Kanisa lawahifadhi watoto waliokuwa wakipigana vita

MAKEN,Sierra Leone

KANISA Katoliki nchini Sierra Leone limeanza kuwahifadhi watoto ambao walikuwa wakipigana katika kikundi cha waasi nchini humo.

Akizungumza na Shirika la Habari la Kimisionari la Misna ,Askofu wa Jimbo Katoliki la Makeni ,Mhashamu Giorgio Biguzzi alisema kuwa wasichana na wavulana 86 walikabidhiwa katika Shirika la Misaada la Kikatoliki (CARITAS) jimboni humo.

Shirika hilo limesema kuwa jimbo hilo limeandaa sehemu maalumu kwa ajili ya watoto hao kwenye shule ya sekondari ya Mtakatifu Francis huko Makeni.

Askofu Biguzzi alisema kuwa kukabidhiwa kwa watoto hao ni ishara ya matumaini nchini Sierra Leone.

Mhashamu Biguzzi aliongeza kuwa zaidi ya watoto 5000 wamekuwa wakitumiwa na serikali pamoja na waasi nchini humo.

"Watoto wengine 5000 wanatumiwa na waasi kama watumishi wao na wasichana wanatumiwa kwa ukahaba" alisema Askofu Biguzzi.

Tangu kuwekwa kwa mapatano ya kuacha vita kwa muda nchini Sierra Leone ,Julai mwaka juzi , Kanisa Katoliki limekuwa likisaidia kurudisha askari hao watoto katika maisha yao ya kawaida.

Mwaka jana Jimbo la Makeni lilitoa chakula, nguo pamoja na kuwasomesha watoto wapata elfu moja.

Wakristo Nigeria wampelekea malalamiko ya unyanyaswaji wa sharia Rais Obasanjo

KANO, Nigeria

CHAMA cha CAN ambacho kimeundwa na Wakristo wa Jimbo la Kaskazini mwa Nigeria la Zamfara kimedai kuwa kimepeleka malalamiko yake kwa Rais wa nchi hiyo,Olusegun Obasanjo ya kupinga madhara wanayofanyiwa waumini wake kutoka kwa vikundi vya Kiislamu katika eneo hilo.

Wawakilishi wa Chama hicho cha CAN katika jimbo la Zamfara ambako viongozi wake walitangaza sharia za kiislamu tangu mwaka jana, wametaja baadhi ya malalamiko hayo kuwa ni pamoja na kulazimishwa kuvaa mavazi ya Kiislamu kwa wanawake wote wa jimbo hilo, wakiwemo wale wa dini ya kikristo

Chama hicho kinadai pia kuwa serikali ya jimbo la Zamfara imeamuru pia maduka yote ya eneo hilo kufungwa wakati wa sala, hasa siku ya Ijumaa.

Msemaji wa Chama hicho cha Wakristo, David Mawashe amesema kuwa hatua hizo ni kinyume na ahadi za Gavana wa jimbo hilo Ahmed Sani kuwa utekelezaji wa sharia hizo za Kiislamu hautowahusu waumini wa dini nyingine.

Jimbo la Zamfara lenye wakazi wengi Waislamu, ni serikali ya kwanza ya kijimbo nchini Nigeria kujitangaza kuwa na mamlaka yanayofuata Sharia za kiislamu tangu kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini humo Mei mwaka juzi.

Rais Arafat alaani mauaji ya polisi

GAZA,Palestina

RAIS wa Wapalestina ,Yasser Arafat amekilaani kwa ghadhabu kubwa kitendo cha mauji kilichofanywa na vikosi vya Israel dhidi ya Polisi watano wa Palestina.

Arafat amekiita kitendo hicho kama kichafu na kisicho cha uadilifu na kwamba taifa la Wayahudi ndilo litakalochukua dhamana ya mauaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya mazungumzo yake na mjumbe maalumu wa Jumuiya ya Ulaya huko Mashariki ya Kati Bw. Miguel Moratinos,Rais Arafat alisema kuwa mmoja kati ya polisi hao waliouawa, alikuwa macho, lakini wengine wote walikuwa usingizini.

Amesema jambo la kusikitisha ni kwamba polisi hao walikuwa ni miongoni mwa polisi ambao kwa ushirikiano na vikosi vya Israel wamepewa jukumu la kulinda vituo vya upekuzi vya Kijeshi.

Umoja wa Mataifa kutuma wajumbe Afrika

BARAZA la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa litawatuma wajumbe wake katika ziara ya siku 10 barani Afrika kwa ajili ya kuangalia jinsi ya kuharakisha juhudi za kumaliza mgogoro wa vita vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliodumu kwa muda wa miaka mitatu sasa.

Mabalozi wa nchi 12 katika jumla ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama wataondoka Jumatano ijayo na kuzitembelea nchi zote zinazohusika katika mgogoro huo wa Kongo kwa kuanzia Johannesburg nchini Afrika Kusini na kumalizikia Kampala Uganda Mei 25 mwaka huu. Hatua muhimu ya duru hiyo itakuwa Mei 22 wakati ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa utakapokutana mjini Lusaka na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi sita zilizopeleka majeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na viongozi wa waasi wenye silaha wanaopambana na serikali ya Rais Joseph Kabila. Ujumbe huo utajadiliana na vikundi vilivyosaini Mkataba wa amani wa Lusaka juu ya utekelezaji wa ratiba kamili ya kuondolewa kwa majeshi ya wapiganaji na upokonyaji silaha wa vikundi vya wanamgambo wanaohusika pia katika mgogoro huo wa Kongo.