Mpingo: Mti wa Tanzania uliopamba sanaa ya Ulaya

Getruda Madembwe na Masha Otieno

Safari ya kwanza ya Mpingo, mti mweusi unaosifika kote duniani huanzia kwenye mapori yaliyoko Kusini mwa Tanzania.

Hapa ndipo mti huo hutoka na kujikuta umesafiri, kuvuka mipaka na kufikia nchi za Magharibi kama Uingereza, Sweden, na hata Marekani.

Kwa asili Mpingo ulianza kutumiwa na wamakonde katika Sanaa miaka mingi sana kabla hata wamisionari wa kwanza hawajafika Afrika.

Baadhi ya wachonga vinyango hodari wa Kimakonde waliopata kuhojiwa wanaelezea kuwa hapo awali mpingo ulitumika kuchonga tu sanaa za kujifurahisha, kuburudisha macho, na kuwakilisha aina fulani tu za ujumbe wa kitamaduni katika jamii ya wamakonde.

Ni baada ya kuja Wazungu kuuona na kuupeleka Ulaya mwanzoni mwa miaka ya 60 ndipo sifa za mpingo zilipoanza kuvuma nchi za ng'ambo.

Wazungu walipogundua kwa mti huu haufai peke yake kutengeneza vinyago peke yake bali hata samani na ala za Muziki.

Ni baada ya viwanda vya ala za muziki katika nchi za Sweden, Uingereza na Marekani kuanza kuutumia mpingo kutengenezea ala hizo katikati mwa miaka ya 1960 ndipo Kampuni ya kutengeneza filamu ya 'Holywood' kwa kushirikiana na chama cha 'International Geographic Society' cha Marekani na Idara ya Maliasili Tanzania iliposhirikiana kutengeneza sinema maalum juu ya Mpingo ili itangaze sifa zake kote duniani.

Sinema hiyo ambayo imepata kuvutia kwenye matamasha mbalimbali ya maonyesho ya filamu inaitwa 'Mpingo a tree that make Music' ikimaanisha 'Mpingo mti unaotengeneza muziki'.

Waliotengeneza filamu hiyo hawakosea hata kidogo kutoa jina kama hilo kwa picha yao, kwani Mpingo leo ni mmoja wa miti ambayo ala zake zinatamba kwenye kumbi za burudani na starehe barani Ulaya.

Nchini Marekani karibia ala zilizo nyingi zinatumiwa kwenye mziki wa Jazz zimetengenezwa kwa Mpingo moja ya ala kama hizo ni pamoja na 'Flute', Saxaphone, organ na Violin hata Fidla.

Viwanda vingine vya ala za Muziki mfano kile kilichoko mji wa 'Uppsala huko Sweden kimemudu kutumia mtu wa Mpingo kutengenezea magitaa aina ya 'Banjo'

Mpingo umetangaza jina la Tanzania katika nchi nyingi duniani. Bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa kutokana na mti huu zimejizolea sifa Kem kem kwenye maonyesho ya Kibiashara na ya sanaa nchi za nje.

Lakini pamoja na kuwa mti huu mweusi umekuwa balozi mzuri wa Tanzania nchi za ng'ambo katika nyanja ya sanaa hapa nchini mti huu bado unakumbwa na hatari.

Kasi ya uharibifu wa mazingira katika mapori ya mikoa ya Kusini ambako mtu huu unapatikana ni moja ya vitu ambavyo visipotipiwa macho utaupelekea mpingo kutoweka na usionekane na vizazi vinavyokuja.

Mwanzoni mwa miaka ya 1970, serikali kwa kushirikiana na idara ya Misitu hapa nchini ilianzisha kampeni maalum katika Mikoa ya Kusini ambapo ilielimisha na kuwaelewesha wananchi wanao kaa maeneo Mti huu unakopatikana umuhimu wa kuhifadhi Mpingo.

Kampeni hiyo ilizaa matunda kwani kwa kiasi fulani baadhi ya wananchi walianza kupanda miche ya mti huu adimu na muhimu katika soko la sanaa.

Baadhi ya watalii toka Ulaya ambao walipokuwa katika nchi zao walivutiwa mno na sanaa zilizotokana na Mpingo hata wamefikia hatua ya kufunga safari kuja Tanzania kujionea wenyewe uoto wa asili wa mti huu muhimu.

Biashara ya Vinyago vilivyotengenezwa kwa mpingo toka Tanzania, ni mojawapo kati ya biashara zenye soko kubwa barani Ulaya.

Wafanyabiashara wengi wazalendo wananufaika na kujiingizia fedha za kigeni kwa kusafirisha Mpingo na Vinyago vyake kwenda katika nchi za Japan,Ujerumani,Ufaransa, Italia na Ubelgiji.

Moja ya sanaa ambazo zimekuwa zikitengenezwa na kuwakilishwa kupitia kwa Mpingo ni pamoja na kabila la Wamasai, ngoma zetu, sura za mizimu, wanyama wa porini na shughuli za kijadi katika jamii.

Ujumbe wote huu usingeweza kuwafikia wazungu nchi za ng'ambo kama siyo kupitia kwa mti Mpingo,. kweli mti huu umekuwa balozi mzuri wa utamaduni wa Tanzania katika nchi za nje.