waliweka Nadhiri za Maisha wakati mabradha saba na masista 22 waliweka nadhiri za muda (Uprofesi wa muda).

Askofu Mwalunyungu aliwahimiza kuzingatia kuwa, kuishi kiaminifu katika nadhiri zao, ni sawa na kuziishi Heri Nane alizotoa Yesu kule mlimani.

Heri hizo nane ni: Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika; Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.

Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa jili yangu (Mt. 5: 3 -11)

Wakati huo huo: Askofu Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa, amewahimiza waamini jimboni kwake na nchini kote kwa jumla, kuongeza juhudi katika kuchangia kwa hali na mali kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (AMECEA -2002), unaotarajiwa kufanyika nchini Julai 14 hadi 28, mwaka kesho. Mkutano huo utakaofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam, unatarajiwa kuhudhuriwa na maaskofu zaidi ya 100 na wajumbe wapatao 240 toka nchi mbalimbali.

Nchi za AMECEA ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Eritrea, Zambia, Malawi na Sudan.

Kufanyika kwa mkutano huo wa kimataifa nchini Tanzania, ni heshima kwa Kanisa nchini na kwa Watanzania wote kwa jumla.

Ni wajibu wa kila Mkatiloki, Mkristo, Mtanzania na wote weye mapenzi mema, kuchangia kwa hali na mali ili kuufanikisha.