TAARIFA MAALUM

SIKU YA 34 YA UPASHANAJI HABARI ULIMWENGUNI.

DHAMIRA : "KUMTANGAZA KRISTO KATIKA VYOMBO VYA HABARI MWANZONI MWA MILENIA MPYA".UJUMBE WA BABA MTAKATIFU: 6 AGOSTI, 2000

Wapendwa Dada na Kaka,

Dhamira ya siku ya 34 ya Upashanaji Habari, kumtangaza Kristo katika vyombo vya habari mwanzoni mwa Milenia, ni mwaliko wa kuangalia mbele lile changamoto tunalolikabili, na pia kuangalia nyuma mwanzoni kabisa mwa Ukristo wenyewe kwa ajili ya kupata mwanga na ujasiri tunaouhitaji. Kitu muhimu cha ujumbe tunaoutangaza daima ni Yesu mwenyewe: "historia yote ya binadamu kwa kweli husimama ikimwekea yeye: nyakati zetu sisi wenyewe na wakati ujao wa ulimwengu huangazwa kwa uwepo wake (Fumbo la Umwilisho, 1).

Sura za mwanzoni za kitabu cha Matendo ya Mitume hutoa taarifa yenye msisimko wa utangazaji juu ya Kristo uliofanywa na wafuasi wake wa kwanza -Utangazaji ambao ulikuwa wa papo kwa papo, uliojaa imani, na wenye kushawishi na ukawa umefanyika kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Jambo la kwanza na la muhimu, wafuasi walimtangaza Kristo kama jibu lao kwa amri aliyokuwa amewapa. Kabla ya kupaa mbinguni anawaambia hivi Mitume: "Mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi" (Mndo. 1:8). Na hata kama hawa "hawana elimu, watu wa kawaida" (Mndo 4:13), wanaitikia upesi na kwa ukarimu.

Baada ya kutumia muda katika kusali wakiwa pamoja na Maria na wafuasi wengine wa Bwana, na wakitenda kufuatana na maongozi ya Roho Mtakatifu, Mitume wanaanza kazi ya kutangaza Injili wakati wa Pentekoste (taz. Mndo.2). Tunaposoma kuhusu matukio yale ya ajabu, tunakumbushwa kuwa historia ya Upashanaji Habari ni namna ya safari, kutoka kule kwenye ule mradi wa kiburi wa Babeli na kuanguka katika fujo na kuingia katika ile hali ya kutoweza kuelewana kati ya watu iliyotokea, (taz.Mw.11:1-9), hadi Pentekoste na zile karama za ndimi za moto, ikiwa ni utengenezaji upya wa mawasiliano ambayo yana kiini chake katika Yesu, kwa njia ya tendo la Roho Mtakatifu.

Kwa hiyo kumtangaza Kristo hupelekea hadi kwenye makutano kati ya watu katika imani na mapendo kwa kiwango chenye kina sana cha ubinadamu wao; Bwana Mfufuka mwenyewe anakuwa ni chombo halisi cha Mawasiliano kati ya Kaka na Dada ndani ya Roho Mtakatifu. Pentekoste ni mwanzo tu. Hata baada ya kutishwa na kulipishwa kisasi, Mitume hawakatishwi tamaa ya kumtangaza Bwana: "Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia: (Mndo. 4:20).

Petro na Yohane waliambia Baraza la Kuu la Wayahudi. Hakika majaribu yenyewe huwa ni chombo kwa ajili ya kazi ya kitume. Wakati madhulumu makali yanapotokea mjini Yerusalemu baada ya kifodini cha Stefano yakiwalazimisha wafuasi kutoroka, "wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakihubiri neno" (Mndo 8:4).

Moyo hai wa ujumbe ambao Mitume walihubiri ni kusulubiwa kwa Yesu na ufufuko wake - ushindi hai dhidi ya dhambi na kifo. Petro anamwambia yule akida Kornelio na nyumba yake: "walimwua wakamtundika mtini, lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika......

Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu - Huyo, manabii wote walimshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi" (Mndo 10:39-43).

Ni dhahiri kwamba mazingira yamebadilika kwa vikubwa sana katika milenia mbili. Hata hivyo hitaji lile la kumtangaza Kristo bado lipo. Wajibu wetu wa kutoa ushuhuda kwa kifo cha Ufufuko wa Yesu na uwepo wake wenye kuokoa katika maisha yetu ni dhahiri na wenye nguvu kama ulivyokuwa wajibu wa wafuasi wa kwanza. Tunapaswa kutoa habari njema kwa wale wote ambao wako tayari kuisikia.

Utangazaji wa moja kwa moja na wa binafsi - yaani mtu mmoja akishirikishana imani na mwenzake katika Bwana Mfufuka ni ya lazima; hivyo ndivyo zilivyo na aina nyingine za mapokeo ya kueneza neno la Mungu.

Lakini pamoja na hayo, utangazaji siku ya leo hauna budi kutendeka pia ndani na kwa njia ya vyombo vya habari. "Kanisa litajiona ni lenye lawama mbele ya Bwana kama halingetumia njia hizi zenye nguvu" (Papa Paulo VI-Utangazaji wa Injili, 45).

Faida ya vyombo vya habari haiwezi kamwe kusemwa mno siku ya leo - Ujio wa chama cha taarifa ya habari ni kweli mapinduzi ya kitamaduni, na hivyo kufanya vyombo vya habari

"kuwa ni Arcopagus wa nyakati za kisasa" (Utume wa Mkombozi, 37), ambapo ukweli wa mambo na mawazo na tunu daima hubadilika kwa njia ya vyombo vya habari, watu hukutana na watu wengine pamoja na matukio mengine na hujenga maoni yao kuhusu ulimwengu wanamoishi.

Hakika wanatengeneza ufahamu wao kuhusu maana ya maisha kwa wengi, mang’amuzi ya kuishi kwa vikubwa hutokana na mang’amuzi ya vyombo vya habari (taz. Halmashauri ya Kipapa ya Mawasiliano, Aetatis Novae, 2). Utangazaji wa Kristo sharti uwe ni sehemu ya mang’amuzi haya.

Kwa kawaida, katika kumtangaza Bwana, Kanisa sharti litumie kwa bidii na kwa ufundi vyombo vyake vya mawasiliano kama vile vitabu, magazeti, majarida, radio, televisheni na vyombo vingine.

Wapashanaji habari wakatoliki hawana budi kuwa washupavu na wenye mawazo mapana katika kuendeleza vyombo vipya vya upashanaji habari na mbinu za utangazaji.

Lakini, kwa kadri inavyowezekana, Kanisa lazima litumie nafasi nzuri ambazo hapatikana katika vyombo vya habari visivyo vya kidini.

Tayari vyombo vya habari hutoa mchango katika utajiri wa kiroho kwa njia nyingi - Kwa mfano, programu nyingi za pekee zinatendeka ulimwenguni kote kwa wasikilizaji kwa njia ya ‘cast za satellite’ wakati wote wa mwaka wa Jubilei Kuu.

Lakini kwa upande mwingine huonyesha ile hali ya kutokuwa na msimamo hata huweza kuonyesha uadui, kwa Kristo na ujumbe wake katika sekta fulani fulani za utamaduni wa kawaida. Ingawaje, lakini, mara nyingi kuna hitaji la aina fulani la "kutafiti dhamira" kwa upande wa vyombo vya habari, ambalo hupelekea kwenye utambuzi wenye hoja kuhusu mwelekeo wa upande mmoja au hali ya kukosa heshima kwa imani za watu za kidini na kimaadili.

Matumizi ya vyombo vya habari hudai hali ya kuwa makini kwa mahitaji ya binadamu, hasa wale walio wadhaifu, waliojeruhiwa, wenye kudharauliwa, huweza kumtangaza Bwana kimya kimya.

Lakini, licha ya utangazaji wa kimyakimya, wapashanaji habari wa Kikristo wanapaswa pia kutafuta njia za kusema waziwazi juu ya Yesu msulubiwa na mfufuka, juu ya ushindi wake dhidi ya dhambi na kifo, kwa namna inayofaa kwa chombo kile cha habari kinachotumika na kulingana na mawazo ya wasikilizaji.

Ili kulitekeleza jambo hilo vizuri huhitajika mafunzo na ujuzi wa kitaalam. Lakini, kunahitajika kitu kingine zaidi.

Ili kuweza kutoa ushuhuda kwa Kristo ni lazima kukutana naye mtu mwenyewe na kudumisha uhusiano binafsi naye kwa kwa njia ya sala, Ekaristi Takatifu na upatanisho wa kisakramenti, kulisoma na kulitafakari neno la Mungu, mafunzo ya mafundisho ya Kikristo, na kuwahudumia wengine.

Pia ikiwa jambo hilo ni la hakika, hiyo itakuwa ni hasa kazi ya Roho Mtakatifu zaidi kuliko juhudi zetu sisi.

Kazi ya kumtangaza Kristo siyo tu ni wajibu, bali ni upendeleo - Hati ya ‘Fumbo la Umwilisho: inasema hivi: "safari ya waamini kuelekea milenia ya tatu haijaelemewa na uchovu ambao mzigo wa miaka elfu mbili wa historia ungeweza kuletwa nayo. La, Wakristo wanaonja kutiwa nguvu mpya, wakifahamu kuwa, wanaupelekea ulimwengu mwanga wa kweli, yaani Kristo Bwana katika kazi ya kumtangaza Yesu wa Nazareti, aliye Mungu kweli na Mtu kamili, Kanisa huwafungulia watu wote yale matarajio ya kufanyika "miungu" na hivyo kuwa binadamu zaidi".

Jubilei Kuu ya miaka 2000 ya kuzaliwa Yesu kule Bethlehemu lazima iwe ni bahati na pia changamoto la wafuasi wa Bwana kutoa ushuhuda ndani na kwa njia ya vyombo vya habari, kwa Habari Njema ya Wokovu isiyo ya kawaida na yenye kuleta faraja Katika "mwaka huu wa upendeleo".

Twaomba vyombo vya habari vitoe sauti kwa Yesu mwenyewe, kwa uwazi na furaha, pamoja na imani, matumaini na mapendo.

Kumtangaza Kristo katika vyombo vya habari mwanzoni mwa Milenia mpya siyo tu ni sehemu ya lazima ya utume wa Kanisa ya Uinjilishaji, lakini pia ni jambo la maana sana, lenye kuleta mwangaza na matumaini, lenye kujaa utajiri wa ujumbe wa vyombo vya habari. Tunamwomba Mungu awabariki wale wote wanaomheshimu na kumtangaza Mwanae, Bwana wetu Yesu Kristo, katika ulimwengu mpana sana wa vyombo ya mawasiliano.

Imetolewa:

Vatican Januari 24, 2000.

YOHANE PAULO II.

Buriani Padre Wendelin

Na Padre Raphael Kilumanga

MPENDWA Wendelin (84) Padre wa Kwanza mkongwe kati ya Wamisionari wakapuchini nchini Tanzania ameaga dunia Julai 28 na kuzikwa Agosti 2 mwaka huu katika makaburi ya Msimbazi Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Ibada ya misa takatifu ya kumuombea marehemu Padre Wendelin ambaye alifika nchini mwaka 1946 iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Mhudumu wa shirika la Wakapuchini nchini ndugu Beatus Kinyaiya aliyewasili siku hiyo ya mazishi kutoka Uswisi na paroko wa Msimbazi padre Ambrose Mosha walimsaidia Muadhama Kardinali katika misa hiyo iliyohudhuriwa pia na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania

Maelfu ya waamini walihudhuriwa pia ibada ya misa na mazishi wakiwemo watawa, mapadre wakapuchini, mapadre wakazi wa Dar na kutoka majimbo ya Mahenge na Mbulu ambako Padre huyo alifanya kazi ya Kichungaji.

Akiongea mara baada ya mazishi , Padre Beatus Kinyaiya alisema kuwa marehemu Wendelin licha ya kupooza tangu mwaka 1997 hakuogopa kufa.

"Ndugu Wendelin aliishi vizuri... kadiri Mungu alivyotaka," alisema Mhudumu huyo (Provinsyali) na kuongeza kuwa Padre Wendelin aliupokea ugonjwa wake na kujiandaa ipasavyo na kuwataka watu waige mfano huo mzuri.

Aidha ujumbe wa wanaparokia ya Dawd, jimbo la Mbulu ulimwelezea Padre Wendelin muasisi wa parokia hiyo na ambaye aliishi huko 1978 hadi 1990 kuwa ni mtu aliyependa maendeleo ya watu na ujume huo ulitoa ubani kwa ajili ya misa ya kumuombea Padre Wendelin na sh. 50,000 ikiwa ni rambirambi kwa shirika hilo.

Akielezea maisha ya marehemu Wendelin wakati wa misa ndugu Donat Mueller Mhudumu wa Wakapuchini San Dominiano Msimbazi alisema kuwa marehemu alipata nguvu ya pekee kwa sababu alikuwa kwanza mtawa, mkapuchini na kama mtawa hodari aliyeweza kufanya kazi ya utume.

Padre Wendelin alizaliwa parokia ya Guntershausen jimbo la Basel, Uswisi Februari 20,1916, katika familia ya watoto 12 kati yao mapadre watatu mmoja wa jimbo na wawili Wakapuchini.

Ingawa alisoma katika sekondari ya Wabenediktini lakini Septemba 11, 1937 alijiunga na Shirika la wakapuchini Wafransisko. septemba 14, 1938 aliweka nadhiri ya kwanza; Septemba 18, 1942 alipata daraja ya upadre na kutumwa Afrika mwaka 1945 ambako alifika 1946 kwa meli iliyotokea Ureno.

Padre Wendelin alifanya uchungaji Mahenge katika parokia za Mkasu, Itete, Iragua, Mofu, Biro na Mchombe.

Aidha alihudumia Moshi katika parokia za maua na Himo na jimbo la Mbulu akiwa Rhotia na Dawd.

Vile vile alifanyakazi Dar es Salaam katika parokia za Magomeni, Msimbazi na Kipatimu.

Alikuwa pia mlezi wa wanovisi Kasita Mahenge na aliishi pia Kola jimbo la Morogoro.

APUMZIKE KWA AMANI

AMINA

Wakati Huo Huo: Shirika hilo Agosti 3 lilifanya sherehe za jubilei ya wanashirika wake saba watano wao wakifanya Jubilei ya Utawa ya miaka 50 (Dhahabu) na wawili ya miaka 25 (Fedha).

Waliosherehekea Jubilei ya Dhahabu ni ndugu Angelico dell'Amico,Egidio Guidi, Beda Scherer, Wolfram Burkart na Donat Muller na walioadhimisha jubilei ya fedha ni ndugu Stephen Mboya na William Mchunguzi.

Hongereni Sana ndugu Wakapuchini