Afisa wa Vatican asema Rwanda inategemea msamaha

KIGALI, Rwanda.

AFISA mmoja wa Vatican, amewataka Wakatoliki kuweka kando mara moja chuki zao na kufungua sura mpya ya Injili inayozingatia msamaha.

Afisa huyo alitoa wito huo wakati akifunga Sherehe za mwaka wa Uinjilishaji za kanisa nchini Rwanda hivi karibuni.

"Wakatoliki wa Rwanda, jifunzeni kujenga mwanzo mpya kutokana na majeraha yenu. Sio kwa ajili yenu pekee, bali Waafrika wote na kwingineko," alisema afisa huyo, Kardinali Roger Etchegary, wakati wa misa iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Mwaka 1994, Kardinali wa Kifaransa, alishuhudia kwa macho, machafuko mabaya katika historia ya Rwanda, wakati Waasi wa Kihutu walipowaua Watutsi wapatao 500,000, wengi wao wakiwa wamehifadhiwa katika makanisa ya Kikatoliki walipopewa hifadhi kama wakimbizi.

Kardinali Etechegary alisema ziara yake ya mwaka 1994 katika eneo la maafa, ilimuachia taswira yenye ushahidi wa mauaji ambayo haiwezi kusahaulika.

Akisisitiza kusameheana, Kardinali Etechegary, alisema kanisa linapenda wananchi wa Rwanda kutambua kuwa mzizi mkuu wa matatizo yanayotokana na machafuko, ni dhambi.

"Mpaka mtu afikie mzizi wa matatizo ya uovu, yatazidi kusambaa kama magugu na mwenye bustani atajaribu sana kuyaangamiza. Ni Mungu pekee anayeweza kuzivunja mbinu za uovu na kutusaidia," alisema.

Kardinali alisema Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alimtuma huko kuelezea matumaini ya Kanisa, yasiyo na mwisho juu ya Injili.

AMNESTY International yailaumu Israel kuwaua Wapalestina

SHIRIKA la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu, (AMNESTY International), limeilaumu Israel kwa kutumia nguvu nyingi kupita kiasi na hatimaye kuwaua watu wakiwamo wanamgambo wa Kipalestina katika kukabiliana na machafuko.

Machafuko baina ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina, yamedumu kwa takribani miezi 4 sasa.

Timu ya AMNESTY International, iliyotembelea Israel na Palestinahivi karibuni, iligundua kuwa, Israel iliuwaua watu kadha ambao ilishindwa kuwatia nguvuni kwa urahisi.

Shirika hilo limesema matumizi ya nguvu za kupita kiasi, yanahujumu utawala wa kisheria na kuchochea ghasia katika eneo hilo.

Koffi Annan achunguza wanaokula rushwa kwa wakimbizi Kenya

UMOJA WA MATAIFA,

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan, amesema umoja huo umedhamiria kuchunguza kwa kina tuhuma za maafisa wa shirika linaloshughulikia wakimbizi(UNHCR), za kupokea rushwa ili kuwapeleka wakimbizi walio Kenya katika nchi tajiri za Ulaya.

Habari zilizopatikana toka Umoja wa Mataifa zinasema, uchunguzi huo umekuwa mgumu na wa hatari zaidi kiasi cha kuulazimu umoja huo kuhamisha maafisa wake watatu kwenda nje ya nchi.

Habari zinasema hali hiyo imetokana na wengi wao kupokea vitisho vya kuuawa.

Amewaonya maofisa wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, kuhudumia wakimbizi nchini Kenya, kuwa watakaobainika kuwa hatiani kwa kupokea fedha hizo, ili kuwapeleka ng’ambo wakimbizi, watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kupigwa faini.

Umoja huo unafanya uchunguzi wa madai kwamba, baadhi ya maafisa nchini Kenya, wanapokea rushwa ya wastani wa Dola za Kimarekani 5000, ili kuwahamishia wakimbizi hao katika nchi za Australia, Canada pamoja na Marekani.

Inadaiwa kuwa magenge ya wahalifu nchini Kenya, yanahusishwa na kashfa hiyo na Umoja wa Mataifa umezitaka nchi zinazopokea wakimbizi wanaohamishwa ambazo ni Australia, Canada, Marekani na Uingereza, kusaidia katika uchunguzi huo.

Kenya inahifadhi kati ya wakimbizi 200,000 wengi wakiwa kutoka katika nchi za Somalia, Sudan, Ethiopia na maeneo ya Maziwa Makuu.

Kila mwaka Umoja wa Mataifa huhamisha kati ya wakimbizi 8000 na 11,000 wanaobainika kushindwa kurudi makwao kwa sababu mbalimbali, kuwapeleka ng’ambo.