Ufundi wa majamvi unanisaidia katika Kilimo - Chacha

"Watu wanapendelea ufundi wangu na hata vitu hivi kwa kuwa hapa Tarime majamvi hayatumiki kuuzia mitumba tu, bali hata wengine wanayatumia kulalia kama godoro na kitanda na hata wengine wanayotumia kama pazia au Celing board.

Pamoja na kupendelea bidhaa zangu sifanyi choyo maana maarifa hayahitaji Choyo na ndiyo maana nimeshawafundisha watu wengi namna ya kuyatengeneza. Siwezi kuwa mchoyo maana na mimi nilifundishwa na Mkenya wa Turkana" Ndivyo Bw. John Chacha (32) mkazi wa kijijini Magena alivyoliambia gazeti hili wilayani kwake .

alisema sanaa hii aliyoianza mwaka 1984, baada ya kuhitimu elimu ya msingi Shuleni Magena, imemfanya yeye mkewe na mtoto wao waishi maisha ya raha na kuchochea mafanikio katika kilimo chake.

Anaongeza kuwa kipato chake kilichangia mahari ya kumuolea mke huyo.

"Kwa mtaji huu, ninategemea kujenga nyumba ya kisasa miaka miwili ijayo na pia nianze kuuza dagaa kwa wingi" anasema.

Akizungumzia soko la kazi ya sanaa yake ya utengenezaji majamvi , ambayo huyatengeneza kwa kuhitaji kamba za nyuzi za katani, matende anayokata mtoni na kuyaunganisha kwa sindano baada ya kuyaanika juani kwa juma moja na kisha kuyashona nyuzi tatu katikati na pembeni,

Bw. Chacha alisema huuzia nje ya soko kuu la Tarime kila Jumapili (siku ya Gulio) na wateja wengine humfuata nyumbani mmoja mmoja kutokana na ustadi na ubora waliogundua katika sanaa yake.

"Nyuzi ninazonunua za Sh 1800/= hutengeneza majamvi makubwa 20 na mimi huuza kati ya sh 250/= hadi 600/= kwa lile kubwa. kwa wiki naweza kutengeneza majamvi madogo 40 na makubwa 20 "mimi ni fundi mzoefu bwana" alijitapa Chacha.

Aliyataja matatizo anayopambana nayo katika kuendeleza kipaji cha usanii wake na kujipunguzia ukali wa maisha kuwa ni pamoja na kunusurika kung'atwa na nyoka katika mito hususan Nyamusi wenye nyoka wengi, maji kufurika mtoni na hata ndugu wengine kupenda kupewa jamvi bure au kukopa bila kukumbuka kulipa.

"Hata hivyo inabidi uwe mvumilivu ili ufanye mambo yako," anasema.

Aliwashauri vijana kutokung'ang'ania vitendo vya uhalifu na kutafuta kuajiriwa ofisini tu bali wajiunge katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali na kujiwekea malengo mazuri ya siku zao za usoni. Analaani mno kitendo cha vijna kujikalia vijiweni na kipiga zogo na kukielezea kuwa ndicho huwakaribishia mawazo ya uhalifu