Make your own free website on Tripod.com

Ijue nchi ya Vatikani

NCHI hiyo inamvutia kila msomi kutokana na upekee wake, yaani, kiongozi wake ni Baba Mtakatifu.

Vatikan ni nchi ndogo sana kuliko nchi yoyote huru duniani.

Huwezi kuelewa historia yake bila kuelewa historia ya uhusiano wake na Baba Mtakatifu.

Kihistoria, umuhimu wa Baba Mtakatifu ulianza pale Watawala wa Kirumi walipoanza kuishi katika mji wa Costantinople katika karne ya mwanzo. Warumi waliposhambuliwa na watu kutoka Asia, ni Baba Mtakatifu aliyekuwa mkombozi wao.

Mfano mzuri, ni Baba Mtakatifu Leo Mkuu, aliyezuia maadui kuteka Roma mwaka 452. Mwaka 754, Baba Mtakatifu Stefano wa Tatu, alimzuia Mfalme wa Walombardia kuiteka Roma.

Alimshinda kwa msaada wa Mfalme wa Ufaransa. Ushindi huo uliongeza mipaka ya utawala wa Baba Mtakatifu.

Nguvu za utawala wake ziliongezeka wakati Ulaya iliposambaratika kwa sababu ya matatizo ya kisiasa na tishio la maadui kutoka Mashariki. Wazungu walimkimbilia Baba Mtakatifu.

Walimwona kama mkombozi wao dhidi ya maadui wao. Aidha, walimwona kama mtawala anayeweza kuwaunganisha kwa misingi ya imani ya Kikristo. Ndiyo maana, hakuna mtu aliyepinga mchango wake katika siasa za kimataifa. Aliweza kuhukumu kesi mbalimbali hata zile zisizohusu Kanisa.

Mwaka 1859, ukubwa wa eneo lake la utawala, lilikuwa maili 17,218 za mraba katika nchi ya Italia. Watu 3,124,688 walikuwa chini ya utawala wake. Kwa bahati mbaya mwaka 1870, alishambuliwa na majeshi ya Italia na kukimbilia Vatikani.

Tangu hapo, hadi mwaka 1929, Mababa Watakatifu walikuwa wafungwa wa hiari ndani ya Vatikani.

Baba Mtakatifu Pio wa Kumi, hakukubali kupoteza utawala huo wa kisiasa kwa sababu kungeathiri uhuru wa Kanisa. Aidha, kungeruhusu mwingizo wa sheria zinazopinga Kanisa na taasisi zake.

Ndiyo maana mnamo Februari 11,1929 kulifanyika mapatano kati ya Kiti cha Kitume na Serikali ya Italia. Sehemu ya kwanza ya mapatano hayo ilikuwa Serikali ya Italia kutambua uhuru wa nchi ya Vatikani chini ya utawala wa Baba Mtakatifu.

Vatikani ina eneo la eka 108.7 za mraba yaani, nchi ndogo sana kuliko nchi yoyote huru duniani. Ndani yake, kuna Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Makao Makuu ya Vatikani, Makumbusho ya Nyumba ya Sanaa, Maktaba, utangazaji na magazeti, redio, bustani, posta, benki na ofisi.

Kwa kuwa ni Makao Makuu ya Ulimwengu ya Kikatoliki, Vatikani ina wafanyakazi au waajiriwa wengi zaidi kuliko raia. Idadi ya waajiriwa inazidi 4,000. Mnamo mwaka 1974,Vatikani ilikuwa na raia au wenyeji 300. uraia wa mtu unatokana na kuwa na ofisi ndani ya Vatikani.

Sehemu ya pili ya mapatano ya 1929 kati ya Kiti cha Kitume na Serikali ya Vatikani inasema kuwa Kiti cha Kitume kitakuwa na utawala juu ya Kanisa la Mtakatifu Paulo nje ya kuta, Ikulu ya Gandolfo, eneo la Mahakama ya Kanisa (Rota), Makao Makuu ya Uenezaji wa Injili, Idara ya mafundisho ya Imani, Kanisa la Mtakatifu Yohana Laterani, Kanisa la Mtakatifu Maria Mkuu, eneo la Mtakatifu Kalisti, na eneo la Idara inayoshughulikia makanisa ya Mashariki.

Mengine ni pamoja na Chuo Kikuu cha Gregoriana, Chuo cha Biblia na baadhi ya nyumba zinazotumiwa na wanafunzi Wakatoliki wanaosoma katika vyuo vikuu vya Roma. Sehemu hizi zote haziwezi kuchukuliwa na serikali ya Italia na wala kulipa kodi Serikalini.

Rejea: PAZHAYAMPALLILT. A Commentary on the New Code of Canon Law, KJC Publications, Bangalore, 1985.

Imeandaliwa na David Mubirigi wa Seminari Kuu ya Segerea.

Baba Mtakatifu azuru parokia ya 296

Vatican City

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili wiki hii aliitembelea parokia ya 296 iliyopo mjini Roma.

Watoto walikuwa wa kwanza kumlaki baada ya kuvuka barabara ya parokia akielekea umbali wa mita 200 ambako ujenzi wa kanisa jipya unaendelea kwa heshima ya Mt. Edith Stein, Mwanafalsafa Myahudi, aliyeamua kubadili maisha yake na kujiunga na utawa wa Wakarmaliti na kufia Auschuitz.

Jirani mmoja wa karibu na eneo hilo Bi. Torre Angella, alisikika akimlalamikia Baba Mtakatifu juu ya kukosekana kwa huduma muhimu katika eneo hilo, Baba Mtakatifu alimtia moyo kufuatia ujenzi wa kanisa unaoendelea katika eneo hilo na kwamba litazinduliwa rasmi Desemba mwaka huu.

Baba Mtakatifu pamoja na wakaguzi wa eneo hilo aliadhimisha misa iliyohudhuriwa na watu zaidi ya 2000.

Alisema anamshukuru Mungu majaliwa yake kwani Ijumaa ya Mei 25, mwaka huu, alitimiza miaka 81.

Ingawa wakazi katika eneo hilo wameamua kusherehekea sikukuu kabla ya siku hiyo aliwataka wananchi katika eneo hilo kuchukua muda mwingi kujifunza maisha ya Mt. Edith Stein aliyetangazwa mwaka 1998.

Alilinukuu shairi aliloandika Edith mwaka 1933, akienda kuonana na Mama Mkuu wa Wakarmeliti huko Ujerumani akisema, "Shughuli na mihangaiko ya binadamu haitasaidia lolote, ila ukuu wa Mungu nami natamani kuushiriki."

Aliwapa Sakramenti ya Ekaristi watoto 8 akiwataka kuunganika na Kristo kila siku ya maisha yao hasa kwa kujiweka safi wakati wakishiriki Sakramenti ya Kitubio.

Maaskofu Hispania waipinga serikali mintarafu dawa za kutoa mimba

MADRID, Hispania

MAASKOFU Kusini mwa Hispania, wamepinga amri iliyotolewa na maofisa wa Andalucia inayotaka maduka yote ya dawa, yatoe huduma ya dawa zinazotumiwa wakati na baada ya kutoa mimba.

Taarifa iliyotolewa na maaskofu hao hivi karibuni, ilisema amri hiyo ya Serikali siyo ya haki na kwamba inakiuka haki za binadamu na sheria za nchi hiyo kuhusu mwanamke anayetakiwa kutoa mimba na kwa wakati gani.

Wamesema kuwa sasa taifa linafuata misingi inayokwenda kinyume na maadili ya jamii na kupuuza ukweli kwamba mwanadamu ni kiumbe maalumu anayestahili kulindwa kwa nguvu zote na kuheshimiwa.

Kwa muda wote, Kanisa Katoliki limekuwa likipinga kwa nguvu swala la utoaji mimba, uamuzi ambao katika baadhi ya maeneo duniani, limepitishwa na kutambuliwa kisheria.