Watoto wa mitaani Dogodogo Centre waimbaji wanaotia majonzi

INGAWA baadhi ya wanajamii wamekuwa wakiwachukulia watoto wa mitaani kama watu wasioweza kufanya lolote zuri, dhana hiyo potofu inapingwa vikali na usanii mahiri ulio bayana kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Dogodogo Center cha jijini Dar es Salaam. Watoto hao hutumia vipaji vyao katika kupanga na kutoa sauti nzuri katika nyimbo zinatia majonzi na kutoa mafunzo kadhaa kwa jamii namna ya kuwalea na kuwaendeleza.

Watoto hao wa mitaani maarufu kwa jina la Chokoraa kule nchini Kenya, wamekuwa wakiimba kwa kutumia magita ya kisasa, marimba na vinanda na hivyo kuweka historia kwa nchi ya Tanzania kwa uimbaji wao wa kuvutia unaozungumzia mazingira yaliyowakabili hata kuwapelekea kulelewa hapo.

Uimbaji wa Watoto hao mitaani ambao ni wa kutumia magitaa na kinanda, unafanywa na watoto hao ambao hazina hiyo ikitunzwa vizuri ni faida na manufaa kwa taifa la Tanzania na jamii nzima kwani zipo siri nyingi lakini moja wapo ni kule kuzingatia umuhimu wa usanii na michezo kwa watoto kwa ajili yakukuza upeo na uwezo wa akili.

Watoto hao ambao wengi wao wamebahatika kusoma ikiwa ni pamoja na masuala ya ufundi katika vyuo kadhaa vya ufundi kikiwemo Chang’ombe kinachomilikiwa na kituo hicho na wengine kusomeshwa shule za msingi,

Mwalimu na msanii wa kikundi Bw. Shadrack Masaga alisema tangu alipoanza kukifundisha kituo mwaka 1997 kikiwa na watoto wanne na sasa kinao 14,anazidi kukiri kuwa watoto hao wa mitaani wanavyo vipaji vingi vilivyofichika hivyo jamii haina budi kuviendeleza kwani hata idadi yao katika kikundi hichi inazidi kuongezeka na wanang’aa zaidi wanapotumbuiza katika shughuli maalumu kama vile kwa mabalozi.

Miongoni mwa nyimbo zilizoimbwa na chokoraa hao na kutia majonzi yaliyowatoa watu machozi ni ule usemao, "Watoto wote wana haki sawa si wa kike si wa kiume; wote wana haki sawa. Watoto wanatakiwa wapewe elimu na malezi yaliyo bora.watoto ni warithi wa nchi hii hivyo haki zao lazima wazipate"

Hata hivyo alisema tatizo kubwa linalokikabiri kituo hicho kinachisimamiwa na Bw. Nicholaus Shemsa, ni baadhi ya watoto kukaidi na kukwepa kwenda shule wanapofikisha umri unaotakiwa na wengi wao wakipendelea michezo na usanii mbalimbali kama huu wa uimbaji.

Bw. Shadrack Masanga anatoa wito kwa jamii kutambua na kuvithamini vipaji vya watoto hao kwani vingi vimefichika kutokana na mazingira magumu wanayokabiliana nayona hivyo kujenga moyo wa kuwasaidia