Jimbo la Kahama lapata Askofu Mpya

l Mhashamu Shija ajiuzulu kwa uzee

l Mteule asema ingawa ni kazi ngumu anasema NDIYO

Na Josephs Sabinus

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amemteua Makamu wa Mkuu wa Shirika la Mapadre wa Maisha ya Kitume katika Kazi ya Roho Mtakatifu(ALCP/OSS), Padre Ludovick Joseph Minde, kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Askofu Mteule Minde, anashika nafasi ya Askofu wa sasa, Mhashamu Matthew Shija, ambaye amejiuzulu baada ya kufikia umri wa kupumzika ambao kwa mujibu wa Sheria za Kanisa Katoliki, ni miaka 75.

Kwa mujibu wa taarifa toka kwa Afisa Habari wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Raphael Kilumanga, Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania, ulitangaza uteuzi huo wa Baba Mtakatifu, Jumamosi iliyopita (Mei 26, 2001).

Askofu Mteule alizaliwa Januari 12, 1954, huko Kibosho katika Jimbo Katoliki la Moshi ambako pia, alipata Sakramenti ya Ubatizo.

Mhashamu Minde ni mtoto wa sita kati ya 11 wa familia ya Mzee Joseph Ndasika Minde(92)na marehemu mama yake Bibi Maria Joseph Mukure.

Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alijiunga na Seminari Ndogo ya St. James, Moshi. Mwaka 1979, alijiunga na Shirika la mapadre wa maisha ya Kitume katika Kazi ya Roho Mtakatifu(Apostolic Life Community of Priests in the Opus Spritus Sancti).

Alichukua masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho, Moshi na Masomo ya Teolojia katika Seminari Kuu ya Segerea iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Juni 26, 1986, alipata daraja Takatifu ya Upadre.

Mwaka 1990, Baba mtakatifu alipotembelea Tanzania kwa ziara ya kichungaji, alitoa nafasi ya masomo kwa mapadre watano wa Tanzania kwenda Roma kwa masomo ili baadaye, warudi kusaidia katika malezi ya vijana katika Seminari Kuu.

Kwa bahati nzuri, Askofu Mteule Minde, alikuwa miongoni mwa mapadre hao watano waliopata nafasi ya kwenda Roma kwa masomo.

Tangu mwaka 1990 hadi 1995, alikuwa Roma akijifunza Maandiko Matakatifu na kujipatia Shahada ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Urbaniano, Roma.

Amewahi kuwa Mlezi Msaidizi katika nyumba ya Malezi ya Sanya Juu-Sabuko kati ya miaka ya 1986 na 1988.

Baadaye, kati ya miaka 1988 na 1990, alifanya kazi ya uchungaji katika Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria katika Jimbo katoliki la Shinyanga, akiwa Paroko Msaidizi.

Aidha, kati ya mwaka 1995 na 2000, alikuwa mmoja wa washauri katika Halmashauri Kuu ya Shirika lake na pia, kuanzia mwaka 1995 hadi 2000, amekuwa Mlezi, Mwalimu wa Maandiko Matakatifu na Baba wa Kiroho katika Seminari Kuu ya Segerea.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar-Es-Salaam, siku chache baada ya kutangazwa uteuzi wake, Askofu Mteule alisema, "Utume huu mpya nimeupokea kwa mshituko mkubwa kwani katika maisha yangu, sikutarajia hasa ukitilia maanani uzito wa wadhifa wa kiaskofu katika Kanisa na jamii ya watu."

"...Lakini kwa vile ninaamini kuwa ni Mungu mwenyewe aliyenikabidhi utume huo, ninasema NDIYO; nikiweka imani na matumaini yangu yote kwake kwa kuwa ndiye anayefahamu ugumu wa kazi hii lakini akaniteua," alisema Mhashamu Minde.

Askofu Mteule alisema ili afanikishe utume wake katika Kanisa, anaomba ushirikiano na wanajimbo wote na waamini wa Kanisa la Tanzania kwa jumla.

"Ninaomba tuwe na ushirikiano wa dhati kati yetu sisi wenyewe na huku tukishirikiana na Mungu na kanisa zima kwani tukiwa na ushirikiano wa kina kati yetu na Mungu na Kanisa, yote yanawezekana," alisema.

Serikali inayochuma pesa kwa wagonjwa haifai - Pengo

l Ashauri namna ya kupata pesa bila kuua wagonjwa

Getrude Madembwe na Neema Dawson

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema serikali yoyote inayochuma pesa kutokana na magonjwa katika jamii, haifai na ni heri itafute pesa hiyo kwa kulipisha kodi katika vinywaji.

Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati wa uzindunzi wa kliniki(MCH) na jengo la wazazi katika Zahanati ya Parokia ya Mtakatifu Camillius iliyopo Yombo, katika Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-Salaam.

Alisema huduma ya afya haina budi kutolewa bila ya waathirika kutozwa pesa kwa kuwa mtu hawezi kuishi bila kukumbwa na maradhi tofauti na vitu vingine ambavyo anaweza kuvikwepa hivyo, ni muhimu ikatolewa bila malipo ili kila anayeathirika, aipate kirahisi.

"Ukitoza kodi kwenye pombe mtu anaweza akaacha asiinywe au hata sigara; akaamua kuacha. Sasa ukitoza katika huduma ya afya, mtu anaweza kuacha kuugua?" alihoji.

Aliongeza kuwa, "Na hata hiyo serikali ikiwa inafikiria kupata pesa kwa njia ya kuwalipisha watu wake ili wanunue dawa wanapoumwa, inakuwa haiwatendei haki wananchi wake".

Alisema Kanisa Katoliki na taasisi nyingine za kidini, linatoa huduma za afya na matibabu si kwa ajili ya kujipatia pesa au faida, bali kwa ajili ya kuwasaidia watu.

Alishauri serikali yoyote inayotegemea malipo ya huduma ya afya, taasisi au watu binafsi, kuacha kufanya hivyo na badala yake, watoe huduma hizo kwa nia ya kuisadia jamii.

Hata hivyo, Kardinali Pengo alisema anamshukuru Mungu kwa kuwa hali hiyo ya Serikali kutaka ijipatie pesa kutokana na kuwahudumia kiafya wananchi wake, bado haijafika Tanzania.

Aidha, Kardinali Pengo aliwataka waganga wa zahanati hiyo, kufanya kazi kwa moyo wa upendo na kujitolea na kuzingatia maadili ya kazi yao, badala ya kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi yao binafsi.

"Mfanye kazi hii kwa kujitoa mhanga kwani waganga wanatakiwa wawe na moyo wa upendo na wasitafute wawe na mishahara mikubwa kwani hakuna mtu ambaye anaridhika na mishahara yetu; labda wafanyabiashara," alisema Kardinali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam, Dk. Deo Mtasiwa, alilipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango wake mkubwa katika kuisaidia wananchi katika huduma mbalimbali ikiwamo huduma muhimu ya afya.

Dk. Mtasiwa alizishauri taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kuwa Kanisa hilo, halilengi maeneo ya mjini tu, bali hutoa huduma zake kwa jamii nzima wakiwamo waishio maeneo ya mbali na miji.

Alisema inatumia nguvu zake nyingi, kuhakikisha inaweka mfumo imara wa kurekebisha mazingira ili yawe mazuri na yanayowezesha uanzishwaji na utoaji wa huduma za taasisi mbalimbali za dini na za kibinafsi kwa misingi ya usawa.

Jengo hilo ni miongoni mwa kumi yanayotarajiwa kujengwa kwa ufadhili wa baraza la Maaskofu Katoliki la Italia. Yatagharimu shilingi milioni 700. Wafadhili wengine wa mradi wa majengo hayo ni Serikali ya Italia, Wilaya ya Bolzano iliyopo Italia pamoja na watu wengine binafsi.

Uzindunzi wa kliniki(MCH) na jengo la wazazi katika Zahanati ya Parokia ya Mtakatifu Camillius iliyopo Yombo jijini Dar-Es-Salaam, ulifanyika Mei 29, mwaka huu.

Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele kuisaidia jamii katika utoaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwa ni pamoja na afya, maji na elimu. Wananchi wengi wamekuwa wakisifia ubora wa huduma hizo.

Umoja wa Mapadre Wazalendo Rulenge walaani mauaji ya PADRE

Na Padre Ben Rwegoshora, Rulenge

UMOJA wa Mapadre Wazalendo Tanzania (UMAWATA), Jimbo Katoliki la Rulenge mkoani Kagera, umelaani mauaji ya kikatili ya Paroko wa Parokia ya Marusangamba, Padre Evarist Bakanyendera(39).

Padre Bakanyendera aliuawa na majambazi Aprili 17, mwaka huu, katika kijiji cha Murubanga wilayani Biharamulo, wakati akienda kutoa huduma za kichugaji kigangoni.

Katika mkutano wa umoja huo uliofanyika hivi karibuni Jimboni Rulenge, chini ya Mwenyekiti wake, Padre Patric Shumbusho, mapadre hao wakiwa na Mkuu wa Jimbo,

Askofu Severine NiweMugizi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), walisema wamesikitishwa vikali na mauaji hayo sambamba na mengine yanayofanyika sehemu mbalimbali duniani.

Waliyalaani mauaji, kero na vitendo vingine viovu vinavyofanyika katika mikoa ya Kagera na Kigoma kutokana na uwepo wa wakimbizi katika maeneo hayo. "Pamoja na kwamba tunaamini wakimbizi hufanya matendo hayo maovu kwa ushirikiano na raia, bado lawama kubwa zinaelekezwa kwa wageni hawa kwani tangu kufika kwao, matukio ya mauaji, uporaji na ubakaji yamekuwa mengi huku yakiongezeka siku hadi siku katika maeneo yetu," walisema mapadre hao katika tamko lao lililosainiwa na Mwenyekiti huyo, Padre Shumbusho.

Wajumbe wa kikao hicho wameiomba Serikali kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kuhakikisha wanarejesha usalama wa raia na mali zao.

Marehemu Padre Bakanyendera, alipata daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1999. Aliuawa kikatili na majambazi kwa kunyongwa karibu na kambi ya wakimbizi ya Kitali.

Majambazi hao walipora pikipiki ya Padre huyo pamoja na vifaa vyote alivyokuwa navyo kwa ajili ya ibada. Watu kadhaa wakiwemo wakimbizi toka kambi ya Rukole wanashikiliwa na polisi mkoani Kagera wakituhumiwa kuhusiana na tukio hilo.

'Mbona hakuna viwete wanaoombewa wakatupa magongo?'

l Wanaoponya wadaiwa kutembea na watu wao kufanya danganya toto

Na Josephs Sabinus

"HAO wanaojiita wana uwezo wa kuponya; mbona Muhimbili, Bugando kuna wagonjwa wengi, wanateseka na kujifia wenyewe; kwanini hao waponyaji kama kweli wanafanya kazi ya Mungu; hawaendi huko wakawasaidia, badala yake wanaitisha mikutano na kukusanya pesa?"

" Ni nani hapa ambaye ndugu yake alikuwa mlemavu au kiwete; akapelekwa kuombewa akawa mzima? Au ni nani anamfahamu jirani yake au yeyote aliyepelekwa kuombewa kwenye hiyo mikutano, akashikwa kichwa akatupa magongo yake na mpaka sasa ni mzima?"

Hayo yalisemwa na Katibu wa Parokia ya Mtakatifu Maurusi- Kurasini iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Bw. Cletus Majani, wakati akitoa mada katika semina ya wazazi na wasimamizi wa watoto wachanga waliobatizwa Jumapili iliyopita. Semina hiyo ilifanyika Jumamosi jioni kanisani hapo.

Alisema ni makosa kwa Wakristo hususan Wakatoliki, kudanganywa na badala yake kukubali na kufuata imani nyingine ambazo alisema kimsingi, ni sawa na kuchezewa maigizo.

"Unajua kinachofanyika ni watu kuitana hapo kwenye mikutano, hao wanaojiita waponyaji, wakaja na watu wao wanaojua kucheza maigizo, wakaigiza vizuri kuwa ni viwete, wakawadanganya muda huo tu, wakaondoka.

Wengine ni wataalamu wa kuigiza; ni kama wacheza disko, wanaigiza kama viwete na wanacheza kweli utadhani kiwete anataka kuanguka; sasa ndivyo watu wanavyodanganywa," alisema Majani na kuongeza,

"...Wanakuja na watu wao, wanawadanganya kisha wanakusanya pesa. Ndio maana hata uzunguke unalia katika maeneo unayoishi huwezi kumpata mtu ambaye aliombewa; akaponywa sasa akatupa magongo yake; nani."

Aliwahimiza wazazi na wasimamaizi wa watoto wanaobatizwa kujua wajibu wao katika kumlea na kumfanya mtoto kukua katika malezi na maadili safi ya Kikatoliki. "... msimamizi una jukumu kubwa kuona mtoto anakua, anaoa au kuolewa katika madili safi. Pia ni jukumu lako kuona anadumu katika imani. Unatakiwa umlee asivute bangi, asitumie dawa za kulevya na ni wewe unayetakiwa kuona mtoto analelewa vizuri sio anatoka hapa, kesho tunamkuta anacheza shoo kwenye disko," alisema.

Akizungumzia umuhimu wa mishumaa Majani alisema, "... si kwa ajili ya matumizi ya mwanga pindi umeme unapokatika bali hata kama mtoto ameugua usiku, uwashe, piga magoti muombe Mungu akuangazie umpe dawa na huu mshumaa hautakiwi kuisha kwa kuwa ukiwasha mwingine kwa kuutumia, unakuwa umeugawia huo mwingine baraka sawa na huo ulio nao sasa."

Akizungumzia dawa za asili, Katibu wa Parokia alisema kimsingi hazuii kutumia dawa za jadi bali akinachosisitizwa ni kuzitumia kwa utegemezi wa nguvu za Mungu, badala ya kuwatumaini waganga wa jadi kama miungu na wapiga ramli kwani ni hatari na wanavuruga uhusiano ndani ya wanajamii

Jogoo wa Askofu Mtega auzwa laki 1.2/=

l Waamini wachanga milioni 2.7 kukarabati kanisa

Na Padre Simplisius Kapinga, Songea

WAKRISTU wa Kanisa Katoliki Songea mjini wamechanga shilingi milioni 2.7 kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa la Mtakatifu Matias Kalemba Murumba, lililopo mjini Songea.

Kati ya fedha hizo, shilingi milioni moja na roho ni fedha taslimu na milioni moja na nusu ni ahadi. Mchango huo ulifanyika Jumapili ya Sikukuu ya Kupaa kwa Yesu Mbinguni katika ibada iliyoongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu, Norbert Mtega.

Katika ibada hiyo, Askofu Mkuu Mtega alipewa zawadi ya jogoo aliyenunuliwa papo hapo kwa shilingi 120,000/=. Fedha hizo, ziliingizwa kwenye mfuko wa kukarabati kanisa hilo.

Kwa mujibu wa Paroko wa Kanisa hilo, Padre Paul Chiwangu, ukarabati wa kanisa hilo unatazamiwa kugharimu shilingi milioni 11. Fedha hizo zote zinatazamiwa kuchangwa na Wakristo wa kanisa hilo ambao idadi yao ni 43,000 katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Kanisa la Mtakatifu Mathias Kalemba, lilijengwa miaka 33 iliyopita. Mwaka jana lilifanyiwa ukarabati wa ndani. Mwaka huu utafanyika ukarabati wa nje na mazingira yanayozunguka kanisa hilo.

Akiwakaribisha waamini kwenye ibada hiyo, Askofu Mkuu Norbert Mtega aliwaambia Wakristo kuwa, Kanisa katika Jimbo la Songea, limekwishatimiza miaka 100 toka Wamisionari wa kwanza waanze kutangaza Habari Njema kwa watu.

Aliwambia kuwa, katika kipindi hicho, Wakristo wa Songea; kizazi hadi kizazi, wangetazamiwa wajifunze kutegemeza Kanisa la mahali na hata kutuma Wamisionari mahali pengine.

Kumbe kwa hali halisi, inaonekana Wakristo hawajafikia hatua ya kujitegemea na hata kutegemeza Kanisa la mahali. Kiongozi huyo wa Kanisa, aliwataka Wakristo wa Kanisa la Songea kujitoa mhanga katika kutegemeza Kanisa lao.

Unganisheni nguvu kuwalea watoto- Wito

Na Shelter Kindoli, TIME

MWINJILISTI wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) anayejulikana kwa jina la Mama Manyonga amewataka Watanzania kuwa na umoja katika kuwalea watoto katika adabu na maaadili mema ya Kikristo

Alitoa wito huo alipokuwa akihubiri katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Watoto iliyofanyika katika Kanisa la Ukonga jijini Dar-Es-Salaam Jumapili iliyopita.

Kila mwaka Kanisa hilo huadhimisha Sikukuu ya Watoto kwa ajili ya kuwelea katika maadili ya Ki-Mungu.

"Kulea watoto sio kazi ya mzazi moja bali ni kazi ya kila mtu kwa sababu watoto wetu ni Kanisa la kesho," alisema .

Mwinjilisti huyo aliongeza kuwa, uwezekanao wa kuwapata watoto wenye tabia njema na wenye kuifaa jamii utakuwepo endapo tu, jamii itakuwa tayari kushirikiana katika kuwalea .

Alisema wazazi na walezi wengine wanalojukumu kubwa kuwagharamia malezi bora ya watoto na pia, kuyaheshimu malezi hayo na hata kuwaheshimu watoto wao kama navyoelezwa katika Maandiko Matakatifu.(Waefeso 6:4).

"Watoto wanahitaji heshima kubwa toka kwa wazazi kama vile wazazi wanavyohitaji kupata heshima toka kwao," alisema.

Alisisitiza kuwa endapo jamii itazembea katika kuwapa watoto maadili mema, hasara ambayo ni matokeo ya hali hiyo, itakuwa kwa jamii nzima na sio mtu au familia binafsi.

Alibainisha kuwa vijana wengi wanaojihusisha na vitendo viovu katika jamii, ni wale ambao hawakupata malezi katika jamii zao na pengine hata wanajamii hawakuasaidiana katika jukumu hilo na matokeo yake, ni usumbufu kwa jamii yote kama unavyoonekana siku hizi.

"Vijana wasiopata maadili mema ya Ki-Mungu kupitia kwa wazazi na walezi wao, huipa jamii hasara kwani wanapoamua kuiba mara nyingi huibia jamii na wala sio wazazi wao au walezi wao wenyewe. Tazama sasa jamii imekuwa katika hali ya mashaka kutokana na mambo maovu yanayofanyika nchini siku hadi siku," alisema .

Aliishauri jamii kuwa na ushirikiano katika kuwalea watoto katika msingi mzuri ili kutokokeza maovu na hivyo, kuifanya nchikuwa katika hali ya utulivu na amani.

'Upungufu wa mapadre usikwamishe Injili'

Leocardia Moswery na Elizabeth Steven

Upungufu wa mapadre na ongezeko la waamini, havipaswi kuwa kigezo cha kushindwa kutangaza Injili kwa kuwa kila mmoja wa waamini anao wajibu wa kutekeleza jukumu hilo; Amesema Askofu Method Kilaini.

Mhashamu Kilaini, aliyasema hayo Jumamosi iliyopita, katika ibaada maalumu ya kuadhimisha Siku ya Mwenyeheri Isdori Bakanja.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika Kituo cha Kitaifa cha Halmashauri Walei kijulikanacho kama Bakanja TEC Laity Centre katika eneo la Ukonga- Sitakishari jijini Dar-Es-Salaam.

Mhashamu Kilaini alisema licha ya jimbo kukabiliwa na upungufu wa mapdre kutokana na wingi wa waamini, hali hiyo haipaswi kamwe kuwa kikwazo cha kusababisha kushindwa kuitangaza Injili kwa kuwa kila mmoja anawajibika katika kazi hiyo.

"Hapa Dar-Es-Salaam, tunashukuru tunao wakristo wengi sana lakini, mapadre tulio nao ni wachache; hawatoshi. Lakini, pamoja na uchache huo wa mapadre, napenda kuwaambia kuwa na nyinyi mnayo nafasi kubwa ya kuwa mapadre katika kuihubiri Injili hasa mkianzia katika ngazi ya familia zenu," alisema Mhashamu Kilaini.

Aliwahimiza waamini wote kuiga ujasiri wa Mwenyeheri Bakanja wakizingatia mambo muhimu matatu yaani kuwa na imani, kuonesha imani hiyo na kuigharimia imani hiyo.

Mhashamu Kilaini pia, aliwahimiza waamini kutokuwa waoga katika kuiishi imani yao na hivyo, kuwa tayari kuteseka na ikibidi kufa wakiitetea imani.

Siku hiyo, Kituo cha Walei cha Bakanja kilikusanya shilingi 1,085,000 kwa njia ya kuuza vitu mbalimbali ikiwa kama njia ya kuchangia mfuko wake.

Hata hivyo, habari zaidi zilizopatikana toka kwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Utume wa Walei wa TEC Padre Nicolous Segeja, muda mfupi kabla hatujaenda mitamboni zilisema kuwa hadi sasa tayari shilingi 1,132,000 zimekwisha patikana pamoja na vifaa vyote vya misa.

Baadhi ya bidhaa zilizouzwa kwa njia ya mnada ni pamoja na kanzu, za aina nne, altare iliyonunuliwa kwa shilingi 135,000 na Bi. B. Mkwawa, kabati ndogo ya vitabu vya misa na Misale.

Vingine ni Kitabu cha Masomo. Kitabu cha Kumbukumbu ya Mwenyeheri Bakanja kilinunuliwa kwa shilingi 15,000 na Bi. A. Machibya.

Kanda ya video ya Kiswahili iliuzwa kwa shilingi 30,000 wakati ya Kiingereza iliuzwa kwa shilingi 35,000. Altare ya kioo iliuzwa kwa shilingi 30,000.

Siku hiyo kulikuwa na kusimikwa msalaba juu ya paa la nyumba, kubariki jiwe la msingi, altare, Biblia na mavazi ya misa yatakayotumiwa na kituo hicho.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na waamini mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzani(TEC), Padre Pius Rutechura, wafanyakazi mbalimbali wa TEC pamoja na Kwaya ya Watakatifu Wote ya TEC ambayo ilitumbuiza siku hiyo, na viongozi wa Halmshauri Walei, ngazi ya taifa.

Wengine waliohudhuria ni viongozi wa Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA) ngazi ya Kitaifa, mapdre mbalimbali kutoka maeneo ya Segerea na Ukonga pamoja na marafiki na majirani mbalimbali wa kituo cha Bakanja.

Askofu Kilaini ahimiza umuhimu wa jumuiya ndogondogo

l Mtoni wapania kuvuna maendeleo

Na Gabriel Mduma

ASKOFU Msaidizi Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Methodius Kilaini amesema maendeleo yoyote ya parokia hayana budi kwenda sambamba na uimarishaji wa jumuiya ndogondogo za Kanisa.

Akizungumza na wajumbe mbalimbali waliokuwepo katika Ukumbi wa Kiroho wa Mbagala jijini Dar-Es-salaam, katika hafla ya chakula cha hisani, kilichoandaliwa na kigango cha Mtoni Kijichi Jumapili iliyopita, Askofu Kilaini alisema endapo uimarishaji wa Jumuiya ndogondogo utafanyika, utarahisisha mipango mbalimbali na utendaji wa Kanisa.

"Siku zote nasema ujenzi wa kanisa, ofisi na nyumba za mapadre, unawezakana kama tutajenga jumuiya ndogondogo na kuziimarisha", alisema.

Aidha, Askofu Kilaini alisema jumuiya zitakazoanzishwa na parokia, hazina budi zishirikishwe katika masuala mbalimbali ya kuziendeleza parokia ili ziwe na nguvu ya kumtangaza Kristo.

Katika chakula hicho cha hisani kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya parokia na nyumba ya padre ya parokia tarajiwa ya Mtoni Kijichi, Askofu Kilaini aliinadi picha yake kubwa ya ukutani iliyonunuliwa kwa shilingi 600,000/=.

Katika hafla hiyo ambayo ni ya mwanzo kufanikisha azma ya ujenzi huo, kiasi cha fedha taslimu kilichokusanywa kilikuwa ni shilingi 635,000/= wakati ahadi mbalimbali zilikuwa ni shilingi 325,000.

Ujenzi huo unahitaji shilingi milioni 80 kukamilika.

Kigango cha Mtoni Kijichi kilianzishwa 1990, kikiwa na jumuiya tatu na kuendeshea shughuli zake za ibada katika majengo ya Benki Mbagala 1996.

Kigango hicho kina waamini wapatao 1604. Kimejiwekea malengo ya muda mrefu katika kujiimarisha ikiwemo ujenzi wa hosteli yenye gorofa tatu sambamba na ujenzi wa zahanati na shule ya watoto wadogo.

Waamini wa Msimbazi wapongezwa

Na Pelagia Gasper

WAAMINi wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Msimbazi katika Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-salaam, wamepongezwa kwa kuwa wanaonesha mwamko na moyo wa kulitegemeza Kanisa badala ya kuwategemea wamisionari na hivyo, kuinua hali ya maendeleo katika parokia hiyo.

Akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake katikati ya juma, Paroko wa Parokia Katoliki ya Msimbazi katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Padre Ambrose Mosha, alisema kutokana na waamini kuelewa umuhimu huo, wameleta maendeleo mbalimbali katika Kanisa ikiwa ni pamoja na kupambana na umaskini.

Akitoa mfano wa Parokia yake ya Msimbazi katika kupiga vita umaskini, Padre Mosha alisema kuwa, Oktoba 15, mwaka jana, ilianzisha mfuko maalumu wa Mshikamano kwa ajili ya kupambana na umaskini.

Mfuko huo unajulikana kama "Msimbazi Parish Solidarity Fund",na ulianzishwa siku ya Jubilei ya Familia Kuu Dunia ambapo waamini waliiadhimisha kiparokia na mzinduzi wa mfuko huo alikuwa Padre Julian Kangalawe(kwa sasa ni Monsinyori).

Alisema mfuko huo kwa sasa unasaidia katika kuwahudumia wasiojiweza katika parokia hiyo na akawapongeza waamini wa Parokia ya Msimbazi kwa kuuanzisha na kuuendeleza.

Alisema katika mazungumzo hayo ofisini kwake kuwa, mwaka huu mfuko huo unatarajia kupata zaidi ya shilingi milioni 60 endapo kila muumini atatoa mchango wake wa shilingi 500 kwa mwezi.

Alisema fedha hizo zikipatikana, zitawekwa benki na faida itakayopatikana itatumika kuwasaidia maskini na wasiojiweza hata katika parokia nyingine.

Akizidi kuzipongeza juhudi za waamini wake katika kujiletea maendeleo, Padre Mosha alisema wamepanua shule ya ushonaji ambayo kwa sasa inaweza kupokea wanafunzi 180 badala ya 70 kama ilivyokuwa awali.

Alisema kwa kushirikiana na kituo cha kusaidia walioathirika na UKIMWI (PASADA), parokia yake ina mpango wa kuunda kikundi cha kuelimisha jamii juu ya kanuni za afya hasa jinsi ya kukabiliana na UKIMWI.

Katika kuendeleza Jubilei Kuu ambayo ilimalizika Januari 6, mwaka huu, uongozi wa parokia ya Msimbazi umeweka mikakati ya kutoa semina kuanzia ngazi ya familia, jumuiya na hatimaye parokia nzima.

Alisema uchache wa mapadre na makatekista, ni tatizo kubwa katika kukabiliana na ongezeko la waamini wa Kikatoliki na kwamba hata hivyo, wanapambana na tatizo hilo kwa njia ya kuwaelimisha waamini juu ya tatizo.

Alisema anawapongeza waamini kwa kuwa wanaliona na kulitambua.

Parokia ya Msimbazi yenye zaidi ya miaka 47, awali ilikuwa chini ya Mapdre Wabenediktini na baadaye, Wakapuchini. Kwa sasa inazo Jumuiya 75 na vigango 9.

Vigango vya parokia hiyo ni Buguruni, Bungoni, Mchikichini, Sharif- Shamba, Mivinjeni, Ilala-Utete, Kigogo A, kariakoo na Kigogo B.

Wanaume wahimizwa kuwa makini yatima wasiteswe

l VIWAWA Kawe wapata uongozi mpya, wataka kondomu zipuuzwe

Na Getrude Madembwe

WANAUME katika jamii wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto yatima katika familia zao, hawatumikishwi, hawateswi wala kunyanyaswa na badala yake, wanachukuliwa kama sehemu kamili ya familia.

Pia, waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani wameshauriwa kuwachukulia wafanyakazi hao kama watoto wao na kuwaelekeza wanapokosea badala ya kuwapa adhabu kali zikiwamo kuwachoma moto, kuwatukana matusi makali na kuwasimanga hali ambayo inawaathiri kiafya mno kisaikolojia.

Ushauri huo umetolewa na Paroko wa Parokia ya Kawe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre Yudas Shayo wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake jijini Dar-Es-Salaam katikati ya juma lililopita mintarafu maisha ya yatima katika familia.

Alisema tabia ya baadhi ya wazazi wa kiume kutowajali yatima katika familia zao kwa kuondoka na kurudi nyumbani bila kuwajalia hali wala maisha yao wanapokuwa nyumbani, ni kichocheo kwa watoto hao kupata manyanyaso bila wanyanyasaji kuhofia uovu wao kujulikana kwa yeyote.

Alisema ni makosa kwa akina mama ambao wamejijengea moyo wa chuki kwa watoto yatima na wengine walio chini ya uangalizi wa malezi yao, kwa madai kuwa hawakuwazaa na hivyo, huenda siku za mbele watoto hao hawatawajali wala kuwakumbuka kwa mema.

Padre Shayo alisema ni muhimu wazazi wa kiume wakawa karibu ili kujua hali ya maisha ya watoto anaolelewa nao kwani baadhi ya akina mama wanatabia ya kuwanyanyasa watoto wasio wazaa pindi mwanaume anapokuwa hayupo nyumbani na anaporudi, hujifanya kuonesha mapenzi.

Alisema hali hiyo huwaongezea ukiwa na upweke watoto wa namna hiyo.

Alishauri jamii ielimishwe zaidi juu ya kuwapa upendo watoto yatima sawa na waliokuwa wanaupata kwa wazazi wao badala ya kuwanyanyasa hali ambayo inawaongezea machungu katika maisha.

Wakati huo huo: Vijana Wakatoliki wafanyakazi (VIWAWA), parokiani Kawe, wamewashauri vijana kupuuza ushauri unaotolewa na baadhi ya watu na taasisi juu ya matumizi ya kondomu kama njia ya kuepuka maambukizi ya UKIMWI na badala yake, waepuke kabisa vitendo vya kujamiiana kabla na nje ya ndoa.

Katibu wa VIWAWA parokiani hapo, Bi. Prisca James, alisema kwa kuwa hivi sasa vimeibuka vikundi mbalimbali vinavyotoa ushauri juu ya mambo mbalimbali tofauti, ni vema jamii ikawa makini kuchambua yenye faida, na yanayoweza kuiangamiza kimwili na kiroho.

"Kusema eti kijana atumie kondomu kujikinga na UKIMWI ni hatari. Kinachotakiwa ni kumuomba Mungu akupatie mchumba ili mfunge ndoa naye siyo kudanganyana kwa kondomu kwa kuwa zinakiuka maadili ya ki- Mungu sio kinga sahihi ya UKIMWI," alisema.

Bi. Prisca alishika wadhifa huo kufuatia uchaguzi wa kawaida uliofanyika Jumapili iliyopita katika ukumbi wa parokia hiyo ambapo mwenyekiti aliibuka kuwa Deodatus Mtenga, akisaidiwa na Joseph Dismas. Katibu Msaidizi aliibuka kuwa Agnes Mweza. Lukrecia Byalushengo, alichaguliwa kuwa Mweka hazina akisaidiwa na Theresia Emmanuel.

Mwenyekiti Mstaafu wa VIWAWA parokiani, Frolian Chadade, alisema kwa kawaida VIWAWA hufanya uchaguzi kama huo baada ya miaka mitatu. Aliongeza kuwa wanatarajia kuanzisha miradi mbalimbali ili kuwasaidia vijana wasio na ajira parokiani hapo.

Majambazi wapora wafanyabiashara 14/=m wakienda mnadani

l dereva ajeruhiwa kwa risasi shingoni

Na Ndechongia Charles, Morogoro

WATU saba waosadikiwa kuwa ni majambazi, wamepora shilingi 14,530,000 toka kwa wafanyabiashara tisa waliokuwa wakisafiri kati ya mji wa Ifakara na kitongoji cha Itete Wilayani Ulanga katika mkoa wa Morogoro.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Christopher Shekiondo, amesema watu hao wakiwa na bunduki aina ya Shortgun, waliteka gari aina la Toyota Land Cruser lenye nambari za usajili TZ 88891 lililo kuwa na wafanyabiashara tisa waliokuwa wakienda mnadani.

Kamanda Shekiondo amesema tukio hilo lilitokea Mei 29, Mwaka huu, majira ya saa 7 mchana katika kijiji cha Makafuni Lupilo Wilayani Ulanga.

Alisema majambazi hayo yalitokomea msituni baada ya kupora fedha hizo.

Kamanda Shekiondo alisema dereva aliyekuwa akiendesha gari lililotekwa Bw. Taji Mohamed (60) alijeruhiwa vibaya kwa risasi shingoni na katika mkono wake wa kushoto.

Alisema dereva huyo amelazwa katika hospitali ya Mtakatifu Fransics ya Ifakara huku hali yake ikiwa mbaya sana.

Kwa mujibu wa Bw. Shekiondo, hadi sasa hakuna mtu aliyekwishakamatwa kuhusiana na uporaji huo na kwamba, polisi walayani Ulanga wanaendelea na msako.

Tume ya Haki na Amani Arusha yavalia njuga mauaji ya mtoto mlemavu

Na Festus Mangwangi, Arusha

OFISI ya Tume ya Haki na Amani ya Jimbo Katoliki la Arusha imelaani vikali na kuamua kuvalia njuga, mauaji ya hivi karibuni ya mtoto mlemavu Lazaro Simanga wa Kigango cha Mundarara kinachohudumiwa na parokia ya Ngorongoro.

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo jimboni Arusha, Bw. William Kessy amesema katika mazungumzo yake na waandishi wa habari ofisini kwake kuwa, Tume inayaona maauji hayo kama unyanyasaji na ukiukaji wa haki za binadamu.

Hata hivyo, Bw. Kessy amesema hajapata taarifa rasmi na ya kina toka kwa Mjumbe wa Tume ya haki na Amani wa kigango hicho.

"Mara niliposikia kuhusu tukio hilo, niliandika barua kwa wenyeviti wa parokia zote jimboni na nakala kwa maparoko; nikiwataka wawajibike kutoa taarifa za kina kuhusu masuala mbalimbali ya uvunjaji wa haki na amani iwe kwa makusudi au kwa kutojielewa", alisema Bw. Kessy.

Alisema ofisi yake imechukua muda kulitolea tamko tukio hilo kwa kuwa kwa mujibu wa taratibu za kiutendaji, ofisi haiwezi kutoa tamko rasmi au kufanya lolote kabla ya kupata taarifa rasmi za kina na za kweli hasa kwa maandishi toka ngazi inayohusika.

"Jamii inapaswa kuelimishwa na kusaidiwa kuhusu ukiukwaji wa haki za mwanadamu siyo tu, jimboni au mkoani Arusha, bali pia nchini," alisema na kuongeza,

"Tunatarajia kuendesha semina mbalimbali juu ya haki na amani jimboni mara baada ya uchaguzi wa viongozi katika jumuiya ndogondogo za Kikristo, vigango na parokia utakapokamilika".

Inadaiwa kuwa mnamo, Aprili 26, mwaka huu, Bw. Simanga Ole Kauwe, alimwua kikatili mtoto wake, Lazaro Simanga kwa kuwa ni mlemavu. Kufuatana na taarifa zinazofanyiwa uchunguzi na polisi mkoani hapa, mauaji hayo yanayokiuka haki za binadamu, yanadaiwa kufanywa na watu watatu ambapo mpaka sasa baba mzazi na mtu wa pili, wameshakamatwa na wanaendelea kuhojiwa na polisi.