Make your own free website on Tripod.com

Riwaya

Ni nani mbaya wangu?(3)

Naomba uondoke haraka kabla Mama-Chacha hajarudi". akamaliza na kuondoka.

Sikumjibu lolote. Niliona hamna namna nikasimama na kuondoka kuelekea kwa shangazi yangu kabla usiku haujaingia.

Nilianza kuwaza na kuangaika sana moyoni. Nilihofu kuna hatari Philipo akanigeuzia kibao. Nilijishauri kurudi kwa mume wangu Denis lakini niliogopa kuaibika hasa nilipokumbuka barua ya kashfa niliyomwandikia Denis na kuiacha mezani ili aisome pindi atakaporudi toka kibaruani.

Saa kumi na mbili barabara niliingia nyumbani kwa shangazi. Wote niliwakuta yeye na mumewe. Walishangaa sana kuniona ninaingia jioni ile na begi langu la kaki. Hata hivyo walinikaribisha kwa mikoni miwili.

Baada ya muda si mrefu wenyeji wangu na hasa shangazi alianza kuniuliza zaidi juu ya ugeni wangu. Na katika hali ya kawaida, unapomwona mtu amekuja nyumbani kwako ghafla, ni sharti umuulize ujio wake ni wa namna gani .

Shangazi nae alinihoji maswali kama mawili hivi lakini sikuweza kujibu kitu nilikuwa bado nina wasiwasi na sikujua nianzie wapi kujieleza.

"Hivi wewe mwanangu Hawa akili yako imekalia wapi!? Yani leo ninakuuliza hujibu unanikodolea macho tu kama vile haunifahamu! Hebu tueleze au kuna tatizo lolote?". aliuliza shangazi tena kwa ukali sana.

"Hapana Shangazi, sina habari mbaya sana ila tu nimekuja hapa kujihifadhi baada ya Denis kunitimua kuwa niondoke kwake eti kwa kuwa sijamzalia mtoto".

Nikaona nimfunge kamba shangazi ili anipe walau hifadhi ya muda wakati ninatafuta ufumbuzi mwingine.

"Laa! mtoto wewe, hebu nieleze vizuri usinitanie.Yani jinsi Denis anavyokupenda vile, leo amepagawa vipi mpaka kufikia uamuzi wa kukufukuza? Hapana., huo ni uongo mtupu.Bado sijaamini yani" alisikitika sana

Shangazi aliamini na kuzingatia kuwa Denis si mwepesi wa kuchukua uamuzi wa kipuuzi hivyo. Akakubali niendelee kuishi hadi hapo hali halisi itakapojulikana.

Denis alinipenda sana na ninajua dhahiri kuwa alisikitishwa sana na uamuzi wangu wa kumtoroka mtoto wa watu! iSijui alitumia mbinu gani laki, ilimbidi apeleleze kwa kina hadi akajua ni mahali gani nilikuwa nimekimbilia.

Ni baadaye nilipotambua kuwa kazi hiyo aliifanya kwa muda wa siku tatu bila mafanikio wala kujua nilikuwa wapi. Siku ya nne pasipo kuamini macho yangu huku nukiandaa chakula cha mchana nyumbani kwa shangazi, ninamuona mtu amesima.akitazama huku nikipepeta ule mchele pale nje.

Nae anaonekana mtu asiye yaamini macho yake. Hata kipofu angeweza kumuona na kujua wazi kuwa Denis alikuwa analia kilio cha moyoni. tena kiliocha majuto. Haamini macho yake baada ya kuniona pale.

Aibu iliniongezeka hasa baada ya kuona amemkuta shangazi na sasa ukweli au uongo, vitabainika wazi. Sikujua na nilishindwa kujua sasa nitaongea nini mbele yao.

nilitamani kutoroka kwa kuwa uongo wangu sasa unakwenda kujulikana na kuniharibia jina zaidi. Nikajiona niko Jehanamu ya namna yake.

Chakula kilikuwa tayari na wote niliwakaribisha mezani wakati huo mwili nilihisi kutokuwa wangu. Nilifikiri na kujiuliza kuwa endapo mambo yataniwia magumu nitakimbilia wapi?

Hata hivyo, nilimwomba Mungu kimoyomoyo aniepushie dhoruba ya kila namna. Nilisahau kuwa maovu ninayoyafanya yanaweza kufanya maombi yangu yasiitikiwe na Mwenyezi Mungu.

Denis akakataa chakula kwa madai kuwa hajisikii. Ni dhahili kuwa Denis alikuwa amegubikwa na mshangao ulioajaa huzuni isiyosimulika.

Nadhani alikuwa ameijia kitu kimoja peke yake; kunifuata mimi Hawa .Sura yake ilionekana mithili ya mtu iliyefiwa na mwanaye wa pekee hali iliyonifanya nimhurumie kiasi kwamba ningeweza kumrudia. Lakini, wapi; walishamaliza Waswahili waliposema sikio la kufa, halisikii dawa."

Zilipita dakika kama nne hivi tangu tulipomaliza kupata lunch. Baadaye shangazi akatuita wote na Denis, na mumewe. Akatuomba tuketi.

Nilijiona kama niko uchi wa mnyama. Nikajihisi mapigo ya moyo kutowajibika sawa sawa. Usione ajabu nikikueleza kuwa muda huo tayari nilikuwa nimeishajisaidia haja ndogo pale pale kitini. Na wala si lengo langu kukuambia ili uanze kunicheka na kunitangaza.

Shangazi akaanzisha mazungumzo na kila mmoja alikaa kimya. "Mwanangu Denis!" "Naam Shangazi" Denis aliitika kwa upole.

"Ni vipi umeamua kumfukuza mkeo kwa sababu isiyo na maana unamwambia hajakuzalia mtoto! Hivi unadhani hiyo hali ya kutopata mtoto kaifurahia yeye?" aliuliza shangazi huku akimkazia Denis macho kwa ukali.

"Lakini wanawake jamani! Ndivyo alivyokuelezeni! Hawa! Ndivyo ulivyoamua kudanganya! Shangazi,! Mimi sijamfukuza na nimekuwa nikimtafuta kwa muda wa siku tatu kumbe alikuja hapa!?

"Naomba umuulize aeleze mbele ya wote kama kweli nilimfukuza kwangu," alieleza Denis huku akitikisa kichwa kwa mshangao

Baada ya maelezo ya Denis, shangazi alinigeukia kunitaka nieleze ukweli juu ya mada hiyo ngumu. Lakini, kabla hajaanza kuniuliza lolote mumewe akamkatiza.kwa muda wote, alikuwa bado hajaongea nenombali na kusikiliza huku amekunja miguu yake mithili ya namba nne.

"Nadhani hili si swala la kufanyia mzaha hata kidogo! Unatakiwa kueleza bila woga ili ukweli upatikane. Endapo mumeo kakufukuza kwa kigezo kuwa huzai, au umeamua kumkataa kwa sababu unazozijua, useme useme wazi.". alisema mzee huyo.

"Baba, sioni haja ya kwenda mbali zaidi. Nimeamua kumtaa Denis kwa sababu mbili za msingi kwanza nimemkataa na kumtoroka kwa sababu hajanilipia mahari, pili simtaki kwa kuwa ananipiga na kunisingizia mambo ya uongo, sina zaidi" Nikajibu kwa ujasiri nisiojua nilipoupata.

Baada ya maelezo yangu, Denis akaonekana kuhuzunika sana. Bila uongo akajikuta anapenga kamasi zilizoambatana na machozi. nina hakika hata kama ungelikuwa wewe ungehuzunika sana baada ya kukataliwa na mwanamke umpendaye. Lakini basi tu Denis angefanya nini mwenye uamuzi ni mwanamke.

Sasa zamu ilibakia kwa shangazi na mumewe kutoa ushauri kwani kila mmoja yaani mimi na Denis tulikuwa tayari tumeshatoa maelezo yetu, lakini Mungu bariki shangazi namumewe wlaishauri iwe kama nilivyoamua kuwa nimemkataa Denis. Walimshauri Denis akubali uamuzi wangu ingaswa aliwaeleza wazi kuwa bado alikuwa ananipenda kwa dhati, mwishowe walimsindikiza akarudi kwake akiwa mwenye huzuni iliyojaa mshangao mkubwa.

Nilifurahi sana mara nilipoona Denis ameridhika kutengana nami. Vile vile nilifurahi kwamba shangazi amenikubalia kuishi kwake hadi nitakapopata mchumba mwingine.

Lakini kwa upande mwingine karoho kalikuwa kananiuma kila nilipokumbuka furaha na mapenzi ya mume wangu Denis. Lakini ninakuomba tu ndugu msomaji usinilaumu sana maadamu nimeamua kukuletea hii historia ya majuto.

Zilikuwa zimepita siku nne tangu nilipoondoka kwa mume wangu. Bado nilikuwa ninasumbuliwa na kitu kimoja nilijiuliza sana ni kwanini Philipo hajaonekana hapa kwa shangazi kama tulivyoongea.

Muda wote nilikuwa ninakaa mbele ya nyumba ya shangazi nikitarajia kumwona mpenzi wangu Mwalimu Philipo.

Ilikuwa saa kumi jioni siku hiyo ambapo kwa ghafla nilimwona Philipo akiibukia ule upande wa Kusini mwa nyumba ya shangazi. Alikuwa kavaa lile shati lake la bluu na kuchomekea kama kawaida yake. vile vile alionekana mwenye furaha, alipita moja kwa moja hadi niliposimama nilimlaki kwa furaha isiyomithilika.

"Hallow Hawa, habari za tangu Ijumaa" alinisabahi huku akinionyoshea vidole vyake vya mkono wa kuume.

'Salama Philipo waonaje hali?' nilimjibu na muda huo tulikuwa tumekumbatiana na kupeana busu za mahaba. Hatukujali wapita njia ambao daima huwa hawakatiki Nyamwaga Road ulioko Mashariki mwa mji huu wa Tarime.

Philipo aliniomba twende kupumzika katika nyumba za starehe huku tukiyapanga kikamilifu maswala yetu ya kuoana. Sikuwa na sababu ya kumpinga, hivyo aliniongoza hadi sehemu moja nyeti na maridadi sana ijulikanayo kama, ''Twiga Bar and Guest House' tuliingia humo na Philipo aliagiza bia mbilimbili baada ya kuchagua siti za nyuma na kuketi.

Nilishangaa sana kwamba siku hiyo Philipo hakuwa na tamaa ya kunihitaji kwa karibu kabla ya mengine kama ilivyokuwa kawaida yake.

Tulikata maji tangu saa kumi hiyo mpaka saa mbili usiku wote tulilewa sana kiasi cha kutojitambua. Nilikuwa siwezi kutembea pasipo kushikiliwa.

Hali kadhalika Philipo naye ndiyo alikuwa kazidiwa zaidi tumbo lake lilionekana kutuna sana mithili ya chura aliyeshiba na udenda ulikuwa haumwishii mdomoni. kwa ujumla wote tulionekana kama mabwege tu pale baani.

Badala ya kutazama video wateja waligeuzia macho yao kwetu wakitushangaa jinsi tulivyokuwa tunafanya vitimbi. Mara tuvue nguo na kuangua kilio mara tupande juu yameza na kulala, Jamani Pombe!

Hatimaye wahudumu walipoona tunazidisha vituko walitubeba mzega mzega na kutupeleka ndani ya chumba cha namba sita ambacho Philipo alikuwa amenunua. Hii ilikuwa ni historia ya aina yake kwa watu kulewa mpaka wajisaidie baani!

Kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu, siku iliyofuata tuliamka salama tulikuwa sasa tunajitambua kabisa. Ilikuwa yapata saa mbili unusu asubuhi.

Hali ya hewa ilikuwa ni ya mawingu mawingu yaliyoambatana na baridi kiasi.