Naitwa Ramadhani lakini sijui mlango wa msikiti wala kanisa- Dk. Remmy

lAliwahi kuwa mtoto wa mtaani

lHuimba baadhi ya mambo yaliyomsibu Maishani

LITAJE mahali popote nchini, hata vijijini penye mawasiliano hafifu, jina lake linajulikana. Huyo ni Dk. Remmy au Ramadhani Mtoro Ongala Mungamba ambaye ana asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Remmy ambaye ni Mkurugenzi wa Bendi ya Muziki ya Super Matimila, anajulikana zaidi kutokana na uimbaji wake unaogusa maisha ya ya kila siku ya watu. Mwanamuziki huyu mwenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa muziki wiki hii aliongea na gazeti hili juu ya masuala kadhaa yanayohusiana na maisha yake kama inavyosimuliwa na NEEMA DAWSON.

Dk. Remmy, aliingia nchini Tanzania mwaka 1978. Kwa mujibu wa maelezo yake aliletwa hapa nchini na mwanamuziki mwingine maarufu mwenye asili ya Kikongo, Mzee Makassy ambaye siku hizi ameacha muziki wa dansi na kuwa Mlokole anayeimba nyimbo za dini za Kikristo pekee.

Akiwa ameishia darasa la tano tu, Dk. Remmy mwenye umri wa miaka 53 hivi sasa, ameoa mke Mzungu na amejaliwa kupata naye watoto.

Anaeleza kuwa kisa cha yeye kushindwa kumaliza shule ni kufariki kwa wazazi wake angali mdogo na kumwacha akiwa yatima. Baba yeke, Remmy anaeleza, alifariki wakati yeye akiwa na umri wa miaka minane (8) tu na mama yeke naye akafariki miaka sita baadaye wakati akiwa na umri wa miaka 14, na hapo ndipo aliposhindwa kuendelea na shule.Dk. Remmy alienda wapi baada ya kuachwa yatima? Anasema alichukuliwa na Baba yake mdogo, ambako aliishi maisha ya kunyanyaswa ambayo hatimaye yalimfanya akimbilie mitaani na kuwa ombaomba.

"Baba yangu mdogo alikuwa akiniacha nyumbani, akirudi akikuta paka amekula mboga naambiwa ni mimi. Siku nyingine naenda kuchunga, ngedere wanakula mahindi naambiwa ni mimi," anasema Dk. Remmy ambaye ametunga wimbo kuhusiana na masahibu hayo yaliyomkumba katika maisha.

Nyimbo nyingi alizoimba mwanamuziki huyo zinanukuu Maandiko Matakatifu yaani Biblia. Kwanini Bw. Remmy wewe hupenda kuimba kwa kunukuu Biblia wakati wewe ni Muislamu? Hilo ni swali mojawapo aliloulizwa. "Ni kweli naimba kwa kunukuu Biblia, ni kitabu kizuri; Lakini mimi si Muislamu wala si Mkristo-sina dini," anasema na kuongeza kuwa tangu azaliwe hajawahi kuingia msikitini wala kanisani.

Anasema jina la Ramadahani alipewa na Baba yake mzazi ambaye alikuwa Muislamu, lakini yeye mwenye hajui lolote kuhusu Uislamu. Kadhalika Dk. Remmy ameeleza kuwa hajawahi kuimba nyimbo kwa kutumia Koran ambacho ni Kitabu Kitukufu cha Waislamu kwa vile hakielewi.

Akiwa chokoraa (mtoto wa mtaani) Dk. Remmy alikutana na kujiunga na kikundi cha muziki wa dansi cha Succes Bantou nchini Congo Kinshasa. Aliimba pamoja na bendi hiyo na walimpenda sana kwa vile waligundua ana kipaji kikubwa cha uimbaji, lakini hawakumjali kwa avile alionekana kuwa mtoto tu wa mitaani, kwa hivyo hakunufaika na kazi aliyokuwa akiifanya.

Baadaye ndipo alipokutana na kuchukuliwa na mwanamuziki maarufu Mzee Makassy na kumleta hapa nchini Tanzania akiwa kama kibarua na hatimaye kuweza kufanikiwa kuanzisha bendi yake ya Matimila iliyo na wapigaji wa vyombo 12 na waimbaji 4.

Dk Remmy Ongala maarufu kwa jina la Dokta anasimulia kuwa jina hilo la Dokta alilipata kwa waandishi wa habari kunako miaka ya 1980 baada ya kuimba wimbo uitwao 'Siku ya kufa' uliompa umaarufu mkubwa.

Remmy anasema anaamini kuwa sanaa ya muziki ina nguvu kubwa kwani hata Mitume Paulo na Sila wanatajwa katika Biblia kuwa wakiwa gerezani waliweza kuimba hadi milango ya gereza ikafunguka yenyewe. Yeye pia anaamini kuwa nyimbo zake zina mguso na zimekuwa zikiwaponya wengi kutokana na matatizo mbali mbali ya maisha.

Pamoja na kutokuwa na dini rasmi, Remmy anaamimi kuwa kuna Mungu aliyeumba Mbingu na nchi na kwamba huyo ndiye mwenye mamlaka juu ya vitu vyote.

Remmy anasema anamshukuru Mungu kwa mafanikio aliyoyapata kwani akikumbuka alikotoka na wakati ambao yeye alikuwa akiwafanyia watu kazi na sasa anajifanyia mwenyewe ni jambo la kumfurahisha sana.