Riwaya

Ni nani mbaya wangu?

Na Christopher Gamaina

‘OH maskini wa Mungu! Nimejipotezea bahati. Ni kwa ujinga wangu mwenyewe nimedanganyika na kurubunika kirahisi namna hii! Kumbe ndivyo walivyo hawa mapakashume!’. Nilijiuliza thuku nimejivika kipande pekee cha khanga ya India hali nimejikalia kwa huzuni pale ukutani.

Penzi letu motomoto, pevu na tamu likadumu kwa takribani miezi sita tu na ghafla John akanipiga stop na kuvunja ubalozi baina yetu.

Uamuziwa John kulikatili penzi letu niliupokea kwa hali mbaya kabisa katika masikio na moyo wangu. Nilimlaumu sana ingawa niliamini wazi kuwa ni dhahiri alikuwa amechoshwa na vitendo vyangu viovu kuvunda, kunuka hata na hata kukinai machoni mwa wana wa Adam.

"Nasema samahani tena samahani sana Hawa, nimegundua na kuamini kuwa wewe hunifai na hunifai kwa kuwa ni-kichampioni tena kile wanachita siku hizi kuwa IP yaani International prostitute. (Malaya wa kimataifa) Nimekataa sitaki na nimeapa sikutaki. Tena sitaki!"

Hayo ndiyo maneno aliyonibomokea John mara nilipomwuliza kisa na mkasa wa kulivunja penzi letu tena kwa ghafla. Akayatamka bila hofu soni wala, uchungu wowote.

Niliivuta kumbukumbu ya maisha yangu kwa takribani miaka minne iliyopita nilipoamua kuondoka nyumbani kwetu. Nilikuwa bado ni mdogo sana na yalikuwa yamekatika majuma manane au tisa hivi, tangu nilipohitimu elimu yangu ya msingi.

Uamuzi huo potovu na wa aibu sana hususani kwa mtoto wa kike, niliuchukua baada ya kukerwa na ugomvi wa baba yangu ambaye karibu kila siku alikuwa akinikemea akinikaripia kwa kile aichokiita umalaya wangu ambao hata mimi ninakiri kuwa niliuanza tangu nikiwa shule.

"Unaniabisha sana hapa kijijini mwanangu Hawa! Mbona usijitulize kama wasichana wengine! Punguza vitendo vya umalaya na ni hatari sana. Hujui hali ya siku hizi. Mwanagu chunga sana ungali mdogo!

Elewa vitendo hivyo siku moja vitakufikisha pabaya, vitakuja kukupatia mzigo ambao hautapata mbeleko ya kuubeba! Aliniasa baba huku machozi yakimtiririka kwa uchungu sana. Alionesha hali ya wasiwasi sana juu ya kitu fulani hapo mbeleni dhidi yangu.

Lakini pamoja na huo wosia wa baba, sikuwa na wasiwasi wala sikujali chochote, nilipuuza tu na kujua ni unoko wa wazazi.

Ni dhahiri nilikuwa mtu wa makuu. Niliendelea kuwa mwalimu wa kuwanyang’anya wanawake wa pale kijijini waume zao ingawa nilikuwa msichana mdogo tu; wa miaka 17. Lakini nilikuwa na bahati sana kwani sikuwahi kufumaniwa na mume wa mtu hata mmoja kati ya 11 niliokuwa nikishiriki nao pendo haramu pale kijijini.

Siku moja niliamua kukimbilia mjini kwa mama mdogo baada ya kuona mambo yanaanza kunichachia pale kijijini. Binafsi nilifurahi sana maana niliamini nitaendesha mambo yangu kwa uhuru wa kutosha pale mjini. na hasa ukizingatia mjini palivyo na raha!

"Loh! Hapa poa sana, ma - mdogo akinikubalia niishi hapa, mambo yatakuwa fiti sana" nilijisemea moyoni muda mfupi tu baada ya kuwasili nyumbani kwa mama mdogo. Siku hiyo niliwakuta wakiandaa kifungua kinywa.

Sijui ilikuwaje , lakini baada ya siku tatu, kumbe tayari baba akapata taarifa zangu kuwa kwashemejiye (ma-mdogo) maarufu kama Mama-Ali.

Hata hivyo alitulia tu hadi wiki ya pili alipowasili mjini tulipoishi. Siku hiyo alitukuta tukifungua kinywa.

baada ya kukaribishwa na kuwa na mazungumzo kadhaa na mama mdogoa katika chumba cha wageni, huku kikiandaliwa chochote, baba akamwita mama mdogo kwa maongezi nyeti. Ndivyo nilivyoamini.

Sijui walizungumza nini, lakini, kwa kuwa imani ndiyo iponyayo, naamimi alitaka kujua sababu ya utoro wangu nyumbani. na ninavyomfahamu baba, sijui kama alimficha lolote kuhusu tabia yangu ya ukahaba nilipokuwa nyumbani.

Nakumbuka ilikuwa Ijumaa majira ya saa tatu usiku baada ya kumaliza maakuli na kisha mama mdogo akaniita sebuleni na kuniomba niketi. hata hivyo, sikuwa na wasiwasi wowote. Nilijua upo ujumbe mahususi anaotaka kunitonya.

"Keti mwanangu Hawa!"alisisitiza ma- mdogo na kuendelea, "Kumbuka mama yako alipofariki, wewe ulikuwa mdogo sana na baba yako ndiye aliyesumbuka kwa kila tatizo lililokukabili.

Akakulea na kukusomesha mpaka umefikia umri huu ulionao leo. Usijione mrembo, urembo huo ameufanikisha baba yako vinginevyo usingefikia hapo.".

Hakuishia hapo, akaendelea, "Kama mama mdogo wako nakusihi kuachana na tabia yako mbaya aliyonieleza baba yako.ili tusije tukachukuliane ubaya.

Sitaki kuona au kusikia ukiendelea na tabia hiyo aliyonileza Mwanangu, dunia hii siyo ya kukimbilia mara leo hapa, mara kesho hapa . Hivi unashindwakukaa na kutulia sehemu mmoja kama mtoto wa kike? Umenielewa?",

"Nimekuelewa mama." niliitikia na kisha sote tukaingia vyumbani mwetun kupambana na ndoto za usiku huo.

Usiku mzima wa siku hiyo sikupata usingizi wa kuridhisha, nilipata usingizi wa mang’amung’amu tu. Nilianza kuchanganyikiwa kila nilipoona na kutafakari namna mambo yanavyozidi kuniwia mabaya na magumu zaidi kinyume na mategemeo yangu.

Bila kutegemea wala kujua ni kwanini, nikaanza kuhisi kichefuchefu kwa muda, halafu nikajipa ujasiri uliniondolea bughudha katika ubongo wangu.

Si kwamba ninajisifia kwa ushetani wangu, na wala sikuambii ili na wewe ukawatangazie watu ili kila nitakapopita wanitazame kwa macho ya kunizomea na kinisuta, la hasha, ninakudokezea tu siri hii.

Siku iliyofuatia niliamua kuwasiliana na wapenzi wangu watatu ambao tayari nilikuwa nimeishawapata kwa siku hizo chache.

Niliwambia kila mmoja kwa wakati wake, tuwe tukiyafanya maswala yetu kwa siri na tahadhari kubwa. Nilitumia utaalamu wa maneno hata waliotaka kunihoji zaidi, wakanielewa na kukubaliana nami kirahisi tu.

Agenda yangu kwa wakati huo, ilikuwa kuanza kutoa ridandasi. Nikaanza kujishauri ili nisije kumuudhi ma mdogo hali ambayo ingesababisha anitimue nikose pa kukimbilia.

Najijutia mwenyewe kwa kuwa ingawa nilijaribu kujituliza walau kwa wiki moja, bila haya nilianza, tena kwa kasi kubwa ya kutisha kwa kuwachanganya na kuwabadilisha wanaume mithili ya mwanaume mwenye mashati mengi.

Katika mtaa wa Majengo na hata ule wa Starehe, hakuna ambaye hakufahamu jinsi nilivyokuwa mkarimu kwa masuala ya ukahaba

Nilikuwa ninajihisi kama ndimi nyota ya pekee duniani, niliye maridadi na mwenye furaha kwa masaa 24. Sikujua kuwa furaha hiyo ndiyo itageuka na kuwa kilio cha huzuni leo hii! na kamwe sikuamini kuwa hizo zilikuwa ndoto zitakazogeuka kuwa jinamizi kisha zinirudi namna hii.

Sikuelewa kuwa malipo ya uzinzi yapo na kwamba nitakujayapata. Siku moja. minong’ono iliyonifanya nitoroke kule kijijini, ikaanza kusikika hadi hapa mjini nilipokimbilia.

Sijui ni kwanini ugomvi kati yangu na ma-mdogo ulikuwa hauishi lakini, nadhani, dharau ile niliyoionesha baada ya kujisahau hadi kuwazoeza wapenzi wangu kuja hadi nyumbani bila kujali kuwa nilikuwa ugenini, huenda ikawa sababu kubwa.

Ninaamini hata wewe mpenzi msomaji utaishutumu sana tabia yangu hiyo lakini, naomba univumilie nikueleze hasara niliyoiambulia maskini wa Mungu ili kupitia kosa langu, ujue la kufanya au kujifunza.

Walahi Mungu saidia! Hawa bila kutegemea ilitokea siku moja nikajaliwa kupata mchumba hapa hapa mjini Tarime. Sikuamini macho yangu kuwa ni kwani hii ni bahati ambayo kamwe sikuitegemea kulingana na sifa ya umalaya niliyokuwa nimetunukiwa na waungwana.

Niliona kuwa ni njozi ya mchana ambayo daima huwa haina ukweli wowote ule.kwani kwa namna jinalangu lilivyokuwa limeharibika, nani angetegemea hawa kupata mchumba?

Basi bwana, mchumba huyu hakuwa Musa wala Hasani bali alikuwa kijana mmoja mrefu wa wastani na mpole sana maarufu kwa jina la Denis.

Baada ya mazungumzo ya kina wote tulikubaliana kuoana kwa kuwa huo ndio wajibu wa karibu kila binadamu. Ni dhahili kuwa Denis alikuwa amevutika sana juu yangu, kwani baada ya siku tano alinichukua hadi kwake na mara tukaanza maisha ya pamoja kama mume na mke.

Vile vile, Denis aliahidi kupeleka mahari nyumbani kwetu mara atakapoipata.

Watu wengi wakiwamo wazee wangu, hawakuamini masikio na macho yao waliposikia na kuona nimeolewa. Hakika walinishangaa sana. Wengi walijiuliza tena na tena ‘imekuaje Denis kijana mwenye busara na hekima ya kutosha amepotoka na kumwoa kahaba aliyekubuhu kiasi hiki?!" "Hakika kweli bahati ya mtu haikingwi, Hawa kaolewa kweli !?"

Hayo ndiyo maneno yaliyotawala midomo ya watu karibu kila pembe ya mji wa Tarime.

Zaidi ya hapo, baba alifurahi sana alipoona nimeolewa. Aliamini sasa nitatulia na kujirekebisha katika tabia na vitendo vyangu.viovu.Siamini kuwa alifurahi kwa kuwa sasa tapata mahali kama wenyeji wa wilaya yetu wanavyowatumia mabinti zao kama vitega uchumi vya familia, la hasha, ni kwa kuwa aliamini kuwa sasa upo uwezekano wa kuepuka na magonjwa hatari yanayotokana na uzinzi.

Siku zilipita na kupita kidogo. Baba akatutembelea nyumbani kwetu ili waklau atujulie hali na mme wangu. Pia alipata wasaa kuniketisha kitako akinishauri mambo mengi sana yenye hekima na maadili mema hususani kwa mwanamke aliyeolewa.

‘Umepata mume mwanangu, hiyo ni bahati ya pekee toka kwa Mungu lazima uelewe hilo. Inakupasa kumshukuru Mungu kwa karibu zaidi na zaidi kuwa mwangalifu na makini sana ili bahati hiyo isisije ikakuponyoka .

"Usidanganyike na mashauri ya watu wasiopenda kuona wenzao wakiendelea na kusema, "huyu mmeo si mzuri!’ Lazima uelewe kuwa hakuna mwanaume mbaya wote ni sawa!" aliniasa baba na baada ya muda tulipeana bai bai akarudi kijijini akiwa mwenye furaha isiyomithilika.

Baada ya miezi kadhaa hali ya afya yangu ilionesha mabadiliko, ikaanza kuwa nzuri tofauti kabisa na siku za nyuma. Ile tabia ya kurukaruka na wanaume mapakashume, ikapungua ingawa sikuiacha kabisa.

Ukweli ni kwamba, kila nilichokihitaji Denis hakunikaripia yaani alinihudumia kila kitu kuanzia nguo mpaka vipodozi. Aliniheshimu, akawatii na kuwaheshimu sana ndugu jamaa na marafiki zangu.

Alikuwa tayari kuwasaidia kila walichokihitaji kulingana na uwezo wake. Mume wangu Denis hakuwa mtu wa makuu.

Ingawa sina ushahidi ninaapa na kukiri wazi kuwa, Denis alikuwa mwaminifu wa ndoa yetu. Maskini mume wangu Denis hakuwa mtu wa kutawaliwa na tamaa mbaya kama walivyo wanaume wasio na utu.

Lakini ingawa kwake ilikuwa hivyo, Hawa sikujali na wala sikutaka kulinda heshima na uaminifu huo katika ndoa yetu changa. Najilaumu na naomba mnisamehe na wengine mkome asiwepo wa namna yangu.

Bila soni nilianza kuiharibu ndoa yangu kwa kujitembeza kama bidha mbovu isiyonunuliwa sokoni.

Niliendelea na zoezi hilo kwa muda mrefu bila mume wangu kugundua. Hata wakati fulani, nilikuwa nikichelewa na kurudi nyumbani saa mbili usiku lakini Denis aliponihoji nilijitetea mpaka akaiva, akalainika na kunisamehe. Niliamini kuwa tayari alishakuwa zezeta hasemi wala haambiwi mbele yangu.

alikuwa mwepesi wa kusamehe kila nilipomwangukia kuomba radhi na huo ukawa mtindo na mazoea.. Sidhani kama kuna kijana mpole kama mume wangu Denis na kama wapo basi katika mia wapo wawili au mmoja.

Mara nyingi Denis alikuwa akiniomba na kunishawishi sana kuhudhuria mafunzo ya Biblia katika ibada ya Jumapili kwa kuwa ndio iliyokuwa siku yetu ya kuabudu. Hata hivyo kwa kujilazimisha tu, niliweza kuhudhuria mara moja moja huku nikitoa visingizio mbalimbali mara leo ninaumwa leo sikufua na kunyosha nguo"

Simsingizii Denis mume wangu hakuwa mbishi wa kunikubalia badala yake alijiondokea mwenyewe kuelekea kanisani hali mimi huku nyumbani nikipata nafasi ya kuwasiliana na spea taili zangu.

Ilikatika miaka miwili na bado nilikuwa sijajaliwa kupata mtoto. Nilianza kuhofu kuwa pengine Denis atanikana kuwa labda kizazi changuni ni kibovu na ndio maana sizai.

. Ni wazi kuwa kumkataa mwanamke kuwa hazai ni uamuzi ambao huchukuliwa na baadhi ya wanaume wenye imani potovu. Denis hakuwa na wazo la namna hiyo. Alinishauri twende hospitalini kupimwa ili kujua tatizo linalopelekea kutopata mimba.

Lakini kabla ya hatua hiyo, mara nyingi nilikuwa nikijiwazia moyoni kuwa huenda hali hii inanipata kufuatia vitendo vyangu vya uasherati ninavyofanya tena bila tahadhari yoyote licha ya kujua kuwa ni hatari kwa afya, ni chukizo kwa wanajamii na ni chukizo hata kwa Mungu.

Siku moja tuliongozana hadi hospitali ya serikali. Ikabidi tuchukuliwe vipimo vya maabara baada ya kutoa maelezo yetu