Picha na mengine juu ya Fr. Kija

Toleo Maalum

HISTORIA FUPI YA MAREHEMU PADRE NORBERT JUMA KIJA TANGU KUZALIWA 1957 HADI KIFO 2000

Padre Norbert Juma Nimage Kija alizaliwa mwaka 1957 katika kijiji cha Kijereshi wilaya ya Magu katika mkoa wa Mwanza.

Marehemu Padre Norbert Juma Kija ni mtoto wa familia ya Mzee Seif Masanja na Mama Modesta Kija.

Alizaliwa katika familia ya Kiislamu na alikuwa Muislamu hadi alipoamua yeye mwenyewe kubadili dini na kuwa Mkristo Mkatoliki.

Februari 27, 1974, alipata Sakramenti ya Ubatizo na Ekaristi Takatifu katika parokia ya Malili. Machi 9, mwaka huohuo, alipata Sakramenti ya Kipaimara katika parokia hiyo ya Malili.

Akiwa kijana katika parokia hiyo, Marehemu Padre Norbet Kija alianza kutumikia kabla ya kubatizwa. Wakati huo Mhashamu Askofu Aloysius Balina, akiwa Paroko.

Askofu Aloysius Balina alivutiwa sana na mwenendo wake. Marehemu alipenda sana mambo ya kanisa kiasi kwamba, Paroko wake alimpatia kazi ya kuuza magazeti ya Kanisa.

Marehemu alipendezwa sana na jina la Frateri Norbet Ngusa, aliyekuwa mwaka wa kichungaji ndipo marehemu alipoamua kubatizwa kwa jina hilo.

Marehemu Padre Kija, alikuwa karibu sana na Padre Aloysius Balina, aliyekuwa Paroko wake wakati huo.

Kwa jinsi hiyo, Marehemu alimkabili Paroko wake na kumweleza nia yake wito wa Upadre. Paroko wake alimwelekeza na akatuma maombi Makoko Seminari, kwa bahati mbaya Gombera wa Seminari ya Makoko hakuweza kumjibu kwa sababu jina alilotumia Marehemu lilikuwa la Kiislam, "Juma Seif."

Kwa bahati sana Gombera huyo alitembelea Parokia ya Malili na ndipo hapo Padre Aloysius Balina alipomfahamisha kuwa kijana huyo si Muislamu bali alishabatizwa na kuwa Norbert.

Kwa maelezo hayo, Gombera wa Seminari ya Makoko alikubali na kutoa fomu zilizomwezesha marehemu kufanya mtihani wa kujiunga na Seminari hiyo.

Pamoja na kuwa Gombera, Paroko wake aliendelea kumsaidia Marehemu katika kumlipia ada na kumpatia maadili mazuri.

Hali hiyo, iliendelea tangu wakati wa malezi na masomo yake hadi kifo chake.

Tunamshukuru sana Baba Askofu Aloysius Balina kwa msaada wake huo, Mungu azidi kumbariki na kumjalia ufanisi mwema katika kazi zake.

Marehemu Padre Norbert Juma Nimage Kija alipata elimu yake katika shule zifuatazo:-

Ø    Malili shule ya msingi mwaka 1967- 1974.

ØMakoko Seminari kidato cha kwanza hadi cha nne 1975 hadi 1978.

ØNyegezi Seminari kidato cha tano na cha sita mwaka 1979 hadi 1981.

Ø    Jeshi la kujenga Taifa kwa mujibu wa taifa mwaka mmoja 1981 hadi 1982 katika kambi ya Bulombora.

ØNtungamo Seminari- Filosofia miaka miwili toka 1982 hadi 1984.

ØKipalapala Seminari - Teolojia miaka mitano toka 1984 hadi 1989.

Padre Kija alipewa Daraja ya Ushemasi Desemba 15, 1988 katika parokia ya Ng’wanangi na baadaye, Daraja Takatifu ya Upadre Agosti 3, 1989 katika parokia ya Chamugasa.

SHUGHULI ZA KITUME.

Mara baada ya Upadrisho wake, Marehemu Padre Kija alipangiwa kufanya kazi za kitume katika parokia ya Ng’wanangi.

Mwaka 1991 alihamishiwa katika parokia ya Shinyanga Mjini kama Paroko Msaidizi, Mkurugenzi wa Baraza la Walei na Idara ya Upashanaji Habari wa Jimbo hadi mwaka 1993, alipohamia Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania huko Dar-Es-Salaam.

Marehemu alikuwa na vipaji vingi sana, kati ya vipaji hivyo alipenda sana kusaidia vijana katika kujiandaa kukabiliana na maisha.

Upendo huo ulijionesha katika kuwabana vijana na kuwaeleza ukweli na kukemea mambo mabaya yaliyojionesha katika matendo na maneno yao ilipobidi kufanya hivyo.

Padre Kija hakuogopa kusema ukweli juu ya baya aliloliona kwa mtu yeyote yule bila kujali umri au wadhifa alionao.

Pamoja na tabia hiyo, yeye mwenyewe alikuwa ni mpole na mtu wa tabasamu siku zote, mtii na mnyenyekevu wa kukubali na kurekebisha makosa aliyonayo endapo ataambiwa na mtu yeyote yule.

Daima alipenda kusikiliza ushauri na maelekezo mbalimbali aliyoambiwa na wenzake.

Hakumpuuza mtu yeyote wala kubagua, bali wote walikuwa ni wake bila kujali busara ya mtu, wadhifa wala umri.

Mtu yeyote alipomwendea kwa ukali alipenda sana kumwomba wasalimiane kwanza kabla ya kumgombeza. Hali hiyo, inaonesha ni jinsi gani Marehemu alivyokuwa mnyenyekevu.

Marehemu Padre Kija alikuwa na karama ya ubunifu wa maendeleo na hasa mbinu mpya za Sayansi na Teknolojia.

Ubunifu huo ulianza kujionesha mara tu, alipohamia Parokia ya Shinyanga mjini na kuwa Mkurugenzi wa Idara mbili zilizotajwa awali.

Katika kipindi kifupi alichokuwa hapo, aliziwezesha idara hizo kupata usafiri wa gari. Na zaidi ya hilo alifufua Idara ya Upashanaji Habari iliyokuwa imefungwa kwa muda.

Kutokana na mbinu zake mwenyewe aliiwezesha idara hiyo kufungua duka la vitabu pamoja na uuzaji wa picha za Watakatifu, Rozari na Visakramenti mbalimbali. Hali iliyopelekea kupata mafanikio makubwa, kwani kwa muda mfupi ofisi hiyo ilikuwa tayari na mashine za kisasa za kurudufu makaratasi na fotokopi.

Yote haya yanaonesha kuwa, alikuwa na tabia ya kujisomea na kuelewa dunia ianavyokwenda. Marehemu Padre Kija hakuwa mchoyo, bali alikuwa mkarimu na mpenda maendeleo kwa vijana na Kanisa kwa jumla.

Hali ya kupenda maendeleo haikuishia jimboni kwake tu, iliendelea kujionesha hadi alipohamia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Akiwa huko Marehemu Padre Norbert Juma Kija, alipelekwa Chuo cha Jamii, Nyegezi kilichopo jijini Mwanza (sasa hivi Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino).

Marehemu alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uandishi wa Habari na kuwa mwanafunzi bora wa mwaka huo wa 1995. Aliwasaidia wanafunzi wenzake kuwafundisha kompyuta.

Ujuzi wake wa kutumia kompyuta, uliwafanya walimu wake waendelee kumuita kuja chuoni hapo kufundisha somo hilo.

Baada ya kuhitimu masomo yake hayo, alirudi Dar-Es-Salaam, katika ofisi za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kufanya kazi ya Afisa wa Habari (Press - Secretary) wa Baraza hilo.

Kutokana na utendaji wake bora Maaskofu walimteua kuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Upashanaji Habari. Akiwa na wadhifa huo aliimarisha vema idara hiyo na kuleta mafanikio makubwa ya kulifanya gazeti la KIONGOZI litoke kila wiki badala ya mara moja kwa mwezi.

Gazeti hilo limekuwa na mafanikio makubwa hadi hivi sasa.

Akiwa katika ofisi hiyo, Marehemu Padre Kija alitumia vyanzo vyake vyote vya pesa, ikiwa ni pamoja na wafadhili wake binafsi kwa ajili ya matumizi ya ofisi.

Baadhi ya vitu alivyofanya ni pamoja na ununuzi wa kompyuta mpya za kisasa pamoja na mashine ya kuchapia (Printer) mpya na ya kisasa ya yenye nguvu na uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa haraka zaidi na nadhifu.

Aidha, alitumia ujuzi wake wa kompyuta kuingiza programu mbalimbali na kuwafundisha wafanyakazi namna ya kuzitumia. Sababu ya utendaji wake mzuri wa kazi aliteuliwa pia kuwa Katibu wa mikutano ya wakuu wa idara, pia aliombwa kusimamia mawasiliano na matumizi ya simu katika idara zote za TEC.

Aliteuliwa pia kuwa mjumbe katika kamati ya kufufua bodi ya TMP huko Kipalapala. Kwa kumbukumbu kubwa siku za hivi karibuni ameiwezesha ofisi hiyo kupata gari jipya.

Marehemu Padre Norbert Kija, hatasahaulika pia katika majimbo mengi ya Kanisa katoliki nchini.

Alisafiri katika majimbo mbalimbali kufunga kompyuta na kuziwekea programu pamoja na kuwafundisha matumizi yake. Aliwaungia na kuwaungaishia mawasiliano kwa njia ya Internet na hasa E-mail.

Pamoja na hayo, alitumia muda wake mwingi kuwezesha ufungaji wa vituo mbalimbali vya kurushia matangazo vikiwemo vituo vya Morogoro, SAUT Mwanza na Sumbawanga.

Aliwezesha miradi mbalimbali kupata wafadhili. Nia yake hasa ilikuwa kuwezesha maendeleo ya mtu binafsi kwa nia ya kuiendeleza jumuiya ya Kanisa na chini nzima ya Tanzania.

Aidha alisaidia kupata fedha zilizowawezesha wajumbe mbalimbali wa majimbo yote nchini kuhudhuria warsha, semina na masomo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kwa juhudi hizo, yeye mwenyewe aliweza kuhudhuria mikutano mbalimbali ya kimataifa. Baadhi ya mikutano hiyo ni ule mjadala wa kufutiwa madeni nchi ambazo hazijaendelea huko Cologne - Ujerumani.

Katika mkutano huo yeye mwenyewe alitoa mawazo na hoja zake binafsi kwa niaba ya wananchi wa Tanzania na kutetea mada hiyo.

Marehemu Padre Kija baada ya kurudi jimboni Shinyanga mwezi Aprili Mwaka huu, alijishughulisha sana katika ujenzi wa kituo cha kurushia matangazo cha jimbo ‘REDIO FARAJA FM STEREO’. Pia, alijitolea muda wake pamoja na fedha zake kuharakisha ujenzi wa jengo la Redio hiyo unafanikiwa.

Pamoja na udhaifu wa mwili aliendelea kufanya kazi hasa za kompyuta, ujenzi, usimikaji wa mnara wa kurushia matangazo na kuandaa wafanyakazi wa Redio Faraja.

Cha ajabu mno, katika usaili wa kuajiri, hakujali wafanyakazi katika redio hiyo, aliweza kugundua mara moja kipaji cha kila mtahiniwa na kukiheshimu.

Na kama alikuwa na wazo lolote juu ya mtahiniwa na wasimamizi wa redio, alilisema mara moja bila kusita endapo ana uhakika nalo.

Na kama hakuwa na uhakika mara moja alikwenda kulisoma kwenye vitabu na kufanya mawasiliano mbalimbali na wataalam kwa njia ya Internet na hivyo, kupata uhakika wa swala hilo.

Hali hiyo alimfanya marehemu kuamua kufunga simu yake yeye mwenyewe chumbani mwake. Marehemu aliendelea hivyo hivyo bila kujihurumia wala kunung’unika bali alivumilia mateso na mahangaiko kwa utulivu na amani hadi hapo alipoaga dunia tarehe Septemba 19, 2000 majira ya saa nne asubuhi.

 

 

 

RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA,

APUMZIKE KWA AMANI

AMINA.