Igizo la TAUSI si mali Kenya

WAKATI mchezo wa tamthilia wa TAUSI umeonekana kuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania walio wengi hali hii ni tofauti kwa baadhi ya wakazi wa nchi jirani ya Kenya. Katika makala haya mwandishi Dalphina Rubyema anaelezea zaidi.

"Mimi kwanza nashangaa kuona Watanzania walio wengi wanaufurahia mchezo wa Tausi huku kwetu Kenya hakuna anaye ushabikia mchezo huu na kama kuna wanaoufurahia ni wachache sana" anasema Bi. Betty Kweyu mwenyeji wa Nairobi nchini Kenya.

Bi Kwayu ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini humo anaendelea kusema kuwa wengi wa wakazi wa nchi hiyo hawafurahishwi na mchezo wa Tausi kwa vile hawapendelei lugha ya Kiswahili.

"Kwanza hao wahusika hawatoi ujumbe wao kwa kutumia kiswahili fasaha, isitoshe hata hiyo lugha ya kiswahili kwetu kidogo inatupiga chenga wangekuwa wanatumia kiingereza, nadhani kila mtu angekuwa anaufurahia" anasema wakati alipohojiana na mwandishi wa makala hii jijini Dar es Salaam.

Anaongeza, "hata siku moja huwezi kumkuta mtu anawasha TV eti kuangalia mchezo wa TAUSI. kwanza hata waigizaji wenyewe mimi si waelewi, Who is Dama by the way? anahoji Bi Kweyu kwa mshangao.

Naye Bw. Elichado Kamau Mkazi wa Kikuyu nchini humo anasema kuwa mchezo huo wa TAUSI hauna mvuto sana kwao kwa vile wahusika hujipachika sifa kuwa elimu yao ni ya Chuo Kikuu kitu ambacho alisema siyo cha ukweli.

"Tunakatishwa tamaa na maneno yao ya uongo kwani washiriki hujipachika sifa kuwa wamemaliza Univeristy hivyo mchezo wao ni wa kisomi sisi tunawaelewa sana, kama kuna mtu mwenye digrii kwenye mchezo huo hawazidi watatu" alisema Bw. Kamau ambaye yuko jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Shughuli za kibiashara.

Pamoja na mchezo huo wa Tausi kuonekana kuwa jalala nchini Kenya hapa Tanzania ni kivutio kikubwa wa watoto na wakubwa kwani lugha inayotumika ya kiswahili inaeleweka.

Mchezo huu unavutia zaidi kwa Lindi ambaye anaigiza kama mtoto wa mitaani 'chokoraa' na wenzake Vita na Joto wanaonekana kuwa chachu ya mchezo huo ambao hapa nchini huonyeshwa katika televisheni ya ITV.

Rhoda ambaye anaigiza kama shangazi yake Lindi anaonekana kama mwanamke mwenye roho mbaya ambaye alimfanyia unyama Lindi hadi akaondoka nyumbani kwao kwa kunyanyaswa na shangazi yake Rhoda na baada ya wazazi wake kufariki. na mama yake Lindi ambaye ni marehemu kumtokezea Rhoda kama mzuka na kumuonyesha vituko vya kutisha kwa kumnyanyasa mwanae, Rhoda anaonekana kutoogopa na ndiyo kwanza anaonekana kuzidi kumnyanyasa Lindi.

Katika mchezo huo Bw. Kasri anaonekana akiishi kwa maadili ya kidini ya kiislamu na familia yake yenye watoto watatu wa kike, Sitti, Rukia na Rehema lakini familia hiyo inakuja kubadilika baada ya Bi. Zuri mkewe Kasri kunaonekana kutowapenda watoto wa mumuwe ambao walifiwa na mama yao.

Katika familia hiyo, Sitti anaonekana kupenda sana maadili ya kidini lakini hali hiyo inakuja kubadilika baada ya kujiunga na Chuo Kikuu kwani huko aliweza kukutana na Dama mtoto wa Bw. Sango na Bi. Muhonja ambaye anamfundisha kunywa pombe na hatimaye anafanikiwa kumwingiza katika mapenzi na Mjuba matokeo yake anapata mimba na kufukuzwa nyumbani kwao.

Mjuba ambaye ni kaka yake Dama anapokwenda kumweleza taarifa mama yake Muhonja kuwa anataka kumwoa Sitti, Muhonja anakataa kwani tayari alikuwa na Mchumba Tina Binti wa pekee wa Jesca Brown.Hali hii inamchanganya Sitti kwani Mujuba baada ya kukataliwa na mama yake anaamua kutoroka kwenda Afrika ya Kusini huku nyuma Sitti anaamua kutoa mimba na hatimaye hiyo mimba inamlaani na kuwa kichaa.

Mtoto ni mtoto, Mzee Kasri anaamua kumpeleka Sitti hospitali baada ya kuanguka chini na kuzimia wakati alipokuwa nyumbani kwa Baba yake. Huko Hospitalini Sitti anafokewa kimiujiza hofu inazidi nyumbani kwa kasri.

Washiriki wengine katika mchezo huo ni Kibibi, Ashina, Ondieki, Bw. Sango, Zinzi, Dk. Kurya. Bi. Popo, Master Sugu, Eboso, Sikitu, Mponda na wengine.

Mchezo huu ambao huonyeshwa kila siku ya Jumapili unafurahisha sana Watanzania walio wengi kiasi cha kutaka uonyeshwe kila siku badala ya kuonyeshwa kwa dakika 45 tu.

Hata hivyo baadhi ya washiriki wamejitoa katika mchezo huo akiwemo mshiriki Mkuu Sitti, ambaye kwa hivi anashughulikia biashara zake na Mjuba ambaye amekwendwa Marekani kusoma.