Riwaya

Ni nani mbaya wangu?(4)

Wote tulikuwa tunajihisi wenye njaa sana. Philipo aliagiza tuletewe nusu kilo ya nyama ya mbuzi iliyochomwa pamoja na ugali sahani mbili.

Baada ya kula tulijiteremshia soda mbilimbili kisha tukarudi kulala.

Baada ya kukidhiana haja zetu vya kutosha, Ghafla Philipo alianza kuonesha mabadiliko. Hawa nilianza kuingiwa na wasiwasi mkubwa. Philipo hakuwa mtu wa hasira lakini sasa alionekana mwenye hasira huku akinitamukia maneno ya kashfa. Mara oh siku hizi inaonekana nimeshapata mshikaji mwingine, mimi siwezi kuoa mtu malaya hivi asiye niheshimu. Mh! kwa kuwa ni mtu mzima nilielewa hizo zilikuwa dalili mbaya lakini, sikuyajali hayo kwani nilijua siku zote haziendi sawa.

Niliona kukaa kimya tu hakutanisaidia lolote, hivyo nilijitoa moyo na kuuliza Philipo ana maana gani kunitamkia maneno ya ajabuajabu hivyo. Jibu nililolipata sikuwa ninalitegemea, aliniambia, 'umeshaniudhi sana tena sana, na tangu leo sitaki tujuane malaya mkubwa wee!'. kisha alisimama akaondoka zake huku akiwa ameyajenga matuta usoni.

Niliona ni aibu kubaki pake chumbani peke yangu, niliondoka nikajikokota hadi kwa shangazi na siku hiyo nililia sana. Sikujua nifanye nini baada ya Philipo kunirubuni niondoke kwa mume wangu na kisha kunikataa. Shangazi pamoja na mumewe aliniuliza niseme nilipolala jana lakini nashukuru tu, kwamba nilifanikiwa kuongopa wakanikubalia.

Niliendelea kukaa kwa shangazi hapo huku nikijishughulisha na ufumaji wa vitambaa. Baadhi ya wanawake walionifahamu walinishutumu sana walipoona nimeachana na mume wangu Denis kwa hakika hiyo ilikuwa aibu kubwa hata kwa ndugu na jamaa zangu.

Biashara yangu ya kuuza mwili wangu nilizidi kuiendeleza siku hata siku, nilikuwa nikijinunulia nguo za gharama kutokana na pesa nilizokuwa nikipewa na wanaume walio ni kodi. si hayo tu bali pia nilijipodoa kwa mikorogo mbalimbali na upende usipende ungeniona lazima tu ungenipenda kwa jinsi nilivyoonekana mrembo mzuri wa kuvutia.

Siku moja asubuhi nilimwona Denis akija pamoja na rafiki yake mpendwa Justin. Kama kawaida yangu nilikuwa nimekaa mbele ya nyumba shangazi hakuwepo; walikuwa wameenda vibaruani hivyo nilikuwepo mimi na binamu zangu watatu umri chini ya miaka minane.

Sikuamini macho yangu Denis hakuwa yule niliyemfahamu alikuwa kavalia viwalo na alionekana kupendeza sna alionekana mwenye furaha isiyomithilika, walipofika tulipeana salamu kama kawaida kisha wakaketi pale pale kwenye msingi nilipokaa. nilitaka niondoke pale lakini Justin aliniomba nitulie kwanza.

"Hatuna haja kuongea mengi ila tu tumekuja kukufauata twenda nyumbani" Justini alisema ili hali Denis naye akitikisha kichwa. Kumbe Denis alikuwa ameshauriwa na wazazi wake anifuate kwa kuwa hilo halikuwa jambo geni. Mwanamke aliyeolewa anaweza kurubunika na kutoroka lakini huwa radhi kurudi kwa mumewe kama atafuatwa na mumewe kwa utaratibu wa kibinadamu.

Kweli nilitamani kumrudia Denis lakini niliogopa kuchekwa na watu anaachika mwenyewe halafu anamrudia tena. mawazo hayo yalinitawala katika ubongo wangu nikajikuta nawajibu visivyo, niliwaambia sitaki kurudiana na Denis kama yeye ndiye mwanaume peke yake katika mji huu wa Tarime, waliudhika sana na waliondoka bila kunikwaheri. ' Najua tu atakuja kujikomba nimrudie tena na sitakubali haraka mpaka nitakapoamua kwa hiari yangu mwenyewe !?' nilijisemea moyoni.

Lakini mawazo yangu hayakuwa kama nilivyodhani Denis hakuwa na hamu tena ya kuja kunibembeleza nimrudie, alijenga chuki juu yangu na wala hakutaka kunisalimia kila tulipokuwa tukikutana mitaaani nilikuwa nikitumia ujumbe kuwa anifuate lakini mara nyingi alinijibu kuwa wakati tayari umeshapita na huo muda mchafu hanao tena alizidi kunichukia siku baada ya siku, cha ajabu mimi nilianza kumpenda kupindukia.

Vijana wengi wakiwemo wavuta bangi, wezi na wazururaji walikuwa wakiingia pale kwa shangazi kila mara wakinifuatilia baada ya kung'amua kuwa sina uchoyo wa mahaba, Shangazi yangu alianza kutoa lawama dhidi yangu na kuniambia waziwazi kuwa niondoke zangu ili nisije nikawasababishia shari ya kuvamiwa. mimi nilijidai kama sisikiii ingawa nilikuwa na masiko tena makubwa tu.

Kila mtu alinitambua kuwa mimi ni changudoa niliyekubuhu katika mji huu mdogo. Naelewa utakuwa mgumu wa kuamini lakini huu ndio ukweli wa mambo, nilikuwa nikiwahudumia kimwili hata ndugu watatu wa tumbo moja bila ya wao kugundua. niliendelea na ukahaba wangu na kuhofia kuadhiriwa na magonjwa ya kisasa, Leo hii ndio ninakumbuka hilo lakini nijiepushe vipi ili hali tayari nimeishakwisha!.

Hali ya afya yangu ilianza kudhoofika siku baada ya siku, nilokonda na kupandisha mabega na nywele zilianza kuonesha mabadiliko ambayo yalinitia wasiwasi, "Chakula ninakula kama kawaida hivi ninaisha hivyo kwa nini!? nilijiuliza sana.

Wapenzi wangu wote wanikimbia baada ya kuona hali yangu inazidi kutisha nilibakiwa na mpenzi mmoja tu huyu aliitwa John, yeye alikuwa mgumu kugundua na kushtukia, alitokea kunipenda sana na alinihudumia kila nilichoomba, kila nilipohitaji kutibiwa Baadhi ya watu walimshangaa sana jinsi alivyoambatana nami kama vile mawingu na mvua.

Nilitamani kuwapata wapenzi wangu wengine lakini kamwe sikuwapata, kila mtu aliniogopa jinsi nilivyoonekana kukonda na kunyong'onyea, nilijihisi mnyonge sana wa uzito wangu niliogopa kuonekana mchoni pa waungwana.

Nilijilaumu sana niliposikua kuwa Denis ameoa mwanamke mwingine tena mrembo mara dufu yangu kitu kilichonisumbua na kuumiza moyo wangu ni pale nilipoambiwa kuwa tayari wamejaliwa kupata mtoto kwa muda wa mwaka mmoja tu. habari hizo sikuzipokea kwa uzuri katika masiko na moyo wangu.

'Kifo cha nyani miti yote huteleza' John naye alianza kunikwepa kisiasa kila tulipokutana alitoa sababu zisizo na kichwa wala mkia zaidi ya hayo, alianza kuninyima matumizi kwa kisingizio kuwa hali ya uchumi imekuwa ngumu.

Sikuwa tena na vipodozi vya aina yoyote tofauti na yale mafuta ya Mamis tena kikopo cha shilingi mia, nilionekana kuchakaa kweli kweli, Hamu ya chakula iliniisha nikawa nikihitaji kupata chai ya maziwa au soda peke yake, Hakuna aliyeweza kunihudumia vitu vya namna hiyo mashavu yalianza kunishuka katika hali ya kuhuzunisha sana nilijiona kama mtu asiye na haki ya kuishi katika dunia hii ya Musa.

Bila ya kutegemea nilianza kutembelea sehemu za vibaruani nyakati za usiku na nilikuwa nikiwapata wazee ambao walikuwa wakinitimizia haja yangu kimwili. John aligundua huo upuuzi wangu, hivyo akawa amepata kisingizio tosha cha kuachana nami.

Katika pita pita yangu siku moja nilikutana na John, ilikuwa jioni na hali ya anga ilikuwa shwari tu.

Alishangaa kuona jinsi nilivyoraruka kuanzia nguo mpaka mwili aliinita pembeni mwa barabara kuu iendayo Sirari na Mara tukanza mauzungumzo.

"Samahani sana Hawa, naomba tangu leo uelewe nimevunja uhusiano wangu na wewe! Kumbe wewe U- malaya hivi!

Licha ya tahadhari zote nilizochukua, nimekataa. tangu sasa sikutaki tena! Bai bai" alisema na kuondoka.

Nilibaki nimeduwaa huku nikiwa nimeachama mdomo kwa takribani dakika sita hivi. niligundua sasa mwisho wangu umekaribia nilirudi nyumbani nikiwa nimechanganyikiwa kupita kawaida.

Shangazi yangu aliwaomba wazazi wangu wanafuate baada ya hali yangu kuzindi kuniharibikia, vidonda vilianza kuniandama tangu mdomonni hadi sehemu nyingine.

Nilijihisi wazi kuwa nina mdudu wa kisasa habari za vifo vya baadhi ya wapenzi wangu zilikuwa zinikinifikia mara kwa mara nilielewa wote hao walikuwa wanangamizwa na mdudu Ukimwi.

"Ukahaba jamani! Walinirubuni wanaume wa nje nikaivunja ndoa yangu sasa sitamaniki tena nimejitafutia makubwa na kujipotezea bahati ya kuifaidi dunia hii ya Musa. leo hii ninaonekana kama mzee wa miaka themanini na ninachokisubiri si kingine chochote bali kifo tu". Oh, Ukahaba jamani !!?' Huku nikiendelea kukingojea kifo, Hawa ninajuta na kulia sana.

Sasa hata mimi mwenyewe sijui kama ndimi chanzo cha mauti yao au ndio chanzo cha mateso yangu. Kama ni wao,

NI NANI MBAYA WANGU?

.............Mwisho..............