Make your own free website on Tripod.com

KUFUATIA AJALI ZA ELLIS PARK NA KOKSTAD

Maaskofu Afrika Kusini wawafariji waathirika

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

BARAZA la Maaskofu Wakatoliki nchini Afrika Kusini(S.A.C.B.C), limeungana na taifa zima kuwatumia salamu za rambirambi waliothirika na ajali za hivi karibuni zilizotokea katika maeneo ya Ellis Park na Koksta nchini humo.

Baraza hilo limeelezea kushitushwa kwake na taarifa ya matukio mawili makubwa na ya kihistoria ambayo pia ni ya kusikitisha kufuatia ajali hizo zilizopoteza maisha ya watu kadhaa na wengine kujerhiwa.

Kwa mujibu wa taarifa ziliyopatikana na kusainiwa na Rais wa Baraza hilo, Askofu Wilfred Kardinali Napier OFM, kwa pamoja Baraza hilo la Maaskofu linatoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu waliokufa katika mazingira magumu kufuatia ajali hizo.

Taarifa imesema Baraza hilo la Maaskofu linawaombea waliofariki wapokewe mikononi mwa Mungu na wale waliojeruhiwa katika ajali hizo zilizotokea wakati wa kipindi cha Pasaka, wapone.

Kardinali Napier katika salamu hizo, amesema Maaskofu Wakatoliki nchini Afrika Kusini, wanatoa salamu za pole kwa majeruhi waliolazwa hospitalini wakiwahakikishia maombezi ya sala ili waweze kupona haraka.

"Zaidi, tunawapa pole waliojeruhiwa na kuwahakikishia kuwa tunawaombea ili wapone haraka," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema kuwa, katika kufanya hivyo, maaskofu hao wanaungana na Yesu Mfufuka ambaye pia ni mponyaji katika kuwafariji na kuwaponya haraka majeruhi hao wa ajali zilizotokea nchini humo hivi karibuni.

Mvua yaangusha ukuta wa Kihistoria Roma

ROMA, Italia

MVUA kubwa iliyonyesha Jumapili ya Pasaka huko Roma, imeangusha ukuta wa kihistoria uliojengwa kulinda mji wa Roma dhidi ya maadui wa Ukatoliki mwishoni mwa Karne ya Tatu.

Sehemu ya ukuta huo wenye urefu wa mita sita, ilianguka Jumapili hiyo ya Pasaka kufuatia mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha na kuufanya kubaki na urefu wa ndoo.

Hakuna taarifa zozote za mtu kupoteza maisha wala kujeruhiwa kufuatia tukio hilo ingawa kuna habri kuwa wakati wa tukio, watu kadhaa walikuwa wakitembea katika eneo hilo lililopo nje kidogo ya jiji la Roma kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.

Mamlaka ya Roma imesema ukuta huo utajengwa upya lakini, kwa sasa utabaki umefungwa hadi uchunguzi wa chanzo cha kuanguka kwake, utakapokamilika.

Habari zaidi zinasema sehemu ya ukuta iliyoanguka ilifanyiwa ukarabati karibu miaka 400 iliyopita na ukuta huo ulijengwa mwishoni mwa karne kama tatu zilizopia baada ya waamini Wakatoliki kutishiwa kushambuliwa na watu wasioamini dini upande wa Kaskazini wa mjini mwa nchi ya Italia.

Mashariki ya Kati bado kwawaka moto

TEL AVIV, Israel

GHASIA za Wapalestina dhidi ya Israel, bado zinaendelea licha ya mashambulizi ya Jeshi la Israel katika maeneo ya Ukanda wa Gaza.

Wiki iliyopita wapiganaji wa Kipalestina wamekuwa wakivishambulia vikundi vya askari wa Kiyahudi. Mashambulizi hayo yametokea saa chache baada ya Jeshi la Israel kutangaza kumaliza mashambulizi yake katika ukanda huo.

Katikati ya juma lililopita, Rais George Bush wa Marekani alimpigia simu, Waziri Mkuu wa Israel, Ariel Sharon na habari zilizopatikana baadaye zilisema wamekubaliana kuwa, Israel iache mashambulizi dhidi ya Wapalestina.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Mary Ellen, alisema kuwa Bush na Sharon walikubaliana kuwa mashambulizi hayo, yatakoma mara moja.

Hata hivyo, Rais wa Syria, Bashar Al- Assad, amesema hatapuuza mashambulizi yaliyofanywa na ndege za Israel katika vituo vyake vya kijeshi Kusini mwa Lebanon.

Mashambulizi makali ya Waisrael katika maeneo ya Wapalestina yalianza Jumatatu, wakati askari wa Israel walipokalia eneo la kilomita 2.5, Mashariki mwa Ukanda wa Gaza.

Hadi sasa kwa kipindi cha takriban miezi sita, ghasia katika maeneo ya makazi ya Wapalestina zimekwisha sababisha watu zaidi ya 470, wengi wakiwa Wapalestina, kupoteza maisha.