Mabanda ya Nyerere yalivyompatia umaarufu mama Kiduo

Na Neema Dawson

INGAWA baadhi ya Wanajamii wamekuwa wakilalamikia tatizo la usokefu wa ajira na kukaa bila kujishughulisha na hususani wanawake ambaoi wamekuwa wakichukuliwa kuwa ni watu wasioweza kufanya lolote zuri, dhana hiyo potofu inapigwa vikali na mama Kiduo ambaye ni mahiri kwa utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za kisnanii. Mama huyu ameunda mfano wa banda lililotumika kuhifadhia mwili wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na anauza sanaa hiyo kama mapambo na kumbukumbu.

Mama Kiduo ambaye ni maarufu kwa jina la Mama Bonge amekuwa akijishughulisha na shughuli nyingi za mikono kama ufumaji wa vitambaa, utengenezaji wa mapambo kadhaa ya nyumbani.

Lakini hatua yake ya kubuni na kutengeneza sanamu ya banda alilohifadhiwa Nyerere ambalo lilipendwa na watu wengi imempatia umaarufu mkubwa kwani wanunuzi wake licha ya kununua kwa ajili ya kumbukumbu ya Baba wa taifa, hawawezi pia kusahau mtengenezaji.

"Bonge" anaeleza kuwa vifaa anavyovitumia kuundia mabanda hayo ni makaratasi ya X- ray yaliyokwishatumika ambayo huyaokota baada ya kutupwa kutoka mahospitalini na kuyasugua kwa kutumia mchanga ili yang'ae. Hata hivyo anasema upatikanaji malighafi hiyo ni mgumu kwani hawezi kununua filimu hizo ambazo ni ghali sana madukani.

Mama huyu na kundi lake la wasanii hawakuanzia katika uundaji wa banda la Mwalimu Nyerere tu, bali Wahandisi wengi wa majengo huwapelekea ramani za majengo wanayotaka kujenga wawaundie kwa kutumia maboksi, ili iwe kielelezo kwa mafundi wanapojenga majengo hayo.

Utengenezaji huo wa mabanda na nyumba huwapatia fedha ya kuweza kuyaendeleza maisha yao ya kila siku kwani kila banda huuzwa kwa kati ya shilingi 8,000 na 10,000.

Mama Ashura Kiduo, anaelezea kuwa ingawa alishafanya kazi ya kuajiriwa katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu akiwa Katibu Muhtasi, anaiona kazi ya hii ya kujiajiri kuwa bora zaidi kwani ana uhuru zaidi na anajipatia kipato kikubwa zaidi.

Kiduo alianza kujishughulisha na kazi za mikono tangu alipokuwa na umri wa miaka 15 na hadi sasa ana umri wa miaka 45.

Mbali na shughuli hiyo mama huyu pia anafanya anashughulika na ufugaji wa kuku, ulimaji wa mchicha, ufundi na cherehani, hali hivyo anajiingizia kipato kikubwa kutokana na shughuli anazozifanya.

Bi Ashura amewaasa wanawake wote hapa nchini kujishughulisha na kazi ndogo ndogo za uzalishaji na wasifikiri kuwa hazina maana kwani hizo ndizo zitakazowasaidia kuinua maisha yao.