UJUMBE WA PASAKA -2000

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

Wapendwa Wana Wa Mungu.

Wapendwa Wote Wacha Mungu.

KRISTO NI YULE YULE ..........JANA LEO NA DAIMA.

Wapendwa,

Neno "Pasaka" si neno jipya linaloanza kusikika zama zetu, la hasha! Wayahudi, kabla ya kuzaliwa KRISTO walianza kutamka neno Pasaka.

"Waliadhimisha sikukuu ya Pasaka tarehe 14 ya mwezi wao Kiyahudi uitwao NISAN (yapata tarehe ya kwanza ya mwezi Aprili katika Kalenda yetu). Kwa sikukuu hii walikumbuka wakati malaika mwangamizi alipowaua wazaliwa wa kwanza katika kila jamaa ya Wamisri bila kuwaua wale wa jamaa ya Waebrania"

Wayahudi walitambua na kukata shauri kuadhimisha kila mwaka siku kuu ya Pasaka ili kumshukuru Mungu aliyeingilia kati mateso yao kwa kuwaletea hata kuwatoa mikononi mwa Farao wa misri. Wakaanza safari ya kurudi makwao walitoka utumwani na wakajipatia uhuru wao.

Leo hii "Pasaka siyo Sikukuu nyingi bali ndiyo sikukuu ya Ma-siku-kuu. Mtakatifu Athanasi aliita Pasaka "JUMAPILI KUU" Katekisimu ya kanisa katoliki (KKK 1169)*

Kwetu sisi Waamini Wakristo: kwanza, tunaichukulia Pasaka kwa maana ya kuadhimisha fumbo la kifo cha Yesu Mwokozi kilichotutoa kutoka katika hali ya utumwa wa shetani na kutuweka huru (KKK654); tumekuwa si watumwa tena wa Nguvu za giza yaani Shetani na vishawishi vyake, kwani siku ya Ijumaa Kuu Kristo amemwaga damu yake. Akatutakasa kwa bei ya damu hiyo na akatununua kwa ya thamani mno ya damu yake Mungu kweli na mtu kweli.

Pili, tunahakikisha Pasaka imekamilishwa kwa ufufuko wa Bwana wetu uliokuwa pigo kubwa ambalo kwake Kristo Yesu alikiponda kifo (KKK 1169) na kuwezesha sisi waaminini kushiriki neema ya Mungu (Rum6:4).

Hivyo ushindi wa Kristo juu ya kifo na uwezo mpya wa sisi kushiriki neema ya Mungu,vinatufanya sisi tuhesabiwe haki kwa "kutufanya hai pamoja na Kristo".Hakika "Tumeokolewa kwa ajili ya imani na jambo hili si matokeo ya juhudi zetu"(Efeso 2:5,8).

Kutokana na umuhimu wakePasaka mwaka huu wa Jubilei Kuu mwaka 2000 huwa na uzito wa namna yake,tunataka kumwonyesha Mungu shukrani zetu kwa mipango yake mizuri ajabu kwa ajili ya wokovu wetu sisi wanadamu.

Ukweli hata hatujui tufanye nini cha kuridhisha ili kukidhi upendo wa Mungu kwetu. Nia tunayo sana lakini tunaona tuna deni kubwa na shukrani yetu kuu kwa Mungu ni kufanya TOBA, NA TENA KUFANYA MATENDO MBALIMBALI YA UPENDO NA HURUMA.

Zinaonekana pia juhudi za kuabudu sakramenti Takatifu ya Ekaristi katika maparokia mengi wakimalizia na Baraka Kuu. Nawapongeza sana na kuwaomba wengine waige mifano yao.Ni jambo la Baraka na Neema nyingi kuabudu na kuipa heshima kubwa na ya pekee Sakramenti ya Ekaristi. Zaidi sana wapendwa wangu juhudi hizo zote zilenge hasa kutugeuza mioyo. Hatuwezi kujivunia ukristo wetu kama sisi Wakristo tunaanzisha na kuchochea chokochoko ili kuleta magomvi na hata vita katika Taifa la Tanzania.Imani yetu ni imani yenye amani. Kristo amekufa kwa ajili ya AMANI YETU. Alipowatokea mitume baada ya Ufufuko mara kwa mara aliwasalimu akisema AMANI KWENU.

Sisi Wakristo tunasherekea Ufufuko wa Yesu lazima tuwe vyombo thabiti vya amani tukizingatia Hekima na Heshima anayostahili kila mtu. Hali kadhalika mienendo yetu na ilingane na Ukristo wetu.

Tuachane na dhuluma na rushwa ambayo kwa tabia yake hunyonga hakiza maskini na wanyonge.Tuulaani vikali ushirikina kwani huo unapandikiza sumu yaani chuki na kugawa mioyoni mwa watu hata ndugu wa damu moja.

Tuachane na ulevi kwani taifa kamwe halitajengwa kwa mbinu za ulevi. Ulevi ukikithiri, watoto wetu watarithi umaskini. Lakini fungueni macho ndugu zangu na muone jinsi ulevi unavyozidi kulikumba taifa letu.Ulevi ni tishio kubwa kwa maendeleo ya familia na taifa. Tusilifumbie macho.

Wenye ndoa safi na takatifu zingatieni sana ndoa zenu. Na kila Mkristo austahi na kuutunza safi mwili wake kwani ni hekalu la Roho Mtakatifu na kwa kufanya hivyo, mtaepuka kwa sehemu kubwa sana janga la kupatwa na kusambaza UKIMWI.

Tunawasifu na kuwapongeza mliompokea mgeni wetu rasmi wa Jubilei Kuu maparokiani mwao. Naam, Msalaba Mtakatifu umepokelewa na kushangiliwa vyema popote ulipopita.

Tumearifiwa kuwa hata baadhi ya wasio Wakristo waliomba paroko awaruhusu kuupokea na kuubeba Msalaba pamoja na Wakristo. Paroko aliwaruhusu.Waliubeba na wakafurahi. Walionja heri kubwa sana. Kristo ni yuleyule... Jana, Leo, na Daima.

Na NDOA POA JE ?

Hili si jina linalostahili Sakramenti ya Ndoa lakini, msemo huu hutumika katika jimbo lingine kumaanisha ndoa nyingi zinazofungwa kwa pamoja na bila gharama ya maandalizi, bila mbwembwe wala madoido yoyote.

Tunawapongeza wote waliorekebisha uchumba sugu na kufunga ndoa. Naam, sasa zinafungwa ndoa nyingi maparokiani.Tunakiri kuwa mwaka huu makundi makubwa yanarudi nyumbani kwa Baba.

Ninahimiza waraka wangu kwa kuwahimiza fanyeni yote kwa imani. Wa heri wanaosadiki bila kuona!!

"Ndugu, tuombeeni na sisi pia." (2Thes. 5:25)

"Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. Tunawatakieni neeme ya bwana Wetu Yesu Kristo (2Thes.5:28)

YEYE NI YULE YULE,

KRISTO,JANA,LEO,DAIMA

Telesphor Mkude

Askofu wa Morogoro