LAS VEGAS; Vinyozi walioibuka kwa vishindo

"Siku moja kabla ya sikukuu na hata zile za siku za wikiendi ama kweli; uongo . Hizo ni siku tunazojivunia usanii wetu katika kunyoa mitindo mbalimbali.

Ni siku zinazotufanya tuamini kwa kuwa wanaorandaranda mitaani ovyo wakisingizia ukosefu wa ajira, wanafanya makusudi na Serikali na jamii kwa ujumla hawana budi kuwadhibiti".

"Mfano, 24/12 mwaka jana tulipata wateja 46 tuliwanyoa tangu asubuhi hadi saa 6 usiku. Hizi wikiendi nyingine tunapata wateja kati ya 15-20 kwa siku na zile siku nyingine za kawaida hupata 8-12 na siku mbaya pengine tunaambulia wateja watano tu"

Ndivyo walivyosema vinyozi maarufu wa Las Vegas Hair Cutting Saloon, iliyopo Keko Machungwa jijini Dar es Salaam.

Vijana hao Salehe Mohamed maafuru kwa jina la Ngozi (30) na Nassib Hussein (26), wanaitaja siku ya jumatatu kama ni siku mbaya zaidi katika biashara yao na wanasema wameamua kuitumia kwa mapumziko.

Wasanii hao maarufu kwa mitindo ya unyoaji ikiwemo English Style, Afro - Style, Push Back, American Base na Cutting za mitindo mbalimbali, wanasema usanii wao hawakuupata katika darasa lolote, bali tu ni kipaji kilichochowewa na utundu wao tangu wadogo na wanataja gharama za unyoaji kuwa ni Sh 500/= kwa wakubwa na gharama ya kunyolea watoto na ndevu ni sh 300/=.

"Utundu wa kunyoa niliuanza kwa kujifundisha mwenyewe wakati tukicheza tangu utoto wangu nikiwa shule ya Msingi Jeshi la Wokovu hadi 1985 na hata 1990 baada ya kumaliza Form Four, Kibasila niliendelea nao na watu wakazidi kunisifia nami nikaongeza bidii" anasema Bw. Ngozi.

Naye Salehe anasema, "Hata mimi usanii wa kunyoa sikuusomea popote. Tulianza kwa kunyoana kimchezo tukiwa wadogo lakini hadi nilipomaliza Kigoma Sekondari 1994 wanafunzi wengi walikuwa wananisifu na kunitegemea niwanyoe".

Wakilielezea gazeti hili namna walivyoanza na kujiunga na Sanaa hiyo, Bw. Salehe alisema hivi karibuni, "Licha ya kuwa na Form IV tuliona tukianza kutafuta ajira ofisini, kuni zitaisha hali mboga haijaiva, tukatafuta kazi yenye mtaji mdogo tuiwezayo (hakutaja kiasi) tukaiona hii iliyopo kwenye damu zetu"

Wanasema walianza kwa kutumia vifaa duni mno vya kunyolea lakini kutokana na utaalamu wao na kuipenda kazi wakapata wateja wengi kwa muda mfupi na kuachana na ofisi walioanzishia chini ya miti na sasa wako katika hali nzuri.

"Moyo wa kuithamini kazi yetu ndio umesababisha leo tunatumia ofisi nzuri kama hii yenye feni na vifaa vingi vya kisasa.

ili kuondokana na maambukizo ya magonjwa ya ngozi kama upele, mba na fangasi lazima tunawekea dawa wateja baada ya kunyolewa" alisema Nassib

Wanasema tatizo kubwa linalowakabiri ni kushindwa kuwafundisha vijana wengine ili wajiunge nao.

"Hakuna mteja anayekubali kinyozi ajifunzie kwake na pia hawataki kunyolewa na mtu wasiyemfahamu, ili ajiunge inabidi akae zaidi ya miezi 3 ili azoeleke kuwa ni wa hapa" alisema Salehe.

Tatizo lingine ni baadhi ya wateja kukopa na wanapodaiwa huwa wakali wengine ni wale wanaonyolewa kisha wanadai wamenyolewa nywele nyingi, "Hao sisi huamua kuacha bila kuwadai" akaongeza Salehe.

Wanyoaji hao maarufu ambao wateja wao wakubwa ni askari polisi, na vijana wengine na wanasema kazi hiyo imewanufaisha sana hata kuwasomesha ndugu zao na kuwapa mahitaji ya kila siku.

Wanasema wanatarajia kupanua ofisi yao na kutafuta uwezekano wa kufunza na kutoa ajira kwa vijana wenzao wenye moyo wa uchapakazi. "Hata Mungu aliagiza asiyefanya kazi asilia na pia unamsaidia mwenye nia na mwelekeo wa kusaidiwa" anaongeza .

Wanatoa wito kwa jamii kuzithamini kazi halali za wenzao na kuongeza kuwa ingawa Serikali inahimiza vijana kujiunga katika vikundi ili kupata misaada mbalimbali ikiwemo mikopo, yale mazingira yanayokuza wigo wa rushwa na "Undugunization" yaondolewe maana wanadai uchunguzi wao umebainisha kuwa wanaokopesha ni wenye ndugu na refa katika ofisi husika na hivyo hao ndio wanakingiwa vifua.

Wanasema hali hii itapunguza kasi ya vijana kuzamia katika uhalifu.