Make your own free website on Tripod.com

Malezi kwa ajili ya mazungumzo : wajibu wa wakristo na Waislamu

Ujumbe kwa ajili ya kuhitimisha Ramadan 'Id Al- Fitr 141 A.H/ 2000 B.K

KATIKA kuhitimisha Ramadhani Mwadhama Francis Kardinali Arinze, Rais wa Tume ya Mahusiano ya Dini za Kikristo na zisizo za Kikristo ametuma ujumbe ufuatao:-

Marafiki Wapenzi Waislam,

1. Awali ya yote napenda kuwapeni matashi yangu mema kabisa kwa jili ya 'Id al - Fitr' inayohitimisha mwezi wa Ramadan.

Ramadan ni kipindi cha kutathimini mahusiano na Mwenyezi Mungu na mahusiano na wanadamu wenzetu; ni kipindi cha kumrudia Mwenyezi Mungu na kuwaendea kaka na dada zetu. Kufunga ni moja ya njia ya kumcha Mwenyezi Mungu, kuwasaidia maskini na kuimarisha vifungo vya familia na nguzo za urafiki. Kufunga ni aina ya malezi kwani kunafunua wazi wazi udhaifu wetu na kutufungua tuwe wazi mbele ya Mungu kusudi tuwe wazi kwa watu wengine.

Ingawa mfungo mnaoufanya ninyi una hali na nidhamu zake pekee, kufunga ni zoezi lililomo pia katika Ukristo na katika dini nyingine. Mwezi huu unatupatia fursa muafaka kujikumbusha, kama asemavyo Papa Yohane Paulo II, 'vifungo vya kiroho vinavyotuunganisha sisi sote'.

2. Mwaka 2001 umetangazwa na Umoja na Mataifa kuwa ' Mwaka wa Kimataifa wa Mazungumzo kati ya Ustaarabu mbalimbali.' Hii ni fursa kwetu ya kutafakari misingi ya mazungumzo, matokeo na matunda ambayo humo wanadamu wanaweza kuyavuna. Mazungumzo ya ustaarabu, ya tamaduni, mazungumzo kati ya dini na dini, si kitu kingine zaidi ya kukabiliana kibinadamu kwa lengo la kujenga utamaduni wa upendo na amani. Sisi sote tunaalikwa kuendeleza mazungumzo kama hayo kadiri ya mitindo yake mbalimbali, kama njia ya kutuwezesha kutathimini tamaduni na dini nyingine.

3. Wale wote wanaohusika na malezi ya vijana wanatambua fika hitaji la malezi kwa ajili ya mazungumzo. Wakati wa kuandamana na vijana kupitia njia za maisha, pawe na uangalifu kwa maandalizi yanayohitajika kwa ajili ya kuishi katika jumuiya iliyo na makabila mengi, tamaduni nyingi, na dini nyingi. Kabla ya yote, malezi hayo yana maana ya kupanua taswira yetu kwa upeo mpana zaidi ili tuwezeshwe kuona mbali zaidi ya nchi yetu, ya kabila letu, ya mapokeo ya utamaduni wetu, hata tukamwone mwanadamu kama familia moja pamoja na tofauti zake, na pamoja na matamanio yake. Haya ni malezi katika tunu za msingi wa hadhi, amani, uhuru na mshikamano wa binadamu. Malezi haya yanaamsha hamu ya kuwajua watu wengine, kuwezeshwa kushiriki mateso yao na kutambua vionjo vyao vya ndani kabisa. Malezi kwa ajili ya mazungumzo yana maana ya kukuza tumaini kwamba hali za magomvi zaweza kumalizwa kwa njia za kujitosa au mtu binafsi au kama kikundi.

Malezi kwa ajili ya mazungumzo si kwa ajili ya watoto na vijana tu, bali pia ni muhimu kwa watu wazima kwani mazungumzo ya kweli ni jambo endelevu.

4. Mwezi Oktoba mwaka 1999, ' Mkesha wa Millenia ya Tatu' kulikuwa na kusanyiko la dini mbalimbali. Ushirikiano miongoni mwa dini mbalimbali uliwaleta pamoja pale Vatikano takriban watu 200 kutoka mapokeo mbalimbali ya dini zipatazo 20. Waislamu 36 kutoka nchi 21 tofauti, walikuwepo na walishiriki kikamilifu katika maazimio na katika kuandika Ujumbe wa Mwisho. Ujumbe huu unakazia umuhimu wa malezi ya kuendeleza ufahamu , ushirikiano na kuheshimiana. Ujumbe huu unakazia umuhimu wa malezi ya kuendeleza ufahamu, ushirikiano na kuheshimiana. Ujumbe huo unaoorodhesha baadhi ya njia na nyenzo za kutekelezea malezi haya: kushikiza familia, kuwasaidia vijana katika kuunda dhamiri, utoaji habari za kweli juu ya dini mbalimbali, hasa katika vitabu vya kiada, kuheshimu vyombo vya habari kwa ajili ya dini mbalimbali ili kila moja iweze kujitambua kutokana na sura inayotolewa.

5. Ripoti ya mwisho ya Kusanyiko hilo ilihusu pia malezi kama ufunguo kwa ajili ya kukuza mapatano miongoni mwa dini mbalimbali kwa kuheshimu mapokeo mbalimbali ya dini. Je ni lazima kurudia kile walichokisema washiriki kuhusu malezi? Kwamba, zaidi ya ujuzi wa dini nyingine, malezi ni mlolongo unaomwezesha mtu kufikia kuwathamini watu wengine kwa njia ya usikivu halisi na heshima ya kweli. Je, hii siyo sanaa ile iliyo bora sana kujifunza kuheshimu na kupenda ukweli, haki, amani na upatanisho?

6. Sala na kufunga humwezesha kila mmoja wetu kutekeleza vizuri zaidid wajibu zetu, pamoja na ile kulea vizazi vichanga zaidi ya juu ya mazungumzo ya ustaarabu na dini. Mwenyezi Mungu atusaidie kujipatia lengo hili kwa njia iliyo bora kadiri iwezekanavyo. Kwa nafasi ya Id al - Fitr Mwenyezi Mungu awajalieni neema ya utulivu na fanaka, akawamiminie baraka maridhawa.tuna hakika kwamba Mwenyezi Mungu anaisikiliza sala inayoinuliwa kwake kutoka moyo ulio mnyofu: kwenu ninyi, kama vile kwetu sisi, Yeye ndiye Mungu aliye Mkarimu.

Kardinali Francis Arinze

Rais wa Tume ya Mahusiano ya Dini za Kikristo na zisizo za Kikristo.