Make your own free website on Tripod.com

Mjue Mwanamke aliyejiajiri kwa kucheza Sarakasi

Na Dalphina Rubyema

MARA nyingi jamii imezoea kuwaona wacheza sarakasi wa kiume tu. Hali hii ni tofauti kwa BI. Mastura Khamis, mkazi wa Buguruni Malapa jijini ambaye amejiingiza katika mchezo huu ambao ni kuvutio cha wengi.

Bi. Mastura (26) ambaye alianza kujiingiza katika ulimwengu wa Sarakasi mnamo mwaka 1995, anasema mchezo huu ambao umemwingizia maelfu ya fedha anaupenda kwa vile ni fani ambayo haikimbiliwi na watu wengi hususan wa jinsia yake kutokana na ugumu wake.

‘Naupenda sana mchezo wa Sarakasi kwa vile siyo common kwa watu na pia unasaidia sana kujenga afya na kuniweka fiti. Kuna fani nyingine ambazo hukimbiliwa na watu wengi lakini huu wa sarakasi unachezwa tu na wateule hata wasichana rafiki zangu huwa wananishangaa’ anasema Mastura.

Akielezea jinsi gani alivyojiunga na mchezo huo Bi. Mustara anasema kuwa wakati anasoma shule ya msingi ya mazoezi Butiama mkoani Mwanza, hakuwa na wazo lolote juu ya mchezo huo.

Lakini, ghafla wazo hili lilikuja kuibuka mwaka 1994 wakati alipokuwa kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Tweyambe iliyopo mkoani Kagera.

‘Tulipokuwa kidato cha nne mkoani Kagera shuleni kwetu walifika vijana sita wacheza sarakasi kweli mchezo yao ilinivutia sana ingawa niliumia roho kuona mchezo huo unawashirikisha wavulana tu bila wasichana’ anasema Mastura.

Anaendelea kusema kuwa baada ya kumaliza kidato cha nne, alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Omulutunguru kilichopo mkoani Mwanza alikofanikiwa kuukuta mchezo huo aliotamani.

Anaendelea kuwa, muda mfupi baada ya kufika chuoni hapo bila kuchelewa alijiunga na kikundi cha sarakasi ambacho kilikuwa na watu 18 wakiwemo wavulana 14 na wasichana 4.

Anasema sababu iliyowafanya wasichana wengi washindwe kushiriki katika machezo huo kuwa ni kutokana na woga ambapo alidai wasichana wengi huwa wanaona woga.

"Wengine wanakasumba ya kusema chezo huu ni wa wanaume peke yao kitu ambacho mimi nakipingia" anasema.

Anasema ujuzi na uzoefu alioupata wakati akiwa anasoma katika chuo cha Omulutunguru ndio huo uliomfanya aweze kuona maisha siyo magumu sana hata baada ya Serikali kushindwa kutoa ajira kwa walimu kwani akiwa kijijini kwao Misungwi Mkoani Mwanza, aliweza kuonesha michezo yake ya sarakasi ambayo ilimwingizia kipato.

"wakati wenzangu wanasubiri ajira mimi tayari nilishaanza kujiingizia pesa kwani nilionesha michezo yangu kwenye sherehe mbalimbali na hako nilikuwa ninalipwa maelfu ya pesa kwani maonesho yangu nayafanya kwa mapatano maalum ambayo ni kuanzia 20,000-35,000/=" anatamba Mastura ambaye alimaliza kozi ya ualimu mwaka 1997.

Anasema kwa nia kubadalisha mazingira na kutafuta uwezekano wa kujipatia kipato zaidi, Mei mwaka jana aliamua kuukimbia mji wa Mwanza na kuja jijini ambapo anaishi Buguruni Malapa wilayani Ilala na anaendelea na kazi yake hiyo ambapo anasema hali ni nzuri zaidi ikilinganishwa na alivyokuwa Mwanza.

Anaitaji michezo mingine aichezayo kuwa ni pamoja na kuruka ringi yenye kuwaka moto, kutembea na kijiti kilichobeba chupa mdomoni, kubeba chupa zaidi ya moja kichwani huku akiwa amenyoosha mikono yenye kubeba kitu chochote pamoja na kuweka jiti la moto mdomoni na kuitoa bila moto huo kuzimika.

Anaeleza kuwa ukosefu wa vifaa na eneo la kufanyia mazoezi ni miongoni matatizo sugu yanayomkabili ikifuatiwa ni lile la jamii kutozingatia umuhimu wa mchezo huu.

Hata hivyo anasema kuwa kwa kutumia vifaa duni alivyonavyo anaweza kufanya vizuri na amefanikiwa kupanga chumba chake anacholipia sh 6000 kwa mwezi.

Lengo lake ni kujiunga na Chuo cha Sanaa Bagamoyo endapo atapata wafadhili akiwa na nia ya kuongeza ujuzi katika mchezo wake.