BAKWATA, CCT, TEC kukutana na vyama vya siasa

l Wabunge, Serikali kushiriki

Na Neema Dawson

KAMATI ya viongozi wa dini inaandaa kongamano litakalowakutanisha viongozi wa dini toka Jumuiya ya Kikristo Tanzania Tanzania (CCT), Baraza Kuu la Waisalamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na viongozi wa Serikali na vyama vya siasa kujadili namna ya kutatua migogoro ya kisiasa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mwishoni mwa juma, Mjumbe wa Kamati ya Usimamizi ya Viongozi wa Dini ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura alisema Kongamano hilo Maalumu la Kitaifa litafanyika katika Kituo cha Kiroho Mbagala jijini Dar-Es-Salaam, Aprili 18, mwaka huu.

Miongoni mwa viongozi kumi wanaotarajiwa toka serikalini, watakuwamo Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha.

Wengine watakaoshiriki kongamano hilo ni viongozi toka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kikiwamo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake(TAMWA) na Mtandao wa Kijinsia nchini(TNGP).

Alisema kabla ya mada kutolewa, viongozi wakuu wa dini toka BAKWATA, CCT na TEC watatoa nasaha.

Akifafanua zaidi mjumbe huyo toka TEC, aliyeandamana na Mkurugenzi wa BAKWATA, Abbas Kihemba na Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliyekuwa anawakilisha CCT, Eneza Abraham, alisema kuwa wakati Sheikh Mkuu wa Tanzania; Mufti Hemed Bin Jumaa Bin Hemed, atazungumzia amani ya Watanzania, Rais wa TEC; Mhashamu askofu Severine Niwemugizi atazungumzia umoja wa kitaifa. Mwenyekiti wa CCT Askofu Mkuu John Ramadhani atazungumzia juu ya kupatana baada ya kukosana.

Padre Rutechura alisema kuwa katika kongamano hilo litakalowashirikisha wenyeviti, makatibu wakuu na wabunge wa vyama vyenye wabunge, umetengwa muda wa kutosha kujadili na kutoa maazimio yatakayoweka misingi imara na maelewano miongoni mwa wanasiasa na vyama vyao na hivyo, kudumisha amani nchini.

Imefahamika pia kuwa baadhi ya watakao jadili mada juu ya njia bora za kutatua migogoro ya kisiasa nchini katika kongamano hilo ni Bw. Emmanuel Kopwe na Alhaji Kundya.

Februari 8,2001 viongozi wa dini kutoka CCT, TEC na BAKWATA walikutana jijini Dar es Salaam kujadili hali ya kisiasa nchini baada ya maafa yaliyotokea Zanzibar kufuatia maandamano ya wafuasi wa chama cha Wananachi (CUF) yaliyokuwa yamezuiliwa na serikali.

Baada ya mkutano huo viongozi hao walitoa tamko ramsi juu ya hali ya kisiasa nchini. kongamano hili ni matokeo ya mafanikio ya mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa wa 1997 na machafuko ya kisiasa ya Januari 27, mwaka huu.

Mkutano wa Injili 'wagawa dawa' kuepusha machafuko,balaa, Tanzania

Na Elizabeth Steven

MKUTANO wa Injili ulioandaliwa na kanisa la Peace Makers Church(PMC), na kufanyika katika viwanja vya WAPO Mission Center jijini Dar-Es-Salaam, "umegawa dawa" kwa Watanzania ili kulinusuru Taifa lisiangamie kwa machafuko na rushwa.

Mhubiri katika mkutano huo wa siku nane ulioanza Jumatatu iliyopita, Mwinjilisti George Banely kutoka Tanga, alisema katika siku ya tatu ya mkutano kuwa, ili taifa la Tanzania linusurike katika janga la machafuko ya kisiasa na ongezeko la kero ya rushwa na balaa, dawa pekee anayoitoa kwa Watanzania kuepuka maafa hayo ni moyo wa toba ya kweli kwa kila mmoja.

Alisema machafuko ya kisiasa, kero ya rushwa, wizi na matatizo katika ndoa nyingi nchini, ni matokeo ya jamii kuto mtii Mungu na kuwa wagumu kuomba radhi na kwamba dawa pekee, ni kuomba radhi na kufanya toba ya kweli.

"Uovu ni matokeo ya kutomtii Mungu. Kama Watanzania wote wangemtii Mungu, hayo matatizo ya rushwa yasingetokea na wala kusingekuwa na matatizo ya machafuko mengi ya kisiasa," alisema Mwinjilisti huyo maarufu kwa jina la GB.

Mwinjilisti GB, alisema matatizo hayo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na waamini wengi kujionesha machoni pa watu kuwa ni WACHA-MUNGU kumbe ni WAACHA-MUNGU.

Akitoa mfano, alisema kuwa wazee wengi wa makanisa, licha ya kuonekana kuwa waamini wazuri, miongoni mwao wapo yenye imani mbaya za kishirikina na wanaoendekeza matumizi ya hirizi.

"Wazee wengi wa makanisa wakiwa makanisani, ni wacha-Mungu lakini, wakitoka tu, tayari wanakuwa waacha-Mungu; wanapanda ungo(ushirikina)".

Akitoa mfano katika siku ya kwanza ya mkutano, GB alisema inashangaza kusikia kuwa hata katika ajali iliyotokea mkoani Mbeya hivi karibuni na kuuwa watu 31, mtu mmoja mwenye imani za kishirikina bada aya kusikitikia tukio hilo, alikwenda kuzoa ubongo wa maiti ali akaufanyie vitendo hivyo na ndipo akauawa na wananchi wenye hasira.

"Huyo aliyechota ubongo huko Mbeyawakati wenzake wamekufa kwenye ajali, aling’oa nanga ya Yesu na watu wakamng’oa.

Akisistiza umuhimu wa toba ya kweli, alisema endapo kila mmoja angekubali kuomba radhi anapokosea, hata vitendo vya rushwa vilivyokithiri katika Jeshi la Polisi na Mahakama, vingekwisha"Laiti kama Watanzania wangejua kusamehe hata polisi na mahakama wasingekupo lakini, hilo limekwisha limebaki nitamkomesha. ...kama unataka kumkomesha mkeo au mumeo, utaona adhabu utakayoipata toka kwa Mungu," alisema na kuongeza,

"wanaume wengine wanakula mshahara wote kwa siku moja na nusu tu, kisha wakifika nyumbani badala ya kuomba radhi anasingizia eti ameibiwa kumbe wamekula kuku choma na malaya. Hii ni mbaya sana."

Alisema mtu yeyote anayekosea kisha akasema "Nisamehe", anapata baraka saba. Hakuzitaja.

Katika mkutano huo, Askofu Mkuu wa PMC ambaye pia ni Mwenyekiti wa makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), Silvester Gamanywa, alifanya maombi na kuwasisitiza waamini kulisikia, kulitafakari na kulifanyia kazi ipasavyo, Neno la Mungu .

Achomewa nyumba baada ya kutakiwa ahame

l Aliambiwa analawiti watoto, sasa zamu ni yake

l Kuku 40 waunguzwa, hasara 600,000

Na Haruni Makubo, Tarime

MOHAMEDI Werema wa kijiji cha Muriba wilayani Tarime katika mkoa wa Mara, amechomewa nyumba na watu wasiojulikana baada ya kutakiwa ahame kijijini hapo huku akitishiwa kuwa amekuwa akiwalawiti watoto, sasa ni zamu yake.

Akielezea tukio hilo kwa mwandishi wa habari hizi mjini hapa, Bw Werema amesema nyumba yake ya nyasi iliyopo kijijini hapo, iliunguzwa mwishoni mwa juma lililopita na kumtia hasara ya jumla ya shilingi 600,000.

Amevitaja baadhi ya vitu vilivyoteketea katika tukio hilo kuwa ni pamoja na kuku 40, vitanda viwili, na kabati iliyokuwa na vyombo mbalimbali vyote vikiwa na thamani hiyo.

Amesema anashuku kuwa amefanyiwa kitendo hicho na jirani zake ambao umekuwapo uhasama baina yao wakimtaka ahame kwenye eneo wanalodai kuwa, ni ardhi yao(hakuwataja).

Anasema kufuatia hali hiyo ya kulazimishwa ahame, alifikia uamuzi wa kuwafikisha watuhumiwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Nyamwaga wilayani hapa ambapo walihukumiwa kifungo cha miezi mitatu au kulipa faini ya shilingi 3000 kila mmoja.

Alisema siku chache baada ya watu hao kulipa faini, alipokea barua isiyo na jina wala tarehe isipokuwa sahihi ya mtu asiyejulikana iliyokuwa na maneno haya,

"Umetuweka ndani, utakiona cha moto. Umekuwa ukiwalawiti watoto wadogo lakini sasa, sisi ndio tutakulawiti na unatakiwa ufunge vilago ili uondoke."

Alisema anawashuku watu hao kutokana na barua hiyo ya vitisho aliyoipata baada ya uamuzi wa mahakamakuwapa adhabu na kwamba baada ya muda yameanza kutokea.

Ameiomba serikali kumsaidia kuhakikisha kuwa uslama wake unakuwa wa uhakika kwani kwa sasa, anadai uko mashakani kwani ana imani waliotenda kitendo hicho, walitaka kummaliza.

Wakati huo huo: Shirika moja lisilo la kiserikali la mkoani Mara, lijulikanalo kama CADA, linakusudia kumfikisha mahakamani, aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo la Afya na dakatari wa CADA Dispensari ya mjini Musoma kwa ubadhilifu wa shilingi 4,662,562, mali ya shirika hilo.

Uamuzi huo ulifikiwa Jumatatu iliyopita na wajumbe waMkutano Mkuu wa CADA uliofanyika katika ukumbi wa shirika moja lisilo la kiserikali wilayani hapa la SACHITA(Save Chldren of Tarime) na kuwajumuisha wanachama wwa CADA toka wilaya za Serengeti, Musoma na Tarime.

Katika mkutano huo, Rais wa CADA, John O.S. Tangatya, shirika la Medical Express Tanzania, liliwahi kutuma fedha hizo katika akaunti ya CADA Dispensary, lakini Mkurugenzi huyo aliyekuwa pia ni Mhazini wa CADA, hakuziingiza fedha hizo.

Alisema baada ya kupata taarifa ya kutumwa fedha hizo na kugundua kuwa hazijaingizwa kwenye akaunti kama ilivyokusudiwa, alifuatilia hadi Dar-Es-Salaam na kubaini kuwa zilipokelewa na Mkurugenzi wa Afya CADA.

Alisema akiwa safarini, alifunga zahanati hiyo na ofisi zote za CADA zilizokuwa na nyaraka za shirika ili kunusuru hali isizidi kuwa mbaya.

Alifafanua kuwa aliporudi, alikuta Kamati Tendaji ya CADA ikishirikiana na mkurugenzi huyo aliyemaliza muda wake, wamebomoa ofisi na milango ya zahanati na kisha kuchukua vitabu vyote vya mapato na matumizi.

Alisema kisha walificha nyaraka zote na kufunga baadhi ya ofisi kwa makufuri yake.

Alisema hivi sasa Mkurugenzi huyo wa zamani amebadili jina la zahanati hiyo na kuiita KADA badala ya CADA kumaanisha kuwa ni yake binafsi.

Mkutano huo Mkuu ulimchagua Katibu wa CADA, Bw. Eliudy Munanka kuwa Mhazini na pia kamti Tendaji mpya, iliundwa

Kardinali Pengo awatia moyo Mapadre

l Asema wanasaikolojia sio madaktari wa dhambi

l Awataka waanze upya kazi

Na Mwandishi Wetu

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka mapadre kutokata tamaa na kujiona labda wamechelewa na badala yake, sasa waanze kazi upya ili wawasaidie kwa Sakramenti ya Upatanisho wanaokimbilia kwa wanasaikolojia.

Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Misa ya Krisma iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar-Es-salaam, siku ya Alhamisi Kuu ambayo pia ni Sikuku ya Mapadre Duniani.

Ibada hiyo iliwashirikisha pia Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, Provinsiali wa Ndugu Wakapuchini Tanzania, Ndugu Beatus Kinyaiya, mamonsinyori Deogratius Mbiku na Julian Kangalawe, mapadre wote wanaofanyakazi katika Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, watawa, mashemasi na waseminaristi wa Seminari Kuu ya Segerea watawa na mamia ya waamini.

Akizungumzia umuhimu wa huduma ya Sakramenti ya Upatanisho, Kardinali Pengo aliyanukuu mang’amuzi ya baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliyeshuhudia misululu ya waamini waliokwenda kwa mapadre ili kuungama dhambi hasa katika Mwaka Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema kuwa kwa saa nyingi mapadre waliungamisha bila kuchoka wala kuwapo manung’uniko.

"Misululu hiyo inathibitisha kuwa Sakramenti ya Upatanisho haijapoteza maana na thamani yake katika Kanisa," alisema Kardinali Pengo.

Alisema kwa miaka iliyopita sakramenti hiyo ilikuwa katika hali ya wasiwasi (crisis) kutokana na baadhi ya mapadre kutoipa kipaumbele na pia baadhi ya mapadre wenyewe, kutoipokea kabisa.

Alisema hali hiyo iliwafanya waamini kukosa kuona mfano hai na hali hiyo, ikawafanya watu wakimbilie kwa wanasaikolojia ambao si madaktari wa dhambi.

"saikolojia haiifikii Sakramenti ya Upatanisho kwani matatizo ya kiroho ni ya kiroho na hayatatuliwa kwa njia ya kisaikolojia" alisema Kardinali.

Hata hivyo Mwadhama aliwataka mapadre kukuza mbegu hiyo na kuwa wazi zaidi kufungua milango ili waamini wapatane na Mungu. "Ulimwengu unatafuta kupatanishwa na Mungu," alisitiza.kardinali Pengo aliwataka pamoja na mapungufu hayo, mapadre wasijione kama waliochelewa na hivyo kukata tamaa wakisema wamefanya kazi usiku kucha hawajapata kitu bali wajue kuwa wako katika mwanzo wa milenia mpya na kama Mtakatifu Petro, wasikie Neno la Kristo linaloagiza, TWEKA MPAKA KILINDINI" ukiwa mwongozo wao wa kazi hiyo huku wakikumbuka pia kuwa upadre ni paji la upendeleo wa Kristo.

Akinukuu Waraka wa baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kwa Makasisi"DUC IN ALTUM" yaani, Tweka mpaka kilindini, unaonukuliwa toka katika Injili ya Luka 5:5, Kardinali Pengo alisema kuwa baba Mtakatifu katika waraka huo wa kwanza kwa milenia hii, pamoja na kumshukuru Mungu kwa pato la Kanisa na paji lake yaani mapadre, anawashukuru makasisi hao kwa huduma mbalimbali wanazotoa bila manung’uniko.

"Paji hilo lina ugumu wake na kama Kristo mwenyewe, mtakumbwa na matatizo yasiyoeleweka...Mtapata machozi...katika hayo, mengine yanaweza kutoka hata kwa Askofu wenu," alisema na kuongeza kuwa hata hivyo baba Mtakatifu aliwataka mapadre wawe wavumilivu maana kama waraka usemavyo, machozi hayo yanakusanywa kwenye chupa ili kumwagilia shamba la Mungu.

"Mimi binafsi nathamini kila kazi mnayofanya hata nisiposema," alisema.

Afisa wa afya afungiwa msalani na mtumishi wa hospitali

Na Christopher Gamaina, Tarime

BWANA afya wa kata ya Tarime mjini Bw. Msomi amelazimika kuukubali muda wa ziada wa kuendelea kukaa msalani hata baada ya kutamatisha zoezi la kujisaidia baada ya mtumishi mmoja wa hospitali ya wilaya ya Tarime kufunga kwa kufuli mlango wa choo aliyokuwa ndani yake.

Tukio hilo la kipekee kutokea wilayani hapa lilishuhudiwa na mwandishi wa habari hizi mnano machi 28 mwaka huu baada ya kuwasili hospitali hapo ili kuonana na kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo Bw. Kululetela kwa mazungumzo ya kiofisi.

Bwana afya huyo wa kata alikumbwa na mkasa huo wa kukumbukwa wakati alipokuwa ana ‘jisitiri’ katika choo moja ya watumishi wa hospitali hiyo iliyopo hospitalini hapo.

Akizungumza na mwandishi juu ya tukio hilo la aina yake bwana Msomi alisema siku hiyo baada ya kufika hospitalini hapo katika majira ya asubuhi katika shughuli zake za kiofisi punde si punde alijihisi haja hali iliyomfanya kuwahi msalani ili kukabiliana na bughudha hiyo ambayo ni muhimu kwa kila mwanadamu.

Baada ya kuingia humo mtumishi wa hospitali hiyo mama Mbelwa alielekea chooni hapo na kubana kufuli kwa kusahau kuwa kulikuwa na mtu ndani kisha akaondoka zake na funguo.

Baada ya kumaliza haja Bw. Msomi alijaribu kufungua mlango wa choo hiyo ili atoke kuendelea na shughuli zake za kiofisi lakini zoezi hilo liligonga ukuta baada ya kugundua kuwa mlango umefungwa kwa nje.

Bwana Msomi alidai baada ya kuona hivyo ilimbidi kutumia maarifa ya kuzaliwa ili aweze kutoka chooni humo ambapo kwa bahati alifanikiwa kuona kijitundu kidogo katika mlango huo na hivyo kukitumia kuchungulia nje ili kumvizia yeyote atakayekatiza eneo hilo ili aweze kumwomba amfungulie.

‘Nilitumia tundu hilo dogo kuchungulia nje ambapo baadaye nilimwona Bw. Rozana (afisa mmoja anayeshughulika na masuala ya afya) akipita karibu na eneo hilo nikamwita kwa kumaanisha nikamwomba anifungulie’ alidai .

Bw. Rozana alipoangalia mlango huo wa choo alishangaa kuona umefungwa kwa kufuli ndipo bila kupoteza muda alimwagiza mmoja wa watumishi hospitali hapo kumtafuta mama Mbelwa alete funguo wa choo.

‘Hee! Sikukumbuka kwamba kulikuwa na mtu ndani yake, mimi nilifika tu na kubana kufuli, samahani jamani!’ alisema mama Mbelwa huku akitoa ufunguo na kumpatia mtumishi mwenzake ambaye alienda kumfungulia Bw. Msomi.

Baada ya kufunguliwa Bw. Msomi alimtaka mtumishi huyo kuwa makini kwa chochote anachokuwa anakifanya kuliko kufanya mambo bila ya kufikiri kwa kuwa kitendo cha namna hiyo kinaweza kikamfanya mtu akaathirika kiafya kama sio kuchelewa katika shughuli muhimu za kiofisi.

Hata hivyo Bw. Jonas Kisiroche wa kijiji cha Turugeti Wilayani hapa pamoja na watu wengine walioshuhudia tukio hilo walisema ni bora watumishi wa hospitali hiyo wakachagua na kutenga sehemu maalumu kwa ajili ya kutunzia ufunguo wa choo ili kila mwenye kuhitaji kuingia msalani aweze kuchukua na kujifungulia mwenyewe na baadaye kurudisha mahali pake.

UVIKAI watembea kilomita 30 kuwatafuta yatima

Na Neema Dawson

VIJANA 30 wanachana wa Umoja wa Vijana Katoliki Iringa (UVIKAI) parokia ya Consolata, jimboni Iringa, wametembea kwa miguu mwendo 30 takribani kilomita 30 hadi katika Kituo cha Watoto Yatima cha Ipamba kilichopo Tosamaganga kutoa misaada.

Katika safari yao, vijana hao wa kigango cha Consolata, waliwapa yatima hao zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mahindi, nguo, sabuni, daftari, kalamu na pesa walizopata kwa njia ya mchango wa hiari baina yao.

Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka mkoani Iringa zinasema, baada ya kufika katika kituo hicho wakiwa na Mshauri wao, Shemasi Wilhard Kiowi, waliuomba uongozi wa kituo hicho uwape kazi ya kufanya na ndipo mmoja wa masista wa kituoni hapo ambaye jina lake halikupatikana mara moja, aliwapa kazi ya kufyeka nyasi na kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa habari toka kwa Mshauri wa UVIKAI, Shemasi Kiowi, walifanya kazi hiyo barabara. Zinasema baada ya chakula, vijana hao kila mmoja alimchukua kwa mapenzi mtoto mmoja na wengine zaidi, na kuongea nao huku watoto wale wakifurahia kubebwa na wakubwa zao.

Habari zaidi zilizopatikana jijini Dar-Es-Salaam, zinasema baada ya kusali rozari kwa pamoja kwa pamoja katika ziara hiyo ya Machi 17, mwaka huu, watoto hao waliwaburudisha wageni wao kwa nyimbo mbalimbali zilizokuwa na ujumbe mahususi na wa kutia huruma na majonzi.

Wakati huo huo: Vijana hao wa UVIKAI, wameipokea kwa manufaa semina ya mabadiliko ya tabia kwa namna ya pekee ikiwa ni hatua za kupambana na janga la UKIMWI.

Hatua hiyo imefuatia vijana wanne wanachanama wa UVIKAI parokiani Consolata, kuhudhuria semina iliyoandaliwa na chama cha kitume cha "Youth Alive Club", iliyofanyika Desemba mwaka jana katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar-Es-Salaam.

Waliohudhuria semina hiyo jijini Dar-Es-Salaam ni Paschal Mahondo, Elizabeth Kulanga, Vitalis Nyenza, Zawadi Kwavava na mshauri wao, Shemasi Wilhard Kiowi. Kwa mujibu wa taarifa ya Mshauri huyo wa UVIKAI, Shemesi Kiowi, iliyopataikana jijini wiki iliyopita, katika semina hiyo ya Machi 9 hadi 11, mwaka huu, iliyofunguliwa na paroko wa parokia ya Consolata Padre Giaccomo Bakeneli, wana YCS wa shule za sekondari za Mwembetogwa, Lugalo, Kalielo, Mawelewele, chuo cha VETA na vijana wa vigango vitano vya kata ya Consolata yaani, Consolata, Mkwawa, Mgera, Mawelewele na Mapogoro, walishiriki.

Pamoja na mada nyingine zilizotolewa katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Vijana katika Jimbo Katoliki la Iringi, Padre Alphonce Mhamilawa, alizungumza juu ya kujifahamu.

Mada nyingine zilizojadiliwa ni pamoja na wewe ni wa pekee, zawadi ya masiha, madawa ya kulevya, UKIMWI, utoaji mimba na stadi za kazi.

Katika semina hiyo, vijana walihimizwa kuepuka vitendo vya ndoa kabla na nje ya ndoa ili kuepuka uambukizaji wa UKIMWI na utoaji mimba.

Askofu awataka mapadre kuwajali wagonjwa

Na Anthony Chilumba, Kilwa Masoko

ASKOFU Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, amewataka mapadre na waamini wengine jimboni kwake na mahali kwingine, kuwajali wagonjwa mbalimbali waliopo hospitalini na majumbani ili wagonjwa waufaidi upendo wa Kristo.

Askofu Ngonyani ametoa wito huo hivi karibuni katika parokia ya Nyagao, alipoadhimisha misa ya kubariki Mafuta Matakatifu ya Wakatekumeni, Krisima na Mafuta ya Wagonjwa.

Alisema, kwa neema ya pekee, mapadre hawana budi kuwapenda na kuwajali wagonjwa kwa kuwatembelea ili nao waonje upendo wa Kristo kupitia matendo ya viongozi hao wa kiroho.

Licha ya kuwafariji, Askofu amewahimiza mapadre kuwapa wagonjwa huduma za kiroho kwa kuwapaka mafuta na kuwalisha Chakula cha Bwana.

Mkuu huyo wa jimbo amesema, dhamira ya Siku ya Kubariki Mafuta ya Mwaka uliopita, ilikuwa PADRE NA MILENIA YA TATU ambapo alitilia mkazo suala la uinjilishaji mpya.

Amesema dhamira hiyo imefaa zaidi kwa mwaka huu kwa kuwa inakubalika na watu wengi kuwa Milenia ya Tatu imeanza usiku wa manane wa Desemba 31, Mwaka jana na si Desemba 31, Mwaka juzi. Mhashamu Ngonyani alisema tunapoanza mwaka wa kwanza katika karne ya 21 na Milenia ya Tatu, mapadre hawana budi kutafakari wajibu wao juu ya kuponya magonjwa ya mwili na roho.

Kuhusu maisha adili ya mapadre, Mchungaji huyo mkuu wa jimbo aliwahimiza viongozi hao wa kiroho(mapadre) kuishi kadiri ya miiko ya kazi zao na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwakwaza waamini wao.

Amewataka waamini nao wawaombee mapadre na viongozi wote wa kiroho, ili watekeleze kwa ufanisi, majukumu yao ya kichungaji.

Alitumia nafasi hiyo kuwadokeza juu ya barua ya Baba Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili, aliyoitoa wakati wa kufunga Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 iitwayo Mwanzoni mwa Milenia Mpya. (Novo Millenio Ineunte).

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa jimbo, barua hiyo imesisitiza kuwa maisha ya utakatifu ni jukumu la watu wote wakiwamo mapadre, watawa na walei(1Wath.4:3). Aliwataka kuacha utepetevu wa maisha ya Kikristo na kudhamiria kujitoa zaidi kwa Mungu na jirani wakisukumwa na upendo.

Maisha ya sala, kupokea Sakramenti ya Kitubio na kulisikiliza Neno la Mungu, ni miongoni mwa mambo mambo ya kiroho yaliyoainishwa katika barua hiyo ya mwanzoni mwa milenia mpya.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu ngonyania akishirikiana na mapadre wapatao 30 wa Jimbo Katoliki la Lindi na kuhudhuriwa na watawa na walei.

Wafungwa walia na UKIMWI

Waomba Kanisa liingilie kati

Na Leocardia Moswery

WAFUNGWA wa Gereza la Ukonga jijini Dar-Es-Salaam, wameliomba Kanisa Katoliki nchini kuingilia na kutumia nguvu zake zote kuinusuru jamii dhidi ya janga la UKIMWI.

Walitoa ombi hilo katikati ya juma lililopita wakati Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, walipotembelea wafungwa wa gereza hilo kama sehemu ya matendo yao ya huruma kwa kipindi cha Mfungo wa Kwaresima.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa WAWATA ngazi ya jimbo na taifa, Bibi Olive Luena, katika ziara hiyo ya WAWATA katika magereza ya Ukonga na Segerea jijini iliyomhusisha pia Askofu Msaidizi wa Jimbo katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, wafungwa hao walisema kutokana na ugumu na madhara ya tatizo la UKIMWI kwa jamii, ni wakati sasa kwa Kanisa kutumia nguvu zake zote katika kupambana nao.

Bibi Luena ambaye alikuwa akizungumza na gazeti hili juu ya safari yao ya kutembelea magaereza hayo katika mazungumzo yaliyofanyika siku hiyo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar-Es-Salaam, alisema jamii nzima haina budi kuunga mkono juhudi za wafungwa hao kwa kuwa wameliona hilo ni tatizo katika jamii ingawa wao wako kifungoni.

Alisema wafungwa hao waliguswa na na ujumbe wa somo la Injili katika Kitabu cha Walawi 5. "Wafungwa kama watoto wetu, wameomba Kanisa lisaidiane zaidi na wanajamii wengine kupambana na UKIMWI maana wanaona na kusikia ukimaliza watu," alisema.Kwa niaba ya WAWATA jimboni na wote walioshiriki msafara huo, Bibi Luena alimshukuru Mkuu wa Gereza la Ukonga, , Mwita Sawaya kwa kuwapokea kwa ukarimu.

Bibi Luena alisema WAWATA wameamua kuwatembelea wafungwa hao kwa kuwa wanatambua dhahiri kuwa mtoto hakui kwa mama na hata kama akiwa mhalifu, ni jukumu lao kumrudi na sio kumtupa.

Siku hiyo katika ziara zao katika magereza hayo, WAWATA waliwapa wafungwa zawadi mbalimbali kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.

Radio Tumaini 2 kutangaza kwa kiingereza na Kifaransa

Na Dalphina Rubyema

RADIO ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam(Radio Tumaini),sasa itarusha matangazo yake kwa lugha za Kiingereza na Kifaransa.

Matangazo hayo yatapatikana katika redio yake mpya inayojulikana kama TUMAINI 2 kwenye masafa ya FM 105.90.

Kuanza kurushwa moja kwa moja kwa lugha hizo za Kifaransa na Kiingereza, kumekuja baada ya raedio hiyo kuungana na redio nyingine kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Radio hizo ni Radio Canada International (RCI), Radio France International (RFI) Deitche Welle (DW), Radio Netherlands International (RNI) na Swiss Radio Internatonal (SRI).

Uzinduzi wa Radio hiyo ya Tumaini 2, ulifanyika katikati ya wiki katika ofisi za Radio Tumaini zilizopo katika majengo ya Kanisa Kuu la Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam la Mtakatifu Yosefu.

Mabalozi wa nchi mbalimbali walishuhudia uzinduzi huo. Pia, alikuwepo Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, Mkurugenzi Mstaafu wa Radio Tumaini, Padre Jean Francois.

Wakazi wengi wa jiji la Dar-Es-Salaam na maeneo jirani ya Zanzibar, Pwani na Morogoro, wamekuwa wakisikiliza Radio Tumaini 1 inayopatikana FM lakini hivi sasa watanufaika kusikiliza moja kwa moja matangazo kwa lugha ya Kiingereza na Kifaransa kutoka katika nchi zilizotajwa.

Wapangaji kuelimishwa juu ya haki zao

Bilhah Massaro na Getrude Madembwe

CHAMA cha Wapangaji Tanzania kwa kushirikiana na kitengo cha IUT cha Afrika (IUT Focal Point for Africa), kimeandaa mpango kuwaelimisha wapangaji juu ya haki zao.

Akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar-Es-Salaam mwishoni mwa juma, Katibu Mkuu wa chama hicho nchini Bw. Nyamakamba Kafemba, alisema mpango huo ulianza Aprili 4, Mwaka huu.

Alisema hayo ni matokeo ya makubaliano ya Mkutano wa IUT uliofanyika mjini Amsterdam Uholanzi, uliovijumuisha vyama vya wapangaji duniani.

Katika mkutano huo wa Februari mwaka huu, wajumbe walivitaka vyama vya wapangaji Afrika, kufanya jitahada katika miaka mitatu ijayo, kufikiwa kiwango chenye kuhakikisha kuwa, wapangaji wanajua haki zao za kimsingi za upangaji.

Kufuatia pendekezo hilo, lengo ni kubaini kero na matatizo mbalimbali ya wapangaji katika nchi nzima na pia, kuwahamasisha wapangaji wajiunge na chama kwa nia ya kuwasaidia kutatua matatizo.

"...Kuna baadhi ya wapanga ambao hawajajua haki zao. Hivyo wakijiunga na chama hiki, wataweza kufahamu haki zao kwa kuwa wengi bado wananyanyaswa," alisema.

Haki za wapangaji zilizobainishwa katika mpango huo ni pamoja na kumiliki sehemu anayoishi au kupanga bila ya manyanyaso au bugudha yoyote toka kwa mwenye nyumba.

Kutopandishiwa kiholela kodi ya pango bila ya kufuata utaratibu wa sheria na kutolazimishwa kulipia pango kwa pesa za kigeni na pia, mpangaji kutolazimishwa kulipa pango kwa mkupuo wa miezi au miaka kadhaa.

Haki nyingine ni kupata huduma za msingi kama vile choo safi, maji, umeme na matengenezo ya nyumba pindi inapoharibika.

Haki zingine ni kupatiwa mfumo bora wa usafi na mazingira ili kumuondolea mpangaji athari zinazoweza kuhatarisha afya zao kupatiwa sehemu nyingine za kuishi na fidia katika kubomolewa nyumba au maeneo wanayoishi.

Mratibu wa UKIMWI akalishwa 'kiti moto' kwenye kongamano

Ni baada ya kuwaambia watumie kondomu

Ahaha akisema, Yaishe! Yaishe!

Na Getrude Madembwe

VIJANA waliohudhuria Kongamano la Vijana lililoandaliwa na Youth Centre na kufanyika katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii wamempa wakati mgumu,

Mratibu wa Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Dk. Geofrey Somi baaada ya kuwambia wakishindwa kujizuia kufanya mapenzi, watumie kondomu.

Dk. Somi ambay ni Mratibu katika Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, alipatwa na tafrani hiyo baada ya vijana hao washiriki wa kongamano kutaka kujua ukweli kuhusiana na matumizi ya mipira ya kiume na ya kike(kondomu).

Alikuwa akitoa mada juu ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Waashiriki hao walimjia juu wakitaka awambie kwanini anawapotosha.

Kisa chenyewe kilikuwa hivi:

Dk. Somi alisimama mbele ya vijana hao na kuanza kuelezea ni jinsi gani ugonjwa huo hatari wa UKIMWI ulivyoua na bado unaendelea kuua watu wengi duniani.

Akasema kuwa, tafiti walizo nazo za miaka ya nyuma zinaonesha kuwa hata vijijini ugonjwa huo upo.

Alieleza kuwa mara kadhaa, wameku wakiwapima wajawazito kwani wao wanapokuwa na mimba ili kujuahali zao kwa kuwa ndio kioo cha jamii.

"Tunawapima wao kama kioo cha jamii kwani kuna wake za wafanyabiashara, wafanyakazi wa ngazi zote hivyo, tukiwapima wao ndiyo jamii ilivyo na kama wao wameathirika, tunajua idadi ya walioathirika."

Aliendelea kusema, "Sisi kama serikali, hatuwezi kuwaacha watu wafe bila ya kuwambia wasitumie kinga. Kwa mfano, mtu anaambiwa aache kufanya uzinzi lakini hataki."

Akaendelea kuwa, "imaadili mtu hatakiwi kufanya uzinzi hivyo, watu waache zinaa. Lakini, kama wakishindwa basi wawe na mpenzi mmoja mwaminifu. Wakishindwa pia, basi watumie kondom."

Kauli hiyo ikazua utata kwa vijana hao. Baadhi yao wakaanza kunong’ona wakionesha kutoridhika na kauli ya Dk. Somi.

Alipoona minong’ono inazidi kwa washiriki, akatoa nafasi kwa mwenye swali aulize ili aelimishwe.

Wakanyoosha mikono ili kila mmoja apate nafasi ya kuuliza. Kizaazaa kikaanza baada ya mmoja kaliyetambulika kwa jina la Esmail Mgana wa kikundi cha vijana cha News Arts creation, cha Kinondoni.

Akauliza, "Sasa Dk, Mbona mnatuchanganya kuhusu hizo kondomu. Tunavyofahamu, ni kwamba, kondomu hizo zinaweza kupitisha kirusi cha HIV halafu, wewe unatuambia tutumie kondomu. Hauoni hapo mnatuangamiza?"

Dk. Somi akashituka na kumaka, "Basi yaishe! Yaishe tena nasema yaishe. Mimi nipo hapa kwa niaba ya Serikali na ninapowaambia hivyo sina maana mbaya.

Kwanza sitaki kuendelea kujibu kitu yaishe kabisaa; sababu hapa kuna waandishi wa habari wasije wakaninukuu vingine".

Maneno hayo ya Dk. Somi yakazua kelele zaidi katika ukumbi huo kwani vijana hao walitaka aendelee kujibu. Wakapiga kelele wakisema, "Tujibu! Tujibu!" " Endelea! Kwanini mmeandaa kongamano kama mlijua hamtajibu maswali?" " Laima mtujibu... Mnatuchanganya! Mnatuangamiza," wakasema kwa pamoja bila simile.

Huku akionesha dalili za kutoka mbele ya vijana hao, akasema tena ," Nimesema yaishe tena nasema yaishe. Tena yaishe hapa hapa kwa kuwa nyie mnaonekana mnafahamu . Nimesema hata kama kuna mtu mwingine ana swali kama hilo, basi sintalijibu." Hata hivyo baadhi ya vijana hao baada ya Dk. Somi kumaliza muda wake wa kutoa mada yake walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine na kufanya ukumbi huo ubaki na vijana wachache. Akifungua kongamano hilo, Diwani wa kata ya Makumbusho, Anzumuni Jumanne, aliwataka vijana hao kutoiga mienendo isiyofaa na akataka wajue kuwa wapo katika kipindi kibaya chenye magonjwa hatari kama ukimwi

"acheni kuiga vitu visivyo vizuri na maana halafu mnadai kuwa mnaenda na wakati. Kwenda na wakati ni kule kujifunza yale ambayo yapo katika chati kama vile utumiaji wa kompyuta," aliasa.

Akisoma risala ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mratibu wa Kongamano hilo, Emmanuel Kiogolo alisema kuwa, lengo la kongamano hilo ni kuwataka vijana kuwa tayari kubadilika na kuachana na matendo maovu yakiwemo ya madawa ya kulevya.