Majonzi yaligubika Baraza la Maaskofu

 

q       Lapoteza 'nyota' ya matumaini

 

Na Mwandishi Wetu

 

JUMANNE asubuhi, kila mmoja katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alionekana mwenye baridi, amejikunyata, hali yake si nzuri na wala si mbaya. Hakuna mgonjwa. Lakini, nini kimewasibu wasinyae na kugubikwa na majonzi huku wakionekana upweke namna hiyo?

Katika hali isiyo ya kawaida, mchana wa siku  hiyo simu kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa TEC, zinapigwa katika ofisi mbalimbali ya Baraza hili zikimtaka kila mfanyakazi aende kanisani.

Bila kujua hili wala lile, wafanyakazi wote walielekea kanisani, si wafanyakazi peke yao bali hata watu kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki ambao walikuwa wanashiriki Mkutano wa Idara ya Uchungaji, nao pia waliunganika.

Kila mmoja akiwa ametulia kanisani humo, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura, akainuka na kutaka kusema kitu lakini, kabla hajafanya hivyo, akakumbwa na kigugumizi asichokuwa nacho siku zote.

Uso wa Padre Rutechura ambao siku zote huwa ni wenye furaha na matumaini awapo mbele ya wanaTEC wenzake, siku hiyo ukaonekana kinyume kabisa.

Kila mtu akawa na hamu ya kupata ujumbe kutoka kwa Padre Rutechura, ili ajue amekumbwa na masaibu gani.

Akasema kuwa, kipenzi cha wengi, Padre mcheshi, Padre mwenye huruma, Padre asiye mbinafsi, Padre mkarimu kwa watu wote, Padre mtaalamu wa mambo mengi yakiwamo mawasiliano na mambo muhimu ya kiroho, NORBERT KIJA, sasa eti ni MAREHEMU. Eti amefariki dunia. Huzuni na majonzi tupu.

Ni nani anayemfahamu Padre Kija ambaye hakulengwalengwa na machozi baada ya taarifa hiyo iliyotolewa katika kanisa la TEC?

Kisha, Katibu wa Idara ya Liturjia wa TEC, Padre Julian Kangalawe, akaongoza sala kumuombea Marehemu kipenzi cha watu, Padre Kija.

"Mungu akulaze Mahali Pema Father Kija. Lakini Father, tutakuona lini katika dunia hii? Huzuni tupu, majonzi na upweke.

Gazeti la KIONGOZI, Idara ya Mawasiliano, TEC, Tanzania na Kanisa kwa jumla, wanaamini kuwa ingawa kimwili umewatoka, lakini kiroho uko pamoja nao na wana matumaini mtakutana katika Ufalme wa Mungu kwa kuwa maombi yao kwako ni makubwa, vilio vyao ni vingi na hasahasa wanakiri kuwa ulimtumikia vema Mwenyezi Mungu.

Hivi ni nani hakumjua alivyo kuwa na utani kwa watu wengi? Ukiwa nae unajisikia umekaa pamoja na baba yako, umekaa na ndugu katika Yesu na hasahasa umekaa na Mkristo mwenzako?

Jumatano katika ibaada maalumu ya kumuombea kanisani hapo, kwa huzuni kabisa Padre Lucas Mzuanda akasema kuwa ni wazi hakuna ajuae kifo kitampata wapi na hivyo kila mmoja ajiandae wakati wowote kuingia mbinguni huku akiishi maisha mema na kudumu katika sala.

Kifo cha Padre Norbert Kija, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano wa TEC, na Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hili la KIONGOZI, kimetokea Septemba 19, mwaka huu baada ya kuugua akiwa jimboni kwake Shinyanga.