Make your own free website on Tripod.com

Baba Mtakatifu sasa kuzuru Ugiriki, Syria Mei

VATICAN CITY

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, Mei 4 hadi 9, mwaka huu, anatarajia kuzuru nchi za Ugiriki, Syria na Damascus.

Habari zilizopatikana toka Shirika la Habari la FIDES, akiwa katika ziara hiyo, Papa atakutana na maaskofu wa huko ili pamoja na mambo mengine, atajadili hali ya Kanisa Katoliki na namna inavyoedelea katika nchi hizo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Papa ataondoka Roma Ijumaa ya Mei 4, mwaka huu yapata saa 2:30 kuelekea Ugiriki, ambako atatembelea sehemu mbalimbali.

Siku itakayofuata saa 5:45, asubuhi Baba Mtakatifu anatarajiwa kupanda ndege kuelekea Damascus na Syria. Anatarajiwa kurudi Roma Mei 8, mwaka huu.

Habari za hivi karibuni zilisema, Kanisa la Kiorthodox la Ugiriki limekubali ombi la uwezekano wa Baba Mtakatifu, kuzuru Ugiriki na tayari Vatican ilisema inapanga kutangaza utaratibu wa safari.

Msemaji wa Baba Mtakatifu, Joaquin Navarro- Valls, alisema ni matumaini ya Vatican kuwa ombi la kutembelea Ugiriki, litapokelewa.

"Kutokana na uamuzi wa leo, pia kwa umuhimu wake katika ekumeni, umekidhi matarajio ya Baba Matakatifu, tunatumaini yatapokelewa kwa kauli ya neema,"

"Ni matumaini yetu kuwa hija ya Papa kiroho katika nyayo za Mtakatifu Paulo kama yalivyokuwa matamanio, itatangazwa hivi karibuni," alisema Machi 7, mwaka huu.

Maaskofu Wakigiriki 79 wa Kanisa la Kiorthodox la Sinodi Takatifu, walipiga kura kuidhinisha mwaliko wa serikali ya Ugiriki kwa Baba Mtakatifu ikisisitiza kuwa, Papa angetembelea nchi hiyo ya Waorthodox tu kama mhujaji na si vinginevyo.

Askofu Mkuu Paul Fuad Tabet, ambaye ni Mwakilishi wa Kidiplomasia wa Baba Mtakatifu nchini Ugiriki, aliuita uamuzi huo kuwa ni tukio la kihistoria na kwamba unawakilisha Umoja wa Kikristo.

Hata hivyo, alisema ilikuwa mapema mno kusema tarehe kamili ya ziara hiyo ya Baba Mtakatifu.

"Bado kuna vitu vingi vya kufanya lakini, tunatumaini kwamba atakuja hivi karibuni maeneo ya Athens", Askofu Mkuu Tabet, aliliambia Shirika la Habari la Italia (ANSA).

Katika barua yake, Kanisa la Kiorthodox limesema kwamba, katika barua yake ya Februari 9, mwaka huu, iliyoandikwa na Askofu Mkuu Tabet, Baba Mtakatifu aliomba ruhusa kufanya hija katika eneo hilo ambapo Mtakatifu Paulo alihubiri.

"Papa aliomba kujulishwa kama ziara yake ingeweza kuondoa tofauti katika Kanisa letu," ulisema waraka wa Kanisa hilo la Kiorthodox.

Kwa mujibu wa jarida litolewalo na Shirika la Habari la Kanisa Katoliki la Catholic News Services (CNS), Baba Mtakatifu alisema angependa kutembelea maeneo ya Athens kama sehemu ya hija yake inayoendelea ki-Biblia aliyoianza wakati wa Mwaka Mtakatifu wa 2000.

Parokia, Majimbo sasa kuwasiliana kwa mtandao

NEWYORK, Marekani

HUKO Amerika, imeanzishwa huduma ya bure ya mtandao inayosaidia parokia na dayosisi mbalimbali, kupata habari kwa ajili ya magazeti na pia, kuvutia uchapishaji wa matangazo.

Habari zilizopatikana zinasema, huduma hiyo ijulikanayo kama "Yellow Pages dot net; ina lenga kukuza na hata kuongeza idadi ya watu wapatao milioni moja, watakaolisaidia Kanisa kifedha na kuwawezesha kuongoza familia za Kikatoliki kujiendesha zenyewe kibiashara.

Pia, parokia za Kikatoliki, dayosisi na mashirika ya misaada, wanaweza kuorodhesha habari zao katika mtandao huo kwa ajili ya kuangaliwa.

Mifano iliyotolewa inaonesha kuwa, mashirika ya misaada ya Kikatoliki yanaweza kupatikana kwenye mtandao wa www/dot/Catholic Yellow Pages/dot net.

Pia, kuna mtandao wa www/The Florida Catholic/dot/DRG, ambalo ni gazeti la Kikatoliki litolewalo kila wiki. Gazeti hili, ndilo pia huchapisha Catholic Yellow pages.

Baba Mtakatifu azungumzia sayansi, imani

VATICAN CITY,

VYUO vikuu vimeelezewa kama sehemu muhimu kwa jamii kujiamini katika misingi ya sayansi na imani.

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amesisitiza umuhimu wa vyuo vikuu na kusema lazima viwe sehemu muhimu ya jamii kujiamini kimawazo kwa kujua na kutenganisha umuhimu wa kila mmoja na wakati wake baina ya sayansi na imani.

Baba mtakatifu aliyasema hayo mwanzoni mwa juma alipokutana na wanachama 120 wa chuo kikuu kimoja huko Vatican.

Amesema kuwa heshima siyo lazima kwake lakini, ni ishara ya uaminifu na upendo kati ya dini na sayansi na kwamba, ni matunda bora ya ushirikiano.

Papa awatia nguvu wajawazito

VATICAN CITY

BABA Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili, amewahakikishia akinamama wajawazito kuwa, watoto wao, ni mwaliko na matumaini ya maisha katika jamii.

Baba Mtakatifu aliyasema hayo Jumapili iliyopita, alipojitokeza dirishani na kuwasalimia maelfu ya watu waliofurika katika kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Alielezea upendo wake kwa wajawazito wanaopata mahangaiko na mateso mbalimbali katika kipindi cha ujauzito wao.

Jumapili hiyo ya machi 25,ilikuwa kwa ajili kuikumbuka siku ambayo Malaika Gabriel alimtangazia Bikira Maria kuwa, angemzaa mtoto Yesu.(Kupashwa habari ya kuzaliwa Bwana)

Hata hivyo, kutokana na sababu za Kiliturujia, kwa mwaka huu kumbukumbu hizo zimeadhimishwa Jumatatu.

"Waamini watapata nguvu za kiroho na kuwa mashahidi wa Yesu ambaye ndiye Mkombozi pekee wa Wanadamu"

"...Imani inasaidia Neno wa Mungu kuingia ndani ya mioyo ya wanadamu," alisema Baba Mtakatifu wakati akielezea juu ya ile saa ambayo Bikira Maria alisema "NDIYO" kwa Malaika Gabriel.