Michezo

kuuawa kwa mashabiki wa leeds:

Waingereza waapa kulipa kisasi

London, Uingereza

Kufuatia kuuawa kwa mashabiki wawili wa Timu ya Leeds ya Uingereza katika mapigano nchini Uturuki juzi, Waingereza wameapa kulipiza kisasi.

Wakizungumza kwa hasira mwishoni mwa juma, mashabiki wa Leeds waliofurika kwenye Uwanja wa Ndege mjini London, kuipokea timu yao walisema kuwa damu ya wenzao wawili iliyo mwagaika Uturuki lazima italipwa.

Walikaririwa na Televisheni ya SKY wakisema kuwa wao wanasubiri kulipiza kisasi katika mechi ya marudiano itakayochezwa mjini London wiki mbili zijazo.

"Tutapiga yeyote atakaye kuja na timu ya Galatasaray hapa London hata kama atakuwa ni Polisi,".alisikika akisema mmoja wa washabiki hao wenye hasira.

Mashabiki wawili wa timu ya Leeds ya Uingerza waliuawa juzi katika mapigano na wale wa timu ya Galatasaray nchini Uturuki walipokuwa wamekwenda kushangilia timu yao kwenye mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Ulaya.

Katika mechi hiyo iliyochezwa Alhamisi usiku, Leeds ilifungwa mabao 2-0 na wakadai kuwa mabao hayo yalisababishwa na hofu waliyokuwa nayo.

Tayari Chama cha Soka cha Uingereza kulalamikia kipigo hicho cha washabiki wake na kimeonya kuwa hatua zisipochukuliwa, basi huenda soka ya Ulaya ikaingia dosari.

Hata hiyo baadhi ya wataalam wa soka wanadai kuwa Uingereza imeonja adha ya ghasia ambazo washabiki wake wamekuwa wakifanya kila wakati.

Walitoa mfano wa mwaka jana ambapo walianzisha ghasia huko Itali walipokwenda kucheza mechi za awali za Klabu Bingwa ya Ulaya.

Pia washabiki wa soka wa London walileta kasheshe kubwa kwenye fainali za kombe la Dunia nchini Ufaransa mwaka 1998 mjini Paris Ufaransa.

Simba nayo kuwa Kampuni

Na Mwandishi Wetu

Klabu ya Simba ya jijini, inatarajiwa kuwa kampuni kuanzia mwezi Mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mpango huo Bw. Zuberi Athumani, Katibu wa zamani wa Simba Kassimu Dewji ameandaliwa rasmi kugombea nafasi ya Katibu Mkuu kwenye uchaguzi wa klabu hiyo Jumapili hii ili kuongoza mabadiliko hayo.

Mbali ya Dewji pia mweka hazina wa zamani Ayubu Semvua naye ameandaliwa kushika nafasi ya katibu msaidizi ili kuratibu mabandiliko hayo.

Kassimu na Semvua tayari wamepitishwa na Baraza la Michezo la Wilaya ya Ilala kuwania nafasi hizo pamoja na wanachama wengine 43.

Uchunguzi ulifanywa na Gazeti hili umebaini kuwa kampeni hiyo ya kuifanya klabu ya Simba kuwa kampuni inaongozwa na wafanya biashara wakubwa ambao wako tayari kununua hisa.

Mmoja wa wafayabiashara hao ni Mohamed Dewji ambaye Kampuni yake inaifadhili Simba kwa gharama ya sh. Milioni 130.

Uchaguzi wa Simba unaofanyika kesho unafuatia kuwekwa bechi baadhi ya viongozi na Msajili wa Vyama vya michezo nchini Bw. Leonard Thadeo kwa kosa la kukiuka Katiba ya klabu.

Aidha ,mratibu huyo alikiri kuwa mpango wa kuibadili Simba kuwa kampuni umeandaliwa na wanachama waliojaribu kufanya mapinduzi hivi karibuni na kushindwa.

"Sasa tumekubali kuwa mabadiliko ya Simba kuwa kampuni ni lazima ili kuweza kuendelea katika kipindi hiki cha uchumi huria," alisema Athumani na kuogeza kuwa ili hilo litakelezwe wamelazimika kuaanda watu wenye uwezo mkubwa wa uongozi na elimu kushika madaraka.

Mabadiliko ya Simba kuwa kampuni yanafuatia mabadiliko kama hayo yaliyofanywa na watani wao wa jadi Yanga chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa kamati ya muda Abassi Tarimba.

Mbali ya Mohamed Dewji pia imeelezwa kuwa wapo baadhi ya wabunge wa jijini ambao wapo tayari kununua hisa katika klabu hiyo mara tu, baada ya kubadilishwa kuwa kampuni.