Papa ataka dunia ichague kati ya mema na mabaya

YEREVAN, Armenia

BABA Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili, hivi karibuni aliungana na Mkuu wa Kanisa la Armenia kuupa changamoto ulimwengu wa leo kuchagua kati ya mema na mabaya, aliposema kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kutatua matatizo yanayoikabili dunia hivi sasa.

Katika taarifa iliyosainiwa baada ya misa iliyofanyika huko Etchmiadzin ambao ni mji mtakatifu wa kanisa la Armenia, viungani mwa jiji la Yerevan,bila kugusia mvutano wa Marekani na Afghanistan, walisema hiyo ndiyo njia pekee ya kutatua migogoro.

"Hasa hasa leo, masuala tete na changamoto zinazoikabili jumuiya ya kimataifa zinahitaji uchaguzi kati ya mema na mabaya, giza na nuru, ubinadamu na unyama, ukweli na uongo," alisema Baba Mtakatifu katika taarifa ya pamoja na Gregin wa Pili.

Hata hivyo, lengo kuu la ziara ya siku sita ya Baba Mtakatifu iliyomfikisha katika taifa lenye waislamu wengi la Kazakhstan na baadaye Armenia ambalo ni taifa la kwanza la kikristo, lilikuwa ni amani kati ya Waislamu na Wakristo.

Huko Kazakhstan, alizungumzia jinsi Kanisa Katoliki linavyoheshimu dini ya kiislamu, na huko Armenia aliomba upatanisho uwepo kati ya madhehebu mbalimbali ya kikristo.

Katika misa ya asubuhi ya siku ya mwisho ya ziara yake, Baba Mtakatifu aliwahubiria wakatoliki na wafuasi wa Kanisa la Armenia wapatao 10,000. Kanisa la Armenia lilijitenga na Kanisa Katoliki tangu karne ya sita.

"Namwomba Bwana atusamehe kwa makosa yaliyopita yaliyotufanya tusiwe na umoja na upendo unaovuka mipaka yote," alisema katika mahubiri yake yaliyosomwa kwa niaba yake na padre wa kiarmenia.

Baba Mtakatifu pia alizungumzia historia ya Armenia iliyojaa machungu, uvamizi na ukandamizaji, mambo yaliyosababisha vifo vya mamilioni ya watu.

Taarifa ya pamoja ya viongozi hao wawili iligusia pia mauaji ya halaiki waliyofanyiwa Waarmenia katika karne ya 20, yaliyofanywa na majeshi ya Ottoman toka Uturuki, pia mateso ya utawala wa Kisovieti wa miaka 70.

"Maangamizi ya Waarmenia wakristu milioni 1.5, katika kinachoitwa mauaji ya kwanza ya halaiki ya karne ya 20 na maangamizi yaliyofuatia chini ya utawala wa kiimla wa Urusi ya Kisovieti ni misiba ambayo bado iko hai katika kumbukumbu za kizazi kilichopo leo," ilisema taarifa ya pamoja.

Suala hilo ni kama shitaka kwa Uturuki ambayo inakanusha vikali kuendesha mauji hayo ya halaiki dhidi ya Waarmenia. Inabishania idadi ya Waarmenia waliouawa na kusema pande zote ziliathirika baada ya dola ya Ottoman kusambaratika wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.Hata hivyo, Baba Mtakatifu hakuzungumzia suala hilo moja kwa moja na kuliita mauaji ya halaiki.

Kenya yaondoa raia wake Pakistan

NAIROBI, Kenya

KENYA imeanza kuwaondoa raia wake waishio Pakistan, kwa hofu ya kutokea kwa vita katika eneo hilo na nchi jirani ya Afghanistan.

Kwa mujibu wa gazeti la East African Standard, Wakenya kadhaa walianza kurejea nyumbani baada ya kutakiwa kufanya hivyo na serikali yao.

Serikali ya Kenya imeamua kuwaondoa huko kutokana kuwepo na tishio la Marekani kuivamia Afghanistan wakati wowote kuanzia sasa. Pakistan inapakana na Afghanistan.

Miongoni mwa watu wa mwanzo kuwasili ni wanafamilia 14 wa wafanyakazi katika ofisi ya ubalozi wa Kenya waliokuwa wakiishi jijini Islamabad.

Mara baada ya kuwasili kwao Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, watu hao walisema wana furaha kurejea nyumbani.

Kutokana na kuondoka kwao, sasa ubalozi wa kenya huko Islamabad umebakiwa na wafanyakazi saba tu.

Wakenya hao walipokelewa na Meya wa Kisumu, Shakeel Ahmed Shabir ambaye alisema alikuwa akimtarajia mwanawe mwenye umri wa miaka tisa, ambaye mama yake anafanya kazi katika shirika moja la misaada huko Afghanistan.

Kwa mujibu wa Ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje, Simeone Nyakundi, kuna Wakenya wengine 155 wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali vya Pakistan.