Make your own free website on Tripod.com

Riwaya

Milionea Maskini

Na Josephs Sabinus

"MASKINI nifanye nini mie poor Millionare katika dunia hii? Mbona ninapwaya ndani yake mithili ya punje ya mchanga ndani ya bahari ya Hindi! Mie milionea maskini; ninayofuraha gani kama sina..!" Joel alishindwa kuendelea na mtiririko wa maneno hayo aliyokuwa akijisemea pasipo kujijua kuwa yuko peke yake kando ya barabara akiwa ameegemea nguzo ile ya umeme.

Siyo kwamba alikuwa hajitambui kwa kuyasema maneno hayo yaliyowafanya watu wamtazame kama mtu aliyechanganyikiwa, bali pia machozi yalikuwa yamejenga mitaro imara juu ya mashavu yake na kukiloanisha kifua.

Wengi walitaka kujua kilichomliza Joel namna hiyo mara kwa mara. Hawakuwa wakitegemea kumuona tajiri maarufu namna ile akilia machozi hadharani.

Ni nani kati yao ambayo hakuwa anajua namna Joel alivyoibuka kuwa milionea kwa ghafla? Lakini ni nani ambaye angediriki au kufurahia kuongelea swala hilo hali mtu mwenyewe......

Wapo wengine wengi waliodhani kuwa sononeko la Joel lilitokana na ukweli kwamba huko Ulaya alipokwenda labda amegundua kuwa ndiye maskini pekee,tofauti na alivyozoea na kudhani kuwa utajiri huu alionao, huenda hana mpinzani wa karibu.

Ukweli anaujua yeye mwenyewe ndiyo maana anazidi kulia akijutia jina hilo analoliita kwa kiingereza; poor millionare.

Joel Kaeneo; kijana wa kabila la wasukuma haoni suluhisho jema zaidi ya hili hapa duniani.

Tiba pekee anaona ni vema atangulie aende na kuachana na masumbufu haya ya dunia hii ya Musa. yeye ni mrefu wa kadri, rangi yake ni ile ambayo wengi hukosea na kumwita eti ni mweupe. Anao mdomo wa kumwesamwesa na masikio yake ni madogo na mazuri kwa kutazama.

Watu wale walioongozwa na mzee Magabe, walimfuata taratibu hali wakistaajiabia maneno na matendo yake kijana huyu milionea licha ya umri wake wa miaka 23 tu.

Alizidi kukatiza na kukatiza zaidi kwenye vichochoro hata alipoufikia ule mti mkubwa uliopo nyuma ya jengo lile. Aliweka chini mfuko ule mdogo wa nailoni aliokuwa nao.

Hali wakimuangalia kwa makini kwa kuwa tayari walishahisi jambo baya kumtokea, watu wale wakamwona kijana Joel Kaeneo akiviinamia na kuufungua kisha anaitoa ile kamba mpya ya nailoni.

Baada ya kuifunga kwa utaalamu alioridhika nao Joel alipanda juu ya mti ule.

Haikupita muda mrefu mti mzima ulitoa mlio wa mtikisiko wa majani yanapokwaruzana.

Vijana wale waliotaka kwenda kuyanusuru maisha yake walizuiliwa na mzee Magabe ambaye alikuwa amekodoa macho huku akikiandaa vyema kile kisu chake kisichobanduka kiunoni mithili ya Mmasai.

Wengine walianza kuhofu na hata kutaka kutoroka toka eneo lile ili wasishuhudie namna mtu anavyokufa kwa kujiua, eti baadae wawasaide polisi katika uchunguzi, ama kweli hata waliokuwa na mpango wa kujiua kwa kitanzi wamekoma.

Nani arudie wazo hilo hali wameona na kugundua kuwa hata wanaojua kwa dawa, maji au basi kujitia kitanzi na pengine kujibanika kwa moto wa mafuta ya taa; hufikia hatua wakatamani kuokolewa namna hiyo?

Amini usiamini hakuna anayeridhika kuwa afe mpaka dakika ya mwisho. Tazama hata wazee wenye miaka mia na au mgonjwa mahututi mbona huhitaji dawa na kuenda hospitali, ulimwona mgonjwa yule aliyekuwa taabani namna ile hali amebebwa kwenye machela kuelekea Muhimbili kule Dar? Ulionaje lilipokuja kwa kasi gani lile hali waliombemba mgonjwa wakivuka barabara mbona walipomtosa na kumuacha alinyanyuka na kukimbia kwanza na baada ya gari kupita alirudi tena na kulala kwenye machela; kwa nini hakuridhika na uzee afe na miaka yake 94?

Basi ndivyo ilivyokuwa, hatujui kilichoendelea maana mimi niliondoka ila ninachokumbuka ni siku ile nyingine ambayo anga zima la mji huu wa Mwanza lilitawaliwa na hali ya mawingu dalili zilizoashiria mvua kunyesha.

Radi zilizidi kuongeza vimulimuli na ngurumo za kutisha zikisikika kila baada ya sekunde chache. Kisha hali ya ukimya iliongezeka na mara jopo la majaji liliingia pale huku likiongozwa na Changwe.

Mheshimiwa jaji Navatus Changwe aliishika vyema koti yake usawa wa kifua na kupandisha mabega yake juu ishara ya kujiweka smati.

Akaivua ile miwani na kuiweka juu ya meza. akazungusha macho na kuyapitisha kwa wafuasi wake na waendesha mashitaka.

Alishuhudia pia umati ule uliokuwa umefurika pale ili kujua hatima ya milionea maskini.

Alirudisha tena miwani juu ya uso wake na kupekua pekua mafaili yale yaliyotoa sauti ya pekee ya karatasi mahali pale. Vingine vyote vilikuwa kimya mithili ya utupu.

Akakohoa kidogo ili kusafisha na kumeza mate ili kulilainisha. Akaanza ‘Joel! Joel! Kaeneo! Ndiyo wewe?" Jaji aliuliza hali akimuangalia Joel Kaeneo machoni. Uso wa jaji ulikuwa umetengenezwa matuta ya muda ishara ya mshangao.

"Joel Kaeneo mfanya biashara milionea mjini Mwanza unakabiliwa na kosa la mauaji ya kukusudia’ kweli si kweli?" Jaji Changwe akauliza ‘sikutaka kuua mtu’ nilitaka kujiua mwenyewe . anaesema nilitaka kumuua alete ushahidi mbele ya Mahakama hii tukufu’ Joel akaeleza.

"Ndiyo mauji hayo ya kukusudia ninayoyasemea hukutaka kujiua bali ulitaka kuua nafsi yako.

Ujue kuwa kimila, kidini au hata kisheria hakuna mwenye mamlaka ya kuua au kujiua hebu kwanza lieleze jopo hili kisa cha uamuzi wako huu".

"Mheshi..heshi.. Mhe.." Joel Kaeneo anashindwa kutamka kitu anaona gereza linamsubiri akale maharage na kubeba kinyesi kilichojazwa kwa makusudi ndani ya ndoo au basi badala ya kifo alichokitaka, sasa anakwenda kufa kifo toka mahakamani, yote hayo anayaona kinadharia. Anachanganyikiwa maana alichokionja siku ile, utakapo kujua aibu ya maiti kamuulize muosha. Anachanganyikiwa anapoteza fahamu akiwa kizimbani.

Haupiti muda mrefu huku mpango wa maaskari kumuondoa ukifanyika na majaji kupanga siku nyingine kwa ajili ya kesi hiyo, sauti ya kuropoka na kuvunja ukimya uliozidi kutawala na mdawao kuwavamia watu waliokuwepo inasikika.

‘poor milionere! Milionea maskini’ hebu niseme leo maana hatujui ya Mungu’ majaji wanasemezana kidogo na kukubaliana kumruhusu aongee alichokusudia.

‘Ninajua ndimi mdhambi mbele ya Mungu na mbele ya Mahakama hii tukufu lakini ningefanya nini mimi Poor milionere' milionea maskini? Akalitazama jopo lile la majaji walikuwa wakiandika kile alichokisema, kisha jaji Novatus Changwe akatoa mguno wa kumtaka Joel aendelee.

"Nizidi kufanya nini katika uso wa dunia hii?" Joel akahoji na kusema ‘ngoja niwape kisa kizima.

Mimi ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watatu wa familia ile ya mzee Kaeneo, familia iliyokuwa ikiongoza kwa ufukara katika manispaa hii ya Mwanza, nikiwa mtoto wa pekee mwenye umri wa miaka mitano baba alikuwa mlinzi katika kiwanda hiki cha.." akanyoosha mkono ishara ya kuwaonesha kile kilichopo karibu cha kusindika mbegu za pamba.

"Hatujui kama mshahara ndio uliokuwa mzuri au vipi mimi sijui bwana; anayetaka kujua hilo akamuulize marehemu baba huko kaburini.

Lakini kabla yule mdogo wangu wa mwisho Nasra kuanza shule, baba alisimamishwa kazi akakamatwa na hata ile nyumba iliyokuwa inajengwa ikataifishwa. wengi walikuwa na yao ya kusema. "wengine walisema ni mbadhilifu, wengine wakasema ni muhujumu wa uchumi wa nchi".

Kumbe alikuwa ni Milionea Maskini! Hao ni wale maadui wa maendeleo yetu walizipokea taarifa kwa shangwe namna hiyo. Japo ni kweli walianza kutuita milionea lakini baada ya kudabuliwa kwa baba na kufia huko kizuizini hata uji wa muhogo usio na sukari wala chachu ulikuwa ni wa kubahatisha siku moja ambayo Mungu hana hasira?

Ningefanya nini mie na tabu zote hizo zinazonisonga na familia yetu? Kila ninachogusa hakigusiki sasa unadhani mie nifanye nini yaani niendelee kuteseka namna hii hali rafiki yangu yule kanieleza kwa mganga naye amenipa suluhisho nitaitwa lini Milionea yaani kila siku....

Siku hiyo niliwaelekeza wale rafiki zangu ( siwataji majina maana ni too late) walipoingia waliongoza hadi chumbani kule kwa mama wakamteka na kumfunga kitambaa ili kumziba macho, mmoja aliwahi na kunikonyeza ili nikatimize ahadi yangu kwa mganga na kuwa ninaweza.... Mradi tu niwe milionea na kuziepuka tabu hizi.

Nilijihesabia kichwani mara mbili na ile ya tatu ilihitimishwa na sauti ya upanga juu ya kichwa chake mama yangu mzazi; aliyenibeba ndani ya tumbo lake akihangaika kwa miezi tisa yote usiku huo inakamaliza kwa mkono wangu akaenda aka...

Niliyoyafanya kwa wale wadogo zangu wa kike kutokana na imani za kishirikina ili eti niwe tajiri sipendi niseme kitu hata nikipewa elfu kumi sasa hivi.

Kisha tulifanya ‘niko’ na watu hao ambao jamii na majirani wote walitambua kama majambazi wakanifungia chumbani kwangu kwa kufuli ili kupoteza ushahidi na kuepuka kushukiwa kwa upelelezi.

Baada ya siku kadhaa msiba ungali mbichi niliondoka kwenda Geita kwenye machimbo ya dhahabu kama ilivyopangwa kibaya zaidi ni kwamba nauli yangu ilikuwa ni ile ya michango ya rambirambi.

Haya nimefika Geita huku nyuma wadogo zangu sijui kila mtu ajue lake kama mtoto wa kobe na kinyonga.

Inakuwa kama ni bahati siku hiyo ya kwanza tu ninajikuta na bahati siku hiyo ya kwanza tu, ninajikuta na bahati ile ya kuokota madini yale ya thamani kubwa vile.

Niendelee kufanya nini hali tayari maneno yameenea Mwanza nzima hapa sasa ninapoona nuksi na giza tupu maana kila nipitapo watu wananiita Milionea.

Heri niende zangu Ulaya nikajenge na kuishi huko maana sitaweza mambo ya leo sina hiki, naomba ooo! Nipe hiki sitaki usumbufu kama huo"

Joel Kaeneo alitulia akameza mate kisha akaendelea "Nimo ndani ya ndege ninawaza na kuwazua ni kweli ninakuwa milionea sasa lakini huku niendako nitafurahia na nani kama sina mtoto sina wazazi na wala sina ndugu?

Si nitaitwa milionea maskini!.

Laah! Hivi nilimuua mama na kuwadhililisha ndugu zangu kijinsia ili nitajirike sawa kweli imekuwa hivyo lakini, ninayofuraha gani kama watu hao hawapo duniani si nitakuwa milionea wa pesa lakini maskini wa furaha na amani moyoni!!".

"haki iko mbinguni duniani kuna sheria Shauri zao kila mtu achukue taimu zake.

Nikiwa bado kwenye lindi la mawazo mengi mhudumu wa ndege akanigusa begani akanitaaka nimpe tiketi kwa ajili ya ukaguzi.

Niligusa mfuko wa kwanza wa pii wa tatu na hata ndani ya soksi hakuna pesa tiketi wala mali ile iliyobeba umilionea wangu.

Vyote hivi sijui vimeyeyuka upande gani nilipoteza fahamu kwa saa 36 na baada ya kuzinduka nikajikuta niko mikononi mwa polisi nilifikiri kuwa ni laana ziko juu yangu halafu eti wanazubaa nikawatoka kinamna.

Eti unadhani kwa mtindo huo ninayofuraha gani duniani hapa. Milionea nisiye na ndugu wala mtoto pesa au hamjui kuwa mpaka sasa ninatafutwa na polisi!!

Hakuna sababu ya kuitwa Poor milionere heri nife tu" Joel Kaeneo alianguka juu ya sakafu pale pale kizimbani , akafa