Make your own free website on Tripod.com

Papa aanza ziara Ugiriki, Syria

VATICAN CITY

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, Ijuma iliyopita alianza ziara yake ya siku sita katika nchi za Syria, Ugiriki na Malta kufuata nyayo za Mtakatifu Paulo na amesema ana matumaini itazaa matunda ya ushirikiano.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani, amezungumzia matumaini yake katika ziara hiyo na ameomba sala ili kuifanikisha.

Amesma anaamini ziara yake nchini Ugiriki, itaimarisha ushirikiano baina ya Wakatoliki na Waorthodox na kwamba, ziara yake nchini Syria, itawasadia kwa kiasi kikubwa watu wanaoishi katika ulimwengu wa Kiislamu ambao ni karibu asilimia 90 ya watu nchini humo.

Papa anatarajiwa kuikamilisha ziara ya 93 ya kimataifa, nje ya Italia, Mei 9.

Alisema ana matumaini ziara hiyo itatoa changamoto ya Umoja wa Wakristo hususan Waorthodox na kuwa na mazungumzo na ushirikiano pamoja na ulimwengu wa Waislamu.

Baba Mtakatifu amesema anatumaini ziara yake nchini Syria na kwenye msikiti mkubwa wa Damascus, itaongeza nguvu ya mazungumzo ya kidini pamoja na wafuasi wa dini ya Kiislamu.

Lengo la ziara hiyo ni kufuata nyayo za Mtakatifu Paul. Mtume, alipobatizwa na kuwa Mkristo alipokuwa njiani akielekea Damascus.

Mkutano wa jamii za kitume waanza Roma

VATICAN CITY

JUMUIYA 114 za utume duniani zimeanza kikao chake mjini Roma ambapo wakurugenzi wakuu kitaifa, wanakutana kujadili maswala mbalimbali katika mkutano wa kawaida wa mwaka.

Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi 130 duniani chini ya Rais na Katibu Mkuu wa awamu ya nne, waliochaguliwa kuongoza jumuiya hizo.

Miaka iliyopita, idadi ya wanaohitaji iliongezeka kwa asilimia 10 na hii ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Monsinyori Bernad Prince ambaye pia anahusika katika kampeni ya Imani.

Hata hivyo, misaada nayo imeongezeka hasa kutoka katika nchi tajiri ulimwenguni tofauti na nchi masikini ambazo michango yao, imekuwa duni katika jamii.

Wakati wa mjadala kuhusu "Uchungaji", mjadala wa siku mbili Mei 3 na 5, Kardinali Joseph Tomko, ambaye ni Mlezi wa jumuiya hiyo, atakuwa na neno la ufunguzi kwa washiriki wa mkutano.

Baadaye, kuujadili barua ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliyoitoa kuzungumzia utume "Novo Millenio Ineunte".

Siku ya pili ya mkutano, washiriki watajadili mwanzilishi wa utume wa nne katika jumuiya ambapo Padre Paulo muasisi wa utume huo atatangazwa mwenyeheri.

MADAI YA NJAMA ZA KUMUANGUSHA MBEKI

Chama Tawala chakiri kuvurunda

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

CHAMA tawala nchni Afrika Kusini cha ANC, kimekiri kwamba kimeharibu taswira ya nchi hiyo kwa namna kilivyoshughulikia madai ya njama za kumuangusha Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.

Juma lililopita Waziri wa Usalama wa Nchi hiyo, Steve Tshwete, alisema katika mahojiano na Televisheni kwamba kulikuwa na njama za kumuangusha Mbeki na kwamba zilikuwa zikiongozwa na wanachama watatu wakuu wa ANC ambao wameonekana kuwa ni wapinzani wa Rais Mbeki.

Madai hayo yalizusha zahma kimataifa ambapo Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, aliwaunga mkono viongozi hao watatu wa ANC wanaoshutumiwa. Msemaji wa ANC, Smuts Ngonyana, amesema katika mahojiano yaliyoneshwa katika televisheni katikati ya juma kwamba, chama na serikali vimejifunza mafunzo magunu kutokana na namna madai hayo yalivyoshughulikiwa.

Tshwete alitarajiwa kutoa maelezo ya madai hayo Alhamisi iliyopita, mbele ya Kamati ya Bunge. Gazeti la Sunday Times la Afrika Kusini, lilichapisha nyaraka ambapo afisa mmoja wa ANC aliyesimamishwa, amedai kwamba kuna njama za kumdhoofisha Mbeki kwa kujaribu kumhusisha na mauaji ya mwaka 1993 ya mpinzani wake wa kisiasa, Chris Hani.

Marais maadui wa habari watajwa

l Wamo Zemin wa China, Khamenei na Taylor wa Liberia

NEW YORK, Marekani

KAMATI ya Kuwalinda Waandishi wa Habari imesema Rais Jiang Zemin wa China, Ali Khamenei wa Iran, na Rais Charles Taylor wa Liberia, ni miongoni mwa watu kumi duniani ambao ni maadui wakubwa wa vyombo vya habari.

Jiang amekuwa akitokea kwa mwaka mara tano mfululizo katika orodha ya kila mwaka ya Kamati hiyo ya kutetea waandishi wa habari ikiimarishwa kwa kiasi fulani, na hukumu za vifungo ambazo hivi sasa zimeifanya China, kuongoza duniani kwa kuwatia mbaroni waandishi wa habari.

Kamati ilitoa takwimu hizo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Katika taarifa yake, Kamati hiyo pia imesema Jiang anatumia rasilimali kubwa katika kuweka sera ya mtandao wa kompyuta kwa kuhofia uwezo wa mtandao kuvunja msimamo wa taifa wa kuhodhi habari. Hata hivyo, Jiang haongozi nafasi hiyo.

Nafasi ya juu katika orodha hiyo, inashikiliwa na Ayatollah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran ambaye mahubiri yake makali dhidi ya vyombo vya habari Aprili mwaka jana, yalichochea kampeni ya ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari vya mageuzi nchini Iran ambayo inaendelea hadi sasa.

Zaidi ya magazeti 30 yamepigwa marufuku nchini Iran na waandishi mashuhuri wasiiokuwa na upendeleo, wametiwa mbaroni.

Wengine wapya waliojitokeza katika orodha hiyo ni Rais Charles Taylor wa Liberia ambaye ametajwa kuwa amewafunga waandishi wa habari, anachuja utoaji wa habari na kuwalazimisha wengine waachane na kazi hiyo.

Kadhalika, ametajwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Vladimr Putini wa Rusia, na kiongozi wa kijeshi wa Colombia, Carlos Castano.