Riwaya

Ni nani mbaya wangu?(2)

Baada ya kupimwa ilitulazimu kusubiri majibu ya vipimo vyetu kwa muda wa nusu saa. Wakati huo mimi Hawa nilijihisi kama sio mimi. Nilihisi akili kutokuwa yangu, Nikaelewa wazi kuwa lazima tatizo litaniangukia mimi; iwe, isiwe.

Baadaye wote tuliitwa na mganga tukaingia ndani ya kile chumba cha maabara ili tukaelezwe majibu ya vipimo vyetu ili mwenye kuumbuka, aumbuke.

Wakati huo mwili ulizidi kunitetemeka na badala ya kuelekea mbele niliona kama ninaelekea nyuma.

‘Tatizo liko kwa mke wako, wewe hauna tatizo lakini tatizo lenyewe si kubwa ni dogo tu’ alieleza mganga huku akimkazia mume wangu macho yake mekundu mithili ya nyama mbichi.

Halafu mganga alikohoa kidogo na kuendelea, ‘Tatizo hilo litaisha tu endapo mtakubaliana kupunguza safari zenu za kinyumba maana kuzidi kwa vitendo hivyo hasa kwa mwanamke mbali na kuhatarisha maisha kutokana na magonjwa ya zinaa hasa mnapokimbia kimbia nje ya ndoahuku mkikiuka hata Amri ya Mungu, pia huvuruga kizazi kwa wanwake.

Na hii ndio sababu inayomfanya achelewe kupata mimba!".

Baada ya maelezo hayo ya mganga tulivuta shoto kulia kurudi nyumbani huku nikiwa nimekumbwa na hofu ambayo nilikuwa sijawahi kuipata tangu kuzaliwa kwangu.

Nilihofu na kuona kuwa ujanja wangu umegundulika kwa mume wangu. nilielewa wazi kuwa kuna hatari ya kufukuzwa na Denis mara tutakapofika nyumbani kwani maelezo tuliyopewa kule hospitalini, yalikuwa ni ya kweli mtupu na yalinifanya nihangaike hangaike kisaikolojia kama mtoto kindakindaki.

Kwanini nisihofu wakati ninajua yaliyosemwa hayataingia vema akilini kwa Denis mana kuna utaratibu muhimu baina yetu ktika suala hili? hata hivyo, Denis hakuonesha ubaya au hasira yoyotedhidi yangu.

Hali hiyo ilinifanya nizidi kuchanganyikiwa zaidi. Sikujua ana mpango gani, amenisamehe kimwili na kiroho, au anasubiri wakati wa wakati utimie ili anifanyie anavyotaka

Baada ya kuwasili nyumbani niliandaa chakula kama kawaida tukala. Kisha Denis aliniita akanitaka niketi tujadili na kupata muafaka juu ya tatizo letu. "Yesu Wangu" nikajisemea kimoyomoyo kwa hofu mno. "Mmh ! Leo ndio leo. Nilifikiri amesahau kumbe bado..." Kiwewe kikaanza kunipanda.

"Nadhani umeyasikia vizuri maneno ya dakatari. Sijui tuseme nini nadhani hata kila kitu kiko wazi. Kubali usikubali, huwa unanisaliti na kuihujumu ndoa yetu

Lakini ingawa imetokea hivyo, ninakuomba tafadhali sana tangu leo ninakuonya acha tabia hiyo! Kwa leo, sikuadhibu kwa ilolote ila, ninakuahidi iwe ndio mwisho usirudie tena upuuzu wa namna hiyo ! Hivi hujui hatari zake kimwili na kiroho?".

Basi siku hiyo hayo yakaisha hapo na hakuna mtu aliyeyazungumza tena. Tukaendelea kuishi kwa amani na upendo kama awali. Denis hakuonesha chuki au mabadiliko yoyote juu yangu,.

Aliendelea kunihudumia kwa moyo mkunjufu bila kujali ubaya na dharau niliyokuwa nimemfanyia. Kwa kweli kama ni mume, nilikuwa nimempata na hadi leo ninamkumbuka na sitamsahau kwa busara zake ingawa leo mimi Hawa sitamaniki tena. Hii ni kwa kuwa niliichezea shilingi huku nikiwa katika tundu la choo.

Mpenzi msomaji, ninashindwa nianzie na nimalizie wapi kukueleza mkasa huu ulionipata.

Baada ya kitambo kidogo nikajikuta tena nimetumbukia katika uwanja wa uasherati. Sikuuzingatia wajibu wangu na kuelewa kuwa ni mke wa mtu ambaye ninapaswa kujilinda na maadui wanaume wazinzi.

Nikasahau kuwa Denis mume wangu alinionya sana juu ya uovu huo. Mchezo huo wa kuwa jamvi la wageni na tandiko la kukodi kwa wanaume wazinzi, hakika ulikuwa umenitawala tena kwa sheria za ki-mabavu.

Nilikuwa ninaenda na wanaume kwa nadra sana kuvusha siku nzima bila kuugawa mwili wangu .

Ndoa ni kama yai ambalo daima linahitaji uangalizi ili lisije likavunjika halafu pa kulipata pakawa hapaonekai kabisa!" hayo ndio

baadhi

ya maneno waliyoniambia baadhi ya majirani wema ambao waliniona nimo mbioni kuivunja ndoa yangu kwa vitendo vyangu vya ajabu. Mmh ujinga kweli ni ujinga tu. Mimi ingawa nilielewa wazi kuwa maneno hayo yalikuwa ni yenye kunijenga kiroho na kimaisha, niliyapuuza tu, nikaona ni vema niendelee kuifaidi dunia hii kigeugeu.

Nikawaona majirani hao niliwaona kama watu wanaonionea wivu na wanataka kunipokonya asali mdomoni.

Niami nikaona kuiacha asali hiyo ya mapenzi niliyokuwa nimeifumbata kikamilifu ni sawa na kupofuka macho. Sikujua kama asali hii itakuja geuka na kuwa mwarobaini. Asali ambayo hakika sikuitarajia kuwa leo hii itanifanya nishinde mchana kutwa nzima kwa kuzihesabu mbavu zangu ambazo hapo nyuma haikuwa kazi rahisi kuamini kuwa ninazo kwa jinsi zilivyokuwa zimefichika.

"Loh! kumbe kweli nimeamini, majuto ni mjukuu! Hivi ni kweli leo kwamba ni mimi Hawa ndiye leo ninakosa hata kipande cha sabuni jamani!?" kila ninapokumbuka machozi hunitiririka sana.

Nakumbuka miaka mitatu ilikuwa imekaribia kabisa kutimia tangu tulipooana na Denis. Bado Denis alizidi kunipenda kwa dhati na wala hakuwa na mpango wa kuongeza mke wa pili, kama ilivyokuwa kawaida ya wanaume wa kabila la kikurya katika siku za nyuma ninaapa hadharani kuwa Denis hakuonesha kinyongo chochote dhidi yangu.

Aliamini na kunikuabali kuwa mke wake wa maisha na hakuna mwingine.Ni muda huo huo wa mwaka wa tatu ambapo nilianzakutia dosari tena kubwa mno katika ndoa yangu.

Dosari hii ilianza kunipata baada ya kuchanganywa na wanaume wengine niliokuwa nao katika hizo enzi zangu, safari hii walikuwa wapatao watano. Mmoja wao alikuwa Philipo. Huyo alikuwa mmoja wa wapangaji wa nyumba tuliyoishi.

Philipo alikuwa mwalimu kazi ambayo ni tofauti kabisa na ile ya mume wangu Denis ya kufanya vibarua barua. Philipo alikuwa tayari keshaoa na hata mke wake,bado ninamkumbuka sana, aliitwa Mama Chacha.

Sikujua ni kwanini lakini mimi nilianza kushangaa baada ya kuona Philipo anapanga ghafla mipango yake na kuamua kuhama. Nadhani alishagundua kuwa picha imeungua. lakini, kwanini alinificha na wala asinitonye?!

Basi bwana, Philipo mpenzi wangu wa siri na rafiki mkubwa wa mume wangu akaanza kunitwisha magogo ya kilo ambayo bila kutarajia nilijikuta nimeshajitwisha tena bila kata. Alitumia mbinu nyingi sana kunidenda.

Na kali kuliko zote ni ile habari ya kunioa.

"Kama kweli unanipenda kama ninavyokupenda ninanomba uachane na Denis kwa haraka sana! Nitakuoa mke wangu wa pili ukifanya hivyo!!? Aliniahidi Philipo.

"Hautaniuza na kunukana baada ya kuachana na mume wangu?" niliuliza tena na tena. "Ninakuhakishia nitakuoa tena kwa kutoa mahari nyumbani kwenu."

Si unajua tena pesa kwangu ni chungu nzima, mimi mtumishi wa Serikali bwana!" Philipo alisisitiza. Akaahidi zaidi na zaidi kunihudumia vizuri kuliko hata mke wake mke wake, Mama Chacha.

"Vizuri Philipo nimekubali ombi lako lakini usije ukaniacha njia panda!" nilisema huku moyo wangu ukisitasita. "Bwana mimi ninakuambia kweli, kwani si bado huyo Denis alikuwa hajakulipia mahari?"

"Bado" nilijibu lakini....! "Sasa wasiwasi wako uko wapi? achana nae anakakaa bure bila kulipia binti za watu," alidai Philipo huku akiligusa hili bega langu la kulia ambalo leo limepanda na kukaribia kilele cha kichwa changu ambacho nacho nywele zimeshanyonyoka na kukiacha kitupu! uzinzi jamani!.

Siku iliyofuata nilifungasha kila kilichokuwachangu kuanzia khanga mpaka soksi nikaondoka .

Uamuzi huo wa haraka niliuchukua kufuatia ile kauli ya Philipo, "Naomba uachane na Denis kwa haraka sana' Nilienda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Philipo. Kwa bahati nilikuta mke wake hayupo.Alikuwa ameenda sokoni kufanya shopping ya jioni.

Binafsi nilifurahi sana maana niliona huo ndio muda mzuri wa kuongea na Philipo ambaye nilimkuta anasafisha vile viatu vyake vya ngozi nyeusi kwa brashi Nikashangaa namna uso wa Philipo ulivyogeuka siku hiyo tofauti na kipindi kile alichokuwa akinishauri kuhamia nyumbani kwake ili anioe. Sasa ni vipi leo anikaribishe kijuu juu namna hiyo?

Niliona hamna haja ya kufanya papara kumsemesha neno. Nikakaa kimya ili nione ni nini kitakachoendelea. Mara wakaingia watoto wake wadogo .Mmoja nadhani ana umri kati ya miaka miwili au mitatu.Wote walikuwa wakiume.

Philipo alianza kuwaamuru watoto wale, "Msalimie Shangazi yenu huyo, msalimieni!". alisisitiza.

Nikahisi damu ikinisisimka mwili mzima nikakumbwa na hofu juu ya matamshi ya Philipo kwa vijana wake. Lakini basi tu mimi niliendelea kuweka macho kwani hata ingawa watoto waliambiwa kunisalimia hawakunisalimia. Waliendelea kunitazama huku wametulia!.

Zilikuwa zimekatika dakika zipatazo kumi hivi. Philipo alikuwa amemaliza kung'arisha viatu. Akainua macho na kunitazama. Akawataka watoto wakacheze nje. Sababu sikuijua nilisubiri

"Sasa Hawa hebu nisikilize" Philipo alianza na kuendelea,"Hapa tangu usiku tumekuwa na ugomvi mkubwa mimi na mke wangu Mama Chacha juu ya kujihusisha na mambo ya umbea - mbea! Hivyo sikufichi ana hasira sana, kwa hivyo ninakuomba uende kwa yule shangazi yako wa kule Nyamwanga Road ili ujihifadhi kwa muda kisha tutawasiliana kesho kwa ajili ya mipango mingine.