Mashambulizi Somalia yatazaa magaidi zaidi - Askofu aonya

ROMA, Italia

WAKATI wasi wasi kuwa huenda Somalia ndiyo ikawa mlengwa wa mashambulizi ya Marekani dhidi ya ugaidi baada ya Afghanistan ukiendelea, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini humo ameyaonya mataifa ya Magharibi kutoishambulia nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kikatoliki (CNS), kiongozi huyo Askofu Giorgio Bertin alisema kuwa hii "itazalisha tu magaidi zaidi."

Askofu Bertin ambaye ni anaiongoza Djibout pia ni kiongozi wa kitume wa Somalia, aliliambia Shirika la Habari la Fides, kuwa "uingiliaji kijeshi utawasukuma tu watu kuunga mkono Waislamu wenye itikadi kali na kufanaya mambo kuwa mabaya zaidi."

"Ningewashauri viongozi wa mataifa ya Magharibi, kufikiri kwa makini na kutafuta njia nyingine za kupambana na ugaidi," alisema Askofu Bertin.

Wafuasi wa Osama bin Laden, ambaye anatuhumiwa kuhusika na mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani hapo Septemba 11, wanasemekana kufanya shughuli zao nchini Somalia.

Nchi hiyo pia ni nyumbani kwa makundi ya kiislamu yenye silaha ambayo yanatumaini kuunda taifa la kiislamu.

Askofu Bertin alisema kuwa makundi ya kiislamu "si kitisho kwa nchi za Magharibi."

"Ethiopia imekuwa ikipambana nayo kwa miaka sasa na mpaka sasa hayawezi kufanya shambulio lolote kubwa," alisema.

Aliongeza "jambo la pili ni kwamba wafuasi hawa wenye itikadi kali wamejitenga na jamii; Wasomalia hawayatambui."

Wakati huo huo: Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Bwana Donald Ramsfiel alikanusha taarifa kwamba nchi yake ina mpango wa kuishambulia kijeshi Somalia kwa tuhuma kuwa inauhifadhi mtandao wa kigaidi wa al Qaeda unaoongozwa na gaidi wa kimataifa mzaliwa wa Saudi Arabia Osama bin Laden.

Hata hivyo Bwana Ramsfiel alisema nchi yake inaituhumu na kuamini kwamba Somalia inaunga mkono ugaidi na kuwahifadhi magaidi, lakini akasema hiyo haimaanishi kwamba nchi yake ina mpango wa kuishambulia kijeshi Somalia.

Maaskofu wataka Padre aachane na kundi la waasi

ROMA, Italia

MAASKOFU wa Senegal, Guinea Bissau, Cape Verde na Mauritania, wamemtaka kiongozi mmoja wa kidini, kuachana na kundi la waasi analoliongoza likitaka kujitenga na Serikali ya Senegal.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la FIDES lenye makao yake huko Vatikan, Kiongozi huyo, Padre Augustine Diamacoune Senghor, ni Katibu Mkuu wa kundi la waasi la Majeshi ya Ukombozi wa Casamance linalopigana tangu mwaka 1982 likitaka kujitenga na Serikali.

"Tunaelewa kwamba Padre anapaswa kushughulikia haki na amani, lakini hiyo haiwezi kufanyika kupitia chama cha siasa na wala kupitia kundi linalopigana kwa kutumia silaha," maaskofu hao walisema katika wito wao.

Maaskofu walitoa wito wao tokea mji fulani huko Casamance katika mkutano wao wa kwanza kufanyika katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa habari kutoka Shirika hilo la Habari linalotoa habari za kimisionari, maaskofu waliamua kufanya mkutano wao katika eneo hilo ili kupeleka ujumbe kwa Serikali na waasi kuwataka wajitahidi kukaa pamoja na kufanya mazungumzo ya amani.

Habari zinasema, kujihusisha kwa Padre huyo Mkatoliki katika uasi kunisababisha matatizo kwa Kanisa.

Hata hivyo Padre huyo amekataa wito huo wa maaskofu na kusema ataendele kubaki kwenye kundi hilo la waasi.

Mapigano ya Waislamu, Wakristo yaua tisa Nigeria

Kanu, Nigeria

WATU tisa wamefariki Dunia kutokana na mapigano baina ya Waislamu na Wakristo katika Jimbo la Kanu nchini Nigeria

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mapigano hayo ya hivi karibuni yaliwashirikisha wanajeshi na polisi katia jimbo hilo.

Hata hivyo, vyanzo vya habari havikuthibitisha idadi kamili ya watu waliofariki katika mapigano hayo ya kidini.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mapigano ya kidini katika Jimbo la Kanu lenye Waislamu wengi tangu kuanzishwa kwa shari ya Kiislamu, mapema mwaka huu.

Maaskofu wataka tume kuchunguza ugaidi Bungeni

New-Delh, India

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini India, limeitaka Serikali ya nchi hiyo kuunda tume maalumu ya kuchunguza namna mashambulizi ya kigaidi yalivyofanyika katika jengo la Bunge la India.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Baraza hilo, Askofu Mkuu Vicent Cosesao, amesema kuwa Baraza lake limelaumu vitendo vya mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika katika jengo hilo, Desemba 13, mwaka huu.

Askofu Mkuu Cosesao ambaye ni Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la New-Delh nchini humo, alisema anashanga namna vyombo vya upelelezi vinavyoshindwa kupeleleza na hatimaye kugundua mpango mzima wa shambulio hilo.

Amesema Baraza lake linalaani vikali kila aina ya ugaidi na hususan shambulio hilo.

Makamu huyo wa Rais amesema magaidi watumie njia za mazungumzo ya amani kupata wanachodai badala ya kutumia hujuma.

Alhamisi ya Desemba 13, mwaka huu, magaidi walivamia jengo la Bunge la nchini India na kufanya shambulio .

Katika shambulio hilo, watu 12, wakiwamo wanajeshi 7 wa India, walipoteza maisha yao.