IRITUNGU: Ngoma ya Wakurya inayowapandisha mori vijana

lAliyesimangwa hulia na hatimaye kupigana

Na Joseph Sabinus

"Kama mtu ni mwizi, mvivu au malaya; awe wa kike au wa kiume, ni wakati wa ngoma ya Ritungu vijana wanapojitapa ndipo husemwa na kusimangwa. hufikia hatua wengine wakalia, labda kutokana na ulemavu wao, umaskini au basi pengine hata wakidhani labda uyatima wao ndio umekuwa chanzo cha masimango. Mara nyingi huamua kupigana kufuatia muelekeo wa hisia za masimango"

"Mfano,kama mwanangoma amejitapa hata akafichua wazi uvumi uliokuwapo kuwa fulani ana mahusiano mabaya na mkeo; wao husema ALAMOLYA EBHELENGE yaani ANAMSALITI, hapo mwenye mali hupandwa jazba na mori ambayo huhitimishwa kwa ugomvi dhidi ya mbaya wake."

"Ngoma hii inayochezwa huku wana jamii wa rika mbalimbali wakiwemo vijana na wazee wakiishuhudia, huchochea moyo wa ushujaa wa kupambana na adui hususan wezi wa ng’ombe, ushirikiano katika kufanya kazi mbalimbali kama kilimo, ujenzi na ulinzi". Ndivyo alivyosema Bi. Rhobi Fideli (33) mkazi wa kijijini Sirori Simba katika wilaya ya Musoma Vijijini alipozungumza na mwandishi wa makala haya.

Katika ngoma hii inayaochezwa kwa wingi na wakurya wa wilaya za Tarime na Musoma Vijijini, Vijana hupata fursa ya kujitangaza kuwa wako tayari kuoa au kuolewa na hata kila mmoja wao hutaka aoneshe ujasiri wake na kwamba haogopi kitu na yuko tayari kupambana na adui yeyote anayepinga maendeleo yao.

Ngoma ya Iritungu hutumika hasa baada ya vijana kutoka jandoni na sherehe mbalimbali zinazokwenda sambamba na shughuli za jando, harusi, mavuno na hata viongozi mbalimbali wa serikali ngazi ya taifa hupendelea kuitazama na kuishiriki wanapoiona uwanjani " ikifanya vitu vyake"

"Ma-Dj" wa ngoma hii ya wenzetu wakurya hutumia gitaa la kmba nane (ritungu), Vibuyu viwili vinavyowekwa aina fulani ya mbegu au changarawe ili kutoa sauti vinapotikiswa, filimbi ndefu za matundu na hizi za kawida, pamoja na makopo yanayofungwa miguuni mwa mpiga filimbi. (amaghoroo).

Mpiga ritungu pia huwa na fimbo yenye aina fulani ya vikopo maalumu vyenye vyuma ndani yake vinavyofungwa kwenye fimbo hiyo anayoitikisa kwa kutumia dole gumba la mguu na hivyo kutoa sauti nzuri inayomithilishwa na sauti za kengele ndogo za kanisani.

kwa kawaida ngoma hii inayoimbwa kwa lugha asilia ya Kikurya ikiwa na maudhui mbalimbali kutegemea wakati na tukio husika, huchezwa huku wasichana wakiwa vifua wazi na hali wamejifunga vazi rasmi la kanga kwa mtindo maalum.

Wavulana hujipanga katika mstari kila baada ya idadi kadhaa ya nyimbo na ndipo kila msichana huenda kumchagua mvulana anayemtaka ili acheze naye. Mtindo huo huitwa kwa Kikurya "cholo"

Wavulana huwa na kawaida ya kuwa na silaha kama rungu, shoka, panga au fimbo ambazo hucheza huku wamezishikilia mikononi; wakiruka na kuzirusha shingo zao nyuma na mbele.Kwa watazamaji wageni, mchezo huu huogopesha na hata kuonekana kuwa huwachosha wanangoma.

Lakini kwa wenyeji, ni ngoma inayofurahisha, inayovutia na isiyochosha kabisa.

Inapotokea mara kwa mara msichana akamchagua mvulana mmoja tu kucheza nae, hisia nyingi tofauti huanza kujengeka miongoni mwa wanajamii na hata wenyewe kwa wenyewe yaani mvulana na msichana huanza kutazamana kwa "aibu za kishujaa" na hapo mara nyingi huwa chanzo na kichocheo kikubwa cha ndoa za kutoroshana kwa vijana hao.

Hii haina maana kwamba ndio makusudio ya ngoma hiyo , bali hali hii hukemewa na kulaaniwa na jamii husika kwani ndoa hizo huwa ni kinyume cha maadili ya ndoa za Kikurya.

Mara nyingi hutokea kwamba kijana wa kiume ambaye hachaguliwi katika cholo, hujisikia chuki na moyo wa wivu kumtawala. Hivyo, huamua "kuzua vagi" dhidi ya yule mwenye bahati "inayomtilia usiku" hapo pia ugomvi mkubwa mara nyingi huweza kutokea.

"Kijana mmoja anaitwa Kisile wa kijiji cha Kitaramanka kule Musoma aliwahi kupigwa kwa kiboko cha kiboko kwa kuwa eti wasichana wengi walikuwa wanamchagua katika cholo kwa wakati mmoja na hali vijana wengine wakiwa hawapati msichana hata mmoja," alisema Mgaya Brown Wambura alipozungumzia ngoma hiyo.

Ingawa ni vema kudumisha ngoma hiyo inayochochea ujasiri, ushujaa, ushirikiano na mengine mengi mazuri, ni vema jamiii husika ya Wakurya ikakaa chini na kuchambua kuyatoa mabaya yote yaliyomo na yale yalipitwa na wakati kama kama ugomvi na kwenda kucheza ukiwa na silaha hali inayoweza kuhatarisha amani na usalama wa watazamaji na wachezaji wenyewe.