Ususi wa Nywele: Urembo ulioheshimika miaka ya nyuma hadi sasa

Na Dalphina Rubyema

"KWA KWELI vijana wa siku hizi hawatapata kitu cha kujivunia kama enzi zetu sisi. Katika enzi zetu zaidi tulikuwa tunajivunia ususi wa nywele lakini siku hizi vijana wanamitindo ya kuweka dawa badala ya kusuka nywele zao" anasema Bi. Martha Jakono (60) ambaye ni mkazi wa Tabata Liwitini Wilayani Ilala katika mkoa wa Dar es Salaam.

Bibi Martha anaongeza kuwa " Enzi zetu msichana ambaye alikuwa anasuka nywele alikuwa anaheshimika sana kuliko nyie vijana wa siku hizi ambao kuweka dawa mnaona kama fasheni"

"Siyo kwamba tulikuwa hatunyooshi nywele zetu, hapana tulikuwa tunafanya hivyo lakini siyo kwa kutumia madawa makali kama siku hizi na badala yake tulikuwa tunachoma nywele zetu kwa kutumia kitana cha Chuma ama kipande cha mtungi" anasema.

Akifafanua zaidi jinsi gani waliweza kuchoma nywele zao, Bi Martha anasema kuwa walikuwa wanachukua mafuta ya nazi na kujaza kichwani na badala yake hapo waliweka hicho kitana cha chuma ama kipade cha mtungi kilichopasuka kwenye moto mkali.

anaeleza kuwa baada ya hapo walichukua kitambaa na kushika kipande hicho cha mtungi ama kitana na kuanza kuchoma nywele.

"kwa vile kichwani kunakuwa na mafuta ya kutosha mtu anayechoma moto hawezi kuungua hata kama kitana kitakuwa na moto kiasi gani hata kuungua mkono kwa vile kile kitambaa kikubwa unachokuwa umeshikia kitana kinazuia moto huo huo usifike mwilini mwako" anasema.

Bi. Martha ambaye ameweka sheria nyumbani kwake ya kutoweka dawa za kisasa kwa wajukuu wake watatu,Monica (21), Sara (16) na Magreth (14) anasema kuwa yeye binafsi hadi hii leo anamheshimu msichana asiyetumia madawa na anayesuka nywele vizuri.

"Mimi namheshimu sana yule msichana ambaye ana nywele za asili kuliko yule anayeweka madawa ndiyo maana hata wajukuu zangu nawakataza kuweka madawa hayo kwenye vichwa vyao. nashukuru hata wao wameweza kutii amri yangu.

Akitaja aina ya nywele walizokuwa wanasuka wakati wa ujana wao Bi. Martha anasema kuwa mitindo ilikuwa mingi ambapo anataja baadhi yake kuwa ni Upanga wa Jogoo,Nusu Kilimanjaro, Mdomo wa Kuku,Nyota na twende kilioni staili ambayo inaendelea kusukwa hadi hivi leo kwa wanafunzi.Anasema enzi hizo msichana ama mwanamama aliweza kusuka nywele za uzi na kuonekana maridadi.Hata hivyo kulingana na hali halisi, vijana mbalimbali nchini wanaonekana kunogewa na mtindo wa siku hizi ya kuweka madawa kwenye nywele zao, siyo tu kutaka kuonekana nadhifu bali hata kutaka kwenda na wakati.Ingawaje pesa nyingi hutumika kurembesha nywele zao lakini bado wengi wao wanaonekana kutojali hali hiyo pamoja na kwamba wengi bado hawajapata madhara halisi yatokanayo na madawa hayo.

Bibi Kuluthumu Nchimbi (37) mkazi wa Buguruni Malapa yeye anasema kuwa kwa wiki anatumia zaidi ya sh 2000/= kurembesha nywele zake anapozipaka dawa aina ya 'leja Kali'. anasema kuwa mbali na leja vile vile alishawahi kutumia relaksa (Relaxer) aina ya Revolon, Dark in Lovely, TCB pamoja na kutumia mafuta ya Blue Magic, Hair food, Dax, Hair grow na Bima ambayo yananunuliwa kwa pesa nyingi kuanzia sh 800 hadi 3000.

Hata hivyo Bi. Kuluthumu amekiri kuwa madawa ya nywele anayotumia yeye pamoja na watu wengine yana madhara kwani tangu mwaka 1993 alipoanza kuyatumia ana andamwa na maumivu ya kichwa" anasema . Anaongeza kuwa madawa haya na badala yake ataachana nayo ili awe anasuka kwa mitindo kadhaa au awe anavaa wigi kwani madawa yana madhara yake.