Maaskofu Wakatoliki Nigeria wasema Obasanjo hajafanya kitu

LAGOS, Nigeria

Kanisa Katoliki nchini Nigeria, limesema hadi sasa Serikali ya nchi hiyo haijafanya walichotarajia kutoka kwake kwani imeshindwa hata kudhibiti wingu la rushwa linalozidi kusambaa.

Maaskofu wa Kikatoliki nchini Nigeria, walisema katika taarifa yao ya hivi karibuni kuwa Serikali ya Rais Olusegun Obasanjo, hadi sasa haijafanya lolote kuona kuwa inaondoa kero za wananchi tangu iwe madarakani takriban miaka miwili iliyopita licha ya ahadi kemkemu ambazo imekuwa ikizitoa wakati wa kampeni zake.

Katika taarifa yao hiyo baada ya Mkutano wa Mwaka, maaskofu walisema kuwa wimbi la uhalifu, rushwa, upungufu wa mafuta na madhaifu mengine, ni uhakikisho kuwa serikali ya Rais Obasanjo imeshindwa kutimiza ahadi zake za kuondoa kero za wananchi.

Tamko hilo la maaskofu linawagusa wengi kutokana na kwamba serikali ya kiraia ya Rais Obasanjo, imeshindwa kuboresha hali ya maisha ingawa imeongeza uhuru wa kisiasa.

Maaskofu hao pia wameilaumu kasi ya kusambaa kwa Sheria ya Kiislamu ijulikanayo kama "Sharia" katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo.

Inaaminiwa kuwa sharia inapewa nguvu kwa madai ya kisiasa na kwamba serikali imekuwa kimya muda wote licha ya kuwataka viongozi wa kisiasa kujali maslahi ya watu wengine.

Walisema kuwa matumizi ya sheria kali za Kiislamu katika baadhi ya majimbo ya Kaskazini, hayafai na kamwe hayakubaliki.

Walisema wengi wa wanaoishi sehemu ambazo Sharia inatumika, kama sheria za jimbo, wanajisikia kuwa haki zao zimeangamia.

Majimbo kumi huko Kaskazini mwa Nigeria, yamehalalisha au kutangaza mipango ya kuhalalisha matumizi ya Sharia ambayo hujumuisha adhabu kali kwa ulevi, ukahaba na wizi.

Maaskofu hao wamesema kuwa baadhi ya watu wamelazimika kubadili dini kwa sababu ya sheria hiyo ya Kiislamu.

Taasisi za Kikristo kususia uchaguzi wa Bodi za vijiji Pakistani

ISLAMABAD, Pakstani,

IDARA ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu wa Pakstani kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Kikristo nchini Pakstani,wametangaza kugomea Uchaguzi wa bodi za vijiji uliopangwa kufanyika Machi 21, mwaka huu.

Kwa mujibu wa habari zilizotolewa na Shirika la habari la FIDES,Wakristo hao wamepanga kugomea uchaguzi huo baada ya kutokea hali ya ubabaishaji katika uchaguzi wa kwanza uliofanyika Desemba 2000, katika wilaya 18.

Habari zinasema wamefikia uamuzi huo kwa kuwa uchaguzi wa kwanza haukuwa huru wala wa haki.

Katika taarifa yao ya pamoja, wamedai uchaguzi wa kwanza haukuwa wa haki na ulikwenda kinyume na Katiba ya nchi kwa kuzipendelea taasisi zenye idadi kubwa ya watu na hivyo, kuendeleza upendeleo.

Uchaguzi huo wa machi 21, mwaka huu, unatarajiwa kuzihusisha wilaya 21..

Kwa hali ya sasa ya uchaguzi nchini humo tangu mwaka 1979 na kuwekwa kuwa utaratibu wa kudumu, Wakristo wanapaswa kuwachagua Wakristo wenzao ; halikadhalika Wahindu na wengine kufuatia imani zao.