ELATIM : Ngoma ya Kimasai

Elatim ni ngoma ya Wamasai inayochezwa na vijana ambao tayari wameshatahiriwa na wala ngoma hii haichezwi na watoto wadogo,au wakati mwingine huchezwa na wasichana wanaokwenda jandoni kuchezwa ambao ni vigori (tayari wameshavunja ungo).

Ngoma hii pia huchezwa na watu wazima (wazee wenye umri mkubwa) wakati wanapong’atuka katika madaraka mbalimbali ambayo walikuwa wamepangiwa na wanakijiji na wakati mwingine wazee hao huwafundisha vijana ni jinsi gani ya kucheza.

"Elatim wakati mwingine huchezwa na wasichana wale wadogo ambao hupelekwa jandoni kwa ajili ya mafunzo ya kuwa wao sasa ni watu wakubwa wanapaswa kufanya nini na nini hawapaswi kufanya wakati wa ngoma hiyo ikipigwa huchezwa au kuongozwa na kiongozi wa msafara huo ambaye huwa tayari alishavunja ungo muda mrefu(mwali)".Ndivyo alivyosema Bwana Efata Abedlinego (49) mkazi wa Mbagala mision jijini Dar es Salaam alipozungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni.

Katika ngoma hii ambayo huchezwa kwa mori na kabila la wamasai ambao ni wenyeji wa mkoa wa hususani karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania.kawa vijana hapo ndio huwa muda wao mzuri kujitangaza na kutafuta mchumba (hasa kwa wasichana) kwani hapo huweza kujichagulia kijana ambaye ni mkakamavu na aliye tayari kuilinda na kuitunza familia yake pamoja na mifugo yao .

"kwetu Arusha, wakati mvulana anatoka jandoni hucheza ngoma hii kwa uhodari ili aweze kupata mchumba haraka haraka, na wala sio kama huku Dar es Salaam naona baadhi ya wasichana au wavulana wa kimasai wakioana bila ya kufuata mila na desturi"alisema Bw.Abedlinego.

Aidha bw.Abed linego alisema kuwa ngoma hiyo kwa vijana huchezwa kila baada ya miaka saba tangu noma nyingine kuchezwa, "Elatim inapochezwa huwa na maana kuwa kuwa vijana ambao hutoka jandoni ni safi yaani wamesafishwa(wametahiriwa)" alisema na kuongeza kuwa "lakini kwa upande wa wasichana ngoma hii kuchezwa wasichana wanapovunja ungo.

Ngoma ya Elatim mbali na kutumika katika sherehe za kwenda au kutoka jandoni na sherehe mbalimbali ambazo huenda sambamba na shughuli za jando pia hupigwa kukitaarifu kijiji kingine kuhusu wizi wa mifugo endapo umetokea kijijini hapo.

Alisema familia fulani ikigundua kuwa imeibiwa mifugo (mara nyingi huwa ni ng’ombe) hutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye huwatangazia wanakijiji na wakifika nyumbani kwa mwenyekiti huanza kupiga ngoma hiyo ambayo kijiji cha jirani kikisikia huwa tayari kwa kuangalia mifugo itakayoingia kwa muda huo kijijini hapo na hivyo kutoleana ushirikiano wa kudhibiti wizi huo usifanikiwe.

Ingawa ipo haja kubwa, kuepukana na mila mbaya zilizopo katika baadhi ya tamaduni zetu halisi za kitanzania, kama vile kucheza hali umevaa mavazi nusu uchi,kuwa na silaha kali ngomani ambazo ni hatari kwa usalama wa wachezaji hata watazamaji, ni vyema Watanzania wakajivunia mila,desuri na zile tamaduni zao nzuri zisizo na athari mbaya katika jamii badala ya kubobea katika kuigiza mambo ya kigeni. wamasai wa Watanzania wanajitahidi kujivunia utamaduni wao ingawa unazo kasoro za hapa na pale zinazohitaji kurekebishwa ili kwenda na wakati.