Make your own free website on Tripod.com

Papa ataka Waislamu na wakristo kusahau yaliyopita

DAMASCUS, Syria

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amewataka Waislamu na Wakristo kumuomba Mungu awasamehe na kuwawezesha kusahau tofauti zao na hivyo, kuanza maisha mapya ya umoja na mshikamano baina yao.

Aliyasema hayo alipokuwa Damascus nchini Syria katika moja ya maeneo aliyozuru katika ziara yake ya siku sita katika nchi za Syria, Ugiriki na Malta kufuata nyayo za Mtakatifu Paulo.

" Mara kadhaa Waisalamu na Wakristo wamekuwa wakiudhiana na kutuhumiana na sasa, tunahitaji kuomba msamaha kwa Mungu, na kusameheana sisi kwa sisi," alisema wakati akiwahutubia waamini wa Kikristo na Kiislamu, akiwamo Sheikh Mkuu wa Syria.

Hata hivyo, pamoja na wito wa Baba Mtakatifu, nchi za Syria na Islael zimejibizana maneno makali kuhusiana na ziara ya Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani.

Rais wa Islael alimuita Rais wa Syria kuwa ni mbaguzi kwa kumuambia Baba Mtakatifu kuwa Wayahudi ndio waliomsaliti Yesu na Nabii Mohamad.

Katika mwendelezo wa ziara yake akifuata nyayo za Mitume wa zamani wa Kikristo; Paulo na Yohane Mbatizaji, Papa alitembelea sehemu mbalimbali za kihistoria ikiwamo milima ya Golan, inayokaliwa na Waisrael mpakani mwa Syria.

Waislamu nchini Syria, walipinga vikali Papa kusali katika Msikiti mkubwa wa Damascus ambao zamani ulikuwa kanisa wakihofia kuwa hatua hiyo, inaweza kusababisha Utawala wa Vatican kuurejesha msikiti huo katika kanisa.

Serikali ya Syria imeipongeza ziara hiyo na kusema kuwa inachochea umoja na mshikamano.

Wakati huo huo: Katika ziara yake ya pili ya kitume katika nchi ndogo ya Malta yenye idadi kubwa ya Wakatoliki, Papa alisema Malta ni nchi ya kihistoria kwa kuwa Mtume Paulo alipita hapo akiwa mfungwa kuelekea Roma.

Nchi ya Malta, inakadiriwa kuwa na Waristo Wakatoliki wapatao 391,000 sawa na asilimia 91 ya wananchi wote.

Kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alitembelea nchi hiyo kati ya Mei 25 na 27, 1990.