ijue ngoma ya Wamakua inawahusisha vikongwe wa miaka 55

Na Getruda Madebwe

"Unajua watu wengi hufikiri kuwa watu ambao ni wazee hawawezi kucheza; hiyo si kweli kabisa kwa sababu kwetu sisi, ngoma huchezwa zaidi na watu ambao ni wazee wa umri kati ya miaka 50-55"

"Sio kwamba vijana hawapo, la! ila tu ni kwa sabau wazee ndio wanaojua kila aina ya ngoma inayochezwa, inachezwa kwa wakati gani."

Ndivyo Bi. Editha Ndimbo mkazi wa Kunduchi Mtongani jijini Dar-es-Salaam alivyoanza kuielezea ngona ya kabila la Wamakua wakati alipozungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni jijini.

Alisema mara chache ngoma hii huchezwa na vijana endapo tu, wazee hao wana shughuli zingine za kufanya zilizowalazimisha kushindwa kuishiriki kwa kipindi kinachotakiwa.

Shughuli hizo muhimu mara nyingi huwa kama zile za kilimo hasa wakati wapalizi za mazao au wakati wa kuvuna.

Pia ngoma hiyo wachezaji wake huwa wanavalia kanga kwa ndani pamoja na mashuka meusi maarufu kwa jina la kaniki ambayo huvaliwa sehemu za kiunoni pamoja na shanga ambazo huvaliwa shingoni na kichwani.

"Mavazi ambayo wanayatumia wanapocheza hii ngoma ni kanga hata pamoja na mashuka meusi, watu wanayaita kaniki. Vazi lingine naweza kusema ni shanga ambazo mchezaji huvaa shingoni na kichwani," alisema Bi Editha.

Katika ngoma hii ambayo huchezwa na kabila la Wamakua ambao ni maarufu katika ngoma yao hiyo, nihu toka sehemu za Miruchi katika wilayani Masasi, pamoja na wale wa mkoa wa Lindi.

Huo ndio muda mzuri kwa upande wa wazee kukutana na wazee wenzao kuzungumzia mambo mbalimbali yanayowahusu na kujadili yanayopaswa kufanyika pindi wanapomaliza kucheza ngoma.

Inapotokea mmoja kati yao akawa na sherehe au shughuli muhimu kama hiyo katika siku ambayo imepangwa, huwafahamisha wenzake kwa kuwa ndio wakati muafaka wa kufahamishana mambo yanayo kuwa na umuhimu kama hayo ya kifamilia.

"Wazee wakikutana kwenye sherehe ya mtu mzee mwingine, ndipo hapo sasa wanaweza kufahamishana kama kuna mwenzao ambaye ana sherehe siku fulani, au mwezi fulani, labda unaofuata.

Kama ana mazao yake shambani ambayo sasa yako tayari kuvunwa, huu unakuwa muda mzuri wa kuwaambia kwa kuwa watu wengi watakuwepo kwenye sherehe yake kuliko hata kule ngomani ambako walipata taarifa hizo."alisema Bi Editha.

Alisema kuwa ngoma hii haina kipindi maalumu kwani wakati wowote mtu akiihitaji, huwafahamisha watu ili mradi tu, awe na chakula pamoja na vinywaji asilia.

Alizidi kusema kuwa, familia yoyote ambayo haina mtu anayewahusu katika wachezaji hao hulazimika kulipia gharama za fedha ambayo hutumika kwa ajili ya kununulia ngoma pamoja na shanga.