Michezo

Baada ya kushinda katika uchaguzi

 Viongozi Simba wasema wana usongo na Yanga

lWaiomba FAT wawakutanishe

Viongozi wapya waliochaguliwa kuiongoza klabu ya Simba ya jijini wamesema moja ya usongo walio nao, ni kukutana na watani wao wa jadi yanga, ili waoneshe umahiri wao katika nafasi walizopata.

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Juma Salum, alisema kazi ya kwanza itakuwa ni kuisambaratisha klabu ya Yanga na ya pili itakuwa ni kuirekebisha katiba ya klabu ili kuwa kampuni.

Salum alisema kuwa ushindi wao katika uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita, hautakamilika na kuwa na maana kwao hadi watakapoifunga Yanga.

"Tutakiomba chama cha soka nchini(FAT), kitukutanishe na Yanga ili tuoneshe uwezo wetu kwa umma," alisema.

Aliitahadharisha timu pinzani ya Yanga kuwa tayari na kipigo toka Simba kwa kuwa muda wa mgogoro ndani ya klabu yao, umepita.

Naye katibu Mkuu wa klabu hiyo, Kassim Dewji, alitamba na kusema, "Wasipokuwa makini, hawa wapinzani wetu watasambaratika kabisa, Simba ya sasa ni balaa."

Alisema watafurahi sana kama FAT itaipanga klabu yao na Yanga kweye mechi ya kwanza ya ligi ya mabingwa itayoshirikisha timu 8 bora toka katika ligi ya sasa ya makundi.

Dewji alisema, Simba ina nafasi ya kuongoza kwenye kundi lake la Nyanda za Juu Kusini, linalozishirikisha timu za Simba, Majimaji, Prisons, Tukuyu Stars na Lipuli ya Iringa.

Hadi sasa Simba yenye makao makuu yake katika mtaa wa Msimbazi jijini inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi saba (7) na mabao nane ya kufunga ikiwa imefungwa mabao matatu tu.

Simba imepata viongozi wapya Jumapili iliyopita baada ya kudumu katika mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka mitatu na hivyo kushindwa kushiriki michuano ya Kimataifa.

Uturuki yaiangukia Uingereza

LONDON , Uingereza.

ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya mpambano wenye uhasama kuchezwa mjini London Uingereza Alhamisi hii, Serikali ya Uturuki imeomba radhi rasmi Uingereza.

Taarifa iliyotolewa juzi na Serikali ya Uingereza na kukaririwa na Televisheni ya Sky ilisema kuwa, Uturuki imetuma ujumbe rasmi kwa Uingereza na kuomba radhi kufuatia kitendo kilichofanywa na mashabiki wa timu ya Calatasaray cha kuwashambulia wenzao wa Leeds na kusababisha wawili kupoteza maisha katika vurugu hizo.

Taarifa imesema kitendo hicho ni cha aibu kwa serikali na wananchi wa Uturuki na hakitatokea tena kwenye ulimwengu wa Soka.

Hatua ya Uturuki kuiomba radhi Serikali ya Uingereza na chama cha soka cha nchi hiyo, FA, imetafsiriwa kuwa ni cha kupunguza hasira za Waingereza ambao waliapa kulipa kisasi katika pambano la marudiano Alhamisi hii mjini London.

Nalo Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA ), juzi usiku lilitoa uamuzi wa kuwaruhusu mashabiki wachache wa Calatasaray kwenda Uingereza kushangilia timu yao.

Taarifa ya shirikisho hilo imesema, hali ya usalama katika pambano hilo sio ya kuaminika hivyo ni vyema mashabiki wachache wakaenda ili kuepuka hatari inayoweza kuwakumba zaidi.

Aidha, UEFA imeitaka Uingereza kuweka hali nzuri ya usalama katika pambano hilo ili kuhakikisha hakuna hali ya kulipizana kisasi.

Awali mashabiki wa Uingereza waliapa kulipa kisasi katika pambano la marudiano mjini London kwa kile walichodai ni kulipa damu za wenzao zilizomwagwa huko Uturuki.

Katika pambano hilo Leeds inapaswa kushinda zaidi ya mabao 2-0 ili iweze kusonga mbele.

Katika mapambano mengine ya michuano ya Ulaya, timu ya Manchester United ya Uingereza, mwishoni mwa wiki itakuwa na kazi kubwa ya kuikabili timu ya Real Madred ya Hispania katika uwanja wake wa nyumbani wa OLD Tranford.

Katika pambano la awali mjini Madred, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na hivyo kuipa nafasi ya mabao ya ugenini yanayohesabiwa mawili, lakini Manchester nayo ikishangiliwa na mashabiki wake waliozoea ushindi.

Cheasea itakuwa ugenini mwishoni mwa juma ikipambana na Bacelona mjini Hispania. Mechi ya kwanza, Cheasea ilishinda mabao 3-1 nyumbani Uingereza lakini Bacelona ikatamba kuiondoa kwenye mechi ya marudiano mjini Bacelona.