Vatican yazicharukia nchi zinazounga mkono utoaji mimba

l Maaskofu wafurahia kukamatwa aliyemuua daktari aliyetoa mimba

NICARAGUA,

VATICAN imezitaka Marekani na nchi nyingine zinazounga mkono utoaji mimba, kutambua kuwa hakuna mwenye haki ya kuzuia kuzaliwa kwa mtu mwingine kwa kuwa maisha ya mtu yapo mikononi mwa Mungu.

Mwanadiplomasia wa Vatican ambayo ameanza vita ya dunia kupinga vikundi vinavyounga mkono utoaji mimba, aliyeko Umoja wa Mataifa, Askofu Mkuu Renato R. Martino, amesema kuwa Vatican inapinga vikundi vyote duniani vyenye lengo la kutawanya agenda hiyo aliyoiita ya kuua dunia.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, Askofu Mkuu Renato ambaye ni Mwakilishi wa Vatican katika Umoja wa Mataifa, ametoa kauli hiyo wakati wa misa katika sherehe maalumu ya Siku ya Mimba iliyoandaliwa na Serikli ya Nicaragua iliyofanyika Machi 25.

Nicaragua huadhimisha sherehe hiyo kila Machi 25.

Watu 25000, walihudhuria misa hiyo wakiwamo viongozi wa ngazi za juu serikalini na viongozi wa juu katika jamii.

Wakati huo huo: Maaskofu nchini Marekani, wametoa pongezi zao kufuatia kukamatwa kwa mhusika wa mauaji ya daktari aliyetoa mimba katika kesi inayofahamika kama, "Buffalo Abortion Doctor".

Msemaji wa Maaskofu hao wa Marekani, amesema Kanisa linalaani matumizi yoyote ya vurugu katika kukomesha vitendo haramu vya utoaji mimba.

Mtuhumiwa wa mauaji ya daktari aliyehusika kutoa mimba katika Kituo cha Wanawake cha Buffalo, mwaka 1998, Bw. James Cork (46), alikamatwa Machi 29, Mwaka huu na Polisi wa Ufaransa walioshirikiana na Polisi wa Upelelezi wa Marekani (FBI).

Mtuhumiwa alipelekwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji.

Chama cha Kutetea Uhai Tawi la Kongamano la Maaskofu Wakatoliki wa Marekani, kimesema maisha ya binadamu yana thamani ya pekee na kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kuruhusiwa kuua.

Makanisa 13 Yerusalemu yataka Wapalestina, Waisraeli wapatane

JERUSALEMU

MAASKOFU 13 wa makanisa mbalimbali ya Kikiristo nchini Yerusalemu, wametoa wito wa pamoja wakiutaka kumalizika mgogoro uliopo baina ya Waisraeli na Wapalestina kwani unazidi kuathiri vibaya maisha ya maelfu ya wananchi.

Kama maandalizi ya Siku ya Pasaka, viongozi hao wa makanisa walitoa wito huo wakizitaka Serikali za Israeli na Palestina, mamlaka za kisheria na viongozi mbalimbali duniani wakiwamo wa kidini, na watu wote wenye mapenzi mema, watumie uwezo walio nao kutetea maisha ya raia wanaoishi Nchi Takatifu wakiwamo Wakristo, Waislamu na Wayahudi.

Walisema wanaamini kumalizika kwa machafuko hayo yaliyodumu kwa miezi kadhaa sasa, kutatokana na jitihada za pande mbili zinazopingana, kuwa tayari kuheshimiana, kukubaliana na kutambua haki za kila upande huku wakitambua utu na thamani ya uhai.

Katika ujumbe huo, maaskofu wamebainisha kuwa, jitihada za kimataifa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati, hazina budi kuungwa mkono hasa kwa kuzingatia kuwa zinalenga kuimarisha usalama wa watu.

CARITAS yabaini Benki ya Nigeria kuuza wanawake

Nigeria.

SHIRIKA la Misaada la Kikatoliki la CARITAS nchini Italia, limebaini kuwa, kazi ya kuuza wanawake wa Kinigeria kama malaya, inaendeshwa na Benki ya Nigeria.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, shirika hilo hivi karibuni lilionesha ushahidi wa wasichana mbalimbali wadogo ambao waliokolewa katika utumwa huo na Msaidizi wa shirika moja linaloongozwa na Padre Erasto Benzi.

Mkurugenzi wa kikundi cha CARITAS kinachopinga uuzwaji wa wanawake ambaye aliwaokoa wasichana tisa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kutoka kwenye mikono ya wahuska, alisema kuwa, karibu 10 au 12 wanaojitolea, wanahatarisha maisha yao wanapojaribu kuwaokoa wanawake hao.

Kazi hii ni hatari kiasi cha kupelekea waokoaji wanaojitolea kutopenda majina yao yajulikane na pia, wao wenyewe kutopenda kujulikana.

Waokoaji hao wa CARITAS, huwa wanaenda Mashariki ya Soleno, mara mbili kwa kila wiki kwa ajili ya kuunda urafiki na wasichana hao wa Kinigeria na wa Ulaya Mashariki ambao ni malaya.

Wasichana hao malaya ni wa rika tofauti na wenye umri mkubwa, ni wenye miaka 23, wakati mwenye umri mdogo ni mwenye miaka 14.

Habari zinasema waokoaji hao walianza kushituka walipoona matawi ya Benki ya Nigeria yamefunguliwa katika Pwani ya Selono ambapo wanawake ambao wanalazimishwa kuuza miili yao, ni lazima wafungue akaunti katika benki hizo.